Got a TV Licence?

You need one to watch live TV on any channel or device, and BBC programmes on iPlayer. It’s the law.

Find out more
I don’t have a TV Licence.

Habari za moja kwa moja

Na Asha Juma na Ambia Hirsi

time_stated_uk

  1. Video: Tazama jinsi dereva huyu aliyekuwa akifukuzwa na polisi kwa muda mrefu alivyokamatwa

    Video content

    Video caption: Tazama jinsi dereva huyu aliyekuwa akifukuzwa na polisi kwa muda mrefu alivyokamatwa
  2. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo haya ya moja kwa moja. Kwaheri.

  3. Duka la China lafungwa Abuja kwa madai ya kuwabagua Wanigeria

    xx

    Mamlaka nchini Nigeria imefunga duka la jumla linalomilikiwa na Wachina katika mji mkuu wa Abuja kwa madai kwamba kuwabagua wafanyabiashara wa Kiafrika.

    Duka kuu la Abuja linadaiwa "kuruhusu watu wa asili ya Kichina pekee kuendesha biashara zao," shirika la ulinzi la watumiaji la Nigeria lilisema kwenye X.

    Imemwita mmiliki wa duka hilo kuu kwa mahojiano. Baraza la wafanyabiashara wa China nchini Nigeria limekanusha madai hayo ya ubaguzi wa rangi.

    Duka hilo kuu ni mpangaji katika jengo linaloendeshwa na Chama Kikuu cha Biashara cha China (CGCC).

    Boladale Adeyinka, afisa katika Tume ya Shirikisho ya Ushindani na Ulinzi wa Watumiaji ya Nigeria (FCCPC), alisema kuwa shirika hilo limeanzisha uchunguzi kuhusu madai hayo

    Hii inafuatia ghadhabu iliyoenea kwenye mitandao ya kijamii baada ya baadhi ya Wanigeria kuelezea uzoefu wao wa kudaiwa kuzuiwa na usalama walipojaribu kwenda kwenye duka kubwa.

  4. Video: Hatari! Tazama uokoaji wa mtu aliyenaswa ndani ya gari linaloungua

    Video content

    Video caption: Kanda ya video inaonesha uokoaji kutoka kwa gari linalochomeka

    Kamera ya gari ilirekodi wakati madereva wa St Paul, Minnesota, waliposimama katikati ya barabara kuu ili kumwokoa mwanamume aliyenaswa ndani ya gari lililokuwa likiungua.

    Kanda hiyo inaonyesha watu wakijaribu sana kufungua milango ya gari kabla ya mtu kuvunja dirisha la dereva ili kumtoa mtu huyo aliyekuwa amekwama ndani ya gari hilo.

    Dereva huyo alipelekwa katika hospitali ya karibu lakini hakupata majeraha yoyote mabaya

  5. Unai Emery kusalia Aston Villa hadi 2027

    Kocha wa Aston Villa Unai Emery
    Image caption: Villa wako mbioni kufuzu kwa mashindano ya Uropa kwa msimu wa pili mfululizo

    Kocha wa Aston Villa Unai Emery amekubali kurefusha mkataba wake na klabu hiyo hadi 2027.

    Villa walikuwa katika nafasi ya 16 kwenye Ligi Kuu ya England na kupambana kushuka daraja wakati Mhispania huyo alipochukua mikoba ya Steven Gerrard mnamo Novemba 2022.

    Katika mhatua ya kushangaza, Emery, 52, aliiongoza Villa nakuisaidia kumaliza katika nafasi ya saba ili kufuzu kwa Ligi ya Uropa, ushiriki wa kwanza wa klabu hiyo katika soka ya Ulaya tangu 2010-11.

    Msimu huu, wanashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England wakiwa na malengo ya kufuzu Ligi ya Mabingwa.

    Wana pointi sita mbele ya Tottenham, ambao wana michezo miwili mkononi.

    Nafasi ya Emery inaweza kuimarishwa kwa kiasi kikubwa ikiwa atatoa kombe la Ligi ya Mikutano ya Uropa na soka ya Ligi ya Mabingwa.

    Emery anayesifika kwa umahiri wake katika mashindano ya Uropa, ameiongoza Villa hadi nusu fainali katika Ligi ya Mikutano, ambapo watamenyana na Olympiakos ya Ugiriki wakiwa na matumaini ya kutinga fainali ya kwanza ya Uropa tangu 1982.

    Emery alishinda Ligi ya Uropa kwa misimu mitatu mfululizo akiwa Sevilla kabla ya kunyanyua taji hilo mnamo 2021 akiwa na Villarreal.

    Alitumia miezi 18 kuinoa Arsenal, ambayo ilizingatiwa na wengi kuwa haikufanikiwa kwani Gunners walimaliza nafasi ya tano kwenye Ligi Kuu ya England na kutinga fainali ya Ligi ya Uropa 2019, ambapo walipoteza kwa Chelsea.

  6. Hali ya Haiti ni 'janga' na inazidi kuwa mbaya, UN yaonya

    Mama na mtoto

    Watoto milioni tatu nchini Haiti wanahitaji msaada wa kibinadamu huku ghasia za magenge zikiendelea kutatiza utoaji wa misaada, mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, Unicef, amesema.

    Catherine Russell alisema hali nchini Haiti iliyoharibiwa na genge ni "janga" na inazidi kuwa mbaya "kila uchao".

    Aliuambia mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa katika maeneo mengi huduma muhimu zimeporomoka.

    Wakati huo huo, baraza la mpito la rais bado halijaapishwa.

    Wakati Haiti imekuwa ikikabiliwa na magenge kwa miaka mingi, makundi yenye silaha yalizidisha mashambulizi yao mwishoni mwa Februari wakati Waziri Mkuu Ariel Henry aliposafiri kwenda Kenya kutia muhuri makubaliano ya kikosi cha usalama cha kimataifa kutumwa katika taifa hilo la Caribbea.

    Bw Henry alizuiwa kurejea Haiti huku magenge hayo yakishambulia uwanja wa ndege wa kimataifa, na kulazimisha kufungwa kwake.

    Mwezi uliopita alikubali kuondoka madarakani mara baada ya baraza la mpito la rais kuundwa na kusalia nje ya nchi.

    Hata hivyo, uundwaji wa baraza hilo umekumbwa na mifarakano ya ndani.

    Wajumbe tisa wa baraza hilo bado hawajaapishwa ili kuwaweka rasmi madaraka.

  7. Utalii Tanzania: Benki ya Dunia yasitisha kwa muda ufadhili wa mradi wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha

    Sammy Awami

    BBC News, Dar es Salaam

    Ruaha

    Benki ya Dunia imesitisha kiasi fedha za mradi unaolenga kusaidia usimamizi, ustahimilivu na uendelevu wa sekta ya utalii katika maeneo ya Kusini mwa Tanzania.

    Uamuzi huo uliofikiwa tarehe 18 Aprili umetokana na ripoti iliyoandaliwa na taasisi ya masuala ya sera ijulikanayo kama Okland Insitute iliyopo Marekani na kujihusisha na kutetea haki za binadamu Katika ripoti waliyoitoa mwezi Novemba mwaka jana,

    Taasisi ya Oakland iliitaka Benki ya Dunia kusitisha fedha hizo mara moja ikiishutumu Tanzania kwa kunyanyasa jamii zinazoishi karibu na maeneo ya mradi.

    “Mradi wenye thamani ya dola za Marekani milioni 150 uliokuwa na lengo la kuboresha usimamizi wa rasilimali asilia na mali za utalii katika maeneo ya kipaumbele ya Kusini mwa Tanzania - ikiwa ni pamoja na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha (RUNAPA).

    Badala yake, ufadhili wa Benki ulifungua njia kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya jamii zinazoishi karibu na hifadhi hiyo” imesema taasisi ya Oakland.

    Msemaji wa Benki ya Dunia amesema wamesikitishwa na taarifa za ukiukwaji wa haki za binadamu zinazoripotiwa kuambatana na mradi huo.

    "Hivi karibuni, tumepokea taarifa zinazoashiria uvunjaji wa sera zetu katika utekelezaji wa mradi wa Regrow.

    Kwa hivyo, tumekubaliana kusitisha utoaji wa fedha zaidi mara moja” amenukuliwa Msemaji wa Benki akisema. Mradi huu uliojulikana kama Resilient Natural Resource Management for Tourism and Growth (REGROW) ulianza mwaka 2017 ukilenga kuimarisha miundombinu mbalimbali kama vile ujenzi wa barabara, sehemu za kuangalia Wanyama na vituo vya wageni pamoja na kuimarisha ulinzi wa wanyama pori.

    Tayari Tanzania ilikuwa imepokea kiasi cha $100 milioni huku ikitarajia kupata kiasi kilichobaki cha $50 milioni fedha ambazo zililenga kuimarisha sekta ya utalii Kusini mwa Tanzania na kuingizia serikali mapato.

    Juhudi za kupata maoni ya serikali bado zinaendelea.

    Pia unaweza kusoma:

    Ngorongoro :Nini kinachoendelea Ngorongoro?

    Mzozo wa Loliondo: Miaka 30 ya machungu na matumaini

  8. 'Huu ni mwisho wa Ten Hag - hakuna kurudi nyuma'

    .
    Image caption: Erik ten Hag

    Utawala wa Erik ten Hag kama meneja wa Manchester United unafikia kikomo na "hakuna kurudi nyuma", amesema mshambuliaji wa zamani wa ligi ya Premia Chris Sutton.

    United ilitinga fainali ya Kombe la FA Jumapili, lakini ilihitaji mikwaju ya penalti ili kuishinda Coventry, licha ya kuongoza kwa mabao 3-0 zikiwa zimesalia dakika 20 kumalizika kwa mechi hiyo katika uwanja wa Wembley.

    Wako nafasi ya saba kwenye Ligi ya Premia, pointi 16 kutoka kwenye nafasi nne za juu, na walitolewa katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa msimu huu.

    "Kwa kweli sijui Ten Hag anaenda wapi baada ya msimu huu," Sutton alisema kwenye Klabu ya Jumatatu ya Usiku ya BBC Radio 5 Live.

    "Ni mwisho wake sasa - hakuna njia ya kurudi baada ya hapo."

    Kipa wa zamani wa Newcastle na Manchester City, Shay Given alikubali, akisema: "Hakika hatma yake haijulikani

    "Haionekani kuwa hali nzuri kwake - alionekana kupotea wakati fulani kwenye mstari ambapo makocha husimama uwanjani. Kuna malalamishi mengi katika klabu kwa sasa."

    Mabao kutoka kwa Scott McTominay, Harry Maguire na Bruno Fernandes yalikuwa yamewaweka Reds katika udhibiti.

    Ten Hag alimtoa winga Alejandro Garnacho kabla ya bao la kwanza la Coventry, na Kobi Mainoo akatolewa muda mchache baadaye .

    Wote wawili wamekuwa moto wa kuotea mbali kwa United msimu huu.

    "Baada ya mechi, watu wanaangalia mabadiliko ya Ten Hag lakini hata yeye hangeweza kuona hilo wakati hali ilipokuwa mbaya zaidi.

    Walikuwa wakicheza tu," alisema Sutton, ambaye alishinda Ligi ya Premia na Blackburn mnamo 1995."

    Mchezo wao baada ya dakika 70 ulikuwa dalili ya jinsi Manchester United wamecheza msimu huu wote - walipoteza udhibiti."Hawakuweza kudhibiti tena mchezo na hilo limekuwa suala nyeti msimu wote."

  9. Rwanda yakaribisha kupitishwa kwa mswada wa kuwapeleka wahamiaji kutoka Uingereza nchini mwao

    .

    Serikali ya Rwanda imekaribisha habari kwamba Bunge la Uingereza hatimaye lilipitisha mswada wa kuwapeleka wahamiaji haramu katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki na kusisitiza kuwa iko tayari kuwapokea wahamiaji hao.

    Mahakama za Uingereza zimeweka rekodi ya haki za binadamu ya Kigali katika kipaumbele kwa kudai ulinzi zaidi kwa wale waliopelekwa huko.

    Katibu wa habari wa rais na msemaji wa serikali Yolande Makolo amesema, "Tunafuraha kwamba Mswada huo umepitishwa na Bunge la Uingereza. Hata hivyo, haubadilishi kile ambacho tumekuwa tukijua kuwa ni kweli: tumefanya kazi kwa bidii katika miaka 30 iliyopita kuifanya Rwanda kuwa nchi salama kwa Wanyarwanda na vile vile, kwa watu ambao si Wanyarwanda. Hii ndiyo sababu tunaweza kutoa usalama kwa wakimbizi zaidi ya 130,000 ambao tayari wako nchini Rwanda, na kwa nini tunashirikiana na UNHCR kuwaleta wahamiaji waliokwama nchini Libya katika eneo letu ambalo ni salama. Tumejitolea kwa Ushirikiano wa Maendeleo na Uingereza na tunatarajia kuwakaribisha waliohamishiwa Rwanda."

    Mahali ambapo wahamiaji wanatarajia kupelekwa pamekuwa tayari kwa karibu miaka miwili. Vyumba vimepakwa rangi mpya, ishara kwamba wako tayari kupokea wageni.

    Katika mkahawa mmoja uliotembelewa na mwanahabari wa BBC, wananchi walikuwa na maoni tofauti kuhusu mpango wa wahamiaji.

    Mfanyabiashara Emmanuel Kanimba, amefurahishwa na wazo hilo.

    ‘’Watu kutoka maeneo mbalimbali daima huleta mawazo tofauti. Na nina hakika, kwa msaada wa serikali, najua itasaidia nchi kujiendeleza zaidi na kuwawezesha watu hao kujiendeleza wenyewe.

    ‘’Utapata wapi ajira za watu hawa, sisi wenyewe tumehitimu masomo lakini bado hatujapata ajira. Tuko nje kutafuta kazi,’’ raia mwingine ambaye hakutaka kutambuliwa alisema.

    Soma zaidi:

    Mswada wa kuwapeleka wahamiaji Rwanda kuwa sheria baada ya miezi kadhaa ya mabishano

  10. Tazama jinsi helikopta mbili zilivyogongana na kuua watu 10

    Video content

    Video caption: Mgongano wa helikopta angani ulivyonaswa kwenye kamera

    Video inayoonesha mgongano wa angani kati ya helikopta mbili za jeshi la wanamaji wakati wa mazoezi ya gwaride la kijeshi nchini Malaysia imesambazwa sana kwenye mitandao ya kijamii.

    Helikopta moja ilinasa parapela nyingine, kabla ya zote wawili kuanguka chini.

    Watu kumi waliuawa katika ajali hiyo.

  11. Watu wengi wakamatwa huku maandamano ya vyuo vikuu Marekani kupinga vita vya Gaza yakienea

    .

    Maandamano ya kupinga vita huko Gaza yameenea kutoka Columbia na Yale hadi vyuo vikuu vingine nchini Marekani huku maafisa wakihangaika kukabiliana nayo.

    Siku ya Jumatatu usiku, polisi walitawanya maandamano katika Chuo Kikuu cha New York na kukamata watu kadhaa.

    Wanafunzi wengi walikamatwa huko Yale mapema siku hiyo wakati Columbia ilipositisha masomo ya ana kwa ana darasani.

    Maandamano kama hayo yameibuka huko Berkeley, MIT na vyuo vingine kote nchini humo.

    Maandamano na mijadala mikali kuhusu vita vya Israel na Gaza na uhuru wa kujieleza vimetikisa vyuo vikuu vya Marekani tangu kutokea kwa shambulio la Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba.

    Takriban Waisrael na raia wa wageni 1,200 - waliuawa na wengine 253 walirejeshwa Gaza kama mateka, kulingana na hesabu za Israel.

    Israel ilijibu kwa kuanzisha vita vyake vikali zaidi kuwahi kutokea huko Gaza kwa malengo ya kuangamiza Hamas na kuwakomboa mateka.

    Zaidi ya Wapalestina 34,000 huko Gaza - wengi wao wakiwa watoto na wanawake - wameuawa katika mzozo huo, wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas inasema.

    Nchini Marekani, wanafunzi wa pande zote mbili wanasema kumekuwa na ongezeko la matukio ya chuki dhidi ya Wayahudi na Uislamu.

    Alipoulizwa kuhusu maandamano ya chuo hicho siku ya Jumatatu, Rais Joe Biden alisema alilaani "maandamano ya chuki dhidi ya Wayahudi" pamoja na "wale ambao hawaelewi kinachoendelea na Wapalestina".

    Soma zaidi:

    Je, Marekani inapendelea uwepo wa taifa huru la Palestina?

  12. Watu 10 wafariki baada ya helikopta za Jeshi la Wanamaji kugongana angani Malaysia

    .

    Watu kumi wamefariki dunia baada ya helikopta mbili za jeshi la wanamaji kugongana angani wakati wa mazoezi ya kijeshi ya gwaride la Wanamaji wa Kifalme Malaysia.

    Moja ya ndege hizo ilinasa parapela ya ndege nyingine kabla ya zote kuanguka chini, kulingana na video iliyoonyeshwa na vyombo vya habari vya ndani.

    Tukio hilo lilitokea saa 09:30 kwa saa za huko katika mji wa Malaysia wa Lumut, ambao ni kitovu cha kambi ya jeshi la wanamaji.

    Hakuna manusura walioonekana.

    "Waathiriwa wote walithibitishwa kuwa wamefariki kwenye eneo la tukio huku mabaki yakipelekwa katika Hospitali ya Jeshi ya [Lumut] kwa utambulisho," Jeshi la Wanamaji la Kifalme la Malaysia lilisema.

    Imeongeza kuwa itaunda kamati kuchunguza chanzo cha tukio hilo.

    Moja ya helikopta, HOM M503-3 ikiwa na watu saba, inaaminika kuanguka kwenye njia ya ndege.

    Nyingine, Fennec M502-6 iliyokuwa imebeba waathiriwa wengine watatu, ilianguka kwenye kidimbwi cha kuogelea kilichokuwa karibu.

    Idara ya zimamoto na uokoaji ya jimbo hilo ilisema iliarifiwa kuhusu tukio hilo saa 09:50 kwa saa za ndani (01:50 GMT).

  13. Mtengenezaji mikoba maarufu kufungwa jela kwa ulanguzi wa wanyamapori

    .

    Mtengenezaji wa mikoba ya kifahari wa Colombia ambaye alikiri makosa ya kusafirisha mikoba iliyotengenezwa kwa ngozi za wanyama watambaao wanaohifadhiwa amehukumiwa kifungo cha miezi 18 jela.

    Nancy Gonzalez, ambaye ametengeneza mikoba iliyobebwa na waigizaji wa filamu ya Sex and the City na Britney Spears, alihukumiwa Jumatatu katika mahakama moja huko Miami.

    Gonzalez, 71, alivunja mkataba wa kimataifa kwa kuingiza nchini kinyume cha sheria mikoba iliyotengenezwa kwa mamba na chatu.

    Maafisa wanasema aliwasajili jamaa kuleta mikoba hiyo nchini Marekani.

    Colombia na Marekani zote zimetia saini Mkataba wa Biashara ya Kimataifa ya Wanyama na Mimea Walio Hatarini Kutoweka (CITES), ambao hulinda wanyama jamii ya mamba - na chatu, kulingana na taarifa kutoka Idara ya Sheria ya Marekani.

    Biashara ya mamba na chatu haijapigwa marufuku, lakini inadhibitiwa madhubuti chini ya sheria za mkataba huo.

    Gonzalez hakuwahi kupata vibali muhimu vya kuagiza vinavyohitajika na wadhibiti.

  14. Watu watatu wanaoshukiwa kuwa majasusi wa China wamekamatwa nchini Ujerumani

    .

    Mamlaka ya Ujerumani inasema kuwa imewakamata watu watatu kwa tuhuma za ujasusi wa China.

    Mshukiwa mkuu aliyetajwa kwa jina la Thomas R, anatuhumiwa kufanya ujasusi wa Wizara ya Usalama ya Nchi ya China.

    Waendesha mashtaka wanadai mtandao wake uliendesha kampuni ambayo ilishirikiana na mashirika ya utafiti ya Ujerumani.

    Washtakiwa hao wanadaiwa kukusanya taarifa nyeti, ikiwamo miundo ya injini inayofaa kutumika kwenye meli za kivita ili kupeleka China.

    Katika hatua tofauti, wanaume wawili nchini Uingereza walishtakiwa kwa ujasusi wa China baada ya kushutumiwa kutoa taarifa ambazo zinaweza "kuwa na manufaa kwa adui", kulingana na polisi.

    Katika kesi ya Ujerumani, waendesha mashtaka wanadai Thomas R alipata "teknolojia ya kibunifu kwa matumizi ya kijeshi" kwa niaba ya mfanyakazi wa Wizara ya Usalama ya Nchi ya China.

    Pia wanadai alitumia kampuni - inayoendeshwa na washukiwa wengine wawili, walioitwa kama Herwig F na Ina F - ambayo iliwasiliana na watu wanaofanya kazi katika sayansi na utafiti.

    Mradi wa kwanza kuhusu uendeshaji wa injini za baharini zenye ufanisi mkubwa kwa matumizi ya meli za kivita unadaiwa kuwa tayari umekamilika.

    Soma zaidi:

    Fahamu mashirika ya ujasusi yenye uwezo mkubwa duniani

  15. Bellingham ashinda tuzo ya mafanikio ya Laureus

    .

    Kiungo wa kati wa Uingereza na Real Madrid Jude Bellingham ameshinda tuzo ya Laureus World Sports Breakthrough of the Year 2024.

    Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20 amekuwa mchezaji muhimu wa Real kufuatia uhamisho wake wa pauni milioni 89 kutoka Borussia Dortmund msimu uliopita wa joto.

    Alifunga bao la ushindi dhidi ya Barcelona kwenye El Clasico Jumapili na kufikisha mabao 17 kwenye La Liga msimu huu.

    Bellingham pia aliisaidia Real Madrid kuishinda Manchester City kwa mikwaju ya penalti katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa wiki iliyopita.

    Tuzo ya Laureus ya Mwanaspoti Bora wa Dunia ilikwenda kwa mchezaji tenisi Novak Djokovic kwa mara ya tano, huku kiungo wa kati wa Uhispania na Barcelona, Aitana Bonmati akishinda tuzo ya upande wa wanawake.

    Bonmati, ambaye kwa sasa anashikilia Ballon d'Or, aliisaidia klabu yake kushinda Liga F, Kombe la Uhispania na Ligi ya Mabingwa ya Wanawake mnamo 2022-23.

    Pia unaweza kusoma:

    Tetesi za Soka Ulaya Jumanne 23.04.2024

  16. Biden aapa kusambaza kwa 'haraka' msaada mpya wa kijeshi kwa Ukraine

    .

    Rais Joe Biden wa Marekani amemwambia Volodymyr Zelensky "atachukua hatua haraka" kutuma msaada mpya wa kijeshi wa Ukraine, baada ya wabunge wa Marekani kupitisha kifurushi cha msaada cha $61bn (£49bn).

    Baraza la Wawakilishi liliidhinisha mswada huo siku ya Jumamosi baada ya miezi kadhaa ya msukosuko wa kisiasa katika bunge hilo.

    Bw Biden aliahidi msaada "muhimu" kwa Kyiv - ikiwa ni pamoja na ulinzi zaidi wa anga - ikiwa maseneta wataidhinisha mswada huo kama ilivyotarajiwa Jumanne.

    Uhakikisho huo unatokea wakati mashambulio ya Urusi yakiharibu mnara wa TV huko Kharkiv.

    Picha zilionyesha mnara huo mwekundu na mweupe ukiporomoka sekunde chache baada ya makombora ya Urusi kuushambulia siku ya Jumatatu alasiri katika mji wa mashariki mwa Ukraine, ulio umbali wa maili 19 tu (kilomita 30) kutoka mpaka wa Urusi.

    Maafisa wa eneo hilo walisema hakukuwa na majeruhi katika shambulio hilo, huku Gavana wa eneo hilo Oleg Syniehubov akiandika kwenye mitandao ya kijamii kwamba wafanyikazi walikuwa kwenye makazi wakati shambulizi hilo linatokea.

    Bw Syniehubov aliongeza kuwa shambulio hilo limetatiza utangazaji wa televisheni katika eneo hilo.

    Kharkiv imekuwa ikilengwa katika mashambulio ya angani yasiyokoma na vikosi vya Urusi katika wiki za hivi karibuni. Katika ujumbe mtandaoni baada ya shambulio hilo, Rais Zelensky aliandika kwamba ilikuwa "nia ya wazi ya Urusi kufanya mji huo usiwe na watu".

    Aliongeza kuwa alikuwa amemjulisha Rais Biden kuhusu shambulizi hilo, ambalo alisema lilifanyika kabla ya kuzungumza kwa njia ya simu siku ya Jumatatu.

    Soma zaidi:

    Vita vya Ukraine: Je, Ukraine itamudu bila msaada wa Marekani?

    Ni silaha gani muhimu zinazohitajika na Ukraine kuzuia kasi ya Urusi?

  17. Hujambo na karibu katika matangao yetu ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 23/04/2024