AKA: Rapa wa Afrika Kusini aliyeuawa 'alitazamiwa kuafikia makubwa'

AKA

Chanzo cha picha, AFP

Katika wimbo wa ufunguzi wa albamu yake ya solo ya mwaka wa 2011 Altar Ego, AKA alisema "hakuwahi kupanga… hakutaka kuwa mtu mashuhuri".

Lakini msanii huyo wa Afrika Kusini, ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi mjini Durban wiki moja iliyopita, hakusita kuhusu talanta yake.

Siku chache kabla ya kifo chake, ambacho polisi wanaamini kilikuwa mauaji yaliyopangwa, rapper huyo mwenye umri wa miaka 35, aliyeshinda tuzo, alijisifia kuwa mtayarishaji bora wa aina yake.

Msanii huyo ambaye pia alifahamika kwa jina la utani la Supa Mega, alitweet: "Kwa takwimu, kwa kuwa nimetayarisha 90% ya muziki wangu wote, hakika mimi ndiye mtayarishaji mkubwa wa hip-hop kuwahi kutokea Afrika Kusini."

Lakini mnamo 2014, kwenye wimbo Congratulate, moja ya vibao vilivyoimarisha hadhi yake ya megastar, alisema "angeangaza kama almasi ambayo ni ya milele, sasa nipongeze".

Maelfu ya mashabiki - wanaojulikana kwa pamoja kama "The Megacy" - wanatarajiwa kufuatilia mtandaoni au kujitokeza kuhudhuria hafla kumuaga hadharani siku ya Ijumaa mjini Johannesburg, kuhakikisha kwamba ataendelea kung'aa.

Huenda alisema kuwa hakutaka lakini bila shaka alipata hadhi hiyo ya mtu mashuhuri.

Lakini, maisha na kazi yake yalikumbwa na ubishi.

SA

Chanzo cha picha, Getty Images

Kiernan Forbes maarufu AKA, alizaliwa Cape Town mwaka1988, alikuwa mmoja wa wasanii wa hip-hop waliopendwa sana nchini Afrika Kusini baada ya kutoa albamu tatu za solo, na zingine kupitia ushirikiano na wasanii wengine.

Alipokuwa mdogo aliishi na babu na yake huko Mitchells Plain, mojawapo ya vitongoji hatari zaidi vya Cape Town, vinavyojulikana kwa ujambazi na matumizi mabaya ya dawa za kulevya.

Lakini baadaye alihamia Johannesburg na mama yake, ambako alisoma Chuo cha St John, taasisi ya Kianglikana ambayo inajieleza kuwa "miongoni mwa shule mashuhuri za Afrika Kusini".

Hapo ndipo kazi yake ya muziki ilipoanzia, akianzisha bendi ya hip-hop iitwayo Entity akiwa na marafiki zake wawili wa shule ya upili, Sizwe Mpofu-Walsh na Nhlanhla Makena. Waliendelea na hata wakati mmoja kuteuliwa kuwania tuzo ya KORA All Africa Music Award.

"Alitazamiwa kuwa nyota kutoka wakati huo," Mpofu-Walsh, ambaye sasa ni mwandishi na msomi, alisema katika kumbukumbu yake kwenye Twitter.

Baada ya kundi hilo kusambaratika, AKA aliendelea na masomo ya uhandisi wa sauti kisha akatayarisha vibao vya wasanii wakiwemo ProKid na Kuli Chana.

Baadaye alifanya kazi na nyota wa Nigeria wa Afrobeat Burna Boy, pamoja na Da L.E.S, Nasty C na Kwesta.

Idadi kubwa ya wanamuziki, watayarishaji, wanasiasa na watu mashuhuri ambao wametoa rambirambi zao ni ishara ya jinsi kazi yake ilivyotambulika.

Lakini katika miaka mitano iliyopita, uchunguzi juu ya maisha yake ya kibinafsi uliibuka, na habari kuhusu mapenzi yake na talaka za umma zikigonga vichwa vya habari magazetini.

Alichumbiana na watu mashuhuri akiwemo DJ Zinhle, ambaye alizaa naye mtoto wa kike, ambaye sasa ana umri wa miaka saba.

AKA, aliyepigwa picha hapa 2018, alikuwa na binti mmoja kutoka kwa uhusiano na DJ Zinhle

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, AKA, akiwa alikuwa na binti yake aliyemzaa na DJ Zinhle

Pia hakukwepa malumbano ya hadharani na wafanyakazi wenzake wa tasnia hiyo, akiwemo rapa mwenzake wa Afrika Kusini Cassper Nyovest na Burna Boy wa Nigeria.

Wakati wa ghasia za chuki dhidi ya wageni nchini Afrika Kusini mwaka wa 2019, AKA alianza ugomvi na Mnigeria huyo baada ya msanii huyo wa Afrika Magharibi kuwataka wahamiaji weusi nchini Afrika Kusini kujilinda dhidi ya mashambulizi.

Mnamo 2021, kashfa zinazomzunguka rapa huyo zilichukua mkondo mbaya wakati mchumba wake Anele Tembe mwenye umri wa miaka 22 alipofariki katika mazingira ya kutatanisha- alianguka kutoka ghorofa ya 10 ya hoteli ya Cape Town.

Iliaminika kwamba alijitoa uhai. Lakini katika mazishi yake, baba yake, mfanyabiashara maarufu Moses Tembe, alikanusha hilo na kusema binti yake hakutaka kujiua.

Kwa heshima yake, AKA alitoa wimbo wa Tears Run Dry kama ukumbusho wa uhusiano wao.

Lakini mwenendo tofauti wa mwanamuziki huyo uliibuka baada ya kifo cha mwanamitindo huyo, wakati video zilivuja kwenye mitandao ya kijamii, zikionyesha ugomvi kati ya wanandoa hao, huku yeye akivunja milango katika mojawapo wa ugomvi wao.

Katika juhudi za kurejesha heshima yake iliyoathirika vibaya wiki chache baada ya kifo cha mchumba wake, AKA alikana kuwahi kuwa mnyanyasaji. Katika hatua iliyoonekana kama kumuondoa hatiani, waendesha mashtaka wa Afrika Kusini waliamua kutoendelea na kesi dhidi yake.

Baadhi ya watu wa karibu wa AKA walisema kuwa kifo cha Tembe kilimbadilisha akiwemo msanii wa kurekodi na mshindi wa tuzo kutoka Afrika Kusini DJ Oscar Mdlongwa maarufu kwa jina la Oskido.

"Alipoondoka kwenye ulimwengu huu, alikuwa Kiernan aliyebadilika, tuligundua hakuwa Kiernan tuliyemfahamu miaka 10 iliyopita," alisema baada ya kuitembelea familia hiyo kutoa heshima zake mapema wiki hii.

AKA mwenyewe alisema amebadilika.

'Aliuawa mchana kweupe'

Mamlaka inaamini kwamba mauaji yake nje ya mkahawa maarufu huko Durban Ijumaa jioni yalitekelezwa na mshambuliaji wa kulipwa.

Katika picha za CCTV, mwanamume aliyevalia sweta nyeupe na kofia anaonekana akivuka barabara na kuelekea kwa AKA na kisha kufyatua risasi mbili kichwani mwa rapa huyo na kumuua papo hapo. AKA aliuawa pamoja na rafiki yake wa muda mrefu Tebello "Tibz" Motsoane.

"AKA aliuawa mchana kweupe," alisema Waziri wa Uchukuzi Fikile Mbalula ambaye alitembelea familia hiyo Jumapili.

"Tunahitaji kupata undani wa kwa nini hii ilitokea, kwa sababu AKA hakuwa muuza madawa ya kulevya, alikuwa mwanamuziki, kwa nini anastahili kuuawa hivyo?" Aliuliza.

Katika wimbo huo wa ufunguzi wa albamu yake ya kwanza, AKA aliuliza: "Ni nini kingetokea kwa kijana wa kawaida ambaye alikuwa na kipaji cha ajabu?"

Miaka kumi na miwili baadaye swali hilo lilipata jibu la kuhuzunisha.