Kifo cha rais John Pombe Magufuli: Namna 'tingatinga' alivyoiongoza Tanzania kwa miaka sita

John Pombe Magufuli

Chanzo cha picha, Getty Images

Mtoto wa mkulima, John Pombe Magufuli alichukua hatamu kama rais wa Tanzania kwa mara ya kwanza siku aliyotimiza miaka 56 na amekuwa kiongozi ambaye amevuta hisia mseto hasa, katika siku za hivi karibuni kutokana na msimamo wake kuhusu janga la Corona .

Alichaguliwa kwa muhula wa pili mwaka wa 2020 huku upinzani ukilalama kuhusu madai ya wizi wa kura na vitisho.

Kabla ya kuwa rais alipachikwa jina la tingatinga kutokana na namna alivyosimamia mipango ya ujenzi wa barabara nchi nzima akiwa Waziri wa Ujenzi na baadaye akasifika kwa msimamo wake mkali dhidi ya ufisadi na kuchukizwa na uharibifu wa fedha za umma .

Kama rais pia alishtumiwa kwa kukandamiza wakosoaji wake na kuminya uhuru wa kujieleza ,lakini kufuatia kifo chake ,mengi sasa yataangaziwa kuhusu msimamo wake kuhusu namna ya kukabiliania na janga la Corona.

'Corona ni shetani'

Wakati janga la Corona lilipoingia nchini Tanzania Rais Magufuli hakuamini kwamba watu wanatakiwa kusalia nyumbani kama sehemu ya kujikinga .Aliwataka waende makanisani na misikitini kufanya maombi.

"Corona, ambayo ni shetani haiwezi kuishi katika mwili wa Yesu Kristu…itachomeka mara moja," alisema Magufuli akiwa kanisani katika mji mkuu wa Dodoma. Magufuli alijipambanua kama mfuasi thabiti wa Kanisa Katoliki.

A man leaves a steam inhalation booth in Dar es Salaam, Tanzania, on 22 May, 2020

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Magufuli alipigia upatu tiba mbadala kama kujifukiza katika vita dhidi ya corona.

Tangu Juni mwaka wa 2020 alipotangaza kwamba Tanzania haina corona, rais na viongozi wengine wa serikali walionekana kutilia mashaka ufanisi wa matumizi ya barakoa pamoja na ubora wa vipimo vya corona na hata kuzifanyia mzaha nchi jirani zilizotangaza mikakati mbalimbali ya kupambana na corona.

Vipimo vichache sana vilifanywa na hapakuwa na mpango wa kutoa chanjo na kuiacha nchi ikiwa imejitenga na hatua zilizokuwa zikichuliwa na mataifa mengine.

Maelezo ya video, Kifo cha rais John Pombe Magufuli: Tanzia ya rais wa awamu ya tano Tanzania

Lakini alipoapishwa Oktoba mwaka wa 2015 alionekana kama mtu ambaye Tanzania ilimhitaji - mchapakazi na mtu asiyeweza kuvumilia ufisadi.

'Tingatinga' laingia kazini

Hatua zake zilizoangazia utendakazi na matokeo zilipigiwa mfano kote barani Afrika, wengi wakisema kipindi hicho kuwa - dozi yake ilihitajika kwa mataifa kushughulikia masuala yao mengi ya utawala.

Katika siku yake ya kwanza ofisini kama rais alituma ujumbe mkali kwamba asingevumilia tatizo sugu la utoro kazini kwa wafanyakazi wa umma na kuzuru wizara ya fedha na kuuliza walipokuwa maafisa mbalimbali katika wizara hiyo .

Pia alikabiliana na kufuta maelfu ya wafanyakazi hewa kutoka katika mfumo wa malipo ya serikali na 'kuwatumbua' hadharani maafisa waliotuhumiwa kwa ufisadi ama kutofikia viwango vya ufanisi vilivyotakiwa. Wakati mwingine yote hayo yalifanywa katika runinga, mubashara

Alianza pia kwa kukabiliana vikali na alichokiona kama uharibifu wa pesa za umma huku akifuta sherehe ya kuadhimisha siku ya uhuru kwa mara ya kwanza katika miaka 54. Badala yake aliagiza pafanyike kampeni ya usafi nchi nzima na yeye mwenyewe akiwa mstari wa mbele katika shughuli hiyo, akizoa taka nje ya Ikulu.

John Magufuli

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Magufuli alishiriki kampeni ya usafi

Pia alipiga marufuku zafari za nje ya nchi kwa wafanyakazi wa umma.

Katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Magufuli mtindo huo wa uongozi ulimpa sifa sana na hata kauli mbiu zikaibuka kwenye twitter chini ya hashtag: #WhatWouldMagufuliDo.

Mwaka wa 2017 profesa mmoja wa Kenya alichukua hatua ya kufananisha mtindo wa Magufuli wa uongozi kama 'Magufulication of Africa ' wakati akitoa hotuba katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Lakini kuanzia mwanzo ilikuwa wazi kwamba kulikuwa na wingu zito juu ya uongozi wake- hatua na kauli zake nyingi zilianza kubana nafasi ya demokraia nchini Tanzania

line

John Magufuli kwa kifupi

  • Alizaliwa Chato, kaskazini-magharibi mwa Tanzania, mwaka 1959
  • Alisomea Kemia na Hesabu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
  • Alifanyakazi kama mwalimu wa Kemia na Hesabu
  • Alichaguliwa kama mbunge mara ya kwanza mwaka 1995
  • Alikuwa Waziri kamili mwaka 2000
  • Alishinda urais kwa mara ya kwanza mwaka 2015
  • Alishinda awamu ya pili katika uchaguzi wa 2020
line

Mnamo Januari 2016 ikiwa ni miezi miwili tu toka alipoingia madarakani kwa mara ya kwanza, serikali yake ilitangaza kusitisha matangazo mubashara ya vikao vya bunge, ikisema hatua hiyo ni mkakati wa kupunguza matumizi ya fedha za umma.

Upinzani na wanaharakati walichukulia hatua hiyo kama ya udhibiti na si kubana matumizi. Vikao vya bunge vilikuwa vikitumika na wapinzani na wabunge kutoka chama tawala pia kuiwajibisha serikali, na matangazo ya vikao hivyo yalikuwa yakifuatiliwa kwa karibu na wananchi.

Mfano mwingine wa udhibiti umeonekana katika kufungiwa kwa nyimbo ama wasanii ambao wameonekana kukosoa utawala. Mwaka 2017, msanii maarufu wa Tanzania Nay wa Mitego alikamatwa punde tu baada ya kuachia kibao ambacho kilikuwa kikiikosoa serikali.

John Magufuli voting on 28 October 2020

Chanzo cha picha, Aboubakar Famau

Ingawaje rais Magufuli aliagiza kuachiliwa huru kwa mwimbaji huyo siku iliyofuatia, alishauri pia mistari ya kibao hicho kuboreshwa ili kuzungumzia matatizo mengine ya jamii kama ukwepaji wa kodi.

Mwaka wa 2017 mbunge Tundu Lissu ambaye miaka mitatu baadaye aligombea urais dhidi ya Magufuli alijeruhiwa vibaya baada ya kumiminiwa risasi akiwa nje ya nyumba yake katika mji mkuu wa Dodoma.

Lissu aliishtumu serikali kwa kujaribu kumuua katika kipindi ambacho alikuwa ni moja ya wakosoaji wakubwa wa serikali na akikabiliwa na kesi kadhaa za uchochezi ikiwemo kumuita rais Magufuli dikteta. Serikali ilikana kuhusika na shambulio hilo.

Rais Magufuli

Katika kile kinachotafsiriwa na makundi ya kutetea haki za binadamu kama ukandamizaji wa uhuru wa vyombo vya habari utawala wa rais Magufuli ulivifungia kwa muda ama moja kwa moja baadhi ya vyombo vya habari nchini humo. Shirika la Amnesty International pia linaripoti kuwa waandishi nchini humo wana hofu ya kulengwa na mamlaka.

Deni kubwa la kodi

Utawala wa Magufuli pia uliendelea kuchukua hatua nzito na zisizo za kawaida mathalan kupitishwa kwa sheria zilizolenga kuongeza mapato kutoka kampuni za kimataifa za uchimbaji madini.

Mnamo mwaka wa 2017, Acacia Mining, kampuni iliyokuwa ikimilikiwa na Barrick Gold ya Canada ilitozwa mzigo mkubwa wa deni la la kodi la $190 bilioni kutokana na mirabaha ambayo serikali ilisisitiza kuwa inaidai kampuni hiyo, japo kampuni yenyewe ilikana kufanya kosa lolote.

Katika kulimaliza suala hilo, kampuni mama ya Accacia, Barrick Gold ilikubali kulipa dola milioni 300, na kisha ikaivunja kampuni ya Accacia na kuunda kampuni mpya ya uchimbaji madini ya Twiga Mineral huku serikai ikimiliki asilimia 16 ya kampuni hiyo. Barrick na serikali pia zilikubaliana kuhusu ugavi wa mapato ya manufaa ya baadaye ya kiuchumi kwa asilimia 50-50.

Kisha kukawa na suala tata la kuzima majaribio ya kuondoa katazo la wasichana wanaoshika ujauzito kurejea katika mfumo rasmi wa elimu mara baada ya kujifungua.

Lakini hata wakosoaji wanakubali kwamba Magufuli alichangia ukuaji wa Tanzania kupitia miradi mikubwa ya miundombinu kama vile kutengenezwa kwa reli ya SGR ambayo ikikamilika itaiunganisha Tanzania na majirani zake, upanuzi na utengenezaji wa barabara kuu na ujenzi wa mfumo wa usafiri wa mabasi ya mwendokasi jijini Dar es Salaam.

Pia aliongeza uzalishaji wa nishati ya umeme katika gridi ya taifa na kupunguza tatizo la mgao wa umeme. Moja ya mambo makubwa aliyofanya pia ni kulifufua Shirika la Ndege la Air Tanzania.

Former Tanzanian President Julius Kambarage Nyerere

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Magufuli alimtaja kiongozi wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, kama kioo chake katika uongozi.

Magufuli alimtaja kiongozi wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye pia alitetea uhuru wake na wa nchi yake changa kama kioo chake cha uongozi. Yaonekana namna alivyokabiliana na corona ni katika misimamo ya kutaka kuachwa huru na kile ambacho anakiamini.

"...Baba wa Taifa hakuwa mtu wa kuambiwa la kufanya ... hawa wanaoweka haya masharti (ya kujifungia), wamezoea kutoa maagizo haya ambayo hata Nyerere aliyakataa," alisema Magufuli kwa kupiga mfano wa namna Mwalimu Nyerere alivyokuwa akikataa ushauri wa mataifa ya magharibi ambao wajamaa hawakuyaamini.

Kutoka katika lindi la umasikini

Magufuli alizaliwa na kukulia wilayani Chato, kaskazini-mashariki mwa Tanzania pembezoni mwa Ziwa Victoria, na ameeleza katika uhai wake kuwa familia yao ilikuwa ya kipato duni.

Nyumba yao ilikuwa ya nyasi, na alichunga ng'ombe kama watoto wengine wa kiume kijijini kwao na alikuwa akiuza maziwa ili kusaidia kusaka kipato cha familia.

"Ninajua maana ya kuwa masikini," alisema Magufuli kwenye kampeni mwaka 2015 akiahidi kufanya kazi kwa juhudi ili kuwamua hali a masikini nchini humo.

Kabla ya kujitosa kwenye siasa mwaka 1995 na baada ya kumaliza chuo kikuu alifanya kazi kama mwalimu wa hesabu na kemia na pia kama mkemia kiwandani.

Supporters of the CCM party

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Magufuli remained popular across Tanzania despite the criticism

Alishinda ubunge kwa mara ya kwanza mwaka 1995 na moja kwa moja kuteuliwa na rais Benjamin Mkapa kuwa naibu waziri wa ujenzi. Mama Anna Abdallah ndiye aliyekuwa waziri kamili wa ujenzi na anasema kuwa utenda kazi, kujituma na umakini wake uliweza kuonekana toka awali. Katika mwaka wake wa kwanza aliweza kuanzisha ujenzi wa barabara ambayo ilikawia kwa muda mrefu.

Mwaka 2015, ikiwa ni miaka 20 kamili toka ajitose kwenye siasa za ushindani, Magufuli aliingia kwenye kinyang'anyiro cha urais. Japo yeye mwenyewe alisema kuwa alijaribu tu, chama tawala CCM kilimpitisha kugombea na hatimaye kushinda wadhifa huo. Kabla ya kiny'anganyiro mchuano mkali ulikuwa baina ya makada Edward Lowassa na Bernard Membe ambao hata hivyo walikatwa katika ngazi mbalimbali za chama.

Uchaguzi wa 2015 ndio ulikuwa na ushindani mkali zaid katika historia ya nchi hiyo baada ya Lowassa kuhamia upinzani. Hata hivyo Magufuli alipata ushindi wa asilimia 58.

Alinyakua ushindi kwa awamu ya pili kwa kuzoa asilimia 84 ya kura japo wapinzania walisusua mataokeo ya uchaguzi huo wakidai kuwa kulikuwa na wizi wa kura.

Wito wa kutaka viongozi wengine barani Afrika kumuiga Magufuli ulienda ukisuasua kadri ukusoaji dhidi yake kutoka kwa wapinzani, wanaharakati na mataifa ya magharibi ulivyokuwa ukiongezeka.

Lakini kwa kuwa alijitanabahisha kama mzalendo wa kiafrika aliyekuwa akipambana dhidi ya mabeberu waliokuwa wakitaka kuendelea kuinyonya nchi yake, ukosoaji dhidi yake haukumnyima usingizi. Msimamo huo, ndio yawezekana ulichangia namna ambavyo alipambana na janga la corona.

Uchunguzi wa BBC