Got a TV Licence?

You need one to watch live TV on any channel or device, and BBC programmes on iPlayer. It’s the law.

Find out more
I don’t have a TV Licence.

Habari za moja kwa moja

time_stated_uk

  1. Mpaka hapa tumefika mwisho wa matangazo ya moja kwa moja ya ukurasa wetu wa BBC Swahili, tukutane tena hapo kesho...Shukrani!

  2. Mashambulizi ya ndege zisizo na rubani yaua watu 17 huko Tigray - wafanyikazi wa misaada

    Mashambulizi mapya ya ndege zisizo na rubani yamesababisha vifo vya takriban watu 17 katika eneo Tigray linalokabiliwa na vita nchini Ethiopia, wahudumu wa misaada wamesema.

    Matukio hayo yanafuatia mashambulizi mawili sawia kwenye kambi mbili wiki iliyopita ambayo yaliwauwa takriban wakimbizi 60 na wakimbizi wa ndani.

    Hapo jana mitambo miwili ya kusaga unga ililengwa. Wengi waliouawa katika shambulizi la anga katika mji wa Mai Tsebri waliripotiwa kuwa wanawake.

    BBC haijathibitisha binafsi ripoti za hivi punde.

    Wakati kumekuwa na utulivu wa mapigano ardhini baada ya vikosi vya Tigray kurudi nyuma kutoka majimbo jirani za Amhara na Afar, mashambulizi ya angani yameendelea katika hali ambayo imelazimisha Umoja wa Mataifa (UN) kusimamisha operesheni katika baadhi ya maeneo ya Tigray wiki iliyopita.

    Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto limesema kuwa mashambulizi dhidi ya kambi za wakimbizi yanaweza kuwa uhalifu wa kivita.

    Umoja wa Mataifa na Rais wa Marekani Joe Biden wameibua wasiwasi juu ya kuendelea kwa mashambulizi ya angani yanayosababisha vifo vya raia.

    Ethiopia: Mzozo wa Tigray ulivyogeuka vita vya wenyewe kwa wenyewe

    Vita vya Ethiopia: Kwanini kujua kinachoendelea Tigray ni muhimu?

  3. Rwanda kuendelea na mapambano dhidi ya wanamgambo nchini Msumbiji

    Zaidi ya watu 800,000 wamekimbia makazi yao nchini Msumbiji kutokana na ghasia za wanajihadi zilizoanza mwaka 2017.
    Image caption: Zaidi ya watu 800,000 wamekimbia makazi yao nchini Msumbiji kutokana na ghasia za wanajihadi zilizoanza mwaka 2017.

    Wanajeshi wa Rwanda wanatarajiwa kuendeleza mapambano dhidi ya wanamgambo wa Kiislamu nchini Msumbiji, kufuatia makubaliano kati ya nchi hizo mbili kuongeza muda kuhudumu wa kikosi hicho.

    Karibu wanajeshi 1,000 wa Rwanda walipelekwa nchini humo mwezi Julai mwaka jana wakati wapiganaji wa kijihadi walipofanya mashambulizi katika maeneo tofauti na kuteka miji katika mkoa wa kaskazini wa Cabo Delgado.

    Hatua hiyo ilipata mafanikio kwa kiwango fulani dhidi ya wanamgambo hao lakini mashambulizi na utekaji nyara wa mara kwa mara unafanyika, waandishi wa habari wanasema.

    Mateka 30 waliokolewa wiki hii katika wilaya ya Nangade, mamlaka za Msumbiji zinasema, ufanisi huo ulifikiwa kufuatia oparesheni ya pamoja ya wanajeshi kutoka mataifa mengine ya Kusini mwa Afrika.

    Msumbiji: Je, Cabo Delgado ni kituo cha wapiganaji wa Islamic State?

    Cabo Delgado: Uhusiano uliopo kati ya mali asili,uasi na mapigano nchini Msumbiji

  4. Afcon 2021: Je unashaibiki timu gani kati ya Nigeria na Misri?

    Wachezaji wa Nigeriana Misri

    Kikosi cha Augustine Eguavoen cha Super Eagles kina matumaini kuanza mchakato wa kulisaka taji lao la nne kwa kupitia ushindi dhidi ya Wamisri hii leo.

    Mechi hiyo kati ya mibabe hiyo ya Afrika imevutia hamu miongoni mwa mashabiki kote duniani.

    Mechi hiyo ya Jumanne itakuwa ya tisa kati ya nchi hizo mbili katika kombe hilo la Afrika, huku Nigeria ikipigiwa upatu kuibuka washindi baada ya kuwalaza Pharaoh mara tatu licha ya kwamba Wamisri hao walipata ushindi wa 3-1 dhidi ya mabingwa hao wa Afrika magharibi nchini Angola 2010.

    Kikosi cha Kocha Carlos Quiroz kinapigiwa upatu kuibuka mshindi katika kundi hili kwasababu hawajafungwa katika mechi 16 wakiibuka washindi mara 12 na kupata sare nne.

    Huku Pharaoh wakiwategemea Mo Salah na wachezaji kama vile Mohammed El Neni kutoka Arsenal, Kikosi cha Nigeria hakina nguvu kwasababu wachezaji kama vile Peter Etebo, Victor Osimhen, Paul Onuachu na Odion Ighalo hawapo kutokana na sababu mbalimbali.

    Hatahivyo The Super Eagles wana wachezaji mahiri kama vile Iheanacho anayechezea klabu ya Lecester nchini Uingereza na Ahmed Musa katika safu ya mashambulizi.

    Yote unayofaa kujua kuhusu mechi za Afcon 2021

  5. Picha ya ajabu ya kijiko kilichounda kundi la ndege

    ALBERT KESHET

    Mpiga picha wa Kiisraeli alipata picha ya kipekee wakati kundi la ndege lilipounda muonekano unaofanana na kijiko kilicho na sukari.

    Udanganyifu huo ulifanyika wakati maelfu ya ndege walikusanyika na kushuka kama kikundi.

    Albert Keshet alionesha wakati ambapo wanaonekana kama kijiko kimepindika, na kuichapisha kwenye mitandao yake ya kijamii na kusababisha mamia ya maoni wakistaajabu.

    Keshet alichukua picha hiyo kwenye safari yake ya asubuhi ya mapema kaskazini mwa Bonde la Yordani ili kupiga picha za ndege na mimea.

  6. Mshukiwa wa moto uliowaka bungeni Afrika Kusini anakabiliwa na shtaka la ugaidi

    m

    Mamlaka ya mashtaka nchini Afrika Kusini imeongeza shtaka la ugaidi dhidi ya mtu anayeshutumiwa kuchoma moto bunge la nchi hiyo wiki iliyopita.

    Mshukiwa huyo anafikishwa katika mahakama ya Cape Town kuomba aachiliwe kwa dhamana.

    Zandile Mafe amefikishwa mahakamani mara ya pili kufuatia kukamatwa kwake wiki moja iliyopita kwa tuhuma za kuchoma moto bunge.

    Awali alishtakiwa kwa makosa mawili ya kuchoma moto, kuvunja nyumba na wizi.

    Waendesha mashtaka wanadai Bw Mafe alipatikana na vifaa vya vilipuzi na wamemfungulia mashtaka chini ya sheria inayolenga kulinda miundo msingi muhimu nchini humo.

    Wakili wa Bw Mafe, Luvuyo Godla, anasema mteja wake anafanywa kuwa mbuzi wa kafara na anataka aachiliwe kwa dhamana.

    Shtaka la ziada la ugaidi linachukuliwa kuwa uhalifu wa Ratiba ya Sita nchini Afrika Kusini, mojawapo ya makosa makubwa zaidi, na huenda ombi la Bw Mafe la kuachiliwa kwa dhamana likakataliwa.

  7. Mwandishi aliyeko kizuizini Uganda afikishwa mahakamani

    Pen Pinter Prize

    Mwandishi wa Uganda anayetuhumiwa kutuma taarifa za kashfa kuhusu rais na mtoto wake wa kiume kwenye mtandao wa Twitter amefunguliwa mashtaka mahakamani, wiki kadhaa baada ya kukamatwa.

    Kakwenza Rukirabashaija alishtakiwa kwa makosa mawili ya mawasiliano ya kukera na amepelekwa gerezani hadi Januari 21, atakapofikishwa tena mahakamani.

    Wakili wake Eron Kiiza alisema mwandishi huyo alikuwa akichechemea, na aliiambia mahakama kuwa afya yake inadhoofika.

    Wakili huyo hapo awali alisema kuwa mteja wake aliteswa aliipokuwa kizuizini.

    Bw Rukirabashaija alikamatwa mwezi Disemba na wiki iliyopita, mahakama iliamuru aachiliwe bila masharti lakini mamlaka haikuzingatia agizo hilo.

    Siku ya Jumatatu, mahakama iliamuru awasilishwe mahakamani.

    Mashirika ya kutetea haki za binadamu na wanadiplomasia wamekuwa wakitaka Bw Rukirabashaija awasilishwe mahakamani au aachiliwe bila masharti.

    Mwandishi huyo ambaye alishinda tuzo ya PEN Printer International Writer of Courage mnamo 2021, kwa riwaya yake "The Graedy Barbarian" ambayo inaangazia ufisadi mkubwa katika nchi ya kubuni. Bw Rukirabashaija hapo awali alikuwa amekamatwa na kushutumiwa kwa kukiuka sheria za marufuku ya coronavirus na kukuza madhehebu. Wakati huo alisema kwamba alikuwa ameteswa.

  8. Maeneo mengi ya Kenya yakumbwa na tatizo kubwa la ukosefu wa umeme

    KWS

    Kampuni ya usambazaji umeme nchini Kenya Power , imetangaza kwamba kuanguka kwa minara inayodhibiti nyaya za kusambaza umeme kumesababisha ukosefu wa umeme katika maeneo mengi ya nchi kuanzia mapema leo.

    Wakenya kutoka maeneo mbalimbali ya Nairobi na viungani mwake wameripoti ukosefu wa umeme katika maeneo tofauti kuanzia leo alfajiri.

    Tatizo hilo limeathiri biashara zinazotegemea umeme ikiwemo maduka ya kuchomelea vyuma, yale ya wasusi na mengineyo.

    Kampuni ya Kenya power imesema kwamba hitilafu hiyo inatokana na kuanguka kwa minara inayodhibiti kituo cha nguvu za umeme cha Kiambere katika eneo la Embakasi kuanzia mwendo wa saa nne na dakika 45 asubuhi.

    Kituo hicho kinasafirisha umeme kutoka kituo cha Kiambere chenye megawati 168 ambacho ni mojawapo ya vituo vya umeme vya Seven Forks kilichopo Tana River.

    ‘’Tumepoteza umeme kutokana na kuanguka kwa minara katika kituo cha Kiambere kilichopo Embakasi mwendo wa saa nne na dakika 45 asubuhi’’, ilisema Kenya Power katika taarifa yake. ‘’Wahandisi wetu wanajaribu kila njia kurudisha umeme huku marekebisho yakifanywa . Tutawaelelzea wakati wa kurudi kwa umeme hivi karibuni’’, ilisema.

  9. Korea Kaskazini yarusha kombora la pili linaloshukiwa kuepo siku sita

    m

    Korea Kaskazini imerusha kombora linaloshukiwa kuwa la balistiki, chini ya wiki moja baada ya kurusha kile ilichodai kuwa ni kombora la hypersonic.

    Korea Kusini ilisema iligundua uzinduzi huo saa 07:27 muda wa nchini humo, siku ya Jumanne.

    Walinzi wa pwani ya Japan pia waliripoti uzinduzi huo, wakisema Korea Kaskazini ilirusha "kitu kama kombora la balestiki".

    Hatua hii inakuja muda mfupi baada ya nchi sita kutoa taarifa ya kuitaka Korea kaskazini kusitisha "vitendo vyake".

    "Jeshi letu liligundua kombora linaloshukiwa kuwa la balestiki lililorushwa na Korea Kaskazini kutoka nchi kavu kuelekea Bahari ya Mashariki,"

    Mkuu wa Majeshi wa Korea Kusini (JCS) alisema, kuwa mamlaka za kijasusi kutoka Korea Kusini na Marekani ziko katika harakati za kufanya uchambuzi wa kina.

    Uzinduzi wa hivi karibuni unasisitiza ahadi ya kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un ya kuimarisha ulinzi wa nchi hiyo kama sehemu ya vipaumbele vyake vya sera kwa mwaka 2022, ambavyo viliainishwa wakati wa mkutano muhimu mwezi Disemba.

    Siku ya Jumatatu, ujumbe wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, ukiungana na Ufaransa, Jamhuri ya Ireland, Japan, Uingereza, na Albania, ulitoa taarifa ya pamoja kulaani jaribio la wazi la wiki iliyopita.

    "Hatua hizi zinaongeza hatari ya kuenea na kusababisha tishio kubwa kwa utulivu wa kikanda," balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Linda Thomas-Greenfield alisema.

    Kundi hilo liliitaka Korea Kaskazini "kujiepusha na vitendo vya kudhoofisha zaidi na kushiriki katika mazungumzo yenye maana kuelekea lengo letu la pamoja la kukomesha kabisa nyuklia."

  10. Mwanaume mmoja akamatwa kwa kuanzisha programu ya kuuza wanawake wa kiislamu mtandaoni

    m

    Polisi nchini India wamemkamata mwanaume anayeshukiwa kuunda programu iliyokuwa na picha za wanawake zaidi ya 80 wa Kiislamu kwa ajili ya "kuuzwa" mtandaoni mwaka jana.

    Programu hiyo - inayoitwa Solly Deals - iliundwa na getub mnamo Julai 2021.

    Msichana huyo mwenye umri wa miaka 25 alikamatwa siku chache baada ya programu inayofanana na Polly Pay, iliweka picha zaidi ya wanawake 100 wa Kiislamu.

    Wanafunzi wanne waliohusika katika kuunda programu ya pili pia walikamatwa.

    Katika matukio yote mawili, hakuna mauzo halisi yaliyofanyika, lakini lengo lilikuwa ni kuwadhalilisha wanawake wa Kiislamu nchini India.

    Wanawake wengi wa Kiislamu nchini India walikuwa wamezungumza hadharani kuhusu kuongezeka kwa wimbi la utaifa wa Kihindu chini ya Waziri Mkuu Narendra Modi.

  11. Kesi dhidi ya Bobi Wine yafutwa

    m

    Mwendesha mashtaka wa umma nchini Uganda ameondoa kesi dhidi ya kiongozi wa upinzani Robert Kyagulanyi almaarufu Bobi Wine.

    Mwanasiasa huyo alikuwa ameshutumiwa kwa kutoa maelezo ya uongo kuhusu umri wake alipokuwa akisajiliwa kupata diploma katika Chuo Kikuu cha Makerere.

    Bobi Wine hapo awali aliwahi kutiliwa shaka vyeti vyake vya kitaaluma.

    Aligombea dhidi ya Rais wa muda mrefu wa Uganda Yoweri Museveni katika uchaguzi wa mwaka jana na kulalamikia udanganyifu. Bobi Wine ni mkosoaji mkali wa rais.

  12. Watu 14 wafariki katika ajali Simiyu,Tanzania

    th

    Takriban watu 14 wakiwemo waandishi sita wa habari wamefariki dunia katika ajali mbaya ya barabarani iliyohusisha msafara wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza eneo la Chumbe Wilayani Busega Mkoani Simiyu.

    Mkuu wa Wilaya ya Busega (DC) Gabriel Zakaria alithibitisha kwa BBC kuhusu vifo hivyo akisema sita kati ya waliofariki ni waandishi wa habari, madereva wawili na raia wengine sita waliokuwa kwenye basi dogo.

    Alisema jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo iliyojeruhi watu wengine wawili ambao wamelazwa katika hospitali ya Rufaa ya Bugando mkoani Mwanza akiwemo mwandishi mmoja wa habari.

    “Tunasikitika sana kuwapoteza ndugu zetu katika ajali hiyo, tukiwa tunajiandaa kuona wamelazwa, pia tunasubiri kuona nini chanzo cha ajali,” alisema Zakaria.

    Rais Samia Suluhu ameeleza kushtushwa na taarifa za vifo hivyo huku akizipa pole familia za wafiwa .Rais kupitia ujumbe aliouweka kwenye ukurasa wake wa Twitter pia amewatakia ahueni ya haraka majeruhi wa ajali hiyo .

    View more on twitter
  13. Kambi ya wakimbizi ya Mtendeli yafungwa

    Video content

    Video caption: Kambi ya wakimbizi ya Mtendeli yafungwa

    Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa linalosimamia Wakimbizi nchini Tanzania zimefunga kambi ya wakimbizi ya Mtendeli.

    Kwa mujibu wa mamlaka hizo zinasema ni kutokana na ongezeko la kiwango cha wakimbizi wanaoamua kurejea kwao kwa hiari hivyo wamechukua hatua hizo ili kutoa huduma kwa ufasaha kwa kuwaunganisha wakimbizi wachache waliosalia katika kambi moja.

    Zaidi ya wakimbizi elfu moja kutoka Burundi hurejeshwa nchini mwao kila wiki. Humphrey Mgonja alitembelea kambi hiyo iliyofungwa Mkoani kigoma na kuandaa taarifa hii.

  14. Panya maarufu wa Tanzania wa kutegua mabomu na vilipuzi Magawa afariki

    th

    Panya shujaa wa Tanzania aliyetumika kutafuta na kutegua mabomu ya ardhini ardhini na vilipuzi -Magawa amefariki dunia mwishoni mwa wiki .

    Kupitia taarifa katika ukurasa wake wa instagran ,shirika la Apopo limesema Magawa alikuwa na afya njema wiki jana lakini afya yake ilianza kudhoofika mwishoni mwa wiki na kuaga dunia akiwa na umri wa miaka minane .

    View more on instagram

    Panya huyo alisifika sana kwa kusaidia kugunduliwa kwa Zaidi ya mabomu 100 ya kutegwa ardhini nchini Cambodia .

    ‘Mchango wake unaruhusu jamii nchini Cambodia kuishi, kufanya kazi na kucheza; bila hofu ya kupoteza maisha au kiungo. Mnamo Septemba 2020, alikabidhiwa rasmi Medali ya Dhahabu ya PDSA - tuzo ya juu zaidi ya ushujaa ambayo mnyama anaweza kupokea. Mwaka jana wakati Magawa alipostaafu, HeroRAT Ronin alichukua kijiti kama panya mpya wa kuasili.’ Imesema sehemu ya taarifa iliyotangaza kifo cha panya huyo .

  15. Kenya yasitisha safari zote za ndege za abiria kutoka Dubai

    th

    Kenya imesitisha safari zote za ndege za abiria zinazoingia na kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ili kulipiza kisasi hatua ya Dubai ya kupiga marufuku safari zote za ndege za abiria kutoka Kenya kutokana na vipimo bandia ya Covid-19.

    Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini (KCAA) Gilbert Kibe ameliambia gazeti la The EastAfrican siku ya Jumanne kwamba kusimamishwa huko kulianza Jumatatu usiku wa manane kwa muda wa siku saba.

    Marufuku hiyo hata hivyo haiathiri safari za ndege za mizigo ambazo kwa kawaida husafirishwa na wachukuzi kama vile Kenya Airways na shirika la ndege la Emirates kutoka UEA hadi Kenya.

    "Safari za ndege za abiria za ndani na nje kutoka UAE zimesitishwa kwa muda wa siku saba. Tunafanya hivi ili kujibu marufuku ya safari za ndege za abiria za Kenya kuelekea UAE," alisema Bw Kibe Jumanne.

    Marufuku hiyo inajiri siku chache tu baada ya UAE kuongeza muda wa marufuku ya safari za ndege nchini Kenya baada ya kubaini kuwa wasafiri kutoka Nairobi walipimwa na kukutwa na Covid-19 baada ya kuwasili katika taifa hilo la Mashariki ya Kati, licha ya kuwa na matokeo yaliyoonyesha kwamba hawakuwa na virusi vya Covid .

    Virusi vya Corina: UAE yasitisha safari za ndege kutoka Kenya, Tanzania, Ethiopia na Nigeria

    Safari za ndege kutoka Nairobi hadi Dubai zasitishwa

  16. Biden aelezea wasiwasi juu ya vifo vya raia nchini Ethiopia

    th

    Rais wa Marekani Joe Biden ameelezea wasiwasi wake kuhusu vifo vya raia vilivyosababishwa na mashambulizi ya anga ya hivi majuzi nchini Ethiopia wakati alipozungumza na Waziri Mkuu Abiy Ahmed.

    Hii inafuatia ripoti kwamba zaidi ya watu 50 waliokimbia makazi yao waliuawa katika shambulio la anga kaskazini-magharibi mwa Tigray siku ya Ijumaa.

    Taarifa ya Ikulu ya Marekani imesema rais wa Marekani alikaribisha kuachiliwa kwa viongozi wa upinzani na kuahidi uungaji mkono katika kutafuta kumalizika kwa vita kwa njia ya amani na waasi wa Tigray

    Uhusiano haujakuwa mzuri kati ya Washington na Addis Ababa ambapo serikali imekuwa ikisikitishwa na ukosoaji wa mara kwa mara wa ukiukwaji wa haki za binadamu wakati wa vita na waasi wa Tigray.

    Hatua ya Bw Biden na Bw Abiy kufanya mazungumzo ya simu hata kidogo ni ishara ya maendeleo.

    Taarifa ya Ikulu ya Marekani inasema viongozi hao wawili walijadili njia za kuharakisha mazungumzo kuelekea usitishaji mapigano .

    Pia inasema kuachiliwa kwa viongozi wa upinzani hivi majuzi ilikuwa hatua nzuri. Lakini suala la ukatili liliibuliwa tena.

    Mzozo wa Tigray Ethiopia: Ripoti yasema uhalifu wa kivita huenda ulifanyika

    Mzozo wa Tigray: Kufufuka kwa uasi kunamaanisha nini kwa Waziri Mkuu wa Ethiopia?

  17. Milionea muuaji Robert Durst afariki gerezani

    th

    Milionea aliyepatikana na hatia ya mauaji Robert Durst amefariki gerezani akiwa na umri wa miaka 78, kulingana na wakili wake.

    Durst alikufa akiwa mfungwa wa California baada ya kukiri hatia mnamo Septemba ya kumuua rafiki yake Susan Berman.

    Alimuua ili kumzuia kuzungumza na polisi kuhusu kutoweka kwa mkewe. Polisi wanaamini kuwa aliwaua watu wengine wawili.

    Tajiri huyo aliyemiliki mali isiyohamishika kama vile majengo aligeuka kuwa mtoro na bila kujua alikiri katika makala ya mfululizo ya HBO kuhusu kujihusu na mauaji aliyoyatekeleza

    Wakili wa Durst, Chip Lewis, alithibitisha kwamba alifariki katika Hospitali Kuu ya San Joaquin akiwa chini ya ulinzi wa Idara ya Marekebisho ya California.

    Alisema kifo chake kilitokana na "sababu za asili" na kwamba amekuwa akisumbuliwa na masuala mengi ya kiafya .

    Durst alihukumiwa kifungo cha maisha jela mwezi Oktoba kwa mauaji ya Berman mwaka 2000, ambaye alikuwa msiri wake wa muda mrefu na msemaji wake.

    Kesi yake ilikuwa imecheleweshwa kwa zaidi ya mwaka mmoja kutokana na janga la Covid. Siku mbili baada ya hukumu yake alilazwa hospitalini akiwa na Covid na kuwekwa kwenye mashine ya kupumua, kulingana na wakili wake .

    Durst - ambaye familia yake inamiliki msururu wa majengo marefu ya Jiji la New York, ikiwa ni pamoja na uwekezaji katika World Trade Center- alichunguzwa baada ya rekodi yake akikiri kutumika katika mfululizo wa makala ya 2015 ya HBO The Jinx.

  18. Mfahamu refa wa kwanza mwanamke katika mashindano ya Afcon

    Salima Mukansanga ameweka historia kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka huu nchini Cameroon, kwa kuwa mwamuzi wa kwanza mwanamke kwenye mashindano ya wanaume.

    Mnyarwanda huyo mwenye umri wa miaka 33 alisimamia mchuano wa Afcon siku ya Jumatatu.

    View more on twitter

    Huko nyuma ameongoza mechi za Kombe la Dunia la Fifa kwa Wanawake, Olimpiki ya Tokyo 2020, Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake na Ligi ya Mabingwa ya Wanawake ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf) - pamoja na kusimamia michuano ya timu za juu za wanaume nchini mwake.

    Vyombo vya habari vya Rwanda vinaripoti kuwa akiwa kijana Bi Mukansanga alikuwa na ndoto ya kuwa mchezaji wa mpira wa vikapu kitaaluma, lakini akachagua kuwa mwamuzi wa soka miaka 15 iliyopita.

    Yote unayofaa kujua kuhusu mechi za Afcon 2021

  19. Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja hii leo Jumanne tarehe 11 Januari 2022