Got a TV Licence?

You need one to watch live TV on any channel or device, and BBC programmes on iPlayer. It’s the law.

Find out more
I don’t have a TV Licence.

Habari za moja kwa moja

time_stated_uk

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha taarifa zetu za leo .

  2. Israel na Hezbollah washambuliana kwenye mpaka wa Lebanon

    .

    Hezbollah imerusha msururu wa roketi kaskazini mwa Israel, na kuua mtu mmoja, kujibu mashambulio mabaya ya Israeli kwenye kijiji kimoja cha Lebanon.

    Duru za Lebanon zilisema watu saba waliuawa katika shambulio la Israeli usiku kucha huko Habbariyeh, na kuifanya kuwa moja ya mauaji mabaya zaidi katika ghasia za hivi karibuni.

    Israel ilisema wanamgambo waliuawa, akiwemo mmoja aliyehusika katika mashambulizi dhidi ya Israel.

    Kundi la Lebanon lililolengwa lilisema waliouawa walikuwa "waokoaji".

    Mashambulizi hayo yanakuja wakati ambapo kumekuwa na mashambulizi kutoka pande zote mbili karibu kila siku, ambayo yalianza baada ya vita vya Israel na Gaza kufuatia shambulio la Oktoba 7 la Hamas dhidi ya Israeli.

    Hezbollah ni kundi la wanamgambo wa Kishia wa Lebanon wenye uhusiano wa karibu na Iran na mshirika wa Hamas.

    Hezbollah ilirusha makumi ya roketi katika mji wa Kiryat Shmona wa Israel na kituo cha kijeshi siku ya Jumatano asubuhi.

    Huduma ya gari la wagonjwa ya Magen David Adom ya Israel ilisema mfanyakazi wa kiwanda alitolewa kutoka kwenye mabaki baada ya shambulio moja kugonga bustani ya viwanda na kusababisha moto.

    Alikuwa na majeraha mabaya na alitangazwa kuwa amefariki katika eneo la tukio, iliongeza.

    Hezbollah ilisema mashambulizi ya roketi yalikuwa "kujibu mauaji ya Habbariyeh".

  3. M-Pesa kuingia katika soko la Afrika Magharibi

    .

    Kampuni ya Safaricom kutoka Kenya inapanua huduma yake ya kutuma pesa kwa simu ya mkononi ya M-Pesa hadi Afrika Magharibi.

    Huduma hiyo ilipozinduliwa nchini Kenya mwaka wa 2007 ilileta mabadiliko makubwa katika huduma za benki na fedha nchini humo.

    Na sasa inaingia katika soko lenye watu wengi zaidi katika Afrika Magharibi.

    Kuna wateja wengi wapya wa pesa za kupitia simu katika eneo hili kuliko mahali pengine popote ulimwenguni, ripoti ya hivi majuzi ilisema.

    Nchini Nigeria, kwa mfano, chini ya nusu ya watu wazima wote wanasemekana kuwa na akaunti ya benki, kumaanisha wengi wanategemea huduma za pesa za simu kama vile Palmpay na Opay.

    Mipango ya M-Pesa ilitangazwa Jumatatu.

    Ni sehemu ya makubaliano na Access Holdings - kampuni mama ya benki kubwa zaidi barani Afrika, na kikundi cha usimamizi wa utajiri cha Nigeria kiitwacho Coronation Group.

    View more on twitter
  4. Wahamiaji kutoka Asia ya Kati mashakani baada ya shambulio la Moscow

    xx

    Ongezeko la vipigo, uharibifu na matukio ya ubaguzi wa rangi dhidi ya wahamiaji wa Asia ya Kati limeripotiwa nchini Urusi tangu mashambulizi ya dhidi ya Ukumbi wa Jiji la Crocus mjini Moscow Ijumaa iliyopita

    Raia wanne wa Tajikistan wameshtakiwa kwa kuwaua watu 139 katika shambulio hilo, linalodaiwa kutekelezwa na kundi la wanajihadi la Islamic State.

    Washukiwa wengine kadhaa wamekamatwa, wote wenye asili ya Asia ya Kati

    Ukiangazia kuongezeka kwa mvutano baada ya mauaji ya Moscow, ubalozi wa Tajikistan nchini Urusi mwishoni mwa juma uliwatahadharisha raia wake kutotoka nje ya nyumba zao isipokuwa kwa dharura.

    Wahamiaji wa Asia ya Kati ni sehemu kubwa ya idadi ya watu wanaofanya kazi nchini Urusi, haswa katika sekta ya mauzo ya rejareja, usafirishaji na ujenzi.

    Wengi tayari wanakabiliwa na viwango vya juu vya ubaguzi.

    Mwimbaji mzaliwa wa Tajik Manizha Sanghin, ambaye aliwakilisha Urusi kwenye Eurovision mnamo 2021, alilaani "ukatili wa wazi" wa shambulio la Moscow, lakini alionya juu ya "athari ambayo itawapata Watajikistan na wakazi wote wa Asia ya Kati".

    Sasa ni balozi mwema wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi.

    Maelezo zaidi:

  5. Wanne wahukumiwa kifo kwa mauaji ya mwanasiasa wa Tunisia Chokri Belaid

    Mauaji ya Chokri Belaid yalishtua Tunisia
    Image caption: Mauaji ya Chokri Belaid yalishtua Tunisia

    Mahakama nchini Tunisia imewahukumu watu wanne kifo na wengine wawili kifungo cha maisha jela kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya kiongozi mashuhuri wa kisiasa Chokri Belaid mwaka 2013.

    Alipatikana ameuawa kwa kupigwa risasi ndani ya gari lake katika mji mkuu, Tunis, na kusababisha vurugu.

    Mwanasiasa huyo wa mrengo wa kushoto alikuwa mkosoaji mkali wa chama tawala cha Kiislamu cha Ennahda.

    Alidai kuwa ilifumbia macho unyanyasaji unaofanywa na watu wenye itikadi kali dhidi ya watu wasiopenda dini.

    Ingawa Tunisia inatoa hukumu za kifo kwa uhalifu mbaya zaidi, hakuna hukumu ya kifo iliyotekelezwa tangu 1990.

    Badala yake, kwa kawaida hubadilishwa hadi kifungo cha maisha.

    Jumla ya watu 23 wamefunguliwa mashtaka kuhusiana na mauaji ya Belaid.

    "Haki imetendeka," Mwendesha Mashtaka Aymen Chtiba alisema akijibu hukumu hizo sita zilizotolewa Jumatano asubuhi.

    Uamuzi huo ulitangazwa moja kwa moja kwenye televisheni ya taifa baada ya masaa 15 ya kujadiliwa, linaripoti shirika la habari la AFP.

    Wanajihadi wenye utiifu kwa Islamic State walidai kuhusika na mauaji ya Belaid, pamoja na yale ya Mohamed Brahmi, kiongozi mwingine wa upinzani wa mrengo wa kushoto, miezi sita baadaye.

    Mauaji haya yalisababisha maandamano makubwa kutoka kwa Watunisia waliokasirishwa, miaka miwili baada ya vuguvugu la demokrasia la Arab Spring kuanza nchini humo na kuenea mahali pengine katika Mashariki ya Kati.

    Tunisia sasa inatawaliwa na Rais Kaïs Saïed, ambaye mwenyewe ametajwa kuwa ni mbabe baada ya msururu wa unyakuzi wa madaraka ikiwa ni pamoja na kuvunja chombo kikuu cha sheria nchini humo, kumfukuza waziri mkuu na kulivunja bunge.

  6. Mtoto wa aliyekuwa rais wa G. Bissau afungwa Marekani kwa ulanguzi wa dawa za kulevya

    XX

    Mwanawe rais wa zamani wa Guinea-Bissau amehukumiwa kifungo cha miaka sita jela na mahakama ya Marekani kwa kuongoza mtandao wa kimataifa wa ulanguzi wa dawa za kulevya.

    Malam Bacai Sanha Jr, 52, alipanga kutumia mapato hayo kufadhili azma yake ya kuwa rais wa Guinea-Bissau kupitia mapinduzi, mamlaka zilisema.

    Yeye ni mtoto wa Malam Bacai Sanha, ambaye aliongoza nchi hiyo ya Afrika Magharibi kutoka 2009 hadi kifo chake mwaka 2012.

    Sanha Jr amehusishwa na mapinduzi yaliyofeli mnamo Februari 2022.

    Alirejeshwa Marekani mnamo Agosti 2022, kufuatia kukamatwa kwake nchini Tanzania wiki chache zilizopita.

    Kesi yake ilianza kusikilizwa muda mfupi baadaye na Septemba mwaka jana, alikiri kosa la kula njama ya kuingiza dawa za kulevya kinyume cha sheria.

    "Malam Bacai Sanha Jr hakuwa mlanguzi wa kimataifa wa dawa za kulevya," afisa wa FBI Douglas Williams alisema Jumanne.

    "Yeye ni mtoto wa rais wa zamani wa Guinea-Bissau na alikuwa akisafirisha dawa za kulevya kwa sababu maalum - kufadhili mapinduzi ambayo hatimaye yangemwezesha kuwa urais wa nchi yake ya asili ambapo alipanga kuanzisha utawala wa madawa ya kulevya."

    Mamlaka ya Marekani inasema Sanha Jr anaweza kufukuzwa nchini kufuatia kufungwa kwake kwani yeye si raia wa Marekani.

    Sanha Jr mwenye umri wa miaka 52, anayejulikana kwa jina la "Bacaizinho" nchini Guinea-Bissau, ameshikilia majukumu kadhaa serikalini, ikiwa ni pamoja na kuwa mshauri wa kiuchumi wa babake.

  7. Thailand yahalalisha ndoa za wapenzi wa jinsia moja

    .xx

    Thailand imepiga hatua ya kihistoria katika suala la usawa wa ndoa baada ya baraza la mawaziri kupitisha mswada wa kutambuliwa kisheria kwa ndoa za wapenzi wa jinsia moja.

    Bado inahitaji idhini kutoka kwa Seneti na uidhinishaji ngazi ya kifalme ili kuwa sheria.

    Lakini inatarajiwa sana kutokea mwishoni mwa 2024, na kuifanya Thailand kuwa nchi pekee ya Kusini Mashariki mwa Asia kutambua ndoa za jinsia moja.

    Itaimarisha sifa ya Thailand kama kimbilio la wanandoa wa LGBTQ+ katika eneo ambalo mitazamo kama hii ni nadra.

    "Huu ni mwanzo wa usawa. Sio tiba ya watu wote kwa kila tatizo lakini ni hatua ya kwanza kuelekea usawa," Danuphorn Punnakanta, mbunge na mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu usawa wa ndoa, aliambia bunge wakati akiwasilisha rasimu ya mswada huo. "Sheria hii inataka kurudisha haki hizi kwa kundi hili la watu, sio kuwapa haki."

    Soma zaidi:

    ‘Furaha yetu imeongezeka mara tatu’ - Kutana na wanaume wa Thailand walio katika uhusiano

  8. Wizara ya Ulinzi Marekani kuanzisha kambi nchini Haiti kwa ajili ya vikosi vya usalama vya Kenya

    .

    Balozi wa Marekani nchini Kenya Meg Whitman alisema Wizara ya Ulinzi ya Marekani itaanzisha kambi nchini Haiti kwa ajili ya vikosi vya usalama vya Kenya kabla ya kutumwa kwao.

    Akizungumza mjini Nyeri Jumanne, Whitman alibainisha kuwa misheni ya Haiti ni ngumu na kwamba itahitaji polisi wafunzwe upya na kuchunguzwa.

    Mjumbe huyo wa Marekani hata hivyo alisema kwamba inaweza kuchukua muda kabla ya wanajeshi wa Kenya kutua Haiti kwani mabadiliko ya serikali katika taifa hilo la Caribbean yametatiza mambo.

    “Ninataka kumshukuru Rais Ruto kwa kujitolea kujitokeza kusaidia Haiti na kusema kwamba Kenya ina fursa ya kusaidia nchi ambayo ina kaka na dada zake wanaoishi nje ya nchi.

    Alisema Wahaiti ni sehemu ya Waafrika wanaoishi sehemu mbalimbali za dunia,” alisema.

    Kenya imekuwa ikituma timu ya upelelezi kutathmini hali kabla ya wanajeshi hao kuondoka kuelekea Haiti.

    Whitman alisema kuwa timu mbali mbali pia zimetumwa ili kutathmini hali kabla ya kupelekwa yeyote.

    "Huu ni ujumbe mgumu sana sio ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa. Ni aina tofauti ya misheni kwa hivyo polisi wanahitaji kupewa mafunzo, kuchunguzwa na idara ya ulinzi inahitaji kuweka kambi huko Haiti ambapo jeshi la polisi litaenda," alisema.

    Kenya inatarajiwa kupeleka afisa 1,000 wa polisi kurejesha hali ya utulivu katika nchi hiyo yenye matatizo baada ya kuombwa kufanya hivyo na Jumuiya ya Kimataifa.

    Soma zaidi:

    Mambo 5 yanayoelezea mizizi ya kihistoria ya mgogoro wa Haiti

    Wanaume wanaopigana na kiongozi wa genge Barbecue kuwania madaraka nchini Haiti

  9. Kiwanda cha kutengeneza nepi Japan kuanza kutengeza za watu wazima pekee

    .

    Kiwanda cha kutengeneza nepi cha Japan kimetangaza kuwa kitaacha kutengeneza nepi kwa ajili ya watoto wachanga nchini humo na badala yake kitaangazia soko la watu wazima.

    Oji Holdings ndiyo kampuni ya hivi punde kufanya mabadiliko kama haya nchini Japani yenye idadi kubwa ya wazee, ambapo viwango vya kuzaliana viko chini sana.

    Mauzo ya nepi za watu wazima yalizidi yale ya watoto wachanga nchini humo kwa zaidi ya muongo mmoja.

    Idadi ya watoto waliozaliwa nchini Japani mwaka 2023 - 758,631 - ilipungua kwa 5.1% kutoka mwaka uliopita.

    Pia ilikuwa idadi ndogo zaidi ya watoto waliozaliwa katika rekodi nchini Japani tangu Karne ya 19. Katika miaka ya 1970, idadi hiyo ilikuwa zaidi ya milioni mbili.

    Katika taarifa, Oji Holdings ilisema kampuni yake tanzu, Oji Nepia, kwa sasa inatengeneza nepi milioni 400 za watoto wachanga kila mwaka.

    Uzalishaji umekuwa ukishuka tangu 2001, wakati kampuni ilipofikia kilele chake cha nepi milioni 700.

    Huko nyuma mwaka wa 2011, mtengenezaji mkuu wa nepi nchini Japan, Unicharm, alisema mauzo yake ya nepi za watu wazima yamepita yale ya watoto wachanga.

  10. Nusu ya wanawake katika muziki wanakabiliwa na ubaguzi - ripoti

    .

    Nusu ya wanawake katika tasnia ya muziki wanakabiliwa na ubaguzi kulingana na ripoti iliyotolewa.

    Chuki dhidi ya wanawake, ubaguzi wa kijinsia na unyanyasaji bado ni matatizo ya kila siku kwa wanamuziki wa kike nchini Uingereza, ripoti mpya ya kusikitisha imegundua.

    Inasema kwamba thuluthi moja ya wanawake katika tasnia ya muziki wamenyanyaswa kingono kazini, huku wengi wakiripoti kuwa ni kikwazo kwa taaluma zao.

    Wanawake pia wana uwezekano wa kukabiliwa na ubaguzi mara nane zaidi kuliko wanaume.

    Matokeo hayo yanatoka kwa Sensa ya kwanza kabisa ya Wanamuziki wa Uingereza, iliyofanywa na Muungano wa Wanamuziki.

    Ilichunguza zaidi ya wataalamu wa tasnia ya muziki 6,000, kati yao 2,526 walitambuliwa kama wanawake.

    Ripoti ilisema wanawake wanalipwa kiwango cha chini kuliko wanaume, na mara nyingi wanapata kazi kwa muda mfupi, licha ya kufundishwa na kuelimishwa kwa kiwango cha juu.

    Zaidi ya robo ya wanamuziki wa kike (27%) walisema hawakupata mapato ya kutosha kutokana na muziki kuendeleza taaluma, ikilinganishwa na 20% ya wanaume.

    Kwa wastani, wanawake hupata 10% chini ya wenzao wa kiume, na wastani wa mapato ya kila mwaka ya £ 19,850 ikilinganishwa na £ 21,750 kwa wanaume.

  11. Raia wa Gaza waripotiwa kufa maji baada ya kukimbilia misaada ya chakula baharini

    TH

    Ofisi ya vyombo vya habari vya serikali ya Gaza inayoongozwa na Hamas imesema Wapalestina 18 wameuawa walipokuwa wakijaribu kukusanya misaada inayohitajika sana ambayo ilirushwa kaskazini mwa Gaza.

    Watu kumi na wawili walikufa maji walipoingia baharini kuchukua vifurushi vya chakula, wengine sita walikanyagwa hadi kufa katika "mikanyagano" wakati vifurushi vingine vya misaada vilitua chini, taarifa ilisema.

    Inataka "kukomeshwamara moja" kwahatua ya kutupwa kwa vyakula kupitia angani, na kuiita "ya kukera, mbaya,isiyofaa".

    Video, iliyopatikana na Reuters, imeibuka ya Wapalestina waliokuwa wakikimbilia pwani baada ya misaada kuangushwa kwenye ufuo karibu na mji wa kaskazini wa Beit Lahia siku ya Jumatatu.

    Inaonyesha watu wakikimbia huku dazeni za vifurushi vya misaada vilivyowekwa kwenye miamvuli vikielea chini karibu na pwani.

    Israel - ambayo iko chini ya shinikizo kuruhusu misaada zaidi kuingia Gaza kupitia ardhi - inasema iliwezeshavifurushi vyatani 159 za misaada kaskazini mwa Gaza siku ya Jumatatu.

    Marekani inasema ndege mbili aina ya C-17 zilidondosha "miloiliyotayari kuliwa" 46,000 (MREs) kaskazini siku ya Jumatatu, huku Uingereza ikisema moja ya ndege zake aina ya A400M ilidondosha tani 10 za maji, mchele, mafuta ya kupikia, unga,vinywaji vya Watoto.

    Mashirika ya kibinadamu yameonya kuwamisaada inayorushwa kwa njia hiyo haiwezikukidhi hitaji kubwa la chakula na mkakati huo umezua mjadala mkubwa.

    Video content

    Video caption: Raia wa Gaza waripotiwa kufa maji baada ya kukimbilia misaada ya chakula baharini
  12. Israel yasema azimio la Umoja wa Mataifa liliharibu mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza

    Israel inasema kukataa kwa Hamas pendekezo la sasa la makubaliano ya usitishaji vita ya Gaza na Israel kunaonyesha "uharibifu" uliofanywa na azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotaka kusitishwa mara moja kwa mapigano.

    Ofisi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ilisema Israel haitasalimu amri kwa kile ilichokiita "matakwa ya upotoshaji" ya kundi la wapiganaji wa Palestina.

    Ni pamoja na kumalizika kwa vita na uondoaji kamili wa vikosi vya Israeli.

    Marekani ilisema kauli hiyo ya Israel "si sahihi kwa karibu kila jambo".

    Msemaji wa wizara ya mambo ya nje alisisitiza kuwa jibu la Hamas lilikuwa limetayarishwa kabla ya Baraza la Usalama kupiga kura siku ya Jumatatu.

    Wakati huo huo jeshi la Israel imesema imethibitisha kuwa naibu kiongozi wa tawi la kijeshi la Hamas, Marwan Issa, aliuawa katika shambulio lililofanyika kwenye eneo la chini ya kambi ya wakimbizi ya Nuseirat takriban wiki mbili zilizopita .

    "Tumechunguza taarifa zote za kijasusi," msemaji wa Rear Admiral Daniel Hagari alisema. "Marwan Issa aliondolewa kwenye shambulizi hilo."

    Afisa wa kisiasa wa Hamas Izzat al-Rishq alisema "hana imani" na madai ya Israel na kwamba uongozi wa kijeshi wa kundi hilo ndio utakuwa na "semo la mwisho".

    Admiral Hagari alimtaja Issa kama "namba tatu" na "mmoja wa waandaaji" wa mashambulizi ya Hamas kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba, wakati takriban watu 1,200 waliuawa na wengine 253 kuchukuliwa mateka.

    Zaidi ya watu 32,400 wameuawa huko Gaza tangu wakati huo, wakiwemo watu 81 katika muda wa saa 24 zilizopita, kulingana na wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas.

    Soma zaidi:

    Jinsi Marekani 'ilivyoishangaza' Israel katika baraza la Usalama la UN

  13. Vita vya Gaza: Mtaalamu wa haki kutoka Umoja wa Mataifa aishutumu Israel kwa vitendo vya mauaji ya kimbari

    .

    Mtaalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa anasema anaamini Israel imefanya "vitendo vya mauaji ya kimbari" huko Gaza.

    Francesca Albanese, ripota maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, aliwasilisha ripoti yake kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa mjini Geneva siku ya Jumanne.

    Lakini Israel tayari imetupilia mbali matokeo yake.

    Haya yanajiri huku kukiwa na shinikizo la kimataifa kwa Israel kusitisha vita au kufanya mengi zaidi kuwalinda raia.

    Bi Albanese alihitimisha kuwa "kuna sababu za kuridhisha za kuamini kwamba kiwango kinachoonyesha kutendeka kwa uhalifu wa mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina kama kundi huko Gaza kimefikiwa".

    Kabla ya Bi Albanese hata kusimama, matokeo yake yalitupiliwa mbali na Israel, ambayo balozi wake alieleza kuwa ni "upotoshaji wa kutisha wa Mkataba wa Mauaji ya Kimbari".

    Israel kwa miaka mingi imekuwa ikikasirishwa na ajenda ya Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa, ambalo linatoa sehemu nzima - Kipengee cha 7 - kuchunguza hali ya "Palestina na maeneo mengine ya Kiarabu yanayokaliwa".

    Kipengele cha ajenda kiliidhinishwa sio na UN yenyewe, lakini na nchi wanachama wa UN miongo kadhaa iliyopita, na haijawahi kuisha. Hakuna nchi nyingine duniani ambayo ina uchunguzi wa kudumu kama huu, na Israeli inaiona kama ya kibaguzi, na inayolenga kuiondoa Israeli. Inakataa kuhudhuria baraza wakati Kipengee cha 7 kinajadiliwa.

    Soma zaidi:

    Msichana wa Gaza,12, aliyepoteza familia yake yote kwa usiku mmoja

  14. Watu sita wadhaniwa kufariki baada ya meli kugonga daraja Marekani

    .

    Watu sita wamepotea wakidhaniwa kufariki baada ya meli ya mizigo kugonga daraja la kihistoria la Francis Scott Key katika mji wa Baltimore nchini Marekani.

    Walinzi wa Pwani walisema kuwa wamesitisha msako wake na kuanza juhudi za kuwaokoa.

    Magari kadhaa yalikuwa yakivuka daraja hilo lenye urefu wa zaidi ya 2.6km (maili 1.6) lilipoanguka baada ya meli hiyo kugonga nguzo.

    Maafisa wanasema meli hiyo ilikumbwa na "tatizo la umeme nguvu" na ikatoa mawasiliano muda mfupi kabla ya ajali.

    Boti na helikopta zilikuwa sehemu ya juhudi kubwa ya kuwatafuta na kuwaokoa watu sita waliopotea. Wengine wawili walitolewa majini, huku mmoja akiwa katika hali mbaya.

    Admirali Shannon Gilreath wa Walinzi wa Pwani ya Marekani alisema jioni kwamba watu waliosalia waliopotea walidhaniwa kufariki kulingana na joto la maji waliyokuwa wametumbukia na urefu wa muda ambao wamekuwa chini ya maji.

    Mamlaka inasema walikuwa sehemu ya wafanyakazi wa ujenzi waliokuwa wakitengeneza mashimo wakati daraja lilipopasuka.

    Soma zaidi:

    Marekani: Daraja muhimu laporomoka mtoni baada ya kugongwa na meli ya mizigo

  15. Urusi yalaumu nchi za Magharibi na Kyiv kwa 'mauaji yaliyotekelezwa na wanajihadi'

    .

    Maafisa wakuu wa Urusi wameishutumu moja kwa moja Ukraine na nchi za Magharibi kwa kuhusika katika shambulio baya la ukumbi wa tamasha la Moscow, baada ya kundi la Islamic State (IS) kudai kuhusika.

    IS imetoa video ya ukatili huo, lakini Vladimir Putin na washirika wake wawili wamedai wanajihadi hao walisaidiwa na ujasusi wa Magharibi na Ukraine.

    Ukraine imekataa "uongo" wa Urusi.

    Hali hiyo ina uwezekano mkubwa zaidi kwa sababu Marekani ilikuwa imeionya Urusi kuhusu shambulio lililokaribia siku 15 kabla.

    Urusi inasema watu 139 waliuawa wakati watu wanne waliokuwa na silaha walipovamia jumba la tamasha la Crocus City Hall Ijumaa jioni. Wengine 22 bado wako katika hali mbaya, wakiwemo watoto wawili, maafisa wanasema.

    Raia wanne wa Tajikistan wamefikishwa mahakamani wakituhumiwa kutekeleza mauaji hayo. Washukiwa wengine wanne wameshtakiwa kwa kusaidia ugaidi.

    Mshauri wa rais wa Ukraine Mykhailo Podolyak alisema ukweli kuhusu wahalifu na "kutofaulu kwa huduma za usalama za Urusi ni jambo lisilopingika". Nchi za Magharibi pia zimekejeli simulizi ya Kremlin.

    Kiongozi wa Urusi alikiri wakati wa mkutano wa televisheni siku ya Jumatatu: "Tunajua uhalifu ulifanywa na Waislam wenye itikadi kali ... tunataka kujua ni nani aliyeamuru."

    Alidai kuwa maswali mengi yalisalia bila majibu, akirudia madai yasiyo na msingi kwamba washambuliaji walijaribu kukimbilia kusini mwa Ukraine.

    Urusi yawashtaki wanaume wanne kwa shambulio la tamasha la Moscow

    Tazama: Watu wakijificha wakati watu wenye silaha wakiingia kwenye ukumbi Moscow

    Shambulizi la Moscow: Je, Urusi ilipuuza onyo la mashambulizi lililotolewa na Marekani?

    Maadui zetu hawatatugawa - Putin

    Washambuliaji walikuwa na mawasiliano na Ukraine- Idara ya usalama ya Urusi

  16. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 27/03/2024