Idriss Deby: Mfahamu Jenerali Mahamat Kaka mtoto wa Déby aliyerithi madaraka ya Chad

Mahamat Deby

Chanzo cha picha, Getty Images

Jenerali Mahamat alihudumu kama kiongozi wa kikosi cha ulinzi cha rais kama mkurugenzi mkuu wa huduma ya usalama katika taasisi za serikali (DGSSIE) tangu 2014.

Mwaka 2013 alichaguliwa kuwa kiongozi wa jeshi la Chad nchini Mali , ambapo alishiriki katika operesheni pamoja na vikosi vya Ufaransa kabla ya kurudi nyumbani kusimamia DGSSIE.

Alikuwa pamoja na babake alipojeruhiwa katika vita dhidi ya waasi katika mkoa wa magharibi wa Kanem.

Mahamat, ambaye pia anajulikana kama "Jenerali Kaka", ana sifa ya kuishi Maisha ya siri ikilinganishwa na nduguze wa kambo . Hata hivyo ni mwanajeshi jasiri sawa na alivyokuwa baba yake.

"Rais wa taifa hilo [Idriss Deby] aliweka mawasiliano ya [Mahamat] na watu maarufu wa Chad pamoja na maafisa wakuu wa jeshi kutoka kwa mataifa yalio na uhusiano mzuri na taifa hilo. Ilikuwa njia yake ya kumfunza jinsi kuchukua madaraka, gazeti la Jeune Afrique liliripoti.

Marehemu Debi alikuwa na Watoto wengi wa kiume , wengi wao wakihudumu katika serikali katika viwango tofauti.

Kuna uwezekano kwamba kutakuwa na wasiwasi kati ya Mahamat na baadhi ya ndugu zake wa kambo. Upinzani umekataa baraza la kijeshi kusimamia serikali ya mpito.

Gazeti la Le Journal du Tchad liliripoti kwamba waziri mkuu wa zamani Saleh Kebzabo na Mahamat Ahmad Alhabo wa chama cha upinzani cha PLD wametaka serikali hiyo ya mpito kusimamiwa na spika wa bunge.

Hata hivyo, upinzani umegawanyika na hautafaulu kuwasilisha changamoto kwa jeshi.

Jinsi Idriss Deby alivyomtengenezea njia mwanawe

Idriss Deby aliongoza makamanda wake mstari wa mbele vitani

Chanzo cha picha, Marachel Idriss Deby Itno

Maelezo ya picha,

Idriss Deby aliongoza makamanda wake mstari wa mbele vitani

Deby aliiongoza Chad kwa kutumia nguvu, akiwakabili wakosoaji wake kwa kutumia uwezo wake wote.

Kwa mfano Chad haijwahi kuwa na waziri mkuu tangu jaribio la mapinduzi 2018.

Katiba mpya iliopitishwa Disemba 2000 ilibuni nafasi ya makamu wa rais lakini wadhfa huo ulikuwa haujajazwa wakati rais Deby alipouawa.

Kabla ya uchaguzi wa tarehe 11 Aprili, Deby alipinga maandamano ya upinzani akisema kwamba Demokrasia sio machafuko.

Aliendelea kushikilia madaraka kupitia kuwachagua ndugu zake na marafiki kushikilia wadhfa tofauti.

Hatua ya kulimbikiza mamlaka katika jamii yake ilimaanisha kwamba kulikuwa hakuna mrithi wa kisiasa wa bwana Deby.

Hivyobasi haishangazi kuona kwamba jeshi lilichukuwa udhibiti wakati Deby alipofariki. Jeshi lilisema kwamba bunge na serikali limevunjiliwa mbali na baraza la jeshi lenye wanachama 15 limechaguliwa kuongoza serikali ya mpito likiongozwa na Mahamat Deby , ''aliyewekwa ili kuhakikisha kuwa kuna muendelezo wa serikali."

Jeshi litaongoza kwa miezi 18 kabla ya kusimamia uchaguzi mpya. Katiba imeahirishwa na mahala pake patachukuliwa na serikali ya mpito itakayoongiozwa na Mahamat Deby.

Ni dhahiri kwamba, makamanda wa jeshi wanaamini mwanawe Jenerali Mahamat Idris Deby ambaye alikuwa akisimamia kitengo cha walinzi wa rais ndiye mrithi sahihi wa kuendeleza aina hiyo ya utawala.