Bunge la Tanzania laazimia kutofanya kazi na CAG baada ya kumtia 'hatiani' kwa kudharau mhimili huo

Spika Job Ndugai

Chanzo cha picha, Bunge

Maelezo ya picha, Spika Job Ndugai aliagiza CAG ahojiwe mwezi Januari akidai kuwa amelidharau Bunge

Bunge la Tanzania limeazimia kutokufanya kazi na Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za serikali, (CAG) wa nchi hiyo Prof Musa Assad baada ya kumtia hatiani kwa tuhuma za dharau kwa chombo hicho.

Wabunge wamefikia uamuzi huo baada ya Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kutaka waridhie mapendekezo yao dhidi ya CAG.

Kamati hiyo ilimhoji CAG Januari 21 baada ya kufanya mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya redio ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York mwezi Disemba 2018 ambapo alisema kuwa Bunge la Tanzania halina meno na hivyo limeshindwa kuiwajibisha ipasavyo serikali.

"…Kama tunatoa ripoti na inaonekana kuna ubadhilifu halafu hatua hazichukuliwi huo kwangu mimi ni udhaifu kwa Bunge. Bunge linatakiwa liisimamie (serikali) na kuhakikisha kuwa pahali penye matatizo basi hatua zinachukuliwa...Sie kazi yetu ni kutoa ripoti tu na huo udhaifu nafikiri ni jambo la kusikitisha lakini ni jambo tunaamini muda si mrefu huenda likarekebishika. Lakini tatizo kubwa tunahisi kwamba bunge linashindwa kufanya kazi yake kama inavyotakiwa," Profesa Assad aliiambia radio ya UN.

Spika Job Ndugai alilieleza Bunge mwezi Januari kuwa maelezo ya Assad yalioonesha dharau kubwa dhidi ya mhimili huo na kumtaka aende mbele ya kamati kwa hiyari yake, ama apelekwe kwa pingu.

Ripoti ya Kamati

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Maadili ya Bunge, mwenyekiti wa kamati hiyo Emmanuel Mwakasaka amesema: "Tumejiridhisha CAG Assad amelidhalilisha Bunge na Kamati inamtia hatiani kwa kulidharau Bunge na kudhalilisha shughuli za chombo hiki."

Mwakasaka amesema Prof. Assad alikiri mbele ya kamati kuliita Bunge dhaifu lakini alipingana na tafsiri ya neno 'dhaifu' iliyopo kwenye Kamusi ya Kiswahili Sanifu inayosema 'goigoi, hafifu, isiyo imara' akisitiza kiuhasibu udhaifu ni 'upungufu'.

Ruka Twitter ujumbe, 1
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Mwisho wa Twitter ujumbe, 1

"Tuliangalia maana ya neno upungufu kwenye kamusi tukabaini ni 'isiyo kamili, isiyo imara', hivyo alidhamiria kulidhalilisha Bunge," amesema Mwakasaka na kuongeza: "Tulimuuliza CAG Assad kama ataacha kulitumia neno udhaifu akasisitiza ataendelea kulitumia na hakujutia kulitumia dhidi ya Bunge. CAG hakuomba msamaha wala kujutia na akasisitiza ataendelea kulitumia neno hilo."

Kamati hiyo pia imemtia hatiani mbunge wa Kawe (Chadema) Halima Mdee ambaye aliunga mkono kauli hiyo ya CAG kuwa Bunge ni dhaifu.

Kamati imependekeza Mdee asimamishwe kuhudhuria mikutano miwili ya Bunge kuanzia leo Aprili 2.

Ruka Twitter ujumbe, 2
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Mwisho wa Twitter ujumbe, 2

Mdee aliiambia kamati kuwa aliunga mkono kauli ya CAG kwani ana uhuru kikatiba wa kutoa maoni yake.

"...baada ya kumweleza maana ya neno 'dhaifu' kwa mujibu wa kamusi, alikiri kukosea kulitumia kuunga mkono kauli ya Prof. Assad, lakini hakuonyesha kujutia, hivyo alikuwa na dhamira ovu ya kulidharau na kulidhalilisha Bunge mbele ya umma," inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.

Hata hivyo, wabunge wa upinzani wamepingana vikali na ripoti ya kamati hiyo ya Bunge.

Ruka Twitter ujumbe, 3
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Mwisho wa Twitter ujumbe, 3

Kiongozi wa Upinzani Bungeni Freeman Mbowe amelieleza Bunge kuwa hatua hiyo dhidi ya CAG ni kuminya mawazo ya watu.

"Mnataka kuwanyima watu haki na uhuru wa mawazo ilhali Katiba imeruhusu kila mtu, akiwamo CAG ana uhuru wa kutoa mawazo na kueleza fikra zake, kufanya mawasiliano na kutoingiliwa kuhusu taarifa yake...Kamati hii ya maadili haiwezi kutenda haki dhidi ya watu wanaoibua hoja zinazoonekana kutoifurahisha serikali," amesema Mbowe.

Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema naye alisimama bungeni na kusema kuwa chombo hicho ni dhaifu. Hapo hapo, Naibu Spika Dkt Tulia Ackson akaagiza ahojiwe na kamati ya maadili. Baada ya kauli hiyo, wabunge kadhaa wa kambi ya upinzani wakatoka nje ya bunge kuashiria mgomo wao.

Kumwondoa kazini CAG

Kwa mujibu wa katiba ya Tanzania, CAG huondoka madarakani baada ya kufikisha umri wa kustaafu ama kujiuzulu wadhifa wake.

Ibara 144 ya katiba pia inasema CAG anaweza kuondolewa katika madaraka ya kazi yake kwa sababu ya kushindwa kutekeleza kazi zake (ama kutokana na maradhi au sababu nyingine yoyote) au kwa sababu ya tabia mbaya, au kwa kuvunja masharti ya sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Hata hivyo, kuna utaratibu maalumu wa kumwondoa ambapo ibara ya 144 (3) inabainisha kuwa iwapo rais ataona kwamba suala la kumwondoa kazini CAG lahitaji kuchunguzwa, basi atateua Tume Maalum ambayo itakuwa na Mwenyekiti na Wajumbe wengine wasiopungua wawili.

Mwenyekiti na angalau nusu ya wajumbe wengine wa tume hiyo itabidi wawe watu ambao ni Majaji au watu waliopata kuwa Majaji wa Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufani katika nchi yoyote iliyomo kwenye Jumuiya ya Madola.

Iwapo Tume itamshauri rais kwamba huyo CAG aondolewe kazini kwa sababu ya kushindwa kufanya kazi kutokana na maradhi au sababu nyingine yoyote au kwa sababu ya tabia mbaya, basi rais atamwondoa kazini.

Wakati wa uchunguzi, rais anaweza kumsimamisha kazi CAG. Lakini uamuzi huo utabatilika ikiwa Tume itamshauri rais kwamba huyo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu asiondolewe kazini.