Masalia ya mwili wa Augustin Bizimana, mshukiwa mkuu wa mauaji ya Rwanda yapatikana

Masalia ya mwili wa Augustin Bizimana yalipatikana katika kaburi katika eneo la Pointe-Noire inchini Congo-Brazzavill

Chanzo cha picha, IRMCT

Maelezo ya picha, Masalia ya mwili wa Augustin Bizimana yalipatikana katika kaburi katika eneo la Pointe-Noire inchini Congo-Brazzavill

Mabaki ya Augustin Bizimana, ambaye ni miongoni mwa washukiwa wakuu wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994, yamepatikana , mwendesha mashtaka wa vita kutoka Umoja wa mataifa ameeleza.

Mabaki hayo yamepatikana katika kaburi huko nchini Congo-Brazzaville. Majibu ya vipimo vya vina saba yamedhibitisha kuwa ni yeye Bizimana na alifariki miaka 20 iliyopita.

Bwana Bizimana alikuwa waziri wa ulinzi wakati watu 800,000 walipouwawa ndani ya siku 100.

Bizimana alipatikana na hatia katika mahakama ya Umoja wa mataifa mwaka 1998 na kushtakiwa kwa makosa 13 yakiwemo mauaji ya kimbari, ubakaji na kuwatesa watu.

Tangazo la kifo chake limekuja baada ya kukamatwa kwa mshukiwa mwingine mkuu Félicien Kabuga mwishoni mwa wiki huko mjini Paris, ambaye anatuhumiwa kufadhili mkuu wa mauaji ya kimbari.

Mshukiwa mwingine mkuu wa mauaji ya Kimbari ya Rwanda Félicien Kabuga pia alikamatwa wiki hii nchini Ufaransa miaka 26 baada ya mauaji ya kimbari

Chanzo cha picha, US STATE DEPARTMENT

Maelezo ya picha, Mshukiwa mwingine mkuu wa mauaji ya Kimbari ya Rwanda Félicien Kabuga pia alikamatwa wiki hii nchini Ufaransa miaka 26 baada ya mauaji ya kimbari

Wauaji wengi waikuwa wa kabila la wahutu na waliwalenga kundi dogo la watutsi pamoja na wapinzani wao wa kisiasa.

Bado watuhumiwa wengine sita wanatafutwa kuhusika na mauaji hayo ya kimbari, alisema mwendesha mashtaka wa uhalifu wa kivita bwana Serge Brammertz.

Kati ya hao sita, anayetafutwa zaidi ni Protais Mpiranya, aliyekuwa kamanda wa ulinzi wa rais.

Kama ilivyo kwa Kabuga na Bizimana, wanadaiwa kuwa walitoroka na kujificha baada ya mauaji ya kimbari.

Mauaji ya aliyekuwa waziri mkuu na walinda Amani

Bwana Brammertz ni mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya kimataifa wa uhalifu huko The Hague, ambayo inashughulikia uhalifu wa kivita wa Rwanda na iliyokuwa Yugoslavia.

"Bizimana alikuwa anatuhumiwa kuhusika na mauaji ya aliyekuwa waziri mkuu wa Rwana Agathe Uwilingiyimana na raia 10 wa Ubelgiji ambao walikuwa walinda Amani kutoka Umoja wa mataifa na kuua raia wa Rwanda ambao ni watusi kutoka katika mikoa mitano, alisema.

Mshukiwa mkuu wa mauaji ya kimbari Rwanda akamatwa

Matokeo ya kudhibitishwa kwa kifo cha Bizimana yamekuja baada ya uchunguzi kufanyika katika masalia ya binadamu ambayo yalikuwa katika maeneo ya makaburi huko Pointe-Noire nchini Congo, alisema.

Picha za Baadhi ya wahanga wa mauaji ya kimbari ya Rwanda katika moja ya makumbusho ya mauaji hayo nchini Rwanda

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Picha za Baadhi ya wahanga wa mauaji ya kimbari ya Rwanda katika moja ya makumbusho ya mauaji hayo nchini Rwanda

Pamoja na uchunguzi wa vina saba vyake kwa miezi kadhaa, uchunguzi umebaini kuwa kifo cha Bizimana kilitokea mwezi Agosti mwaka 2000, mwendesha mashitaka alisema.

Hata hivyo maelezo ya bwana Brammertz yanatoa ufafanuzi kuhusu kifo cha waziri huyo wa ulinzi ambaye alikufa akiwa na umri wa miaka 46 hivi.

Watu wengi wameshtakiwa katika mahakama ya uhalifu ya kimataifa kwa kuhusika katika mauaji ya kimbari, mamia kwa maelfu walishtakiwa katika mahakama za kijamii nchini Rwanda.