Waliofariki mashambulio ya Baidoa wafika 30

Somali Youth League
Maelezo ya picha, Mgahawa wa Somali Youth League ulikuwa umejaa watu wakitazama mechi

Idadi ya watu waliofariki kufuatia shambulio la al-Shabab katika mgahawa mmoja watu walipokuwa wakitazama mechi ya Arsenal na Manchester United mjini Baidoa imefika 30.

Watu 50 wanauguza majeraha hospitalini, mwanahabari mmoja wa eneo hilo ameambia BBC.

Mji wa Baidoa, ambao ndio makao makuu ya jimbo la Kusini Magharibi, ulikuwa chini ya al-Shabab kabla ya kukombolewa na majeshi ya Ethiopia wakishirikiana na wanajeshi wa Somalia mwaka 2012.

Rais wa jimbo hilo Shariff Hassan ameshutumu shambulio hilo na kuwahimiza wakazi kusaidia na maafisa wa usalama.

Gari lililotegwa mabomu lilitumiwa kulipua mgahawa wa Somali Youth League uliojaa watu waliokuwa wakitazama mechi hiyo ya Ligi ya Premia nchini Uingereza jioni. Baadaye, washambuliaji waliingia ndani

Kwenye shambulio la pili, mshambuliaji wa kujitoa mhanga alijilipua akiwa barabara, eneo lenye watu wengi.

Somali Youth League
Maelezo ya picha, Majumba yaliyokuwa karibu yaliharibiwa na mlipuko huo

Shambulio hilo lilitekelezwa viongozi wa mataifa yanayochangia majeshi kwenye Kikosi cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (Amisom) wakimaliza mkutano wao nchini Djibouti.

Viongozi hao walikubalia kwamba ipo haja ya kutathmini upya mkakati wa sasa wa kukabiliana na wapiganaji wa Kiislamu wa al-Shabab.

Katika siku za karibuni, kundi hilo limezidisha mashambulio, sana likilenga kambi za jeshi na maeneo ya umma.