Got a TV Licence?

You need one to watch live TV on any channel or device, and BBC programmes on iPlayer. It’s the law.

Find out more
I don’t have a TV Licence.

Habari za moja kwa moja

Na Asha Juma na Ambia Hirsi

time_stated_uk

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo ya moja kwa moja. Hadi kesho kwaheri,

  2. Hukumu ya 2020 ya ubakaji dhidi ya Harvey Weinstein yabatilishwa

    Harvey Weinstein

    Hukumu ya ubakaji iliyotolewa 2020 dhidi ya mzalishaji filamu nguli wa Hollywood, Harvey Weinstein imebatilishwa na mahakama kuu ya New York, kwa msingi kwamba hakutetendewa haki katika kesi hiyo.

    Mahakama ya Rufaa iligundua kuwa waendesha mashtaka waliruhusiwa kuwaita mashahidi ambao mashtaka yao hayakuwa sehemu ya mashtaka dhidi yake.

    Uamuzi wake ulisema hiyo ilimaanisha kuwa alishtakiwa kwa makosa ya zamani na sio tu kwa uhalifu alioshtakiwa nao sasa.

    Weinstein, 72, atasalia gerezani kwa hukumu tofauti ya ubakaji.

    Mahakama ilifikia uamuzi huo siku ya Alhamisi, ikisema kwamba kesi hiyo "ilikubali kimakosa ushahidi wa bila kushtakiwa, madai ya vitendo vya ngono vya awali dhidi ya watu wengine isipokuwa walalamikaji wa uhalifu wa msingi.

    "Suluhisho la makosa haya makubwa ni shitaka jipya."

    Mmoja wa majaji waliopinga hata hivyo alisema kuwa kutokana na uamuzi huo alisema, "Mahakama hii inaendelea kuzuia mafanikio ambayo waathirika wa unyanyasaji wa kingono wamepigania katika mfumo wetu wa haki ya jinai".

    Mashtaka dhidi ya Weinstein yalianza mwaka wa 2017 na kuibua vuguvugu la #MeToo, ambalo lilifichua unyanyasaji wa kingono katika viwango vya juu zaidi vya tasnia ya filamu ya Hollywood na kwingineko.

    Alikabiliwa na kesi mbili: huko New York, ambapo alifungwa kwa miaka 23 mnamo 2020 kwa kuwabaka wanawake wawili; na huko California, ambapo alihukumiwa kifungo cha miaka 16 kwa kumbaka mwanamke katika hoteli ya Beverly Hills.

  3. 155 wafa, zaidi ya 200 wajeruhiwa kwa mafuriko Tanzania

    Alfred Lasteck

    BBC News, Dar es Salaam

    Mafuriko

    Watu 155 wamepoteza maisha na wengine zaidi ya 230 kujeruhiwa nchini Tanzania kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini humo, amethibitisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo.

    Aidha takribani watu 200,000 na zaidi ya kaya 51,000 zimeathirika huku miundombinu mbalimbali ikiharibika.

    Akitoa taarifa ya mwenendo wa mabadiliko ya hali ya hewa, athari zake na hatua zinazochukuliwa na serikali bungeni leo, Waziri Mkuu amezitaka kamati zinazosimamia maafa kwenye ngazi za wilaya, mkoa na taifa kuchukua hatua za haraka pindi hali ya dharura inapojitokeza ili kupunguza athari.

    Majaliwa alieleza kuwa zaidi ya nyumba 10,000 sambamba barabara na reli nazo zimeathirika.

    Alisema hali ya joto duniani imesababisha mvua ya El Nino ambayo imeleta mvua kubwa katika maeneo mengi nchini.

    ''Hapa nchini, mwezi Oktoba hadi Desemba, mwaka jana kulikuwa na ongezeko kubwa la mvua ambapo jumla ya mililita 534.5 zilipimwa ikilinganishwa na mililita 227.2 kwa mwaka 2022 ikiwa ni ongezeko la asilimia 135. Vilevile, ongezeko hilo la mvua kubwa limeshuhudiwa katika kipindi cha mwezi Januari hadi Aprili 2024 na utabiri wa hali ya hewa unaonesha kuwa mvua za masika zitaendelea hadi mwezi Mei, 2024,” alisema Majaliwa huku akisema mvua za Januari mpaka Aprili zimekuwa na madhara.

    Mafuriko

    Aliitaja baadhi ya mikoa iliyoathirika zaidi kuwa ni pamoja na Pwani, Morogoro, Dar es Salaam, Kilimanjaro, Mbeya na Kigoma.

    Mikoa mingine iliyopatwa na madhara ni; Arusha, Mtwara, Lindi, Shinyanga, Kagera, Songwe, Rukwa, Manyara, Geita, Iringa na Dodoma.

    Hata hivyo, ametoa pole kwa waathiriwa na ameshauri wananchi kuchukua tahadhari wanapopita kwenye barabara na sehemu zilizo na maji.

    Wananchi wa maeneo mbalimbali wameiambia BBC kuwa , serikali inapaswa kusaidia familia zilizoathirika kwa chakula, vifaa tib ana malazi katika kipindi hichi.

    Mkazi mmoja wa wilaya ya Siha, kaskazini mwa Tanzania amesema, "Sijawahi kuona aina hii ya mvua kabla iliyoleta majanga. Miaka ya nyuma tulikuwa na El Nino lakini haikuharibu nyumba zetu kama ilivyo sasa…

    “ …leo sina kitu, Nyumba imeharibika, mali nazo zimeenda, mimea imeharibika lakini naona ni athari za mabadiliko ya tabia nchi lakini pia ukiangalia tumeharibu mazingira na tumekata miti mingi hivyo madhara lazima yatukute,” alisema mkazi huyo.

  4. Crystal Palace imeweka bei ya pauni milioni 60 kwa Olise na Eze

    k
    Image caption: Michael Olise, kushoto, na Eberechi Eze

    Crystal Palace watakubali ofa kwa washambuliaji nyota Eberechi Eze na Michael Olise ambazo zinaanzia pauni milioni 60 au zaidi kwa kila mchezaji.

    The Eagles wako salama kutoshuka daraja wakiwa kwenye ligi kuu ya Uingereza kwa msimu wa 12, na wanasema kuwa kifedha hawana haja ya kumuuza mchezaji yeyote.

    Lakini kwa kuzingatia sifa nyingine za Eze mwenye umri wa miaka 25 - hasa katika wiki za hivi karibuni na Olise, 22, wanakubali kwamba zipo timu zitataka kuwanunua katika msimu huu wa joto.

    Na Palace wanahisi kwamba pauni milioni 60 kwa kila mchezaji ndio bei ya kuanzia kwa timu zinazovutiwa ikiwa wanataka kuingia kwenye mazungumzo.

    Wote Olise na Eze walitia saini mikataba ya muda mrefu msimu huu na Palace wako katika nafasi nzuri ya mazungumzo.

    Msimu uliopita Eze alitakiwa na Manchester City lakini mabingwa hao walimsajili Matheus Nunes wa Wolves badala yake, huku Chelsea walijaribu bila mafanikio kumsajili Olise bila mafanikio kwa ada ya pauni milioni 35.

  5. Namibia yakasirishwa na watalii waliopiga picha za utupu katika mlima wa mchanga jangwani

    XX

    Mamlaka nchini Namibia zimeshutumu watalii waliopiga picha uchi katika moja ya vivutio vya juu nchini humo - eneo la ‘Big Daddy dune’ katika jangwa la Namibia.

    Baadhi ya wageni waliliambia gazeti moja la eneo hilo kuwa walishangazwa na tabia hiyo na kutaka watalii hao kuchukuliwa hatua.

    Watalii hao ambao hawakutajwa majina wanaweza kuwekwa kwenye orodha ya wanaofungiwa kuingia katika hifadhi zozote za Namibia, msemaji wa wizara ya utalii aliviambia vyombo vya habari vya ndani.

    Picha na video za watalii hao zilisambazwa kuzua hisia kali.

    Kenneth Nependa, makamu mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Utalii vya Namibia, aliiambia tovuti ya habari ya Namibian Sun kwamba tabia hiyo inahatarisha kuvutia watalii "Inachukiza sana na kwa kweli [inaleta] taswira mbaya kwa Namibia,"

    Bw Nependa alisema, akiongeza kuwa eneo la milima wa Big Daddy sio tu mahali pa kupumzika kwa watalii bali kwa familia pia.

    Haijabainika ni nani alichukua picha hizo na video ya watalii hao watatu wa kiume, wanaoonekana wakiwa uchi kabisa kwenye kichanga, karibu na nguo zao.

    Mamlaka haikujibu mara moja maswali ya BBC kuhusu utambulisho wa watalii hao.

  6. Wafungwa watoroka baada ya mvua kuharibu gereza la Nigeria

    Gereza la Suleja

    Zaidi ya wafungwa 100 wametoroka jela karibu na mji mkuu wa Nigeria baada ya mvua kubwa kuharibu sehemu waliyokuwa wakihifadhiwa.

    Kwa mujibu wa mamlaka, wafungwa 118 awali walikimbia Gereza la Suleja lakini 10 wamekamatwa.

    Msako umeanzishwa ili kuwatafuta wengine. Utambulisho wa wafungwa hao haujabainika kufikia sasa lakini kuna hofu kuwa baadhi yao wanaweza kuwa hatari.

    Hata hivyo taarifa kutoka katika gereza hilo ilisema wanafanya kazi na vyombo vingine vya usalama na kwamba watu wanapaswa kuendelea na shughuli zao za kawaida bila hofu yoyote.

    "Kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama [sisi] kufikia sasa tumefanikiwa wakamata wafungwa 10 waliokuwa wakitoroka na kuwaweka chini ya ulinzi, huku tukiendeleza msako mkali wa kuwakamata wengine," ilisema taarifa kutoka kwa mamlaka ya magereza ya Abuja.

    Iliongeza kuwa vituo vingi vya magereza huko Suleja, kilomita 50 kutoka Abuja vilijengwa wakati wa ukoloni na hivyo vimezeeka na ni dhaifu.

  7. Macron: "Vita vya Ukraine ni tishio kwa usalama wa Ulaya"

    Macron

    Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameainisha maono yake ya siku zijazo kwa Ulaya yenye nguvu na inayoweza kukabiliana na changamoto za kimataifa kama vile vita vya Urusi nchini Ukraine.

    Sharti la lazima kwa usalama wetu ni kwamba Urusi haitashinda vita vikali inazopiga dhidi ya Ukraine," Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema..

    Katika hotuba yake kuu, Macron alionya juu ya hatari inayokodolea macho Ulaya katika muongo ujao.

    "Ulaya inakabiliwa na tishio na inaweza kufa, na inatutegemea sisi tu," Macron alisema, akionya kwamba Ulaya haijajiandaa vyema kwa changamoto mpya katika ulimwengu ambapo "sheria za mchezo zimebadilika."

    Aliitaja mzozo wa Ukraine kuwa "tishio kuu kwa usalama wa Ulaya" na kutoa wito wa kuimarisha uwezo wa ulinzi wa Ulaya.

    "Tunahitaji kujiimarisha kimkakati kwa ulinzi wa kuaminika wa Ulaya," Macron alisema, akiongeza kuwa Ulaya haiwezi kuwa "kibaraka" wa Marekani.

    Hii si mara ya kwanza kwa Macron kusema kwamba Ulaya haiwezi tena kutegemea Marekani kwa ulinzi, na kwamba jeshi la kweli la Ulaya linahitajika kuwalinda watu wake.

    Maelezo zaidi:

    Urusi lazima ishindwe lakini ‘isisambaratishwe’ asema Macron

    Kwa nini onyo la Putin linachukuliwa kuwa hatari baada ya kauli ya Macron?

  8. 93 wakamatwa Marekani huku maandamano ya kupinga vita vya Gaza yakipamba moto

    Waandamanaji wanaounga mkono Palestina walitiwa mbaroni kwa makosa ya kuingia katika Chuo Kikuu cha Kusini mwa California
    Image caption: Waandamanaji wanaounga mkono Palestina walitiwa mbaroni kwa makosa ya kuingia katika Chuo Kikuu cha Kusini mwa California

    Polisi wamewakamata watu 93 katika Chuo Kikuu cha Kusini mwa California (USC) huko Los Angeles kwa mashtaka ya kuingia bila idhini, huku maandamano ya kupinga vita huko Gaza yakizidi katika vyuo vya Marekani.

    Maafisa wa polisi wakiwa na vifaa vya kutuliza ghasia walisafisha kambi inayounga mkono Palestina katikati mwa chuo hicho, na kuwazuia waandamanaji kukusanyika.

    Hatua ya kukamatwa kwa kumekuja saa chache baada ya makabiliano kati ya waandamanaji na polisi katika Chuo Kikuu cha Texas. Makumi walikamatwa huko pia.

    Vyuo vikuu kote Marekani vimeshuhudia idadi ongezeko la ghasia za wanafunzi au wengine wakijaribu kukusanyika kupinga operesheni ya kijeshi ya Israel huko Gaza.

    Mamia ya waandamanaji sasa wamekamatwa kwenye vyuo kadhaa kote Marekani zikiwemo Columbia, Yale na Chuo Kikuu cha New York.

    Vita vya Gaza vilianza baada ya watu wenye silaha wakiongozwa na Hamas kufanya shambulio ambalo halijawahi kushuhudiwa kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba, na kuua takriban watu 1,200 - wengi wao wakiwa raia - na kuwashikilia wengine 253 mjini Gaza kama mateka.

    Zaidi ya watu 34,305 - wengi wao watoto na wanawake - wameuawa huko Gaza tangu wakati huo, wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas inasema.

    Soma:

  9. Rappa wa Iran amehukumiwa kifo, asema wakili

    Rappa wa Iran

    Rappa wa Iran aliyefungwa kwa kuunga mkono maandamano dhidi ya serikali amehukumiwa kifo, wakili wake amesema.

    Toomaj Salehi katika nyimbo zake aliunga mkono maandamano ya mwaka 2022 yaliyozuka kulalamikia kifo cha Mahsa Amini, mwanamke aliyefariki akiwa mikononi mwa polisi baada ya kudaiwa kuvaa hijabu "visivyo".

    Mmoja wa mawakili wa Bw Salehi, Amir Raesian, alisema rappa huyo atakata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.

    Mamlaka za Iran hazijatoa tamko lolote.

    Bw Salehi alikamatwa kwa mara ya kwanza Oktoba 2022 baada ya kutoa taarifa hadharani kuunga mkono maandamano na alishtakiwa kwa makosa mengi.

    Alihukumiwa Julai 2023 kifungo cha miaka sita na miezi mitatu jela baada ya kukwepa hukumu ya kifo kutokana na uamuzi wa Mahakama ya Juu Zaidi.

    Lakini mnamo Januari, Mahakama ya Mapinduzi ya Isfahan ilimshtaki Bw Salehi kwa mashtaka mapya ikiwemo yale ambayo awali ameachiliwa huru, wakili wake alisema.

    Akiongea na gazeti la Sharq siku ya Jumatano, Bw Raesian alisema mahakama ya mapinduzi ilipuuza uamuzi wa Mahakama ya Juu Zaidi wa kusamehe na badala yake ikatoa mashtaka mapya kabla ya kutoa "adhabu kali zaidi".

    Mashtaka ambayo alipatikana na hatia ni pamoja na rushwa duniani kwa mashtaka kadhaa, "Baghi" [uasi wa kutumia silaha], mkusanyiko na kula njama, propaganda dhidi ya taasisi tawala na kuchochea ghasia.

    Bw Salehi ana siku 20 za kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

    Pia unaweza kusoma:

    Ni nchi ngapi ambazo bado zina hukumu ya kifo, na ni watu wangapi wameuawa?

    Zifahamu haki walizonazo wanaohukumiwa kifo duniani

  10. Liverpool: Van Dijk anahoji hamu ya wachezaji wenzake kushinda taji la EPL

    Virgil van Dijk
    Image caption: Virgil van Dijk aliteuliwa nahodha wa Liverpool baada ya Jordan Henderson kuondoka majira ya joto

    Nahodha wa Liverpool Virgil van Dijk ametilia shaka nia ya timu yake kushinda Ligi ya Kuu ya England baada ya kushindwa vibaya katika mechi yao dhidi ya klabu ya Everton.

    Huku zikiwa zimesalia mechi nne, Liverpool sasa wanatarajia kuwa nyuma ya vinara Arsenal, ambao wako mbele kwa pointi tatu, na mabingwa Manchester City.

    Kichapo katika uwanja wa Goodison Park kilikuwa cha pili katika mechi tatu huku msimu wao ukitishia kutoweka.

    "Je, kweli wanataka kushinda ligi?" aliuliza Van Dijk.

    Mabao katika kila kipindi kutoka kwa mlinzi Jarrad Branthwaite na mshambuliaji Dominic Calvert-Lewin yaliwaweka Toffees kwenye njia ya kupata ushindi wao wa kwanza nyumbani kwenye ligi dhidi ya Liverpool tangu Oktoba 2010.

    Ilikuwa ni kipigo kingine baada ya kufungwa 1-0 nyumbani na Crystal Palace siku 10 zilizopita huku wakikosa nafasi ya kurejea kwa pointi na The Gunners

    Van Dijk mkali aliiambia Sky Sports: "Ikiwa utacheza hivi kwa ujumla kwenye mchezo na usishinde changamoto yoyote na kumpa mwamuzi nafasi ya kupiga mpira wa adhabu ugenini basi hatuna nafasi ya kutwaa ubingwa.

  11. Jeshi la Burkina Faso liliwaua wanakijiji 223 katika shambulio la kulipiza kisasi - HRW

    .

    Zaidi ya raia 220, wakiwemo watoto wasiopungua 56, waliuawa kinyama na jeshi la Burkina Faso katika siku moja mwaka huu, Shirika la Human Rights Watch linasema.

    Katika mashambulizi ya Februari 25, jeshi liliua watu 179 katika kijiji cha Soro na wengine 44 katika kijiji cha karibu cha Nondin, uchunguzi wa HRW ulipatikana.

    HRW ilitaja mauaji ya umati "miongoni mwa matukio mabaya zaidi ya unyanyasaji wa jeshi" nchini humo katika karibu muongo mmoja.

    Mamlaka ya nchi hiyo haijatoa maoni yoyote kuhusu ripoti hiyo .

    Mwezi uliopita, mwendesha mashtaka wa umma Aly Benjamin Coulibaly aliomba mashahidi kubaini kundi lililohusika na mauaji hayo ya halaiki. Alitaja idadi ya vifo vya awali kuwa 170 .

    Wanakijiji walionusurika kwenye shambulio hilo waliiambia HRW kwamba msafara wa kijeshi ukiwa na zaidi ya wanajeshi 100 ulishuka katika kijiji cha Nondin, takriban dakika 30 baada ya wapiganaji wa Kiislamu kupita karibu.

    Wanajeshi hao walikwenda nyumba kwa nyumba, wakiwafukuza wakazi kutoka kwenye nyumba zao.

  12. 'Kuwa imara,' wazazi wamwambia kijana wao aliyeshikwa mateka Gaza baada ya video kusambazwa

    .

    Wazazi wa mateka Muisraeli mwenye asili ya Marekani huko Gaza wamemtaka "kuwa imara" baada ya Hamas kutoa video ya uthibitisho kwamba yuko hai.

    Hersh Goldberg-Polin, 23, anaonekana bila mkono wake wa kushoto kwenye klipu fupi uliokatwa wakati wa shambulio la Hamas la tarehe 7 Oktoba kusini mwa Israel.

    Picha hizo hazina tarehe, lakini anasema ameshikiliwa kwa takriban siku 200.

    Wakijibu, mama na baba yake waliomba zaidi kufanywa ili kupata mpango mpya wa kuachiliwa huru kwa mateka.

    Waliitaka Israel, Hamas na wapatanishi Marekani, Misri na Qatar "kufanya makubaliano" ya kutuunganisha "sote na wapendwa wetu na kumaliza mateso katika eneo hili".

    Akizungumza kwa kulazimishwa kwenye video iliyotumwa kwenye akaunti ya Hamas ya Telegram siku ya Jumatano, Bw Goldberg-Polin alisema anahitaji usaidizi wa kimatibabu na alikosoa jitihada za serikali ya Israel kujadili kurejea kwa mateka hao.

    Wiki kadhaa za mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja yameshindwa kuleta makubaliano, huku Hamas ikikataa pendekezo la hivi punde la kusitisha mapigano kwa wiki sita ili kuachiliwa huru kwa mateka 40 kati ya 133 waliosalia. Takriban mateka 30 wanakisiwa kuwa wamefariki.

    Israel inaonekana kusonga mbele na mipango ya mashambulizi huko Rafah, kusini mwa Gaza, licha ya onyo la uwezekano wa madhara ya kibinadamu kwa Wapalestina milioni 1.5 wanaojihifadhi huko.

    Pia unaweza lusoma:

    Kuwatafuta wapendwa waliopotea katika makaburi ya halaiki ya Gaza

  13. Urusi yapiga kura ya turufu ya Umoja wa Mataifa kusimamisha mashindano ya silaha katika anga za mbali

    .

    Urusi imepinga azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalozitaka nchi zote kuzuia mashindano ya silaha katika anga za juu.

    Rasimu ya azimio hilo, lililotolewa na Marekani na Japan, lilitaka kuthibitisha kanuni ambayo tayari imetolewa katika Mkataba wa Anga za Juu wa 1967.

    Marekani imeonya kwamba inaaminika kuwa Urusi inatengeneza silaha za nyuklia za anga za juu na ya kupambana na satelaiti.

    Urusi ilisema "imejitolea kwa dhati" kwa mkataba uliopo.

    Rasimu hiyo, iliyotolewa Jumatano, ilitoa wito kwa "Nchi zote, hasa zile zenye uwezo mkubwa wa anga, kuchangia kikamilifu katika lengo la matumizi ya amani ya anga za juu na kuzuia mashindano ya silaha katika anga za mbali."

    Pia ilitoa wito kwa nchi kuunga mkono Mkataba wa Anga za Mbali, ambapo pande zote zilikubaliana "kutoweka katika mzunguko wa Dunia vitu vyovyote vinavyobeba silaha za nyuklia au aina yoyote ya silaha za maangamizi makubwa".

    Kati ya wajumbe 15 wa baraza hilo, 13 walipiga kura ya kuunga mkono, huku Urusi - moja ya wanachama watano wa kudumu walio na kura ya turufu - ilipiga kura ya kuipinga na China ilijizuia.

    Urusi imepinga azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalozitaka nchi zote kuzuia mashindano ya silaha katika anga za juu.

    Rasimu ya azimio hilo, lililotolewa na Marekani na Japan, lilitaka kuthibitisha kanuni ambayo tayari imetolewa katika Mkataba wa Anga za Juu wa 1967.

    Marekani imeonya kwamba inaaminika kuwa Urusi inatengeneza silaha za nyuklia za anga za juu na ya kupambana na satelaiti.

    Urusi ilisema "imejitolea kwa dhati" kwa mkataba uliopo.

    Rasimu hiyo, iliyotolewa Jumatano, ilitoa wito kwa "Nchi zote, hasa zile zenye uwezo mkubwa wa anga, kuchangia kikamilifu katika lengo la matumizi ya amani ya anga za juu na kuzuia mashindano ya silaha katika anga za mbali."

    Pia ilitoa wito kwa nchi kuunga mkono Mkataba wa Anga za Mbali, ambapo pande zote zilikubaliana "kutoweka katika mzunguko wa Dunia vitu vyovyote vinavyobeba silaha za nyuklia au aina yoyote ya silaha za maangamizi makubwa".

    Kati ya wajumbe 15 wa baraza hilo, 13 walipiga kura ya kuunga mkono, huku Urusi - moja ya wanachama watano wa kudumu walio na kura ya turufu - ilipiga kura ya kuipinga na China ilijizuia.

  14. Xavi kusalia kama kocha wa Barcelona hadi Juni 2025

    .

    Kocha wa Barcelona Xavi atasalia katika klabu hiyo hadi mwisho wa mkataba wake mnamo Juni 2025 baada ya kubadilisha mawazo kwamba huu ungekuwa msimu wake wa mwisho.

    Kocha huyo mwenye umri wa miaka 44 alitangaza Januari kwamba atajiuzulu kama bosi msimu huu wa joto.

    Lakini, huku rais Joan Laporta akitamani abaki, kiungo huyo wa zamani wa Barcelona na Uhispania amebatilisha uamuzi wake.

    Xavi alichukua nafasi hiyo Novemba 2021 baada ya kuachana na klabu ya Al Sadd ya Qatar na kuiongoza Barca kutwaa ubingwa wa Uhispania katika msimu wake wa kwanza kamili wa kuinoa klabu mnamo 2022-23.

    Hata hivyo, wako pointi 11 nyuma ya vinara wa La Liga Real Madrid zikiwa zimesalia mechi sita kuchezwa katika msimu unaoendelea.

    Barcelona iliondoka kwenye Ligi ya Mabingwa wiki iliyopita kufuatia kushindwa katika robo fainali na Paris St-Germain.

    Xavi, ambaye alishinda tuzo 25 wakati wa uchezaji bora katika klabu ya Barcelona, ​​alisema anahisi "amefunguliwa" kufuatia tangazo kwamba atajiuzulu nafasi hiyo mwishoni mwa msimu.

    Alipotangaza kuwa anaondoka baada ya kushindwa na Villarreal, alihisi kwamba halindwi na klabu hiyo na hakukuwa na mwelekeo wazi.

    Lakini tangu wakati huo, Xavi alipohisi anaweza kuchukua mbinu ya utulivu zaidi, matokeo ya timu yaliboreka.

    Walicheza mechi 10 bila kufungwa kwenye ligi kabla ya kufungwa 3-2 na Real Madrid Jumapili.

    Pia unaweza kusoma:

    Tetesi za Soka Ulaya Alhamisi 25.04.2024

  15. Uingereza yaongoza kwa matumizi ya pombe miongoni mwa watoto - WHO

    .

    Theluthi moja ya watoto wenye umri wa miaka 11 na zaidi ya nusu ya watoto wa umri wa miaka 13 nchini Uingereza wamekunywa pombe - na kuifanya nchi hiyo kuongoza kati ya nchi 44 zilizochunguzwa katika ripoti ya wataalam wa afya duniani.

    Wasichana waligunduliwa kuwa na uwezekano zaidi kuliko wavulana kunywa na kulewa wakiwa na umri wa miaka 15 huko Uingereza, Wales na Scotland.

    Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ilisema unywaji wa pombe, ambayo inaweza kuharibu ubongo wa watoto, kumefanywa kuwa jambo la kawaida.

    Ilitoa wito kwa nchi kuanzisha hatua zaidi za kuwalinda watoto.

    Ripoti hiyo iliangalia data kutoka kwa watoto wa umri wa kwenda shule wapatao 4,500 kutoka kila nchi barani Ulaya, Asia ya Kati na Canada mnamo 2021-22 kuhusu uvutaji sigara, bangi na unywaji pombe kati ya vijana.

    Soma zaidi:

    Waridi wa BBC : “Uraibu wa Pombe karibu unitoe uhai wangu"

  16. Mahakama ya Juu ya Marekani kuamua iwapo Trump ana kinga katika kesi ya kubatilisha matokeo ya uchaguzi

    .

    Kesi ya kihistoria, ambayo inaweza kuathiri hatima ya kisheria na kisiasa ya Donald Trump na kufafanua wigo wa mamlaka ya urais, itafikishwa mbele ya majaji tisa wa Mahakama ya Juu ya Marekani siku ya Alhamisi.

    Mawakili wa Bw Trump na Wakili Maalum Jack Smith watajibu hoja zao katika kesi ya iwapo marais wa zamani hawana kinga ya kushtakiwa kwa makosa ya jinai kwa hatua wanazochukua wakiwa madarakani.

    Bw Smith alimshtaki rais huyo wa zamani mwaka jana kwa madai ya kujaribu kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa 2020. Lakini Bw Trump alisema hawezi kushtakiwa kwa mujibu wa Katiba ya Marekani.

    Kesi hiyo imesitishwa huku mzozo huo ukielekea katika mahakama kuu nchini humo.

    Kesi hiyo tayari ni ya kihistoria: Bw Trump ndiye rais wa kwanza wa zamani kushtakiwa kwa uhalifu wa serikali kuu.

    Na uamuzi wa Mahakama ya Juu, ambao hautatolewa hadi Juni, utakuwa pia muhimu.

    Ikiwa mahakama itaamua Bw Trump anaweza kufunguliwa mashtaka, basi kesi hiyo itasonga mbele, lakini huenda itaanza tena mwishoni mwa majira ya kiangazi mapema zaidi, katikati mwa msimu wa uchaguzi wa urais. Iwapo itaamua kuwa ana kinga, Bw Trump anaweza kushuhudia kesi nyingine za uhalifu dhidi yake zikitupiliwa mbali.

    Bw Smith aliishinikiza mahakama kufanya uamuzi mnamo Desemba, lakini ilikataa.

    "Richard Nixon alisema kuwa watu wa Marekani wanastahili kujua iwapo rais wao ni mhalifu," alisema Kermit Roosevelt, profesa wa sheria katika Chuo Kikuu cha Pennsylvania. "Mahakama ya Juu haionekani kukubaliana na hilo. Wako sawa kwa kuzuia hili kuamuliwa kabla ya uchaguzi."

    Soma zaidi:

    Kwa nini Trump ni maarufu miongoni mwa Republican?

  17. Marekani: Bunge la Arizona lapiga kura kufuta marufuku ya uavyaji mimba ya mwaka 1864

    ,

    Bunge la Arizona limepiga kura kufuta sheria iliyodumu kwa miaka 160 inayopiga marufuku uavyaji mimba, ushindi mkubwa kwa juhudi zinazoongozwa na chama cha Democrat kuondoa sheria hiyo.

    Warepublican walikuwa wamezuia majaribio mawili ya awali ya kupiga kura kukomesha sheria hiyo, ambayo inapiga marufuku utoaji mimba kuanzia kutungwa kwake hata kama ni kutokana na ubakaji au uhusiano wa karibu.

    Wanachama watatu wa chama hicho, walionyesha wazi kutokubaliana na hilo siku ya Jumatano na kupiga kura ya kufutwa kwake.

    Mswada huo sasa unaelekea kwa bunge la seneti, ambapo kuna uwezekano mkubwa wa kupitishwa.

    Mapema mwezi huu, mahakama kuu ya jimbo hilo ilifufua sheria ya 1864, na kuibua gumzo kote nchini humo, ambapo wapiga kura wanaunga mkono kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma za utoaji mimba.

    Wiki iliyopita, maseneta wawili wa chama cha Republican walipiga kura kuendeleza mswada kama huo. Hilo linaonyesha kuwa kuna uungwaji mkono wa kutosha wa Republican katika bunge la seneti ili kupitisha mswada huo.

    Gavana wa jimbo la Arizona Katie Hobbs, wa chama cha Democrat, amedokeza kuwa atatia saini mswada huo iwapo utafika kwenye meza yake.

    Soma zaidi:

    Mwanamke anayetaka kukomesha utoaji mimba nchini Marekani

  18. Wito waongezeka wa kufanyika kwa uchunguzi huru wa makaburi ya halaiki Gaza

    .

    Umoja wa Ulaya umeunga mkono wito wa Umoja wa Mataifa wa kufanyika kwa uchunguzi huru kuhusu ugunduzi ulioripotiwa wa makaburi ya halaiki katika hospitali mbili za Gaza zilizoharibiwa wakati wa operesheni ya Israel.

    "Hili ni jambo ambalo linatulazimisha kutoa wito wa uchunguzi huru wa tuhuma zote na mazingira yote, kwa sababu kwa hakika inajenga hisia kwamba kunaweza kuwa na ukiukwaji wa haki za binadamu za kimataifa," msemaji wa EU Peter Stano alisema.

    "Ndiyo maana ni muhimu kuwa na uchunguzi huru na kuhakikisha uwajibikaji."

    Ofisi ya Umoja wa Mataifa ilisema Jumanne wachunguzi wa kimataifa wanapaswa kushirikishwa katika uchunguzi wa kupatikana kwa miili hiyo na kuongeza kuwa "imetamaushwa" na uharibifu wa hospitali mbili kubwa za Gaza, Al-Shifa katika mji wa Gaza na Nasser Medical Complex huko Khan Yunis.

    Shirika la Ulinzi wa Raia la Gaza lilisema Jumanne kwamba wafanyikazi wa afya waligundua karibu miili 340 ya watu wanaodaiwa kuuawa na kuzikwa na vikosi vya Israel kwenye uwanja wa Nasser.

    Jeshi la Israel lilitaja madai kwamba wanajeshi wake walizika miili wakati wa operesheni yake huko Nasser "isiyo na msingi".

    Soma zaidi:

    Umoja wa Mataifa 'watamaushwa' na ripoti za kaburi la halaiki katika hospitali za Gaza

  19. Hujambo na karibu katika matangao yetu ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 25/04/2024