Jovenel Moïse: Mwili wa rais wa Haiti 'ulichanika' kwa kumiminiwa risasi nyingi-mkewe asema

Martine Moise

Chanzo cha picha, Martine Moise/TWITTER

Mjane aliyejeruhiwa wa rais wa Haiti ameelezea wakati wauaji "walipommiminia risasi" mumewe baada ya kupenya na kuingia nyumbani kwao katikati ya usiku.

Martine Moïse alisema shambulio hilo lilitokea haraka sana, mumewe Jovenel hakuweza "kusema hata neno moja".

Rais Moïse aliuawa mnamo Julai 7, ikidaiwa na mamluki 28 wa kigeni.

Bi Moïse pia alijeruhiwa katika shambulio hilo, na alisafirishwa kwenda Miami kwa matibabu.

Jumamosi, alitoa ujumbe wa sauti kwenye ukurasa wake wa Twitter akiapa kuendelea na kazi yake.Watu kadhaa wamethibitisha kuwa ni mke wa rais.

Martine Moise alisema machozi yake "hayatakauka kamwe" kufuatia mawazo ya mumewe Jovenel

Chanzo cha picha, EPA

"Ghafla, mamluki waliingia nyumbani kwangu na kumuua mume wangu kwa risasi," Bi Moïse anasema katika rekodi hiyo, akielezea wakati ambapo washambuliaji walimuua mumewe.

"Kitendo hiki hakina jina kwa sababu lazima uwe mhalifu sugu kumuua rais kama Jovenel Moïse, bila hata kumpa nafasi ya kusema neno moja," aliongeza

Citizens take part in a protest near the police station of Petion Ville after Haitian president Jovenel Moïse was murdered on July 08, 2021 in Port-au-Prince, Haiti.

Chanzo cha picha, Getty Images

Alidai kamba mumewe alikuwa akilengwa kwa sababu za kisiasa - haswa, akitaja kura ya maoni juu ya mabadiliko ya katiba ambayo ingeweza kumpa rais nguvu zaidi.

Watu hao ambao hawajulikani alisema, "wanataka kuua ndoto ya rais".

"Ninalia, ni kweli, lakini hatuwezi kuiacha nchi ipotee," aliongeza. "Hatuwezi kuruhusu damu ya Rais Jovenel Moïse, mume wangu, rais wetu ambaye tunampenda sana na ambaye alitupenda sisi, kupita bure."

Bw Moïse, mwenye umri wa miaka 53, alikuwa rais wa Haiti, taifa maskini zaidi katika Amerika, tangu 2017. Wakati wake katika ofisi ulikuwa mgumu kwani alikabiliwa na tuhuma za ufisadi na kulikuwa na maandamano mengi katika mji mkuu na miji mingine mapema mwaka huu.

Uchaguzi wa bunge ulipaswa kufanywa mnamo Oktoba 2019 lakini mizozo imechelewesha, ikimaanisha Bw Moïse alikuwa akitawala kwa amri. Alikuwa amepanga kufanya kura ya maoni juu ya mabadiliko ya katiba yaliyopendekezwa mnamo Septemba hii.

Maelezo ya video, Polisi wamewatoa kwa umma washukiwa wanaodaiwa kuhusika na mauaji ya rais wa Haiti pamoja na silaha na paspoti zao

Mnamo Februari mwaka huu, siku ambayo wapinzani walitaka aondoke afisini, Bw Moïse alisema jaribio la kumuua na kupindua serikali lilishindwa.

Bado haijulikani ni nani aliyepanga shambulio la Jumatano na kwa nia gani. Maswali kadhaa bado hayajajibiwa, pamoja na jinsi wauaji wanaodaiwa kutekeleza mauaji yake walivyoweza kuingia katika boma lake. Walinzi wa Bw Moïse wanastahili kuhojiwa wiki ijayo.

Kiongozi mmoja maarufu wa upinzani ameelezea waziwazi wasiwasi juu ya tukio hilo. Seneta wa zamani wa Haiti Steven Benoit aliambia kituo cha redio Magik9 siku ya Ijumaa kuwa "sio Wakolombia waliomuua", lakini hakutoa ushahidi kuunga mkono madai yake.

Polisi wa Haiti wamesema wengi wa mamluki walikuwa Wakolombia , wakati wawili walikuwa raia wa pamoja wa Marekani.

Kumi na saba wa kikundi hicho walizuiliwa katika mji mkuu Port-au-Prince baada ya makabiliano ya risasi. Washukiwa watatu waliuawa na polisi, na wengine wanane bado wanatafutwa.

Serikali ya Colombia imeahidi kuisaidia Haiti na juhudi zake za uchunguzi.

Mkurugenzi wa polisi wa Colombia, Jenerali Jorge Luis Vargas, alisema wanajeshi 17 wa zamani wa Colombia walidhaniwa kuhusika.

Men accused of the president's assassination sit against a wall

Chanzo cha picha, Reuters

Idara ya serikali ya Marekani, wakati huo huo, ilisema haiwezi kuthibitisha ikiwa raia wake yeyote alikuwa amezuiliwa.

Walakini, vyombo vya habari vya Marekani na Canada vinaripoti kuwa mmoja wa raia wawili waliokamatwa, James Solages, 35, ni kutoka Florida na alikuwa mlinzi wa zamani katika ubalozi wa Canada huko Haiti.

Jaji anayechunguza kesi hiyo aliambia vyombo vya habari vya eneo hilo kwamba Bwana Solages na raia mwingine wa Marekani, aliyeitwa Joseph Vincent, walikuwa wamesema wako huko kama watafsiri wa mamluki.

"Misheni ili kumkamata Rais Jovenel Moïse ... na sio kumuua," Jaji Clément Noël aliiambia Le Nouvelliste.

Ni nani anayeiongoza Haiti?

Katiba inasema Bunge linapaswa kuchagua rais mwingine. Lakini mizozo ilimaanisha kuwa uchaguzi uliopangwa kufanyika Oktoba 2019 haukufanyika - na Bw Moïse alikuwa akitawala kwa amri wakati maandamano yalipoenea.

Marekebisho ya katiba - ambayo hayakubaliwi na kila mtu - yanaonyesha kuwa waziri mkuu ndiye anayepaswa kuchukua nafasi hiyo.

Lakini Haiti ina waziri mkuu wa muda, Claude Joseph, na mteule mpya, Ariel Henry, ambaye bado hajaapishwa.

Wote wanadai kuwa wapo usukani .

Siku ya Ijumaa, kikundi cha vyama vya siasa kilitia saini azimio la kumtangaza rais mpya - Joseph Lambert - na Bw Henry akishikilia nafasi ya Waziri Mkuu wake.

Hatua hiyo haijafanya mengi kutatua machafuko ya kisiasa na kiuchumi ambayo kwa muda mrefu yamelizonga taifa hilo.