Got a TV Licence?

You need one to watch live TV on any channel or device, and BBC programmes on iPlayer. It’s the law.

Find out more
I don’t have a TV Licence.

Habari za moja kwa moja

Na Lizzy Masinga na Abdalla Seif Dzungu

time_stated_uk

  1. Serikali ya Israel yasitisha matangazo ya Al Jazeera nchini humo

    .

    Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ametangaza kuwa Al Jazeera itafungwa nchini Israel.

    Bw Netanyahu alishutumu mtandao unaomilikiwa na Qatar kwa "uchochezi" na kusema uamuzi wa baraza la mawaziri umekuwa wa kauli moja.

    Al Jazeera imelaani hatua hiyo na kusema ni ya jinai.Waandishi wa habari wa kigeni wamepigwa marufuku kuingia Gaza Kwa miaka mingi, maafisa wa Israel wamekuwa wakishutumu mtandao huo kwa chuki dhidi ya Israel.

    Lakini ukosoaji wao dhidi ya shirika hilo la utangazaji umeongezeka tangu mashambulizi ya Hamas tarehe 7 Oktoba, ambapo watu 1,200 waliuawa na zaidi ya 250 walichukuliwa mateka.

    Watu 128 kati ya mateka hao bado hawajulikani waliko - na kati yao, angalau 34 wanakisiwa kuwa wamekufa.

    Takriban Wapalestina 34,683 wameuawa na 78,018 kujeruhiwa huko Gaza tangu Oktoba 7, kulingana na wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas.

    Mamlaka zinasema Al Jazeera ina uhusiano wa karibu na Hamas, jambo ambalo mtandao huo unakanusha vikali.

    Mwezi uliopita, bunge la Israel lilipitisha sheria inayoipa serikali mamlaka ya kufunga kwa muda matangazo ya kigeni yanayochukuliwa kuwa tishio kwa usalama wa taifa wakati wa vita dhidi ya Hamas.

  2. Vita vya Israel na Gaza: Israel yafunga kivuko cha Kerem Shalom huku makombora yakirushwa kutoka Gaza

    .

    Israel imefunga kivuko cha Kerem Shalom na Gaza baada ya Hamas kurusha makombora kutoka ndani ya ukanda huo, jeshi limesema.

    Takriban watu 10 walijeruhiwa, wengine vibaya, vyombo vya habari vya Israeli vinaripoti.

    Kivuko hicho ni mojawapo ya njia chache za kupata misaada ya kibinadamu katika Gaza.

    Shambulio hilo lilikuja wakati wapatanishi nchini Misri wakifanya mazungumzo na kusuluhisha usitishaji mapigano - na kuwaachilia mateka wa Israel.

    Israel imesema haitakubali matakwa ya Hamas ya kusitisha vita vya Gaza.

    Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limesema makombora 10 yalirushwa kutoka eneo karibu na kivuko cha Rafah kusini mwa Gaza, kilichoko takriban kilomita 3.6 kutoka Kerem Shalom.

    Kulingana na IDF, yalirushwa kutoka eneo lililo umbali wa mita 350 kutoka kwa makazi ya raia na ni"mfano mwingine wa wazi wa unyonyaji wa kimfumo ambao shirika la kigaidi la Hamas linatengeneza vifaa katika maeneo kwa mahitaji ya ugaidi, wakati wakitumia idadi ya raia kama ngao".

  3. Habari za hivi pundeKimbunga Hidaya: Wawili wafariki 80 waokolewa katika mafuriko Lindi, Tanzania

    .
    Image caption: Mafuriko yaliosababishwa na Kimbunga

    Watu wawili wamefariki dunia na zaidi ya 80 wameokolewa wilayani Kilwa mkoani Lindi baada ya mvua kubwa kunyesha jana Mei 4, 2024 na kusababisha mafuriko.

    Kulingana na Mwananchi Digital, Mafuriko hayo mbali na kusababisha vifo, pia yamesomba madaraja na kukata mawasiliano katika eneo la Somanga.

    Akizungumza leo Jumapili, Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji, Mrakibu Msaidizi Joseph Mwasabije amesema, "tumewaokoa watu 80 na wawili wamefariki dunia, ambao wote ni wakazi wa Kilwa mkoani Lindi."

    Mwasabije amesema waliofariki dunia ni mwanaume na mwanamke ambao bado umri wao haujajulikana.

    Wakati huohuo Mwananchi Digital imesema kwamba daraja moja limesombwa na maji na kusababisha mawasiliano kukatika kati ya mikoa ya kusini na Pwani.

    Hali hiyo imetokana na madhara ya kimbunga Hidaya kilichosababisha mvua kubwa katika mikoa ya Lindi na Mtwara na Kisiwa cha Mafia mkoani Pwani.

  4. Habari za hivi pundeIdadi ya waliofariki kutokana na mafuriko nchini Kenya yafikia 228

    .
    Image caption: Mafuriko ncini Kenya

    Idadi ya watu waliofariki kutokana na mafuriko na athari nyingine za mvua kubwa inayonyesha nchini Kenya imeongezeka hadi 228, wizara ya mambo ya ndani ilisema Jumapili.

    Mvua kubwa ambazo zimesababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi kote nchini katika wiki za hivi karibuni zinatabiriwa kuwa mbaya zaidi mnamo Mei.

    Katika taarifa yake, wizara hiyo ilisema mafuriko zaidi yanatarajiwa "katika maeneo ya tambarare, maeneo ya pembezoni na mijini wakati maporomoko ya udongo/matope yanaweza kutokea katika maeneo yenye miteremko mikali,na miinuko ".

    Mafuriko hayo yameharibu nyumba, barabara, madaraja na miundombinu mingine katika eneo kubwa la uchumi wa Afrika Mashariki.

    Takriban watu 164 wamejeruhiwa na hali mbaya ya hewa, wakati 212,630 wamelazimika kuyahama makazi yao, wizara hiyo ilisema.

    th
  5. Kimbunga Hidaya: Mvua kunyesha pwani ya Kenya

    Idara ya hali ya hewa ya Kenya sasa inasema kimbunga Hidaya kilichotarajiwa kimepoteza nguvu zake baada ya kutua nchini Tanzania.

    Hata hivyo, Mkurugenzi wa Huduma za Hali ya Hewa David Gikungu amesema licha ya kudhoofika kwa kimbunga hicho, mvua bado inatarajiwa kunyesha katika maeneo ya pwani ya Kenya.

    Gikungu amesema kaunti za Kwale, Mombasa, Kilifi na Lamu huenda zikakumbwa na mvua za wastani hadi nyingi.

    “Kufuatia kutua kwa kimbunga hicho katika kisiwa cha Mafia siku ya Jumamosi Mei 4, 2024, kimbunga Hidaya kilipoteza nguvu kabisa, mabaki ya mawingu ya mvua yaliyoambatana na kimbunga hicho yameonekana kupungua na kusambaa katika maeneo mbalimbali ya ukanda wa kusini mwa Tanzania. , kama ilivyothibitishwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania," Gikungu alisema.

    Alisema mvua hiyo ya wastani hadi kubwa huenda ikaendelea kunyesha ndani ya siku ya Jumatatu na Jumanne huku ikiambatana na upepo mkali.

    Mkurugenzi huyo alisema upepo huo mkali unatarajiwa kupiga huku mawimbi makubwa ya bahari yakiweza kupanda urefu wa mita mbili.

    Gikungu amesema maeneo mengine ya nchi pia yanapaswa kutarajia mvua za wastani za mara kwa mara kati ya milimita tano hadi 20 hadi mvua kubwa za kati ya 20-50mm.

  6. Video: Tazama daraja la Brazil likivunjika na kutumbukia mtoni

    Video content

    Video caption: Daraja la Brazil livunjika na kutumbukia mtoni

    Kanda za video zinaonyesha mwanamume akikwepa chupuchupu kuangukia mtoni kusini mwa Brazil wakati daraja la barabara lilipokuwa likiacha njia Jumanne.

    Mvua kubwa - iliyosababisha mafuriko makubwa katika jimbo la Rio Grande do Sul - imeua watu 39, na 68 bado hawajulikani walipo, maafisa wa eneo hilo wanasema.

    Makumi ya maelfu wamekimbia makazi yao na kumekuwa na kukatika kwa umeme na kukatika kwa maji.

  7. Raia wa Cuba washawishiwa kujiunga na jeshi la Urusi kwa malipo ya juu na pasipoti

    .

    Huenda Urusi imekuwa ikiwasajili raia wa Cuba kupigana katika jeshi lake nchini Ukraine, utafiti wa BBC umeonyesha.

    Mnamo Septemba na Oktoba 2023, maelezo ya pasipoti za Wacuba zaidi ya 200 wanaodaiwa kujiunga na jeshi la Urusi yalifichuliwa mtandaoni na jukwaa linalounga mkono Ukraine kwa jina InformNapalm.

    Maelezo ya pasipoti yalipatikana, tovuti hiyo ilisema, kwa kudukua barua pepe za afisa wa usajili wa kijeshi wa Urusi huko Tula, kusini mwa Moscow.

    Uchunguzi wa Facebook umeonyesha kuwa majina 31 kati ya yaliyotajwa katika akaunti zilizovuja za Ukraine wamiliki wake wanaonekana kuwa nchini Urusi au wanahusishwa na jeshi la Urusi.

    Baadhi, kwa mfano, wamechapisha picha zao wakiwa wamevalia sare za kijeshi za Urusi, au katika maeneo ambayo yana alama za barabara za Kirusi au nambari za Kirusi. Wengine wanaorodhesha Urusi kama makazi yao ya sasa.

  8. Vita vya Israel na Gaza: Makumi kwa maelfu waandamana kwa ajili ya makubaliano ya kuwaachilia mateka huku mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza yakiendelea

    .
    Image caption: Waandamanaji Israel

    Makumi kwa maelfu ya Waisraeli walikusanyika hadi usiku wa manane wakitaka makubaliano ya kuwarudisha mateka nyumbani, kabla ya mazungumzo zaidi ya kusitisha mapigano.

    Waandamanaji mjini Tel Aviv waliimba "vita si takatifu, maisha ni", huku baadhi wakimtuhumu Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kwa lengo la kurefusha mzozo wa Gaza.

    Ilikuja wakati wajumbe wa Hamas walipokutana na wapatanishi nchini Misri siku ya Jumamosi.

    Kundi hilo lilisema hakuna hatua mpya zilziopigwa lakini likaongeza "duru mpya itaanza" siku ya Jumapili.

    Wapatanishi wameanza tena mazungumzo ya muda mrefu ya kusitisha mapigano mjini Cairo - yaliyosimamiwa na Misri na Qatar - juu ya kusitisha mashambulizi ya Israel huko Gaza ili kuwaachia huru mateka.

  9. Habari za hivi pundeHatari ya kimbunga Hidaya imekwisha

    Tathmini ya mifumo ya hali ya hewa imeonesha kwamba kimbunga Hidaya kimekwisa nguvu baada ya kuwasili nchini Tanzania.

    Mamlaka ya hali ya hewa inasema kwamba kimbunga hicho kilipiga kisiwa cha Mafia saa tatu asubuhi siku ya Jumamosi , takriban kilomita kilomita 130 kusini mashariki mwa mji wa kibiashara nchini Tanzania Dar es Salaam kabla ya kupoteza nguvu zake.

  10. Kenya yatafuta Ksh.720 Bilioni za kuunganisha SGR kutoka Naivasha hadi Malaba kwenye mpaka na Uganda

    Miundo mbinu ya SGR

    Kenya inataka kuimarisha ushirikiano wa sekta binafsi ili kupanua Reli ya Standard Gauge (SGR), ili kuhakikisha usafirishaji wa bidhaa unavuka mpaka bila matatizo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

    Waziri wa Barabara na Uchukuzi wa nchi hiyo Kipchumba Murkomen anasema hatua hiyo pia itaunda maeneo maalumu ya kiuchumi kando ya ukanda huo na kubadilisha miji ambayo maeneo ya kiuchumi yatakuwa.

    Akizungumza mjini Mombasa katika mkutano wa mawaziri, Murkomen alisema sehemu zilizosalia za SGR kutoka Naivasha nchini Kenya hadi Uganda, Rwanda, Sudan Kusini na DRC, zitakamilika, na kwamba wameandaa ramani ambayo itaharakisha utekelezaji wake.

    "Lengo kuu chini ya Mtandao wa Miundombinu ya Kiafrika ni kuhakikisha tunaunganisha Pwani ya Mashariki hapa Mombasa na Pwani ya Magharibi kupitia Duala nchini Cameroun tunatamani kuhakikisha kuwa mawasiliano yanafanyika hadi DRC," Alisema Murkomen.

    "Ninaamini kwamba ndoto ya SGR ipo na tunataka kuitimiza haraka. Tunataka kuinua sekta binafsi na ninajua mradi tulio nao sasa kutoka Naivasha hadi Malaba ikijumuisha uboreshaji karibu na Bandari ya Kisumu unakadiriwa kugharimu nchi takribani dola bilioni 5.3 (Ksh.700.3 bilioni)’' Alisema.

  11. Mwanaume raia wa Nigeria aliyemshambulia mwenza wake kwenye kiti cha magurudumu afukuzwa Kenya

    Kiti cha magurudumu

    Mwanaume mmoja raia wa Nigeria aliyenaswa kwenye video akimshambulia mwanamke Mkenya akitumia kiti cha magurudumu amefukuzwa nchini humo.

    Raia huyo ambaye ametambuliwa kama Nwankwo Noko, alifukuzwa Jumamosi, Mei 4, baada ya kumpiga mpenzi wake, Bi Pauline.

    Noko alinaswa na kamera za CCTV akimpiga mwanamke huyo wa Kenya ambaye alikuwa amefungwa kwenye kiti cha magurudumu.

    Tukio hilo liliionekana kutokea nyumbani . Katika picha hiyo, mwanaume huyo anaonekana akimpiga Pauline asiyejiweza kichwani kabla ya wanawake wengine wawili waliokuwa wakitazama kuingilia kati ili kusitisha tukio hilo.

    Video hiyo ilisambaa sana mnamo Aprili 29 na kumfanya Seneta Mteule Gloria Orwoba kufuatilia kesi hiyo.

    Mjumbe huyo alikutana na mwathirika mnamo Mei 1 na kisa hicho kiliripotiwa katika Kituo cha Polisi cha Karen. "Ni vigumu sana kwa watu kujitokeza hata kwa Pauline kuketi hapa nami ninaposimulia hadithi yake. Ameumizwa kabisa na vurugu za miaka 10," Owoba alisema.

    "Nimethibitisha kuwa mtu aliyeonekana akimshambulia Pauline ni raia wa kigeni na yuko hapa kwa kibali cha kufanya kazi. Pauline ana watoto na mwanaume huyo." Kisha Bi Pauline alifichua kwamba yeye na wafanyakazi wake wawili wa nyumbani walikuwa wametishwa na Noko ikiwa watathubutu kutoa ushahidi dhidi yake mahakamani kuhusu tukio hilo.

  12. Kenya yapiga marufuku shughuli katika ufuo kwa hofu ya kimbunga Hidaya

    Yusuf Jumah

    BBC Swahili

    Kindiki alisema watu wanapaswa kuondoka kwenye ufuo huo hadi saa sita usiku, Jumatatu, Mei 6, wakati Kimbunga Hidaya kinatarajiwa kuisha.

    Waziri wa Usalama wa Ndani nchini Kenya Kithure Kindiki amepiga marufuku shughuli katika ufuo wa pwani huku kukiwa na hofu kwamba kimbunga Hidaya kinaweza kutua wakati wowote kuanzia sasa.

    Waziri huyo aliagiza mashirika ya usalama kutekeleza agizo hilo na kuhakikisha shughuli za ufuo kama vile uvuvi, kuogelea na usafiri usio wa lazima ndani ya eneo la maji ya Kenya zimesitishwa mara moja.

    "Kamati za Usalama na Ujasusi za Kaunti (CSICs) za Kwale, Mombasa, Kilifi na Lamu kwa ushirikiano na Huduma ya Walinzi wa Pwani ya Kenya (KCGS) zimeagizwa kutoa notisi mara moja na kutekeleza kwa uthabiti marufuku ya shughuli za ufuo," alisema katika taarifa yake siku ya Jumamosi.

    Pia aliamuru kuhamishwa kwa makazi yaliyo karibu sana na ufuo kuanzia Jumamosi, Mei 4, saa kumi na moja jioni.

    Kindiki alisema watu wanapaswa kuondoka kwenye ufuo huo hadi saa sita usiku, Jumatatu, Mei 6, wakati Kimbunga Hidaya kinatarajiwa kuisha.

    "Kama hatua ya tahadhari, shughuli ndani ya eneo la maji ya Kenya, kando ya fukwe na ndani ya makazi karibu na ufuo itabidi kuahirishwa kwa sababu za usalama wa umma," alisema.

    Kindiki aliwaonya waaazi wanaoishi karibu na fuo za Kaunti za Kwale, Mombasa, Kilifi na Lamu dhidi ya kujihusisha na shughuli za uvuvi, kuogelea au burudani. Alisema hii ni kutokana na taarifa zinazoashiria uwezekano wa hatari kwa maisha na mali ndani ya maeneo hayo.

  13. Vita vya Israel na Gaza: Mazungumzo ya kusitisha mapigano yashika kasi mjini Cairo

    Kuna onyo la njaa huko Gaza baada ya miezi kadhaa ya mashambulizi ya Israel

    Juhudi zimeongezeka kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza na kuachiliwa kwa mateka, huku mazungumzo yakirejea mjini Cairo siku ya Jumamosi.

    Hamas ilisema ujumbe wake ulikuwa unasafiri ukiwa na "mtazamo chanya" baada ya kusoma pendekezo la hivi karibuni la usitishaji vita.

    "Tumedhamiria kupata makubaliano kwa njia ambayo inatimiza matakwa ya Wapalestina," ilisema.

    Wapatanishi wa Hamas wamerejea katika mji mkuu wa Misri ili kuanza tena mazungumzo ya muda mrefu, yaliyosimamiwa na Misri na Qatar, ambayo yatasimamisha kwa muda mashambulizi ya Israel huko Gaza ili kuwaachia huru mateka.

    Katika taarifa iliyotolewa jana usiku, Hamas ilisema inataka "kukomaza" makubaliano yaliyopo mezani, ambayo yanaonesha kuna maeneo ambayo pande hizo mbili bado hazikubaliani.

    Suala kuu linaonekana kuhusisha iwapo mpango wa kusitisha mapigano utakuwa wa kudumu au wa muda.

    Hamas inasisitiza kuwa mpango wowote unatoa dhamira mahususi kuelekea mwisho wa vita, lakini Israel inasita kukubaliana wakati kundi hilo likiendelea kufanya kazi huko Gaza.

    Inafikiriwa kuwa yanayojadiliwa yanahusisha kusitisha mapigano kwa siku 40 huku mateka wakiachiliwa huru, na kuachiliwa kwa idadi ya wafungwa wa Kipalestina wanaozuiliwa katika jela za Israel.

    Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesisitiza mara kwa mara kutakuwa na operesheni mpya ya kijeshi katika mji wa Rafah kusini mwa Gaza, hata kama makubaliano yatafikiwa. Vyombo vya habari vya Israel viliripoti Jumamosi kwamba msimamo wake haujabadilika licha ya duru ya hivi punde ya mazungumzo.

    Lakini Marekani, mshirika mkubwa wa kidiplomasia na kijeshi wa Israel, inasitasita kuunga mkono mashambulizi mapya ambayo yanaweza kusababisha vifo vya raia, na imesisitiza kuona mpango wa kuwalinda Wapalestina waliokimbia makazi yao kwanza.

    Takribani watu milioni 1.4 wamejihifadhi mjini Rafah baada ya kukimbia mapigano katika maeneo ya kaskazini na katikati mwa ukanda huo.

  14. Kisiwa cha Mafia chakumbwa na athari za kimbunga Hidaya

    Athari za kimbunga

    Wakazi wa kisiwa cha Mafia ni miongoni mwa waliokumbwa na athari za kimbunga Hidaya kilichopiga kuanzia jana usiku na kudumu kwa saa kadhaa.Mwananchi imeripoti.

    Upepo mkali ulioambatana na mvua kubwa umesababisha mafuriko, miti mikubwa ikiwamo mikorosho na minazi kudondoka kwenye makazi ya watu usiku wa manane. Tazama hali ilivyokuwa kwenye baadhi ya maeneo kisiwani Mafia.

    Athari za kimbunga hidaya
    Athari za kimbunga
    Athari za kimbunga Mafia
  15. Kimbunga Hidaya: Upepo mkali, mvua kubwa yashuhudiwa pwani ya kusini ya Tanzania

    Mwenendo wa kimbunga

    Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa ya mwenendo wa kimbunga Hidaya kilichopo karibu na maeneo ya pwani ya Tanzania.

    Taarifa yake imesema hadi kufikia saa 9 usiku wa kuamkia leo, Kimbunga hicho kilikuwa katika eneo la bahari takriban kilomita 125 kutoka pwani ya Kilwa (Mkoa wa Lindi), kilomita 93 kutoka pwani ya Mafia na kilomita 128 kutoka pwani ya Dar es salaam na kasi ya upepo unaofika kilomita 120 kwa saa.

    Tangu usiku wa kuamkia leo, matukio ya upepo mkali na mvua kubwa zinazosababishwa na uwepo wa kimbunga yameendelea kujitokeza ambapo hadi kufika saa 3 asubuhi, kituo cha hali ya hewa cha Kilwa Masoko (Lindi) kimeripoti mvua ya jumla ya kiasi cha milimita 111.3 kwa kipindi cha saa 6 zilizopita.

    Kiwango hiki cha mvua ni kikubwa sana ukizingatia kuwa wastani wa mvua kwa mwezi Mei kwa kituo cha Kilwa Masoko ni milimita 96.6 tu. Hivyo kiasi cha mvua kilichonyesha ndani ya saa 24 katika kituo cha Kilwa Masoko ni takribani asilimia 115 ya wastani wa mvua kwa mwezi Mei kwa kituo cha Kilwa Masoko.

    Viwango vya mvua vilivyopimwa katika vituo vingine katika kipindi hicho ni milimita 90.7 kwa Mtwara na milimita 85.3 katika kituo cha hali ya hewa Naliendele (Mtwara). Kiwango cha mvua cha milimita 90.7 kilichonyesha Mtwara ndani ya saa 24 ni takribani asilimia 168 ya wastani wa mvua kwa mwezi Mei kwa Mtwara (milimita 54).

    Vipindi vya mvua kubwa bado vinaendelea katika maeneo hayo ya ukanda wa pwani ya kusini. Kwa upande mwingine, katika vituo vya hali ya hewa vya Mtwara, Kilwa, Zanzibar, Tanga na Dar es Salaam upepo mkali unaozidi kilomita 50 kwa saa umeweza kupimwa katika nyakati tofauti kuanzia usiku wa kuamkia leo hadi asubuhi ya leo.

    Aidha, kimbunga kinatarajiwa kuendelea kusogea karibu zaidi na ukanda wa pwani ya Tanzania huku kikipungua nguvu taratibu kuelekea usiku wa kuamkia Jumapili tarehe 05 Mei 2024.

    Kimbunga bado kinatarajiwa kuendelea kusababisha matukio ya vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika maeneo ya ukanda wa pwani hususan mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani na Dar es salaam pamoja na kisiwa cha Unguja na maeneo ya jirani. Vilevile, matukio ya mawimbi makubwa baharini yanatarajiwa kuendelea kujitokeza katika ukanda wote wa mwambao wa pwani ya Bahari ya Hindi.

    Wananchi wanaojihusisha na shughuli mbalimbali baharini wameshauriwa kuchukua tahadhari kubwa.

  16. Mexico yapata miili mitatu ilipokuwa ikiwatafuta watalii waliotoweka

    Mamlaka ya Mexico imepata miili mitatu katika eneo la Baja California

    Mamlaka ya Mexico imepata miili mitatu katika eneo la Baja California ambapo ndugu wawili wa Australia na Mmarekani mmoja walitoweka.

    FBI ilisema miili hiyo ilipatikana katika mji wa Santo Tomas na bado haijatambuliwa, mshirika wa BBC wa Marekani CBS News aliripoti.

    Jake, 30, na Callum Robinson, 33, kutoka Perth, na Mmarekani Jack Carter Rhoad, 30, walikuwa kwenye likizo karibu na mji maarufu wa kitalii wa Ensenada.

    Walitoweka tarehe 27 Aprili. Siku ya Alhamisi polisi wa Mexico walimhoji mwanamke mmoja na wanaume wawili kuhusiana na kutoweka kwao. Uchunguzi wa kisayansi utafanywa na maabara ya serikali kutambua miili hiyo, ofisi ya mwendesha mashtaka wa jimbo la Baja California ilisema.

    Ofisi hiyo pia ilibaini siku ya Ijumaa hati za kukamatwa zimepatikana kwa uhalifu wa kutoweka kwa lazima. Mahema yaliyokuwa yametelekezwa hapo awali, lori jeupe lililoungua na simu iliyohusishwa na watalii waliotoweka zilipatikana.

    Timu ikiwa ni pamoja na wazima moto walikuwa wakiwatafuta ndugu wa Robinson na Bw Rhoad katika eneo la mbali la miamba.

    Katika taarifa kwa CBS News, FBI ilisema "haiwezi kutoa maoni" lakini "tunaweza kukuhakikishia kuwa tunatathmini kila kidokezo". "Tunawasiliana na familia ya raia wa Marekani, na tuko imara na washirika wetu wa kimataifa wa kutekeleza sheria katika kutafuta majibu," ofisi hiyo iliongeza.

    Baja California ni mojawapo ya majimbo yenye vurugu zaidi Mexico, huku magenge ya watu wanaojihusisha na biashra haramu ya dawa za kulevya katika eneo hilo yakipigana.

  17. Daktari wa Kipalestina afariki katika jela ya Israel

    Dk Al-Bursh

    Daktari mmoja wa Kipalestina amefariki katika jela ya Israel baada ya kukaa kizuizini kwa zaidi ya miezi minne, vyama vya wafungwa wa Palestina vimesema. Dkt Adnan Al-Bursh, 50, alikuwa mkuu wa madaktari wa mifupa katika Hospitali ya al-Shifa.

    Huduma ya magereza ya Israel ilithibitisha kuwa ukweli taarifa iliyochapishwa tarehe 19 Aprili kuhusu mfungwa ambaye alizuiliwa kwa sababu za usalama wa taifa na alikufa katika gereza la Ofer alikuwa Dk Al-Bursh.

    Hakuna maelezo yoyote yaliyotolewa kuhusu chanzo cha kifo hicho, na jeshi la magereza lilisema tukio hilo linachunguzwa.

    Lakini mashirika ya kutetea wafungwa wa Kipalestina yalisema katika taarifa yake ya pamoja siku ya Alhamisi kwamba kifo cha Dk Al-Bursh kilikuwa "mauaji" na mwili wake bado umesalia chini ya ulinzi wa Israel.

    Dk Al-Bursh alikuwa mkuu wa madaktari wa mifupa katika kituo kikubwa zaidi cha matibabu huko Gaza, hospitali ya al-Shifa, ambayo imevamiwa mara kadhaa na vikosi vya jeshi la Israeli.

    Alikuwa akifanya kazi kwa muda katika hospitali ya Al-Awada kaskazini mwa Gaza alipozuiliwa na wanajeshi wa Israel.

  18. Hidaya: Huduma za vivuko zasitishwa Tanzania kupisha kimbunga

    Kivuko

    Huduma za vivuko zimesitishwa katika mikoa mitatu ya Tanzania . Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (Temesa) umetangaza kusitisha huduma hizo katika mikoa mitatu ya Mtwara, Lindi na Pwani kufuatia tahadhari iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu kimbunga Hidaya.

    Temesa ilitangaza hayo Ijumaa Mei 3, 2024. "Kutokana na kuwepo kwa tahadhari hiyo, Temesa inawajulisha watumiaji wa vivuko kuwa katika baadhi ya maeneo ya Mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani ikijumuisha Visiwa vya Mafia, mikoa ya Dar es Salaam na Tanga kwamba kutakuwa na kusimama kwa utoaji wa huduma ya vivuko ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza," imesema taarifa hiyo.

    Temesa inatoa taarifa hiyo ikiwa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) hadi leo alfajiri Mei 4, 2024 ikisema kasi ya kimbunga Hidaya ni kilomita 120 kwa saa.

  19. Marekani yazilaumu Rwanda na M23 kwa shambulio baya kwenye kambi DRC

    Zaidi ya watu milioni 2.5 wamekimbia makazi yao nchini DR Congo, Marekani inasema, huku wengi wakiishi katika kambi kama vile Shabindu huko Goma.

    Marekani imelilaumu jeshi la Rwanda na kundi la waasi la M23 kwa shambulio baya katika kambi ya watu waliokimbia makazi yao katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

    Takribani watu tisa, wakiwemo watoto saba, waliuawa katika shambulio kwenye kambi ya Mugunga katika mji wa mashariki wa Goma siku ya Ijumaa.

    Jeshi la Congo na M23 walilaumiana kwa shambulio hilo.

    Rwanda, ambayo inapakana na DR Congo, inashutumiwa vikali kwa kuunga mkono kundi la waasi, jambo ambalo inakanusha.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema shambulio hilo la Ijumaa lilitoka katika maeneo yanayoshikiliwa na Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) na kundi la M23.

    Msemaji huyo alisema Marekani "ina wasiwasi mkubwa kuhusu upanuzi wa hivi karibuni wa RDF na M23" mashariki mwa DR Congo na kuzitaka pande zote mbili "kuheshimu haki za binadamu na kuzingatia wajibu unaotumika chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu".

    "Ni muhimu kwamba mataifa yote yaheshimu mamlaka ya kila mmoja na uadilifu wa eneo na kuwawajibisha wahusika wote kwa ukiukaji wa haki za binadamu katika mzozo wa mashariki mwa DRC," waliongeza.

    Picha zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilionesha miili ikiwa imelala chini kwenye kambi hiyo siku ya Ijumaa.

    Wakazi wengi walikuwa wamekimbilia huko kutoroka mapigano katika miji na vijiji vyao.

    Lt Kanali Guillaume Njike Kaiko, msemaji wa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika eneo hilo, alisema shambulio hilo limekuja kulipiza kisasi mashambulizi ya awali ya Wacongo dhidi ya maeneo ya jeshi la Rwanda.

    Rais Felix Tshisekedi, ambaye amekaa wiki kadhaa nje ya nchi, atarejea mwishoni mwa juma hili.

    Wanajeshi wa waasi na serikali wote wameshutumiwa katika miezi ya hivi karibuni kwa unyanyasaji dhidi ya raia wakati wanapigania udhibiti wa maeneo.

    Shambulio la hivi karibuni limetokea siku chache baada ya wapiganaji wa M23 kudai kuwa wameuteka mji wa Rubaya, eneo ambalo ni kitovu cha uchimbaji madini ya Coltan inayotumika kutengenezea simu za mkononi na betri za magari yanayotumia umeme.

    Wakati huo huo, mahakama ya kijeshi mjini Goma imewahukumu kifo wanajeshi wanane wa DR Congo kwa "kutoroka" na "uoga" wakati wa kupambana na vikosi vya waasi, M23, iliyoundwa kama chipukizi la kundi jingine la waasi, ilianza kufanya kazi mwaka 2012 ili kulinda watu wa kabila la Watutsi mashariki mwa DR Congo, ambao kwa muda mrefu walikuwa wakilalamikia mateso na ubaguzi.

    Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wamesema kuwa kundi hilo linaungwa mkono na nchi jirani ya Rwanda, ambayo pia inaongozwa na Watutsi, jambo ambalo Kigali imekuwa ikikanusha.

  20. Kimbunga Hidaya kuendelea kusogea ukanda wa Pwani ya Tanzania leo

    Kimbunga

    Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa ya mwenendo wa kimbunga Hidaya kilichopo katika Bahari ya Hindi mashariki mwa pwani ya Tanzania.

    Mamlaka imesema mpaka kufika saa tatu ya siku ya jana, kimbunga kilikuwa katika eneo la bahari takribani kilomita 230kutoka pwani ya Kilwa (Mkoa wa Lindi) na kilomita 170 kutoka pwani ya Mafia kikiwa na kasi ya upepo inayofikia kilomita 120 kwa saa.

    Uwepo wa kimbunga karibu na pwani ya nchi hiyo umeendelea kutawala mifumo ya hali ya hewa katika baadhi ya maeneo ambapo katika kipindi cha saa 12 zilizopita, vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali vimeendelea kujitokeza.

    Hali ya upepo mkali unaozidi kilomita 40 kwa saa imeelezwa kujitokeza katika vituo vya hali ya hewa Mtwara, Kilwa, Zanzibar na Dar es Salaam na mvua kubwa Lindi na Mtwara.

    TMA imesema kimbunga Hidaya kitaendelea kusogea karibu kabisa na ukanda wa pwani wa Tanzania mchana wa leo tarehe 4 Mei kabla ya kuanza kupungua nguvu kuelekea siku ya kesho.

    Kwa siku ya leo, kimbunga kinatarajiwa kuendelea kusababisha matukio ya vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika maeneo ya ukanda wa pwani hususani mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani na Dar es Salaam pamoja na visiwa vya Unguja na maeneo jirani.

    Unaweza kusoma;

    Yote unayotakiwa kuyafahamu kuhusu Kimbunga Hidaya