Idriss Deby: Upinzani walaani mapinduzi ya ‘kifamilia’ Chad

Mahamat Idriss Déby Itno, one of the late president's sons, is a 37-year-old four-star general

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Mahamat Idriss Déby Itno mwanae Deby sasa ndiye kiongozi wa Chad

Vyama vikuu vya upinzani nchini Chad vinasema uteuzi wa mtoto wa aliyekuwa rais wa taifa hilo Idris Deby ,Mahamat Deby kama kiongozi wa taifa hilo ni "mapinduzi ya kitaasisi".

Déby, 68 - ambaye alikuwa mamlakani kwa miongo mitatu - alikufa baada ya kupigwa risasi wakati akipambana na waasi kwenye mstari wa mbele vitani

Waasi pia wamepinga hatua hiyo, wakisema: "Chad sio ufalme."

Mahamat Idriss Déby Itno, anayejulikana pia kama "Jenerali Kaka", alikuwa msimamizi wa walinzi wa rais na anaongoza nchi kwa miezi 18 hadi uchaguzi.

Serikali na bunge vimevunjwa, lakini wataalam wa katiba wanasema spika wa bunge anapaswa kuchukua nafasi wakati rais aliye madarakani anapofariki kabla ya kuandaa uchaguzi.

Kifo cha Déby kilitangazwa kwenye Televisheni ya serikali Jumanne - siku moja baada ya matokeo ya uchaguzi wa muda kukadiriwa atashinda muhula wa sita ofisini kwa uongozi wa nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta ambayo imekuwa mstari wa mbele katika juhudi za kikanda za kupigana na wanamgambo wa Kiislamu.

Kuna hofu kwamba kifo hicho kinaweza kusababisha kukosekana kwa utulivu wa kisiasa katika nchi kubwa yenye ukame na historia ndefu ya uasi na majaribio ya mapinduzi na ambapo upinzani ni dhaifu na umegawanyika.

Borders have reopened and an overnight curfew has been shortened from 20:00 until 05:00, but security is still tight in the capital

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Usalama bado umeimarishwa katika mji mkuu N'Djamena

Muungano wa vyama vya wafanyikazi umejiunga na upinzani kukataa kuanzishwa kwa Baraza la mpito la jeshi, wakitaka mazungumzo na wafanyikazi wakae nyumbani hadi hapo mwafaka utakapopatikana .

Watu bado wanashtuka nchini humo kufuatia kifo cha Rais Déby - hata wale waliompinga wanashangaa. Idadi kubwa watu iko chini ya umri wa miaka 30 na hawajawahi kujua rais mwingine yeyote.

Katikati ya vipindi, Televisheni ya serikali inacheza nyimbo za maombolezo ya kidini. Ingawa wengine wanaweza kuhisi kuwa ni vizuri kwamba nguvu ya Déby haipo tena, kuna hali ya huzuni kwamba ameenda kwa njia hii.

"Sifurahishwi na jinsi Idris Déby alivyokufa, sio hivyo tulivyotamani kwake, lakini tulitaka aondoke madarakani. Alitufanya tupitie mateso sana, hakuna haki za wanawake nchini Chad. Mpaka leo hakutufanyia chochote, "mwanamke mmoja aliiambia BBC Afrique.

Mtu mwingine alikubali: "Hakuna mtu anayetaka kifo cha mtu maishani, ni mshtuko, lakini tulihitaji mabadiliko. Kwa mabadiliko hatukumaanisha mwanawe au jeshi lolote."

Waasi pia wanazingatia mila ya jadi ya kuomboleza, wakisema wamesitisha harakati zao kusonga mbele kusini hadi baada ya kuzikwa kwa Déby Ijumaa.

Mahamat Idriss Déby Itno ni nani?

Jenerali Mahamat alihudumu kama kiongozi wa kikosi cha ulinzi cha rais kama mkurugenzi mkuu wa huduma ya usalama katika taasisi za serikali (DGSSIE) tangu 2014.

Mwaka 2013 alichaguliwa kuwa kiongozi wa jeshi la Chad nchini Mali , ambapo alishiriki katika operesheni pamoja na vikosi vya Ufaransa kabla ya kurudi nyumbani kusimamia DGSSIE.

Alikuwa pamoja na babake alipojeruhiwa katika vita dhidi ya waasi katika mkoa wa magharibi wa Kanem.

Mahamat, ambaye pia anajulikana kama "Jenerali Kaka", ana sifa ya kuishi Maisha ya siri ikilinganishwa na nduguze wa kambo . Hata hivyo ni mwanajeshi jasiri sawa na alivyokuwa baba yake.

"Rais wa taifa hilo [Idriss Deby] aliweka mawasiliano ya [Mahamat] na watu maarufu wa Chad pamoja na maafisa wakuu wa jeshi kutoka kwa mataifa yalio na uhusiano mzuri na taifa hilo. Ilikuwa njia yake ya kumfunza jinsi kuchukua madaraka, gazeti la Jeune Afrique liliripoti.

Je, Rais Deby alikuwa anafanya nini mstari wa mbele vitani?

Japo baadhi ya watu wanasema ni jambo lilisilo la kawaida kwa Rais kuwa mstari wa mbele vitani, mwandishi wa BBC Beverly Ochieng anaripoti kuwa Rais Idriss Déby alikuwa mwanajeshi wa cheo cha juu cha field marshal na ilikuwa ni jambo la kawaida kwake kuwa mstari wa mbele na wanajeshi wake.

Over the weekend, Chad's soldiers were involved in fierce clashes with the rebels in the north

Chanzo cha picha, Getty Images

Takribani mwaka mmoja uliopita, Déby aliongoza operesheni ya kijeshi akiwa mstari wa mbele na inaripotiwa wanamgambo 1,000 wa Boko Haram waliuawa katika mapambano hayo.

Alipokea mafunzo ya kijeshi nchini Ufaransa na kufuzu kama rubani wa ndege vita.

Déby alikuwa afisa wa jeshi wa cheo cha juu aliporatibu mapinduzi yaliyomng'oa madarakani rais Hissène Habré mwaka 1990. Toka hapo Deby akachukua hatamu za uongozi mpaka umauti ulipomkuta, akiwa vitani.