Pierre Nkurunziza: Nani anaiongoza Burundi baada ya kifo cha Nkurunziza?

Pierre Nkurunziza
Maelezo ya picha, Aliyekuwa Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza

Zaidi ya saa 48 baada ya kifo cha ghafla cha rais wa Burundi Pierre Nkurunziza kumekua na hali ya suitafahamu kuhusu ni nani atakayechukuwa hatamu ya uongozi.

Rais Nkurunziza alifariki siku ya Jumatatu, na serikali ilithibitisha kuwa alifariki kutokana na 'mshutuko wa moyo' baadaye Jumanne.

Msemaji wa serikali ya Burundi Prosper Ntahorwamiye ameiambia BBC kuwa majadiliano yanaendelea kuhusu suala hilo.

"Tunajadili suala hili na mahakama ya katiba, kwa sasa inachachunguza nafasi ya uongozi, na mchakato huo utachukua siku kadhaa", aliiambia BBC.

Nkurunziza alikuwa anajiandaa kumpokeza madaraka rais mteule Meja Jenerali Evariste Ndayishimiye Agosti, 2020.

Bado haijafahamika ikiwa Bwana Nkurunziza alikuwa na virusi vya corona wakati anapata matibabu.

Katiba inasema nini?

Kwa mijibu wa katiba mpya iliyofanyiwa marekebisho Mae 17, 2018, kifungu 121 Spika wa bunge ndiye anastahili kuapishwa kuongoza nchi kwa kipindi cha mpito lakini hilo halijafanyika kufikia sasa.

"Endapo rais atajiuzulu, nafasi yake itashikiliwa na Spika wa bunge la Waakilishihe." kinasema kifungu hicho.

Pierre Nkurunziza

Chanzo cha picha, Getty Images

Burundi imeanza rasmi siku saba za maombolezo kufuatia kifo cha Rais Pierre Nkurunziza huku risala za rambi rambi kutoka kwa viongozi barani Afrika na kwingineko zikiendelea kumiminika.

Rais wa Tanzania, John Magufuli, amempongeza aliyekua rais wa Burundi kwa kile alichokielezea kama uongozi dhabiti.

Hata hivyo Wakosoaji nchini humo wamesema kwamba wanajuta kuwa Bwana Nkurunziza amefariki dunia hata kabla ya haki kishughulikiwa kufuatia dhulma iliyofanywa chini ya utawala wake.

Hali ya familia ya Nkurunziza

Kumekuwa na taarifa za kutatanisha katika mitandao ya kijamii kuhusu hali ya afya ya familia ya Rais Nkurunziza.

Denise Bucumi Nkurunziza mke wa aliyekuwa Rais wa Burundi ameondoka hospitalii jijini Nairobi saa chache baada ya kifo cha mumewe siku ya Jumanne.

Bi Nkurunziza,50, alisafirishwa kwa ndege kutoka Bujumbura hadi Nairobi Mei 28 kutibiwa ugonjwa ambao mpaka sasa haujawekwa wazi.

Maafisa katika ofisi ya rais nchin Burundi walipinga ripoti kwamba Bi Nkurunziza alipelekwa Nairobi kutibiwa virusi vya corona.

Denise Bucumi Nkurunziza

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mke wa Rais Nkurunziza Denise Bucumi Nkurunziza

Afisa wa hospitali ya kibinafsi ambapo mkewe Nkurunziza alikuwa amelazwa ameithibitishia BBC kwamba mama taifa wa Burundi aliruhusiwa kuondoka hapo Jumanne jioni, lakini hakutoa maelezo kuhusu hali yake ya afya.

Mwandisi wa kujitegemea mjini Bujumbura, Burundi, ameifahamisha BBC kwamba Denise Bucumi Nkurunziza aliwasili nchini kutoka Kenya usiku wa Jumanne.

Bi Nkurunziza, ambaye ni mama wa watoto watano na afisa wa zamani wa uhamiaji, amepata umaarufu nchini Burundi kutokana na wakfu wake wa 'Buntu' pamoja na miradi ya kusaidia wanawake.

Burundi inaadhimisha siku saba ya maombolezo kufuatia kifo cha mume wake.

Serikali ya Burundi pia imekanusha madai kuwa mama mzazi wa rais Pierre Nkurunziza amefariki.

Msemaji wa serikali ya Burundi Prosper Ntahorwamiye amesema kuwa mama wa rais Nkurunziza ni ''mgonjwa lakini hajafariki''.

Marais

Nkurunziza ni nani?

Pierre Nkurunziza amekuwa mwanasiasa wa Burundi na kuwa madarakani tangu mwaka 2005.

Bwana Nkurunziza, kijana wa aliyekuwa mbunge, alinusurika mauaji 1993 ya wanafunzi wa Kihutu katika chuo kiuu cha Burundi ambapo alikuwa mhadhiri na kujiunga na waasi wa FDD kundi ambalo baadae lilibadilika na kuwa chama tawala cha CNDD-FDD ambacho alikuja akawa kiongozi.

Alikuwa mwenyekiti wa chama tawala cha CNDD-FDD, hadi alipochaguliwa kama rais wa Burundi.

Maelezo ya video, Safari ya kisiasa ya Pierre Nkurunziza nchini Burundi

Baada ya makubaliano ya Amani ya Arusha kati ya serikali na waasi, Nkurunziza alitajwa kuwa waziri wa mambo ya ndani kabla ya bunge kumchagua kama rais Agosti 2005.

2015, Nkurunziza alichaguliwa katika uchaguzi uliokuwa na utata na chama chake kwa muhula wa tatu madarakani.

Wafuasi wake na wanaompinga Nkurunziza walikosa kukubaliana katika suala la ikiwa ilikuwa halali kwake kugombea tena na maandamano yakafuata.