Raila Odinga: John Pombe Magufuli niliyemjua

Raila Odinga akiwa na Magufuli na mke wake

Chanzo cha picha, Raila Odinga/TWITTER

Kiongozi wa chama cha ODM nchini Kenya Raila Odinga ameandika ujumbe mrefu wa salamu za rambirambi akimbukumba rafiki yake Hayati John Pombe Magufuli.

Amesimulia jinsi alivyopokea habari za kifo cha Magufuli na alivyojaribu kuwasiliana naye wakati uvumi ulipoanza kuzuka kuhusu hali ya Magufuli.

''Wakati uvumi ulipoanza kuzunguka juu ya afya na mahali alipo rafiki yangu Rais John Pombe Magufuli, nilimpigia simu kadhaa.

Baadaye, nilimtumia ujumbe mfupi, zote hazikujibiwa.

Wakati kifo chake kilipodhibitishwa nilikuwa nikijitenga baada ya kupimwa na kupatikana na Covid-19, nilihisi uzito kamili wa msiba.... Ulikuwa ni urafiki uliyojengwa juu ya vita dhidi ya ufisadi na miundombinu bora.

Nilikutana na Dkt Magufuli kwa mara ya kwanza kwenye mkutano wa kimataifa kuhusu miundombinu huko Durban, Afrika Kusini mnamo 2003 wakati wa Serikali ya Muungano wa (Narc) ya Rais Mwai Kibaki.

Wakati huo, Dkt. Magufuli alikuwa ameshikilia nafasi kama hiyo kwa muda nchini Tanzania.

Wizarani, niligundua kwamba nilikuwa nimerithi matatizo makubwa kuliko nilifikiria. Wizara hiyo ilikuwa imejaa ufisadi mkubwa'', ameandika Raila.

Odinga amesimulia jinsi Magufuli alivyompa ushauri kuhusu nia mbalimbali anazoweza kuzitumia ili kupambana na ufisadi katika wizara yake.

''Kisha alinishauri kwamba tuchukue mfumo wa kubuni na kujenga barabara kwa wakati mmoja tofauti na kubuni barabara nzima kwanza, kisha kutoa zabuni na baadaye kuijenga. Hiyo pia, ilikuwa njia ya rushwa.

Ushauri wake ulikuwa kwamba sehemu za barabara ambazo zilikuwa zimebuniwa zinaweza kutolewa na ujenzi ukaanza wakati muundo wa sehemu zingine ukiendelea.

Kwa njia hiyo, tutapata barabara zenye ubora haraka na kwa bei rahisi. Ilikuwa imefaulu nchini mwake na alitaka tuijaribu''.

''Kuanzia hapo, urafiki wetu ulianza. Tulikuwa washauri wa kila mmoja na washirika katika vita dhidi ya ufisadi na wakandarasi walaghai katika sekta ya barabara.

Kabla ya mkutano kumalizika, Dk Magufuli aliniuliza niwalete wahandisi wangu kwenye wizara kwa mkutano na wahandisi wake huko Dar-es-Salaam ili kubadilishana maoni juu ya jinsi ya kutoa miundombinu bora kwa gharama za thamani ya pesa.

Mara moja nilimwagiza Katibu wa kudumu wangu Erastus Mwongera kulikusanya kundi yetu.

Katika Jiji la Dar es Salaam, tulikuwa na majadiliano mengi juu ya njia rahisi, za haraka na nzuri za kuboresha miundombinu''.

Raila Odinga na Magufuli

Chanzo cha picha, Raila Odinga/Twitter

Odinga katika salamu zake za rambirambi alikumbuka safari aliyoifanya nyumbani kwake Magufuli huko Chato.

'Wakati huo, tulimtembelea nyumbani kwake Chato. Nilimwalika pia atutembelee Kisumu na Bondo.

Tuliporejea kufanya kazi hapa Kenya, tuligundua Barabara Kuu ya Meru-Maua kama moja ya barabara muhimu ambazo zilihitaji ukarabati wa haraka na mkubwa.

Nilimwalika Dkt. Magufuli kuzindua ujenzi wa barabara hii, ambayo alifanya.

Niliamuru pia wizara kuiita barabara hiyo jina lake.

Kama Waziri Mkuu katika Serikali ya Muungano Mkuu, nilimtembelea na ujumbe ambao ulikuwa na Seneta James Orengo na Magavana Sospeter Ojaamong na Josephat Nanok miongoni mwa wengine. Katika safari hii, nilizindua ujenzi wa Chuo Kikuu cha Mwanza.

Wakati tunajiandaa kwa uchaguzi wa 2012, Dk Magufuli alikaidi itifaki na kusimama nasi, akihudhuria Mkutano wa Kitaifa wa Wajumbe wa chama chetu ambapo nilikabidhiwa tiketi ya chama kuwania urais. Kufikia wakati huu, tulikuwa washauri wa kila mmoja.'

Odinga aliendelea kusimulia uhusiano wa karibu wa kisiasa kati yake na Magufuli akieleza walivyokuwa wakishirikiana kwa kushauriana kuhusu masuala mbalimbali.

'Wakati Dkt. Magufuli alipotangaza nia yake kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya urais mnamo 2015, nilivutiwa sana kwa sababu mashindano yake yalikuwa mashindano yangu, kama yangu tu yalikuwa yake pia. Tulijihusisha sana na tulifurahi aliposhinda.

Alinialika Dar mara tu baada ya kuapishwa.

Wakati wa ziara hiyo, rais huyo mpya alikuwa wazi, Alisema alikuwa anajua jinsi ya kuendesha wizara; sasa alihitaji ushauri juu ya jinsi ya kuendesha serikali.'

Kando kumsifia jinsi alivyoendesha masuala ya Tanzania kama rais Odinga pia amemtaja Hayati Magufuli kama mtetezi wa bara la Afrika.

'Nje ya Tanzania, shughuli yake nyingine ilikuwa Afrika. Hakuwa na haja na mabara mengine.

Hata barani Afrika, alikuwa akichagua nchi za kuzuru .

Nakumbuka alitembelea Kenya, Ethiopia, Nigeria, Afrika Kusini, Uganda, Rwanda, Burundi na DRC. Vinginevyo, alikuwa Mtanzania aliyejishughulisha na Tanzania'.