Got a TV Licence?

You need one to watch live TV on any channel or device, and BBC programmes on iPlayer. It’s the law.

Find out more
I don’t have a TV Licence.

Habari za moja kwa moja

Na Abdalla Seif Dzungu na Asha Juma

time_stated_uk

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu ya moja kwa moja kwa leo. Kwaheri!

  2. Kimbunga Hidaya huenda kikakumba eneo la Pwani ya Kenya, Serikali yaonya

    .

    Serikali sasa inaonya kuwa huenda kimbunga Hidaya kikakumba eneo la Pwani hivi karibuni kutokana na mvua kubwa inayoshuhudiwa kwa sasa kote nchini.

    Onyo hilo lilitolewa baada ya kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Alhamisi kujadili hatua za ziada za kukabiliana na athari mbaya zinazoendelea za mafuriko, maporomoko ya udongo na maporomoko ya ardhi.

    Baraza la Mawaziri lilielezwa kuhusu utabiri wa hali ya hewa kwa muda wa miezi mitatu ijayo, ambao ulionyesha kuwa mvua za wastani hadi juu ya wastani zitaendelea kunyesha katika maeneo yote ya nchi.

  3. TikTok na Universal kutatua mzozo wa mirahaba ya muziki

    .

    TikTok itarejesha mamilioni ya nyimbo kwenye jukwaa baada ya kusuluhisha mzozo na Universal Music Group kuhusu mirahaba.

    Inamaanisha kuwa watumiaji wataweza tena kutengeneza video zinazojumuisha nyimbo kutoka kwa wasanii wakiwemo Billie Eilish na Ariana Grande.

    Mzozo wa kiasi gani TikTok ilikuwa inalipa ulishuhudia kampuni hizo mbili zikishutumiana kibiashara - na Universal ikawaondoa baadhi ya waimbaji maarufu duniani.

    Lakini mpasuko huo sasa unaonekana kuponywa baada ya makampuni hayo kutangaza "malipo yaliyoboreshwa" kwa wasanii, ingawa hawajafichua ni kiasi gani cha pesa.

    Kampuni hizo zilisema "zinafanya kazi haraka" kurudisha muziki wa Universal kwa TikTok, mchakato unaofahamika kuwa utachukua chini ya wiki mbili.

    Hii itajumuisha kurejesha sauti kwa video ambazo awali zilinyamazishwa wakati wa mzozo.

    Taylor Swift, labda msanii mkubwa wa lebo hiyo, tayari alikuwa amekubali kurudisha muziki wake kwa TikTok - makubaliano ambayo angeweza kufanya kwa kuwa anamiliki hakimiliki ya nyimbo zake.

  4. Iran yawashtaki waandishi wa habari baada ya ripoti ya BBC kuhusu kifo cha kijana aliyekuwa akiandamana

    .

    Mahakama ya Iran imefungua mashtaka dhidi ya "waandishi kadhaa wa habari na wanaharakati" baada ya kuchapishwa kwa ripoti ya BBC inayodai wanaume wanaofanya kazi katika vikosi vya usalama walimnyanyasa kingono na kumuua mwandamanaji mwenye umri wa miaka 16.

    Shirika la habari la Mizan linalosimamiwa na mahakama lilielezea uchunguzi wa BBC Eye kuhusu kifo cha Nika Shakarami mnamo 2022 kama "feki, si sahihi na umejaa makosa".

    Haikubainisha watu walioitwa kwa madai ya "kuvuruga usalama wa jamii".

    Lakini wanahabari wawili wa Iran ambao walikuwa wametoa maoni yao kuhusu ripoti hiyo mtandaoni walisema waendesha mashtaka wamefungua kesi dhidi yao.

    Mmoja wao, Mohammad Parsi, aliandika kwenye mtandao wa X, kwamba Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Tehran ilimwita kwa kuchapisha "makala kuhusu Nika Shakarami na maelezo ya mauaji yake".

    Wa pili, Marzieh Mahmoodi, aliweka ujumbe kuwa "hakuna mashtaka wala maelezo yanayojulikana".

    Siku ya Jumatano, Waziri wa Mambo ya Ndani Ahmad Vahidi alipuuzilia mbali matokeo ya uchunguzi wa BBC akisema ni njama ya maadui wa Iran, na kuwa afisa wa kwanza kutoa maoni yake hadharani.

    "Maadui na vyombo vyao vya habari wametumia ripoti za uongo na zisizo za kweli kutatiza watu kisaikolojia," aliwaambia waandishi wa habari nje ya mkutano wa baraza la mawaziri, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali.

    Bw Vahidi alidai ni "jaribio la kugeuza tahadhari" kutoka kwa maandamano ya sasa ya Wapalestina nchini Marekani pamoja na shambulio la kombora la Iran na ndege zisizo na rubani dhidi ya Israel mwezi uliopita.

    Hakukuwa na maoni ya mara moja kutoka BBC News juu ya taarifa za Bw Vahidi na mahakama.

    Soma zaidi:

    Nyaraka za siri zabainisha vitendo vya vikosi vya usalama vya Iran kuwanyanyasa na kuwaua vijana waandamanaji

  5. Urusi yalaumiwa kwa kuingilia GPS na kuathiri safari za ndege Ulaya

    .

    Urusi inasababisha usumbufu kwa mifumo ya urambazaji ya satelaiti inayoathiri maelfu ya safari za ndege za raia, wataalam wanasema.

    Bahari ya Baltic, Bahari Nyeusi na Mediterania ya mashariki - maeneo ambayo jeshi la Urusi limekuwa likifanya kazi zaidi - yameshuhudia kuongezeka kwa usumbufu wa mifumo ya urambazaji ya Global Positioning System (GPS).

    Hii imesababisha ndege kushindwa kupokea mawimbi ya GPS.

    Mnamo Machi, ndege ya RAF iliyokuwa imembeba Waziri wa Ulinzi Grant Shapps ishara yake ya GPS ilikwama ilipokuwa ikipaa karibu na eneo la Urusi.

    Usumbufu huo unaoendelea ulisababisha ndege ya Finland Finnair kusimamisha safari za ndege za kila siku kuelekea jiji la pili kwa ukubwa nchini Estonia, Tartu, kwa mwezi mmoja, baada ya ndege zake mbili kulazimika kurejea Helsinki kutokana na kuingiliwa na GPS.

    Uwanja wa Ndege wa Tartu unategemea GPS pekee, tofauti na viwanja vingi vya ndege vikubwa ambavyo vina mifumo mbadala ya urambazaji inayoruhusu ndege kutua hata ikiwa mawimbi yamepotea.

  6. Kundi la watu wanaosemekana kuwa Al-Shabaab wauawa nchini Kenya

    .

    Takriban washukiwa sita wa Al-Shabaab waliuawa katika shambulio la kuvizia la vikosi vya usalama vya Kenya katika eneo la Kumba mkoani Lamu siku ya Jumatano.

    Polisi walisema pia walinasa vifaa muhimu.

    Mahali palipotokea shambulizi hilo ni Msitu wa Boni ambapo baadhi ya wanachama wa kundi hilo walisemekana kuwepo.

    Jeshi la Kenya lilianzisha mashambulizi hayo.

    Wafanyakazi hao walisema kwamba baadhi ya wanaume wa Al-Shabaab walifanikiwa kutoroka.

    "Umma unashauriwa kuwa macho kwa sababu operesheni hiyo inaweza kusababisha kuongezeka kwa shughuli za kundi hilo," alisema afisa mmoja.

    Miongoni mwa waliouawa ni mtu anayeaminika kuwa wa asili tofauti na Somali na Waafrika wengine, ambao mamlaka inaamini kuwa ni raia wa kigeni.

    Shambulio hilo lilijiri baada ya kupokea taarifa za kijasusi kuwa kundi hilo lilikuwa linapanga mashambulizi katika eneo hilo.

    Soma zaidi:

    Kwa nini raia hawa wa Somalia wameamua kukabiliana na Al-Shabaab

  7. Jordan: Shambulizi la Israel dhidi ya misafara miwili ya mashirika ya kutoa misaada kuelekea Gaza lazua hasira

    .

    Shambulizi la Israel dhidi ya misafara miwili ya kutoa misaada kuelekea Gaza Jumatano, limesababisha hasira huko Jordan.

    Mashirika ya kutoa misaada yalikuwa yakipita kuelekea vivuko vya Kerem Shalom na Beit Hanoun-Erez, katika kile ambacho kinasemekana ni mara ya kwanza msaada wa Jordan kuingia kupitia kivuko cha Beit Hanoun.

    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jordan, Sufyan Al-Qudah aliiambia BBC Kiarabu kwamba upande wa Israel ulipaswa kutoa ulinzi kwa malori ya misaada dhidi ya mashambulizi yoyote.

    Wizara ya Mambo ya Nje na Masuala ya Raia wa Kigeni ya Jordan pia ilizingatia, katika taarifa ya kushutumu, kwamba serikali ya Israel "ilishindwa kulinda misafara miwili yakutoa misaada na kuruhusu kushambuliwa ikiwa ni ukiukaji wa kikatili wa majukumu yake ya kisheria, kama taifa lenye nguvu linalokalia eneo hilo na majukumu yake ya kuruhusu misaada kuingia Gaza."

    Baadaye siku ya Jumatano, malori 79 ya misaada yaliweza kuingia Ukanda wa Gaza, na kwa mara ya kwanza, malori 31 yaliingia kupitia kivuko cha Beit Hanoun, na lori 48 kupitia kivuko cha Kerem Shalom, kulingana na taarifa zilizoarifiwa BBC na Hussein Al-Shibli, Katibu Mkuu wa Shirika la kutoa Misaada la Hashemite la Jordan.

    Soma zaidi:

    Juhudi za usitishaji mapigano kati ya Israel na Hamas zaendelea Saudia

  8. Urusi imetumia sumu za kuzuia pumzi nchini Ukraine - Marekani

    .

    Marekani imeishutumu Urusi kwa kupeleka silaha za kemikali kama "njia ya mapigano" nchini Ukraine, kinyume na sheria za kimataifa zinazopiga marufuku matumizi yao.

    Maafisa wa idara ya serikali walisema Urusi ilitumia kemikali ya chloropicrin kupata "mafanikio katika uwanja wa vita" dhidi ya Ukraine.

    Madai hayo, ambayo maafisa wa Marekani walisema hayakuwa tukio "la pekee", yangekiuka Mkataba wa Silaha za Kemikali (CWC), ambao Urusi ilitia saini.

    Ikulu ya Urusi bado haijatoa maoni yoyote, lakini imekanusha madai kama hayo hapo awali.

    Shirika la Kuzuia Silaha za Kemikali (OPCW), shirika la kimataifa linalosimamia utekelezaji wa CWC, linasema silaha ya kemikali ni dutu inayotumiwa kusababisha kifo cha kukusudia au madhara kupitia sumu yake.

    Mnamo mwaka wa 2017, OPCW ilisema Urusi imeharibu hifadhi yake ya mwisho ya wakati wa Vita Baridi, kama inavyotakiwa chini ya mkataba wa CWC. Mataifa pia yamepigwa marufuku kutengeneza au kupata silaha mpya chini ya mkataba wa 1993, ambao umetiwa saini na mataifa 193.

    Lakini tangu wakati huo Moscow imeshutumiwa kwa kutoa tamko lisilo kamili la hifadhi yake, kulingana na maktaba ya Bunge la Uingereza.

    Tangu mwaka 2017, Urusi imekuwa ikishutumiwa kwa takriban mashambulizi mawili ya kemikali - shambulio la Salisbury dhidi ya afisa wa zamani wa ujasusi wa Soviet na 2020 ya kumpa sumu kiongozi wa upinzani wa Urusi marehemu Alexei Navalny.

    Chloropicrin - ambayo Marekani inasema Urusi imetumia "kuondoa majeshi ya Ukraine kutoka maeneo yenye ngome" - ni dutu ya mafuta ambayo ilitumiwa sana wakati wa Vita vya kwanza vya dunia WW1.

    Husababisha muwasho wa macho na ngozi na inaweza kusababisha kutapika, kichefuchefu na kuhara, kulingana na Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Marekani (CDC).

    Utumiaji wa kemikali katika vita umepigwa marufuku waziwazi chini ya mkataba wa CWC.

    Soma zaidi:

    Zifahamu sumu zinatumiwa na majasusi kuua watu

  9. Meja Jenerali Fatuma Ahmed ateuliwa kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza jeshi la angani Kenya

    Laillah Mohammed

    BBC Swahili

    th

    Meja Jenerali Fatuma Ahmed ameandikisha historia nchini Kenya kwa kuteuliwa kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza kitengo cha jeshi la angani katika majeshi ya Ulinzi wa Kenya, KDF.

    Uteuzi wake umetangazwa na idara ya ulinzi baada ya kuidhinishwa na Rais William Ruto ambaye pia amemteua Jenerali Charles Kahariri kuwa mkuu wa majeshi.

    Jenerali Kahariri alikuwa anashikilia wadhifa huo akiwa Luteni Jenerali baada ya kifo cha Jenerali Francis Omondi Ogolla mwezi Aprili katika ajali ya ndege.

    Meja jenerali Ahmed amekuwa mwanamke wa kwanza katika miaka kumi iliyopita kupandishwa cheona kuwa Brigedia na tena kuwa Meja Jenerali na kuongoza taasisi muhimu katiika jeshi kama vile kuwa kamanda wa chuo cha mafunzo ya kijeshi cha KMA kule Lanet katika kaunti ya Nakuru.

    Kabla ya uteuzi wake alikuwa katika chuo kingine cha mafunzo cha National Defence College mjini Nairobi kama mmoja wa wakurugenzi.

    Jenerali Ahmed alianza kazi ya uanajeshi mnamo 1984 alipojiunga na Jeshi la Kenya.

    Mwaka mmoja baadaye, alijiunga na chuocha mafunzocha KMA na kupata mafunzo ya kijeshi na kitaaluma kabla ya kufuzu na kuwa Luteni kiwango cha chini na kuwa katika kitengo maalum cha kina dada katika jeshi cha Womens corps.

    Baada ya kuvunjwa kwa kikosi hicho alijiunga na jeshi la angani Kenya Airforce na kujukumikia kazi zake katika taasisi mbali mbali kwenye kambi za jeshi la angani za Moi Air Base Nairobi na Laikipia Airbase Nanyuki.

    Mnamo 2017 Rais Uhuru Kenyatta alimteua kuwa Brigedia wa kwamza wa kike katik jeshi la Kenya na baada ya uteuzi wake mabadiliko makubwa ya kuwajumuisha kina mama katika uongozi jeshini yameshuhudiwa kama katika kitengo cha mawasiliano ambacho kinaongozwa na Brigedia Ziporra Kioko, kitengo cha sheria kinachoongozwa na Brigedia Yvonne Kerubo na mkurugenzi wa tasisi ya usalama na amani IPSTC Brigedia Joyce Sitienei , na afisa anayesimamia kitengo cha kubuni ramani Brigedia Caroline Mutisya .

    Katika uteuzi wa alhamisi hii Rais ammeteua meja jenerali John Omenda ambaye alikuwa mkuu wa jeshi la angani kuwa Luteni Jenerali na kushikilia wadhifa wa naibu mkuu wa majeshi, Meja jenerali Paul Owuor amekabidhiwa wadhifa wa mkuu wa jeshi la majini huku maafisa wengine wakipandhiswa madaraka kutoka Ubregedia na kuwa meja jenerali na kuteuliwa pia kuongoza tasisi mbali mbali

    Unaweza pia kusoma

    Fatuma Ahmed: Wanawake hutekeleza mchango muhimu vitani katika jeshi

  10. Apple yapambana kutatua tatizo la kengele kwenye simu za iPhone

    .

    Kampuni ya Apple inasema inafanya juhudi za haraka kurekebisha suala ambalo lilisababisha kengele za iPhone kutotoa sauti, na kuwafanya watumiaji wao waliolala kupitiliza kulilalamika.

    Wengi, hutumia simu zao kama kengele na baadhi ya walioathirika waligeukia mitandao ya kijamii ili kutoa kilio chao

    TikTokker mmoja alilalamika kwamba alikuwa ameweka " kengele tano" na hazikusikika.

    Apple imethibitisha kuwa inafahamu suala hilo - lakini bado haijaeleza kile inachoamini kinasababisha, au nini watumiaji wanaweza kufanya ili kuepuka kuanza kuchelewa.

    Haijulikani pia ni watu wangapi wameathiriwa au ikiwa tatizo limezuiwa na aina fulani za iPhone.

    Wasiwasi huo hapo awali uliibuliwa na walioshiriki mapema kwenye kipindi cha Leo cha NBC, ambacho kilitoa taarifa hiyo.

  11. Mafuriko Kenya: Watalii 40, wafanyakazi kadhaa waokolewa katika mbuga ya wanyama ya Masai Mara

    .
    Image caption: Mafuriko

    Watalii 40 na wafanyakazi kadhaa waliokolewa katika Hifadhi ya Masai Mara baada ya mto Talek kuvunja kingo zake na kufurika.

    Akizungumza na wanahabari katika hoteli ya Sarova Mara Lodge, Gavana wa Narok Patrick Ntutu alisema hakuna majeruhi wala vifo vilivyoripotiwa.

    Mafuriko yameathiri kambi tisa zikiwemo kambi ya Tipilikwani, kambi ya Mara Leisure, kambi ya Mara Base, kambi ya Olkinyei, kambi ya Mara Big Five, Mariot Camp, Sweet Acacia, Pride Inn Mara na Kananga camp.

    Gavana Ntutu alisema kuwa mto huo ulikuwa umefurika usiku wa manane na kuathiri sehemu za mji wa Talek na kuwaacha wageni wakiwa mekwama katika kambi kadhaa kando ya mto huo.

    Aidha, gavana huyo amesema kata ya Mosiro imeathiriwa sana na mvua zinazoendelea kunyesha huku familia 100 zinazoishi kando ya eneo la Mosiro zikihama makazi yao.

    Gavana huyo amewataka wale wanaoishi karibu na mito hiyo kuhama kwenda katika ardhi salama.

    Kamishna wa Kaunti ya Narok Lotiatia Kipkech alikariri maoni ya gavana huyo kwa kuwaonya wanaoishi karibu na mito kuhamia maeneo salama.

    Lotiatia amewataka wadau hao kuwatahadharisha wananchi wanaoishi karibu na mito juu ya hatari ya mafuriko, na kuongeza kuwa serikali itatumia nguvu kuwahamisha wananchi wanaoishi katika maeneo yanayokumbwa na mafuriko.

    Maelezo zaidi:

    Mafuriko Kenya: Jinsi mafuriko yanavyofichua hali mbaya ya mazingira ya Nairobi

    Barabara 3 zilizofunikwa na mafuriko mjini Nairobi zafungwa

    Mafuriko Kenya: Watalii 40, wafanyakazi kadhaa waokolewa katika mbuga ya wanyama ya Masai Mara

  12. Ajuza raia wa Ukraine atembea kilomita 9 kutoka kijiji kilichokaliwa hadi eneo salama

    .
    Image caption: Lidiia Lomikovska alitenganishwa na familia yake walipokuwa wakijaribu kutoroka majeshi ya Urusi

    Kwa Lidiia Lomikovska mwenye umri wa miaka 98, uvamizi wa Urusi ni mbaya zaidi kuliko Vita vya Pili vya Dunia, ambavyo pia alikuwa aliishi.Amejifunza kuamini hisia zake.

    Ndiyo maana majeshi ya Urusi yalipoingia kijijini kwao Ocheretyne mashariki mwa Ukraine, yeye na familia yake waliamua kuwa ni wakati wa kuondoka.

    Hatahivyo, chini ya makombora mazito, Lidiia hivi karibuni alitenganishwa na jamaa zake, kwa hivyo akaanza kutembea magharibi "Nilichukua fimbo na ubao [kwa ajili ya msaada] na nikaenda zangu," aliiambia BBC.

    "Miguu yangu ilikuwa ikinibeba kwa namna fulani; sikuwa nimeibeba!"Alitembea kilomita 10 (maili 6) hadi alipochukuliwa na polisi wa Ukraine.

    "Hakuna kitu kilichosalia! Kila kitu kiko juu chini!" alionekana akisema video iliyotolewa.

    Kijiji alichoacha nyuma polepole kinabadilishwa kuwa mandhari ya kuzimu kila wanajeshi wa Urusi wanapokaribia .

    Kadiri wanavyokaribia ndivyo mashambulizi ya vifaru yanavyozidi kuwa makali. Vyumba na nyumba zote zinageuka polepole kuwa vifusi na vumbi.

    Soma:

    Vita vya Ukraine: Kwanini Ukraine inaweza kushindwa na Urusi 2024?

    Ni silaha gani muhimu zinazohitajika na Ukraine kuzuia kasi ya Urusi?

  13. Bao la Fullkrug laipatia Dortmund ushindi wa mkondo wa kwanza dhidi ya PSG

    .
    Image caption: Niclas Fullkrug amefunga mabao matatu kwenye Ligi ya Mabingwa msimu huu akiwa na Borussia Dortmund

    Niclas Fullkrug alifunga bao la ushindi katika kipindi cha kwanza wakati Borussia Dortmund ilipoilaza Paris St-Germain 1-0 katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa meci ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa.

    Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ujerumani alitumia mguu wake wa kulia kuipokea kwa ustadi pasi ndefu kabla ya kuupiga mpira kwa mguu wake wa kushoto na kuiweka kifua mbele Dortmund dakika ya 36.

    Baada ya kipindi kibovu cha kwanza, PSG walipoteza nafasi kadhaa za kusawazisha na katika kipindi cha pili, Kylian Mbappe alipiga shuti nje ya lango kabla ya Achraf Hakimi kugonga mwamba wa goli muda mfupi baadaye.

    Fullkrug alipaswa kufunga bao la pili baada ya kazi kubwa iliyofanywa na winga wa Manchester United Jadon Sancho aliyeko kwa mkopo lakini mshambuliaji huyo alipiga nje ya goli akiwa maguu matano pekee karibu na lango.

  14. Moscow: Warusi wamiminika kuona vifaru na silaha za Magharibi zilizokamatwa Ukraine na Urusi

    .
    Image caption: Kifaru cha Marekani kilichoharibiwa Ukraine

    Hili ni jumba kubwa la ukumbusho la Moscow lililowekwa kwa ajili ya kushindwa kwa Umoja wa Kisovieti dhidi ya Ujerumani ya Nazi.

    Onyesho jipya la wazi limefunguliwa hivi karibuni.Lakini halina uhusiano wowote na Vita vya pili vya Dunia.

    Kwenye maonyesho ni vifaa vya kijeshi vya Magharibi vilivyokamatwa na jeshi la Urusi huko Ukraine.

    Ni mataji ya vita na Urusi imeamua kuyapigia debe.Miongoni mwa silaha hizi ni gari la msaada la kijeshi la Uingereza la Husky ambalo lilikuwa limepewa Ukraine.

    Kioo chake cha mbele kimefunikwa na mashimo ya risasi. Kinyume na Husky naweza kuona vifaru vya Magharibi ambavyo vilikuwa vimepelekwa kwa jeshi la Ukraine.

    Kuna kifaru cha Abrams cha Marekani ambacho kiliharibiwa kwenye uwanja

    Je, ni kweli kuwa Hamas iliundwa na Israel?

    Ni silaha gani muhimu zinazohitajika na Ukraine kuzuia kasi ya Urusi?

    Vita vya Gaza: Israeli hupata wapi silaha zake?

  15. 'Wakati ni sasa' kwa makubaliano ya Israel na Hamas huko Gaza - Blinken

    .
    Image caption: Bw Blinken - anaonekana hapa akitembelea kivuko cha Kerem Shalom siku ya Jumatano - alisema msaada zaidi ulikuwa ukiingia Gaza lakini hili lilihitaji kuharakishwa.

    Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken ameiambia Israel na Hamas kwamba "wakati ni sasa" wa makubaliano ya kuleta usitishaji vita huko Gaza na kuwaachia huru mateka waliosalia wanaoshikiliwa.

    Bw Blinken alisema makubaliano yapo mezani na Hamas wanapaswa kukubaliana nayo.

    Wapatanishi wanasubiri jibu kutoka kwa Hamas kwa pendekezo la hivi punde.

    Inaripotiwa kuwa makubaliano hayo yanahusisha usitishaji vita wa siku 40 na kuachiliwa kwa zaidi ya mateka 30 wa Israel kwa kubadilishana na wafungwa wengi zaidi wa Kipalestina.

    "Tumedhamiria kupata usitishaji mapigano ambao unawaleta mateka nyumbani na kuupata sasa, na sababu pekee ambayo hilo halingeafikiwa ni Hamas," Bw Blinken alisema alipokutana na Rais wa Israel Isaac Herzog mjini Tel Aviv.

    "Kuna pendekezo kwenye meza, na kama tulivyosema, hakuna ucheleweshaji, hakuna visingizio. Wakati ni sasa."

    Afisa mkuu wa Hamas amekanusha kwamba kundi hilo ndilo linalochelewesha kuafikia makubaliano hayo mapya.

    Familia za mateka zilikuwa zikiandamana nje na Bw Blinken akawasalimia, akisema kuwaachilia wapendwa wao ndio "msingi wa kila kitu tunachojaribu kufanya".

    Takriban mateka 130 kutoka miongoni mwa 253 waliotekwa nyara na Hamas wakati wa shambulio lisilokuwa na kifani dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba bado hawajulikani waliko.

    34 kati yao wanakisiwa kuwa wamekufa. Wengine wameachiliwa au wameokolewa.

    Israel na Hamas: Nini kimetokea kwa Hamas baada ya miezi sita ya vita Gaza?

    'Tunahitaji muujiza' - Uchumi wa Israeli na Palestina ulivyoathiriwa na vita

    Je, ni kweli kuwa Hamas iliundwa na Israel?

  16. Mamlaka ya hali ya hewa nchini Tanzania TMA yaonya kuhusu kimbunga

    Abdalla Dzungu

    BBC Swahili, Nairobi

    .

    Mamlaka ya hali ya hewa nchini Tanzania TMA imatangaza kuwepo kwa mgandamizo mdogo wa hewa ambao unatarajiwa kutawala na kusababisha mvua kubwa na upepo mkali katika mikoa mitano nchini humo.

    Mgandamizo huo unatarajiwa kuimarika na kufikia hadhi ya kimbunga kamili kufikia leo tarehe 2 mwezi Mei 2024,

    ‘’Hali hiyo inatarajiwa kusogea na kuelekea baadhi ya maeneo ya pwani ya nchi yetu kuanzia usiku wa kuamkia siku ya Ijumaa tarehe 3 mwezi Mei 2024’’, ilisema TMA katika taarifa kwa vyombo vya habari.

    Baadhi ya maeneo yanayotarajiwa kuathiriwa na mvua hiyo pamoja na upepo ni mikoa ya Mtawara , Lindi, Pwani, Morogoro ,Dar es salaam na maeneo Jirani.

    Serikali imewashauri wananchi kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri wa hali ya hewa ili kupata ushauri na mwongozo wa wataalam katika sekta husika kwa lengo la kujikinga na athari zinazoweza kuibuka.

    Mamlaka ya hali ya hewa hatahivyo imesema mgandamizo huo mdogo unatarajiwa kupungua nguvu baada ya tarehe 6 Mei 2024.

    Freddy: Kimbunga kilichodumu zaidi ya mwezi mmoja

    Fahamu namna ya kujihadhari na athari za El Nino

    Sauti zinazoonya kuhusu vimbunga

  17. Natumai hujambo