Got a TV Licence?

You need one to watch live TV on any channel or device, and BBC programmes on iPlayer. It’s the law.

Find out more
I don’t have a TV Licence.

Habari za moja kwa moja

Na Asha Juma, Lizzy Masinga na Ambia Hirsi

time_stated_uk

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo ya moja kwa moja. Kwaheri.

  2. Mgomo wa madaktari wasitishwa nchini Kenya

    xx

    Madaktari nchini Kenya wamesitisha mgomo ambao ulikuwa umelemaza mfumo wa huduma za afya nchini kwa siku 56.

    Muungano wa madaktari na serikali walifikia makubaliano baada ya mazungumzo makali. Moja ya masuala yenye utata bado hayajatatuliwa.

    Madaktari huo sasa wanatarajiwa kurejea kazini ndani ya saa 24 zijazo.

    Hatua hiyo inawapa afuane Wakenya ambao wamekuwa wakihangaika kwa kukosa huduma za matibabu.

    Serikali na chama cha madaktari wameshindwa kufikia makubaliano juu ya huduma na malipo ya madaktari tarajali, ambao ni uti wa mgongo wa mfumo wa afya ya umma.

    Muungano huo unataka madaktari bingwa kulipwa dola 1,500 kwa mwezi, lakini serikali inasema inaweza kumudu kuwalipa dola 500 pekee.

    Kesi hiyo sasa itaamuliwa na mahakama, kumaanisha kuwa madaktari tarajali hawakuwa kazini kwa siku 60 zijazo.

    Soma pia:

    Mgomo wa madaktari Kenya: Umma ulivyobaki njia panda

  3. Mapigano yaripotiwa mashariki mwa Rafah huku Israel ikifungua tena kivuko cha msaada cha Kerem Shalom

    Watu wakikimbia mapigano

    Kumekuwa na mapigano makali na mashambulizi ya mabomu karibu na mji wa kusini wa Gaza wa Rafah, huku Israel ikisema kivuko muhimu cha Kerem Shalom kimefunguliwa tena kwa ajili ya msaada.

    Jeshi la Israel limesema wanajeshi wamewaua wapiganaji wa Hamas mashariki mwa Rafah kama sehemu ya operesheni "sahihi" ya kukabiliana na ugaidi.

    Hamas pia waliripoti vita. Hapo awali, wanajeshi walisema malori yalikuwa yamefika Kerem Shalom, ambayo ilikuwa imefungwa baada ya shambulio la roketi siku ya Jumapili.

    Hatahivyo, shirika la Umoja wa Mataifa lilisema hakuna vifaa vilivyoingia kupitia kivuko bado. Umoja wa Mataifa ulikuwa umeelezea wasiwasi wake siku ya Jumanne juu ya kile ulichokiita "kufungwa" kwa njia mbili kuu za misaada ya Gaza, baada ya wanajeshi wa Israel kuchukua udhibiti wa upande wa Wapalestina wa kivuko cha karibu cha Rafah na Misri.

    Wakati huo huo, mazungumzo kuhusu makubaliano mapya ya kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka yameanza tena mjini Cairo, huku Marekani ikisema inaamini pendekezo lililofanyiwa marekebisho la Hamas linaweza kuleta mafanikio.

    Jeshi la Israel lilipuuza umuhimu wa uamuzi wa serikali ya Marekani kusitisha shehena ya mabomu yenye nguvu kutokana na wasiwasi kwamba Israel ilikuwa karibu kufanya mashambulizi makubwa katika mji wa Rafah.

    Miezi saba ya vita vyake na Hamas huko Gaza, Israel imesisitiza ushindi hauwezekani bila kuuchukua mji wa Rafah. Lakini huku zaidi ya Wapalestina milioni moja waliokimbia makazi wakikimbilia huko kutokana na mapigano.

    Umoja wa Mataifa na madola ya Magharibi yameonya kwamba shambulio la kila upande linaweza kuwa na matokeo mabaya ya kibinadamu.

  4. Baba aliyenaswa katika jengo lililoporomoka Afrika Kusini aokolewa

    Delvin Safers, anayeonekana hapa na mwanawe Zyar, amelazwa hospitalini baada ya kuokolewa

    Waokoaji walishangilia walipopata manusura wengine watatu wakiwa wamekwama chini ya jengo ambalo liliporomoka katika mji wa pwani wa Afrika Kusini wa George siku ya Jumatatu.

    Miongoni mwa walionusurika ni Delvin Safers, 29, ambaye masaibu yake yalifuatiliwa kwa karibu na Waafrika Kusini alipokuwa akiwatumia wazazi wake na mpenzi wake maelezo ya sauti kutoka chini ya vifusi, akiwaambia jinsi alivyokuwa akiwapenda.

    Yeye ni miongoni mwa manusura 29 ambao wameokolewa huku shughuli za uokoaji na utafutaji zikiendelea kwa siku ya tatu kuwapata watu 39 ambao bado hawajulikani walipo.

    Watu saba wamethibitishwa kufariki, na miili yao imetolewa.

    George ni kivutio maarufu cha watalii, kando ya Njia ya Bustani ya kuvutia katika mkoa wa Western Cape.

    Jengo hilo la ghorofa tano liliporomoka lilipokuwa likijengwa.

    Watu wote walionaswa chini ya vifusi walikuwa wafanyakazi katika eneo hilo.

    Baba yake Delvin, Dion Safers, aliiambia BBC kwamba mwanawe alikuwa akipata matibabu hospitalini.

    Dion alikuwa amepiga kambi karibu na eneo hilo tangu Jumatatu, akiwa karibu na kukata tamaa na pia matumaini kwamba mtoto wake angepatikana akiwa hai.

    Hapo awali alikuwa ameeleza jinsi miguu na mkono mmoja wa mwanawe ulivyobanwa chini ya ubao. Operesheni ya uokoaji ni tata, na inahusisha watu 200 wenye mbwa wa kunusa, vifaa vya kunyanyua vitu vizito na kuondoa matofali ya zege na uchafu kwa mikono.

    Kati ya watu 29 walionusurika, sita wana majeraha ya kutishia maisha na 16 wako katika hali mbaya.

    Ramani
  5. Kenya yatangaza siku ya kuwakumbuka waathiriwa wa mafuriko

    Zaidi ya Wakenya 200 wamefariki kutokana na mafuriko hayo

    Kenya ilitangaza Ijumaa hii kuwa sikukuu ya kitaifa kuwakumbuka waliofariki kutokana na mafuriko yanayoendelea nchini pamoja na Wakenya kupanda miti.

    Zaidi ya watu 200 tayari wamekufa kutokana na mafuriko makubwa kote nchini, huku zaidi ya milioni 250 wakiathiriwa na hali hiyo.

    Rais William Ruto alisema Jumatano kuwa siku hiyo itawaruhusu Wakenya kupanda miti ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi ambayo yamesababisha mafuriko makubwa.

    Msemaji wa serikali, Isaac Mwaura, alikuwa amesema notisi maalumu itatolewa ikitaja Ijumaa kuwa Siku ya Kitaifa ya kupanda Miti.

    Alisema baadaye waziri wa mazingira atatoa maelekezo zaidi kuhusu suala hilo.

    Mwaka jana, serikali kwa mara ya kwanza iliwapa Wakenya likizo maalumu ya kupanda miti milioni 100 kama sehemu ya lengo kuu la kupanda miti bilioni 15 katika miaka 10.

    Soma pia:

    Mafuriko Kenya: Jinsi mafuriko yanavyofichua hali mbaya ya mazingira ya Nairobi

    'Nitafanya nini sasa wanangu wamesombwa mbali?'

    Ramani
  6. Diane Rwigara - Mwanaharakati wa Rwanda atangaza nia ya kuwania urais

    Samba Cyuzuzo

    BBC Great Lakes

    Diane Rwigara

    Mwanaharakati maarufu wa Rwanda na mkosoaji wa Rais Paul Kagame ametangaza nia yake ya kuwania urais wa Rwanda kabla ya uchaguzi mkuu wa Julai.

    Diane Rwigara alijaribu hatua hiyo mwaka wa 2017 lakini ombi lake lilikataliwa na tume ya uchaguzi kwa madai kwamba alikusanya sahihi ghushi ili kuidhinisha azma yake ya kuwania urais.

    Bi Rwigara, 42, mkosoaji wa Rais Paul Kagame na chama tawala, alikanusha madai hayo akisema aliondolewa kwa sababu za kisiasa.

    Bi Rwigara, amethibitishia BBC kwamba ananuia kugombea katika uchaguzi ujao.

    Mwezi mmoja baada ya uchaguzi wa 2017, yeye, pamoja na mwanawe na dada yake, walifungwa jela kwa tuhuma za kuchochea uasi, kughushi na kukwepa kulipa kodi, alifutiwa mashtaka na kuachiliwa baada ya mwaka mmoja jela.

    Ikiwa ugombea wake atakubaliwa, anatarajiwa kuwania urais kama mgombea wa upinzani na huru, katika uchaguzi ambapo hakuna upinzani mkubwa unayotarajiwa dhidi ya Bw Kagame.

    Bi Rwigara ni binti wa mfanyabiashara maarufu wa Rwanda, Assinapol Rwigara, aliyekuwa mshirika wa chama tawala, ambaye kifo chake mwaka 2015 kilizua uhasama kati ya familia yake na mamlaka.

    Polisi walisema alifariki katika ajali ya barabarani huku familia yake ikisema aliuawa.

  7. Marekani yabatilisha leseni za mauzo ya 'chip' kwa Huawei ya China

    Marekani ilipunguza kwa kasi uuzaji wa bidhaa kama vile chip za kompyuta kwa Huawei kuanzia mwaka wa 2019

    Serikali ya Marekani imesema imefuta baadhi ya leseni zilizowaruhusu watengenezaji chip nchini Marekani kusafirisha bidhaa fulani kwa kampuni kubwa ya teknolojia ya China Huawei.

    Idara ya Biashara haikubainisha ni vibali vipi vilivyofutwa lakini hatua hiyo imekuja baada ya Huawei kutoa kompyuta inayoweza kutumia AI (akili mnemba) inayoendeshwa na chip iliyoundwa na Intel.

    Watengenezaji chip wa Marekani, Intel walikataa kutoa maoni kwa BBC. BBC pia imewasiliana na Huawei na kampuni kubwa ya Qualcomm ya San Diego kupata maoni.

    Tangu mwaka wa 2019, Marekani imezuia mauzo ya teknolojia, kama vile chip za kompyuta, kwa Huawei, ikibainisha sababu kuwa uhusiano na jeshi la China.

    "Tumebatilisha leseni fulani za mauzo ya nje kwa Huawei," Idara ya Biashara ilisema katika taarifa Jumanne, lakini haikutoa maelezo ya vibali vilivyoondolewa.

    Baadhi ya wabunge wa Marekani walikuwa wamekosoa utawala wa Rais Joe Biden kufuatia uzinduzi wa mwezi uliopita wa kompyuta ya mkononi ya Huawei ya MateBook X Pro.

    Huawei imeathiriwa sana na vikwazo vya biashara vya Marekani lakini hivi karibuni ilionekana kurudi tena.

    Kampuni ya China imefurahia ufufuo hasa baada ya kuzinduliwa kwa simu mahiri ya Mate 60 Pro mwezi Agosti.

    Marekani imeweka vikwazo kwa makampuni kadhaa ya teknolojia ya China katika miaka ya hivi karibuni, huku mvutano kati ya mataifa hayo mawili yenye uchumi mkubwa duniani ukizidi.

    Mapema mwezi huu Rais Biden alitia saini sheria ambayo inaweza kupiga marufuku programu ya video ya TikTok nchini humo isipokuwa iwe inauzwa na kampuni mama ya China. TikTok iliwasilisha kesi Jumanne kuzuia sheria hiyo.

    Beijing imelaani hatua za Washington dhidi ya kampuni zake, na kuzitaja kama 'unyanyasaji wa kiuchumi'.

  8. Kenya: Wasafirishaji haramu wawatelekeza makumi ya Waethiopia vichakani

    Polisi nchini Kenya wanawazuilia raia 24 wa Ethiopia waliokuwa wametelekezwa msituni kaskazini-mashariki mwa kaunti ya Isiolo, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya eneo hilo.

    Raia hao wa kigeni wanasemekana kutafuta usaidizi katika kituo cha polisi cha Merti baada ya watu wanaoshukiwa kuwa wasafirishaji haramu kuondoka Jumapili.

    Wasafirishaji hao wasiojulikana waliripotiwa kukwepa vizuizi kwenye barabara kuu ya Isiolo- Nairobi.

    Wahamiaji hao waliwaambia polisi walikuwa wakisafiria kuelekea Afrika Kusini baada ya kuvuka mpaka wa Kenya na Ethiopia.

    Wageni hao wako chini ya ulinzi wa polisi wakisubiri kufikishwa mahakamani kwa kuwa nchini kinyume cha sheria.

    Polisi walisema wanawasaka wasafirishaji haramu.

    Kenya hutumiwa sana na wahamiaji wa Ethiopia wanaojaribu kuingia Afrika Kusini.

  9. Wakili wa mshukiwa wa mauaji ya kimbari ya Rwanda ajiondoa kwenye kesi

    Yves Bucyana

    BBC Swahili

    Aimable Karasira

    Wakili Gatera Gashabana, anayemtetea Aimable Karasira, amejitoa katika kesi hiyo Jumatano kwa sababu ambazo hazijawekwa wazi na Mahakama.

    Karasira, msanii na mhadhiri wa zamani katika Chuo Kikuu cha Rwanda, alifika mahakamani huko Nyanza kusini mwa Rwanda akiwa amebeba begi lililokuwa karatasi na vitabu, pengine vya jalada la mashtaka na chupa ya maji yake ya kunywa.

    Karasira anatuhumiwa kwa makosa sita, likiwemo la mauaji ya kimbari, kusababisha machafuko ya umma, na kutobainisha chanzo cha mali yake.

    Amekanusha mashtaka haya yote. Mnamo Aprili , 2023 kesi hii ilianza kusikilizwa Mahakama Kuu, chumba cha uhalifu unaovuka mipaka mjini Nyanza, sasa imefikia hatua ya kujitetea baada ya upande wa mashtaka kumaliza kumshitaki na kuwasilisha ushahidi dhidi yake.

    Leo kabla ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa,wakili wake Gatera Gashabana aliyekuwa mahakamani hapo aliiandikia barua mahakama kuwa anajiondoa katika kesi aliyoanza nayo na kisha akaondoka.

    Baadaye mahakama ilitangaza kwamba Gatera Gashabana alijitoa katika kesi hiyo, lakini haikutangaza sababu, hakimu mara moja alimuuliza Karasira iwapo yuko tayari kusikilizwa au anahitaji wakili.

    Karasira aliiambia Mahakama Kumsaidia kumtafutia wakili kwa sababu “sina namna ya kufanya hivyo mwenyewe gerezani’’. Alisema: "Mali yangu ilitaifishwa hivyo ingekuwa vigumu kwangu, nisaidieni kuzungumza na mawakili wengine ninaoweza kuwapata’’

    Mahakama ilikubali kumwezesha, kesi imeahirishwa hadi mwezi Septemba.

  10. Israel yafungua tena kivuko muhimu cha Kerem Shalom kwa ajili ya misaada Gaza

    Jeshi la Israel lilisema malori ya misaada kutoka Misri tayari yalikuwa yakiwasili kwenye kivuko cha Kerem Shalom.

    Israel inasema inafungua tena kivuko cha Kerem Shalom na kusini mwa Gaza kwa ajili ya kupeleka misaada, siku nne baada ya kufungwa kwa sababu ya kurushwa kwa roketi ya Hamas.

    Malori kutoka Misri yakiwa na chakula, maji na dawa yamefika kwenye kivuko hicho, kwa mujibu wa jeshi la Israel.

    Umoja wa Mataifa ulikuwa umeelezea wasiwasi wake siku ya Jumanne juu ya kile ilichokiita "kukatwa kwa mishipa" miwili ya misaada ya Gaza kwa Israel.

    Hatua hiyo Ilikuja baada ya wanajeshi wa Israel kuchukua udhibiti upande wa Wapalestina wa kivuko cha Rafah na Misri.

    Usiku kucha, kulikuwa na mashambulizi mapya ya anga katika mji wa karibu wa Rafah, ambapo jeshi la Israel linasema lilianza operesheni ndogo siku ya Jumatatu.

  11. Wakimbizi wa Sudan watoroka kambi za Umoja wa Mataifa nchini Ethiopia baada ya mashambulizi

    XX

    Maelfu ya wakimbizi wa Sudan wamekimbia kutoka kambi za Umoja wa Mataifa kaskazini mwa Ethiopia kufuatia kuzuka kwa ghasia.

    Wakimbizi watatu waliambia BBC kwamba idadi ya waliokimbia kambi za Komer na Olala inaweza kuwa 7,000.

    BBC haijathibitisha takwimu hiyo kwa kujitegemea.

    Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi bado halijajibu BBC kuhusu tukio hilo lililoripotiwa.

    Lakini hapo awali ilikuwa imesema inafahamu kuhusu wakimbizi walioondoka kwenye kambi zao kutokana na malalamiko ya ukosefu wa usalama.

    Kambi hizo ziko katika eneo la kaskazini-magharibi la Amhara nchini Ethiopia ambako wanamgambo wa eneo hilo wamekuwa wakipambana na jeshi tangu Agosti mwaka jana. Eneo liko chini ya amri ya dharura na bado halijaunganishwa kwenye mtandao.

    Wakimbizi hao walisema kambi hizo zimeshambuliwa na watu wenye silaha katika wiki za hivi karibuni na wizi wa kutumia silaha na utekaji nyara kwa ajili ya fidia ukizidi kuwa kawaida.

    Wametumia usiku mwingi kando ya barabara kuu na karibu na kituo cha polisi katika mji mdogo wa karibu kwa kukosa ulinzi kutoka kwa mamlaka, mkimbizi mmoja aliambia BBC siku ya Jumatano.

    Wakati wa usiku, milio ya bunduki ilisikika ndani ya kambi kabla ya kuondoka, mkimbizi mmoja alisema. “Kama ningebaki kwenye hema langu, labda wangekuja kunipiga risasi. [Sikuweza] kulala vizuri kwa sababu nilihisi niko hatarini” alisema, na kuongeza "usiku, huwezi kukaa mahali hapo kwa sababu ni hatari sana".

    Tangu kuanza kwa vita kati ya jeshi la Sudan na vikosi pinzani vya Rapid Support Forces (RSF) mwezi uliopita wa Aprili, zaidi ya raia milioni 1.5 wa Sudan wameikimbia nchi hiyo.

    Takriban watu 33,000 wamevuka na kuingia Ethiopia, kulingana na Umoja wa Mataifa.

    "Tunahitaji mtu wa kuja kutusaidia," mkimbizi kutoka kambi ya Komer iliyoko kilomita 70 (maili 43) aliiambia BBC.

    “Tulitoka kwenye tatizo; [na] sasa tunakabiliwa na tatizo lingine.”

  12. Wamalawi walioyatelekeza mashamba Israel warejeshwa kwao

    xx

    Serikali ya Malawi inasema Israel imewarejesha nyumbani wafanyakazi 12 wa Malawi waliokuwa wameajiriwa kufanya kazi katika mashamba maalum nchini humo.

    Katika taarifa, Waziri wa Habari Moses Kunkuyu alisema wafanyikazi hao walikuwa na visa halali ya kufanya kazi katika mashamba maalum lakini "wamekiuka kandarasi yao" kwa kwenda kufanya kazi katika duka la mikate.

    Raia hao 12 wa Malawi walikuwa miongoni mwa wafanyakazi zaidi ya 40 wa kigeni waliokamatwa wakifanya kazi katika kiwanda cha kuoka mikate huko Tel Aviv wiki iliyopita.

    Bw Kunkuyu alisema ni kinyume cha sheria kwa mujibu wa sheria za Israel kwa mfanyakazi wa kigeni kubadilisha kazi bila kufuata taratibu zinazofaa.

    Aliwaonya wafanyakazi wote wahamiaji wa Malawi nchini Israel "kuachana na tabia kama hiyo kwani inaiweka nchi hii katika sifa mbaya".

    "Tabia kama hiyo inaweza pia kupunguza nafasi za ajira za watu husika," alisema. Mamia ya Wamalawi walisafiri hadi Israel mwaka jana ili kuziba pengo la wafanyakazi katika mashamba ya Israel, kwani maelfu ya wafanyakazi walikuwa wameondoka kufuatia kuanza kwa vita na Hamas mwezi Oktoba.

    Ilikuja kama sehemu ya mkataba wa mauzo ya wafanyikazi uliotiwa saini kati ya nchi hizo mbili mnamo 2022.

    Wiki iliyopita, baadhi ya Wamalawi Israel waliambia BBC kwamba mishahara duni ndiyo iliyowafanya baadhi yao kuacha kazi zao kwenye mashamba na kutafuta kazi nyingine nchini humo.

  13. Habari za hivi pundeKenya: Rais Ruto atangaza shule kufunguliwa Jumatatu

    Rais William Ruto ametangaza kuwa shule zitafunguliwa Jumatatu, Mei 13, 2023.

    Ruto ametangaza hayo baada ya kupata ushauri kutoka mamlaka ya utabiri wa hali ya hewa nchini Kenya.

    Wiki iliyopita wakati rais anatoa hotuba yake kwa taifa, alitangaza kuwa shule zimefungwa kwa muda usiojulikana kwasababu ya mvua kubwa inayoendelea kunyesha nchini humo.

    Shule zilitakiwa kufunguliwa Mei 6, baada ya kusongezwa mbele kwa tarehe ya awali ya kufunguliwa, Aprili 29, 2023.

  14. Kila mtu yuko salama baada ya jengo kuporomoka Nairobi

    .
    Image caption: Wakaazi wote 34 wa jengo hilo wameokolewa salama, mamlaka zilisema

    Jengo la orofa tano liliporomoka katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, Jumanne usiku na kusababisha operesheni kubwa ya uokoaji, inayoongozwa na Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya.

    Jengo hilo liliporomoka huko Uthiru - viungani mwa jiji - huku ripoti za awali zikionyesha kuwa makumi ya watu walikuwa wamenasa chini ya vifusi.

    Lakini Jumatano asubuhi Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya lilisema wapangaji wote wa jengo hilo wamehesabiwa.

    Wengine kumi waliokuwa na majeraha madogo walitibiwa katika eneo la tukio, shirika la misaada liliongeza.

    Video kadhaa zilizoshirikiwa mtandaoni zilionyesha jengo la ghorofa likiwa limepinda huku watazamaji wakipaza sauti.

    Bramwel Simiyu, afisa mkuu wa usimamizi wa majanga Nairobi, aliondoa hofu ya wakaazi wanne waliotoweka, akiwemo msichana wa miaka 10, akisema wakaazi wote 34 walikuwa wamepatikana na wako salama, tovuti ya habari ya The Star iliripoti.

    "Jengo lilikuwa likizama polepole, na wakaazi wote waliweza kuruka na kufanikiwa kutoka nje ya jengo hilo," Bw Simiyu alisema.

    Hata hivyo, alisema mbwa wa kijeshi wa kunusa watatumwa ili kubaini ikiwa kuna watu zaidi walionaswa kwenye vifusi.

    Taifa hilo la Afrika Mashariki limekuwa likikumbwa na mvua kubwa ambayo haijawahi kushuhudiwa tangu Machi ambayo imegharimu maisha ya watu 238 na wengine 235,000 kuyahama makazi yao.

    Pia unaweza kusoma:

    Mwanamume aliyenaswa chini ya jengo lililoporomoka Afrika Kusini atuma ujumbe kwa familia - Baba amesema

  15. Kenya: Mafuriko yaongeza hatari ya ugonjwa wa kipindupindu huku WHO ikirekodi maambukizi 44

    .
    Image caption: Mafuriko yameathiri watu wengi kote nchini

    Maambukizi 44 vya kipindupindu vimeripotiwa katika kaunti ya Tana River nchini Kenya, huku mafuriko yakiongeza hatari ya kuenea kwa magonjwa yanayotokana na maji.

    Taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ambayo inataja idadi hiyo, inasema maafisa wa Kenya wanaoshirikiana na WHO na mashirika mengine wamekuwa wakifuatilia hali ya afya na mwitikio kote nchini humo kutokana na mafuriko.

    Mafuriko hayo yameathiri zaidi ya watu robo milioni huku vifo 238 vimeripotiwa kote nchini. Tana River ni mojawapo ya kaunti zilizoathiriwa zaidi na mafuriko.

    Siku ya Jumanne, Katibu Mkuu wa Afya wa Kenya Mary Muthoni alisema kuna hatari kubwa ya magonjwa yanayosambazwa na maji kuwa janga ikiwa hayatashughulikiwa kwa wakati.

    Bi Muthoni alizungumza huku yeye na maafisa wengine wa afya wakisambaza bidhaa za kusafisha maji katika mji mkuu, Nairobi.

    Pia alielezea hatari ya magonjwa kutokana na uchafuzi wa chakula na vyanzo vya chakula visivyo salama ambavyo vinazidishwa na mafuriko.

    WHO inasema itaendelea kuunga mkono hatua za dharura za serikali na "kuwa macho kwa milipuko ya magonjwa ambayo inaweza kuenea kwa urahisi ikiwa haitadhibitiwa haraka".

  16. Tume ya uchaguzi Afrika Kusini yakataa ombi la kumuondoa Zuma kama kiongozi wa chama chake kipya

    .

    Tume ya uchaguzi ya Afrika Kusini imekataa ombi la kumwondoa Rais wa zamani Jacob Zuma kama kiongozi wa chama kipya cha Umkhonto weSizwe (MK).

    Ilikuwa ikijibu barua ya mwanzilishi wa Chama cha MK Jabulani Khumalo, ambaye alitaka tume hiyo imwondoe Bw Zuma kama sura ya chama na kutoka kwenye orodha ya wanaotarajiwa kuwa wabunge.

    Bw Khumalo, ambaye alitimuliwa hivi majuzi katika chama hicho, alisema Bw Zuma anashikilia nafasi hiyo kwa njia ya ulaghai kama kiongozi wa chama kipya.

    Pia alimwandikia Bw Zuma, akimsimamisha kazi kwa tahadhari kwa kile alichosema ni "vitendo kadhaa vya utovu wa nidhamu".

    Lakini katika taarifa ya Jumanne, Tume Huru ya Uchaguzi (IEC) ilisema haiingilii masuala ya ndani ya vyama vya kisiasa na ikathibitisha kwamba Bw Zuma alisalia kuwa kiongozi aliyesajiliwa wa chama cha MK.

    "Tume hufanya kazi tu kwa maagizo ya kiongozi aliyesajiliwa wa chama," shirika la uchaguzi lilisema, na kuongeza kuwa Bw Zuma amesalia kuwa kiongozi wa chama cha MK tangu mwezi uliopita.

    Mzee huyo mwenye umri wa miaka 82 amezuia majaribio ya kumzuia yeye, au chama chake kipya, kushiriki uchaguzi mkuu wa tarehe 29 Mei.

    Siku ya Ijumaa, Mahakama ya Kikatiba itasikiliza rufaa ya IEC kuhusu kupigwa marufuku kwa Bw Zuma kuwania kiti cha ubunge.

    Mnamo Machi, tume ya uchaguzi ilijaribu kumzuia bila mafanikio kwa kudharau hukumu ya mahakama.

    Je, chama cha ANC kitaathiriwa na kujiondoa kwa Jacob Zuma?

  17. Miss USA Noelia Voigt amejiuzulu cheo chake, akitaja sababu za afya ya akili

    .

    Bi Voigt, ambaye alishinda shindano la kila mwaka mnamo Septemba, alisema anaamini katika kufanya maamuzi "ambayo yanahisi bora kwako na afya yako ya akili".

    "Kamwe usihatarishe afya yako ya mwili na kiakili," aliandika kwenye Instagram. "Afya yetu ni utajiri wetu."

    Shirika la Miss USA lilisema linaunga mkono uamuzi wake na litatangaza mrithi wake.

    Mmarekani huyo wa Venezuela mwenye umri wa miaka 24, alisema kwamba anatumai "kuendelea kuwatia moyo wengine" anapoanza "ukurasa mpya" maishani.

    "Tanguliza afya yako ya akili, jitetee mwenyewe na wengine kwa kutumia sauti yako na usiogope kamwe yale yatakayotokea siku za usoni, hata kama unahisi kutokuwa na uhakika," alisema.

    Alitoa shukrani zake kwa miezi tisa kama Miss USA, ambayo alisema ilimpa "jukwaa ... kuleta mabadiliko" na pia kutimiza "ndoto ya maisha" na kukutana na "watu duniani kote."

    Miss USA alimshukuru Bi Voigt na kusema kwenye Instagram kwamba "afya njema ya washikaji taji ni kupaumbele".

    Shirika hilo lilisema linakagua mipango ya "kupitisha majukumu kwa mrithi".

    Savannah Gankiewicz wa Hawaii alishika nafasi ya pili baada ya Bi Voigt katika shindano la mwaka jana.

  18. TikTok inashtaki kuzuia sheria ya Marekani ambayo inaweza kupiga marufuku programu hiyo

    .

    TikTok imefungua kesi inayolenga kuzuia sheria ya Marekani ambayo itapiga marufuku programu hiyo ya video nchini humo labda iuzwe.

    Katika jalada hilo, kampuni hiyo ya mitandao ya kijamii imesema kitendo hicho ni "uingiliaji wa ajabu wa haki za uhuru wa kujieleza" wa kampuni hiyo na watumiaji wake milioni 170 wa Marekani.

    Ilisema Marekani ilikuwa imezua "wasiwasi wa kukisia" tu ili kuhalalisha hatua hiyo na ikaomba mahakama isimamishe.

    Rais Joe Biden alitia saini mswada huo kuwa sheria mwezi uliopita, akitoa sababu za usalama wa taifa.

    Hatua hiyo ilifuatia mjadala wa miaka mingi huko Washington, ambayo imedai kuwa umiliki wa TikTok wa Uchina huongeza hatari kwamba data ya watumiaji raia wa Marekani inaweza kuangukia mikononi mwa serikali ya Uchina au kutumika kwa propaganda.

    Hata hivyo, TikTok imeshikilia kuwa inajitegemea, huku kampuni mama ya ByteDance ikisema haina mpango wa kuuza biashara hiyo.

    Serikali ya Uchina imekosoa sheria hiyo kama "uonevu" wa Marekani kwa kampuni ya kigeni na kuashiria kuwa ingepinga uuzaji.

    Soma zaidi:

    Ni kwanini Marekani ina wasiwasi kuhusu usalama wa TikTok ?

  19. Habari za hivi pundeMarekani yafichua kuwa ilisitisha usafirishaji wa mabomu kwa Israel

    .

    Marekani wiki iliyopita ilisitisha shehena ya mabomu kwa Israel kutokana na wasiwasi kuwa ilikuwa ikiendelea na operesheni kubwa ya ardhini huko Rafah, kusini mwa Gaza, afisa mmojamkuu wa utawala anasema.

    Shehena hiyo ilikuwa na mabomu 1,800 ya 2,000lb (907kg) na mabomu 1,700 500lb, afisa huyo aliiambia CBS News, mshirika wa BBC nchini Marekani.

    Israel "haijashughulikia kikamilifu" wasiwasi wa Marekani juu ya mahitaji ya kibinadamu ya raia huko Rafah, afisa huyo anasema.

    Israel haikutoa maoni yoyote mara moja.

    "Msimamo wa Marekani umekuwa kwamba Israel haipaswi kuanzisha operesheni kubwa ya ardhini huko Rafah, ambako zaidi ya watu milioni moja wamekimbilia usalama waobila mahali pengine pa kwenda," afisa wa utawala wa White House alisema.

    "Tumekuwa tukishiriki katika mazungumzo na Israeli katika muundo wa Kikundi cha Ushauri cha Kimkakati kuhusu jinsi watakavyokidhi mahitaji ya kibinadamu ya raia huko Rafah, na jinsi ya kushughulikia tishio dhidi ya Hamaskwa njia tofaurikuliko walivyofanya mahali pengine huko Gaza.

    "Majadiliano hayo yanaendelea na hayajashughulikia kikamilifu wasiwasi wetu. Wakati viongozi wa Israeli walionekana kukaribia hatua ya uamuzi juu ya operesheni kama hiyo, tulianza kupitia kwa makini mapendekezo ya uhamisho wa silaha fulani kwa Israeli ambazo zinaweza kutumika Rafah. Hii ilianza Aprili.

    "Kutokana na uhakiki huo, tumesitisha shehena moja ya silaha wiki iliyopita. Inajumuisha mabomu 1,800 ya uzito wa pauni 2,000 na mabomu 1,700 ya pauni 500. Tumejikita zaidi katika utumiaji wa mwisho wa mabomu ya uzito wa pauni 2,000 na athari ambayo yanaweza kuleta.’

    Soma zaidi:

    Vita vya Gaza: Israeli hupata wapi silaha zake?

  20. Mwanamume aliyenaswa chini ya jengo lililoporomoka Afrika Kusini atuma ujumbe kwa familia - Baba amesema

    .

    Miongoni mwa wale ambao bado wamenasa chini ya vifusi baada ya jengo la ghorofa tano kuporomoka nchini Afrika Kusini ni Delvin Safels, ambaye alikuwa kwenye moja ya orofa za chini wakati jengo hilo linapoporomoka, babake Dion aliambia BBC.

    Waokoaji wamefuatilia eneo la Delvin lakini wanatatizika kumfikia.

    Kijana huyo mwenye umri wa miaka 29 amekuwa akiwatumia ujumbe wa sauti wazazi wake na mpenzi wake, akiwaambia jinsi anavyowapenda.

    Ana maumivu, na mkono na mguu umefungwa chini, na ni baridi na giza.

    "Ninaamini mwanangu atatoka akiwa hai," baba yake Dion alisema.

    Amekuwa akipiga kambi eneo la tukio karibu tangu Jumatatu, akitumai kwamba mtoto wake angepatikana. Anayumba kati ya kukata tamaa na tumaini.

    "Ni kijana mwenye nguvu, nadhani ataokolewa usiku wa leo au hivi karibuni."

    Zaidi ya siku moja baada ya jengo la ghorofa kuporomoka, waokoaji bado wanasaka watu 41 ambao bado hawajulikani walipo katika mji wa pwani wa kusini wa George.

    Takriban watu 34 hadi sasa wameondolewa kwenye vifusi, saba kati yao wamethibitishwa kufariki.

    Manusura na wapendwa wa watu wengine ambao bado wamenaswa bado wamesalia kwenye eneo la tukio.

    Soma zaidi:

    Watu watano wafariki dunia huku zaidi ya 50 wakinaswa chini ya vifusi baada ya jengo kuporomoka Afrika Kusini