Jenerali Seare Mekonen: Kiongozi wa jeshi aliyeuawa katika jaribio la mapinduzi Ethiopia ni nani?

Gen Seare Mekonen:

Chanzo cha picha, ETV

Ethiopia inaomboleza leo baada ya kuuawa kwa kiongozi wa jeshi nchini Jenerali Seare Mekonen aliyepigwa risasi na mlinzi wake hapo jana Jumapili katika mji mkuu Addis Ababa .

Jenerali Seare Mekonen Yimer, mwanajeshi mkongwe wa kikosi cha ulinzi Ethiopia (ENDF), aliteuliwa kama kiongozi wa jeshi mnamo Juni mwaka jana 2018 nchini Ethiopia.

Waziri mkuu Dkt Abiy Ahmed, alimteua Mekonen kumrithi Jenerali Samora Yunus, ambaye amekuwa akishikilia wadhifa huo mkuu katika kikosi chenye nguvu na kilichoogopewa nchini tangu Mei mnamo mwaka 2001.

Jenerali Samora alitimuliwa uongozini miezi miwili baada ya waziri mkuu Abiy kuingia madarakani. na alikuwa mshirika wa karibu wa Meles Zenawi, aliyefariki madarakani mnamo 2012.

Hatua ya waziri mkuu Abiy kumteua Jenerali Seare Mekonen ilitazamwa kama jitihada ya kuidhinisha mageuzi na kuchukuwa udhibiti wa taasisi kuu za serikali nchini humo.

Kadhalika ilikuwa ni fursa kwa waziri mkuu huyo kuidhinisha uongozi wake kwa jeshi la nchi hiyo.

Taarifa za Jenerali Seare Monnen kuuawa kwa kupigwa risasi hapo jana ziliwashutusha wengi ndani na hata nje ya Ethiopia.

Waziri mkuu Abiy Ahmed alikwenda kwenye kituo cha Televisheni akiwa na mavazi ya kijeshi kukemea mashambulizi hayo.

Hiki ni kipindi kigumu kwa Ethiopia na waziri mkuu Abiy, ambaye anakabiliwa na mizozo ya ndani ya nchi.

Tangu uchaguzi wa mwaka jana, Abiy amekua akipambana kumaliza mvutano wa kisiasa kwa kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa, kuondoa makatazo dhidi ya vyama vya kisiasa na kuwashtaki maafisa wanaoshutumiwa kukiuka haki za binaadamu.

ramani

Mambo muhimu kuhusu Jenerali Seare Mekonen:

Mpaka kupandishwa cheo kwake kuwa mkuu wa jeshi Ethiopia, Jenerali Seare alikuwa kiongozi wa pili mkuu wa jeshi na alikwea kwa haraka katika ngazi ya uongozi wa jeshi nchini.

Jenerali Seare Mekonen Yimer, mwenye umri wa miaka 56, ni wa kabila la Tigray, alizaliwa katika kijiji cha Tsimibila katika jimbo la kaskazini la Tigray.

Alikuwa mwanajeshi wa kupambana vita, alijiunga na Tigray People's Liberation Front (TPLF) mnamo 1978 akiwa na umri wa miaka 15 na kwa sehemu kubwa ya ujana wake, alishiriki mapigano dhidi ya utawala wa kidikteta wa Mengistu Hailemariam.

Baada ya utawala wa Mengistu kutimuliwa mnamo 1991, Seare alikuwa kamanda wa operesheni wa eneo la mashariki, linalojumuisha sehemu kubwa ukiwemo mpaka wa nchi hiyo na Djibouti, Somalia na Kenya.

Baada ya kuzuka mzozo wa mpaka kati ya Ethiopia-Eritrea mnamo 1998, alichaguliwa kuwa kamanda wa eneo la Bure kaskazini mashariki mwa Ethiopia, karibu na bandari ya Eritrea- Assab.

Mnamo Julai 1999, rais Negaso Gidada alimpandisha cheo Seare na kuwa Brigedia Jenerali akiwa na umri wa miaka 35.

Baada ya hapo alihamishwa katika eneo la Zalambessa alafu katika eneo la kaskazini Badme hadi kumalizika vita mnamo Desemba 2000.

Kama kiongozi wa kikosi cha ulinzi cha kaskazini, Jenerali Seare alikuwa na jukumu kuu wakati wa vita vya miaka miwili na Eritrea.

Baada ya hapo alihamishwa kuelekea Ethiopia mashariki kama kamanda wa kitengo cha 107 Core.

Mnamo 2012, Seare alipandishwa cheo na rais Girma Woldegiorgis kuwa Meja Jenerali na miaka miwili baadaye akateuliwa kuwa Luteni Jenerali.

Mnamo Februari 2018, alipandishwa cheo kwa mara nyingine kuwa Jenerali kamili na akachaguliwa kama naibu mkuu wa majeshi na rais Mulatu Teshome, mbele ya waziri mkuu aliyekuwepo Hailemariam Desalegn.

Kiongozi huyo wa jeshi aliyeuawa kwa kupigwa risasi ya kifuani na mlinzi wake hapo jana, alikuwa mshauri wa Meles, akiwa amemsaidia kiongozi huyo wa zamani katika kipindi cha mvutano wa ndani ya TPLF mnamo 1998.