Got a TV Licence?

You need one to watch live TV on any channel or device, and BBC programmes on iPlayer. It’s the law.

Find out more
I don’t have a TV Licence.

Habari za moja kwa moja

Na Asha Juma na Ambia Hirsi

time_stated_uk

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo ya moja kwa moja. Kwaheri.

  2. Xabi Alonso kusalia Bayer Leverkusen licha ya kutakiwa na Liverpool

    Alonso

    Xabi Alonso anasema atasalia katika nafasi yake kama meneja wa Bayer Leverkusen msimu ujao kwani anaamini klabu hiyo ndio "mahali pazuri" kuwa kama kocha mchanga.

    Mhispania huyo amekuwa akihusishwa pakubwa na klabu ya Liverpool tangu Jurgen Klopp aliposema atajiuzulu mwishoni mwa msimu huu.

    “Nina hakika ni uamuzi sahihi, nina furaha,” alisema Alonso.

    Leverkusen wanaoelekea kushinda taji la kwanza la Bundesliga, hawajashindwa katika meche yoyote msimu huu.

    Kiungo wa kati wa zamani wa Liverpool Alonso, 42, pia alionekana kama mgombea wa kuinoa klabu yake nyingine ya zamani ya Bayern Munich, ambayo meneja wake Thomas Tuchel pia ataondoka mwishoni mwa msimu.

    Alonso alisema amewaarifu wakurugenzi wa Leverkusen kuhusu uamuzi wake wa kusalia katika klabu hiyo wiki iliyopita.

  3. Jacob Zuma: Rais wa zamani wa Afrika Kusini ahusika katika ajali

    XX

    Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma amehusika katika ajali ya gari lakini hakujeruhiwa.

    Dereva mlevi aligongana na "gari lake rasmi la kivita" Alhamisi jioni, polisi wamesema. Lakini mwanachama mkuu wa chama chake cha uMkhonto we Sizwe (MK) alidai kwamba alikuwa akilengwa.

    Amesimamishwa kazi na chama tawala cha African National Congress (ANC) na anafanyia kampeni MK kabla ya uchaguzi mkuu wa Mei.

    Bw Zuma alikuwa ndani ya gari hilo, pamoja na timu yake rasmi ya ulinzi, lilipogongwa barabarani katika jimbo la KwaZulu-Natal mwendo wa saa kumi na mbili na dakika arubaini kwa saa za huko (16:40 GMT) siku ya Alhamisi.

    "Hakuna aliyejeruhiwa, ikiwa ni pamoja na wanachama wa Huduma za Ulinzi wa Rais. Rais wa zamani alihamishwa na kupelekwa kwenye makazi yake," taarifa fupi ya polisi ilisema.

    Mwanamume mwenye umri wa miaka 51 amekamatwa kwa "kuendesha gari akiwa amelewa na... kuendesha kiholela".

    Mkuu wa uchaguzi wa chama cha MK, Musa Mkhize, ameambia shirika la utangazaji la SABC kwamba anahisi ilikuwa njama badala ya ajali.

    "Kwa bahati mbaya, tumekuwa tukisubiri litokee. Rais alionywa kuwa kabla ya siku ya uchaguzi atakuwa amelazwa hospitalini. Tunawashukuru wajumbe wa Kitengo cha Ulinzi wa Rais waliofanikiwa kumuweka Rais salama," alinukuliwa na News24 akisema.

    Bw Zuma, 81, alihudumu kama rais kuanzia 2009 hadi 2018, alipolazimika kung'atuka kwa sababu ya tuhuma za ufisadi, ambazo anakanusha.

    Maelezo zaidi:

    Jacob Zuma azuiwa kugombea katika uchaguzi wa Afrika Kusini

    Je, chama cha ANC kitaathiriwa na kujiondoa kwa Jacob Zuma?

  4. Kampuni ya utalii yapigwa faini kwa kuwaruhusu wageni kula hadharani Zanzibar

    Watalii Zanzibar

    Kamisheni ya Utalii Zanzibar imethibitisha kuipiga faini ya dola 500 kampuni ya utalii ya Organisateur Francophone Tours and Travel kwa kuruhusu watalii kula hadharani katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhan.

    Katika taarifa Afisa wa Uhusiano wa Tume ya Utalii Zanzibar Mohamed Nassor Bajuni alisema kampuni hiyo ilikiuka miongozo na maagizo yaliyotolewa kwa wafanyabiashara wa utalii wakati huu wa mfungo wa Ramadhani.

    ''Toka kuanzishwa kwa kamisheni huo tunatoa notisi maalumu kwa kipindi cha mwezi wa Ramadhani kuhusiana na suala hili'' alisema Bw.

    Muongoza watalii wa kampuni hiyo, Khamis M. Kahogo pia amezuiliwa kufanya shughuli zozote za utalii kwa muda wa miezi mitatu," aliongeza kusema.

    Kamisheni hiyo imesisitiza umuhimu wa kufuata desturi na mila za visiwa vya Zanziba hasa wakati huu wa mfungo wa Ramadhan.

    Kwanini ni 'marufuku' kula mchana wa mwezi wa Ramadhan visiwani Zanzibar

  5. Kuna tishio la vita na Ulaya haijawa tayari- Waziri Mkuu wa Poland

    Tusk

    Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk ametoa onyo kali kwamba Ulaya imeingia katika "zama za kabla ya vita" na ikiwa Ukraine itashindwa na Urusi, hakuna mtu yeyote barani Ulaya atakayeweza kujihisi kuwa salama.

    "Sitaki kumtisha mtu yeyote, lakini vita si dhana ya zamani," aliviambia vyombo vya habari vya Ulaya ,"Ni kweli na ilianza zaidi ya miaka miwili iliyopita."

    Matamshi yake yalikuja huku Urusi ikianzisha msururu mpya wa mashambulizi ya makombora dhidi ya Ukraine.

    Poland ilisema ndege za Nato ziligombaniwa kulinda anga yake.

    Urusi imezidisha mashambulizi yake dhidi ya Ukraine katika wiki za hivi karibuni.

    Jeshi la wanahewa la Ukraine limesema limeangusha ndege 58 zisizo na rubani na makombora 26 na Waziri Mkuu Denys Shmyhal alisema miundombinu ya nishati imeharibiwa katika mikoa sita, magharibi, katikati na mashariki mwa nchi.

    Bw Tusk, rais wa zamani wa Baraza la Ulaya, alisema Rais wa Urusi Vladimir Putin tayari ameilaumu Ukraine kwa shambulio la wanajihadi kwenye Ukumbi wa Jiji la Crocus mjini Moscow bila ushahidi wowote na " ni dhahiri anahisi hitaji la kuhalalisha mashambulizi makali dhidi ya malengo ya raia nchini Ukraine".

    Alisema kuwa Urusi ilishambulia Kyiv kwa makombora ya hypersonic kwa mara ya kwanza mapema wiki hii.

    Alitumia mahojiano yake ya kwanza ya kigeni tangu arejee ofisini kama waziri mkuu wa Poland mwishoni mwa mwaka jana kutoa wito wa moja kwa moja kwa viongozi wa Ulaya kuongeza juhudi za kuimarisha ulinzi wake.

  6. KFC Nigeria yaomba radhi kwa kumnyima huduma mteja mlemavu

    Nembo ya KFC

    KFC Nigeria imeomba radhi baada ya mamlaka ya uwanja wa ndege nchini humo kufunga moja ya maduka yake kwa madai ya ubaguzi dhidi ya mteja mlemavu.

    Adebola Daniel, mtoto wa gavana wa zamani wa jimbo la Nigeria Gbenga Daniel, alisema katika chapisho kwenye mtandao wa X kwamba aliamriwa kuondoka kwenye duka la KFC kwenye uwanja wa ndege wa Lagos kwa sababu ya kiti chake cha magurudumu.

    Chapisho hilo lilizua ghadhabu kubwa katia hatua ambayo ilisababisha mamlaka ya uwanja wa ndege wa kuanzisha uchunguzi, na kuishia kwa kufungwa kwa tawi hilo.

    Katika mazungumzo marefu, Bw Daniel alielezea kisa hicho, kilichotokea Jumanne, kama "aina mbaya zaidi ya udhalilishaji wa umma" ambayo hajawahi kupata.

    "Leo nilijihisi kuwa mtu duni, nilijihisi kama mbwa mlinzi ambaye haruhusiwi kuingia ndani ya nyumba. Mpweke na kutengwa." Alidai kuwa meneja wa duka la KFC katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Murtala Muhammed mjini Lagos, uwanja wa ndege wenye shughuli nyingi zaidi Nigeria, alimnyima huduma licha rai kubwa kutoka kwa mkewe na kaka zake wawili, waliokuwa wakisafiri naye.

    "Alikataa kusikiliza hoja yetu na kusisitiza kwamba katika [KFC] tawi la Murtala Muhammed, viti vya magurudumu na watumiaji wa viti vya magurudumu vyenye maumbo makubwa havikuruhusiwa katika majengo hayo na tunapaswa kuondoka mara moja," alisema.

    Katika chapisho kwenye X mnamo Alhamisi, KFC Nigeria ilimsikitikia Bw Daniel na kutangaza hatua za kushughulikia hali hiyo, ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa wafanyikazi wake juu ya ujumuishaji na huduma kwa wateja.

    "Tunajutia sana kwa hali aliyopitia mgeni wetu na tunatoa pole za dhati kwa walioathirika," ilisema kwenye X.

    Taarifa hiyo ilifuatia hatua ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege ya Nigeria (FAAN) kufunga mgahawa huo na kutoa agozo kwa KFC kumuomba msamaha Bw Adebola.

    FAAN pia imeamuru KFC kuonyesha sera ya kutobagua watu kama sharti la kufunguliwa tena.

  7. Uingereza: Jeshi laruhusu vikosi vyake kufuga ndevu kwa mara ya kwanza

    '

    Wanajeshi na maafisa sasa wanaruhusiwa kufuga ndevu wanapohudumu katika Jeshi la Uingereza.

    Ndevu na masharubu lazima ziwe nadhifu, zimepambwa vizuri na zitaangaliwa mara kwa mara.

    Sera hiyo inaanza kutumika mara moja kwani ni mara ya kwanza kuruhusu wafanyikazi wake kufuga ndevu.

    Maagizo hayo mapya yanafuatia majadiliano ya miaka mingi kuhusu sera ya Jeshi kuhusu nywele za usoni.

    Mabadiliko hayo yanafuatia mapitio ya sera ya Jeshi kuhusu kuonekana kwa wafanyakazi wake ambayo ilidumu kwa miezi kadhaa, msemaji wa jeshi aliiambia BBC.

    Uongozi wa jeshi kisha ukaangalia matokeo kabla ya kuamua kubadili sera.

    "Tumewasikiliza watu wetu na kuchukua hatua," msemaji huyo alisema.

  8. Israel yashukiwa baada ya mashambulizi ya anga dhidi ya Syria kuwauwa takriban 40

    '

    Takriban watu 36 wameuawa katika mashambulizi ya anga ya Israel karibu na mji wa Aleppo nchini Syria, kwa mujibu wa ripoti.

    Wizara ya ulinzi ya Syria inasema kuwa mashambulizi hayo yalitokea maeneo kadhaa katika vijiji vya Aleppo saa 1:45 saa za huko siku ya Ijumaa.

    Shirika la Uangalizi wa Haki za Kibinadamu la Syria (SOHR) lenye makao yake makuu nchini Uingereza linasema maeneo yaliyolengwa ni maduka ya silaha yanayotumiwa na kundi la wanamgambo wa Lebanon linaloungwa mkono na Iran Hezbollah.

    Israel haitoi maoni yoyote kuhusu mashambulizi yoyote dhidi ya Syria.

    Likinukuu vyanzo viwili vya usalama, shirika la habari la Reuters linaripoti kuwa wapiganaji watano wa Hezbollah ni miongoni mwa waliofariki na kufanya idadi ya vifo kuwa 38.

    Wizara ya ulinzi inasema raia na wanajeshi wa Syria pia waliuawa.

    SOHR, kundi la ufuatiliaji na mtandao mpana wa mawasiliano nchini Syria, linasema "makumi" ya wengine walijeruhiwa.

    Maeneo yanayolengwa ni karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Aleppo, inaongeza.

    Tangu kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria mwaka 2011, Israel imeanzisha mamia ya mashambulizi dhidi ya Syria, mengi yakilenga makundi yenye mafungamano na Iran, muungaji mkono mkubwa wa kundi la wanamgambo wa Palestina, Hamas.

    Mashambulizi hayo yameongezeka tangu Hamas kufanya mashambulizi ya Oktoba 7 na Israel kuanza kampeni yake ya kulipiza kisasi kuliangamiza kundi hilo huko Gaza.

    Hezbollah pia imefanya mashambulizi ya mara kwa mara ya roketi dhidi ya Israel kutoka kusini mwa Lebanon.

    Wizara ya ulinzi ilisema mashambulizi hayo mapya ya anga yalienda sambamba na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani huko Aleppo yaliyotekelezwa na "mashirika ya kigaidi", ingawa haikubainisha iwapo kumekuwa na majeruhi zaidi.

    Soma zaidi:

    Jeshi la Israeli linajumuisha akina nani na ni jamii gani nyingine zinazohudumu katika jeshi hilo?

  9. Urusi yazuia shirika la Umoja wa Mataifa linalofuatilia vikwazo vya Korea Kaskazini

    .

    Urusi yazuia jopo la wataalamu wa Umoja wa Mataifa ambao kwa miaka mingi wamefuatilia vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini.

    Jopo hilo wiki iliyopita lilisema linachunguza ripoti kwamba Urusi ilikiuka sheria kwa kununua silaha za Korea Kaskazini kama vile makombora ya balistiki kwa matumizi nchini Ukraine.

    Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeiwekea vikwazo Pyongyang tangu mwaka 2006 kutokana na mpango wake wa kutengeneza silaha za nyuklia.

    Vizuizi hivyo bado vinatumika - lakini kikundi cha wataalam kilichoundwa kufuatilia ukiukaji sasa kitavunjwa.

    Katika kura ya Baraza la Usalama siku ya Alhamisi, Urusi ilitumia mamlaka yake ya kura ya turufu kama mwanachama wa kudumu kuzuia urejeshaji huo, huku mataifa 13 kati ya 14 wanachama waliohudhuria yakiipigia kura. Uchina, mshirika wa karibu wa Pyongyang, alijizuia kupiga kura.

    Soma zaidi:

    Mashambulio ya NATO ambayo yaliibua enzi mpya ya vita

  10. Bunge la Ufaransa launga mkono mswada wa kupinga ubaguzi wa nywele

    .

    Ufaransa imepiga hatua katika suala la kupiga marufuku ubaguzi mahali pa kazi dhidi ya mitindo ya nywele.

    Mswada umeidhinishwa katika Bunge la Kitaifa na sasa utajadiliwa katika Seneti.

    Sheria itawazuia waajiri kuhitaji nywele kunyooshwa na kwa mitindo ya afro, dreadlock na rasta kufunikwa.

    Mwasilishi wa mswada huo anatumai sheria hiyo itawasaidia wale, haswa watu weusi, ambao wamekabiliwa na uhasama mahali pa kazi.

    Mswada huo haulengi hasa ubaguzi wa rangi, ingawa hiyo ndiyo msukumo wa sheria hiyo.

    Pia utalinda nywele za rangi pamoja na waathirika wa kipara au udazi.

    Ulipendekezwa na Olivier Serva, mbunge kutoka kisiwa cha Guadeloupe cha Karibea cha Ufaransa, ambaye aliwasilisha utafiti wa Marekani ambao ulionyesha kuwa robo ya wanawake weusi walisema wamenyimwa kazi kwa sababu ya jinsi walivyoweka nywele zao wakati wa usaili.

  11. 'Mfalme'wa sarafu za kidijitali ahukumiwa miaka 25 jela

    .

    Sam Bankman-Fried, mwanzilishi mwenza wa shirika la kubadilishana fedha la crypto FTX, amehukumiwa kifungo cha miaka 25 jela kwa kuwatapeli wateja na wawekezaji wa kampuni yake ambayo sasa imefilisika.

    Uamuzi huo unathibitisha kuanguka kwa bilionea huyo wa zamani, ambaye aliibuka kama bingwa wa hadhi ya juu wa sarafu ya crypto kabla ya kufilisika kwa kampuni yake mnamo 2022.

    Alipatikana kuwa ameiba mabilioni ya wateja kabla ya kufilisika kwa kampuni hiyo.

    Timu ya wanasheria ya Bankman-Fried itakata rufaa dhidi ya hukumu yake.

    Ujumbe kutoka kwa wazazi wake ulioshirikishwa na BBC na mwakilishi wa Bankman-Fried ulisema: "Tumevunjika moyo na tutaendelea kumpigania mtoto wetu."

    Awali, kijana huyo mwenye umri wa miaka 32 alisema mahakamani kwamba alijua "watu wengi" walihisi "kukatishwa tamaa".

    "Samahani kwa hilo. Samahani kwa kile kilichotokea katika kila hatua," alisema, akizungumza kwa upole na uwazi kabla ya hukumu yake.

    Kampuni ya FTX ilikuwa mojawapo ya ubadilishanaji mkubwa zaidi wa sarafu ya mtandaoni ya crypto ulimwenguni kabla ya kufilisika kwake, na kumgeuza Bankman-Fried kuwa mtu mashuhuri wa biashara na kuvutia mamilioni ya wateja ambao walitumia jukwaa la kampuni kununua na kufanya biashara ya cryptocurrency.

    Uvumi wa matatizo ya kifedha ulisababisha watu kukimbia kutoa pesa zao mwaka wa 2022, na kusababisha kufilisika kwa kampuni hiyo pamoja na kufichua uhalifu wa Bankman-Fried.

    Alipatikana na hatia na mahakama ya mjini New York mwaka jana kwa mashtaka yakiwemo ya ulaghai na kula njama ya kutakatisha fedha, baada ya kesi iliyoeleza jinsi alivyochukua zaidi ya $8bn (£6.3bn) kutoka kwa wateja, na kutumia pesa hizo kununua mali, kutoa michango ya kisiasa na uwekezaji mwingine.

    Soma zaidi:

    Cryptocurrency: Je, Afrika iko tayari kwa sarafu za kidijitali?

  12. Jacob Zuma azuiwa kugombea katika uchaguzi wa Afrika Kusini

    .

    Rais wa zamani Jacob Zuma amezuiwa kugombea katika uchaguzi mkuu nchini Afrika Kusini utakaofanyika mwezi Mei.

    Tume ya uchaguzi nchini humo (IEC), haijatoa sababu.

    Hata hivyo, hukumu yake ya 2021 na kufungwa jela kwa kudharau mahakama kutaonekana kumuondoa kwenye kinyang’anyiro hicho.

    Uungaji mkono wake kwa chama kipya cha Umkhonto we Sizwe (MK) umeonekana kuwa tishio kwa chama tawala cha African National Congress (ANC), ambacho kimemsimamisha kazi Bw Zuma.

    Zuma mwenye umri wa miaka 81 alihudumu kama rais kutoka 2009 hadi 2018, ambapo alilazimika kujiuzulu kwa sababu ya tuhuma za ufisadi.

    hama kipya cha Bw Zuma kimepewa jina la mrengo wa zamani wa kijeshi wa ANC, na anajiona kama mrithi wa kweli wa mizizi ya mapinduzi ya chama tawala.

    ANC ilikuwa ilitaka shirika la uchaguzi la Afrika Kusini kufuta usajili wa MK, lakini ombi hilo lilikataliwa Jumanne.

    Bw Zuma amekuwa akiongoza kampeni za chama cha MK na lilikuwa jina la kwanza kwenye orodha ya wagombeaji wao, lakini tume ya uchaguzi ilipokea pingamizi dhidi yake kuwa huenda akawa mwanachama wa Bunge la Kitaifa.

    Badala ya kumpigia kura rais moja kwa moja, Waafrika Kusini huchagua wajumbe wa Bunge la Kitaifa. Mkuu wa chama chochote anachopata wengi basi anakuwa kiongozi wa nchi.

    "Katika kesi ya Rais wa zamani Zuma, ndiyo, tulipokea pingamizi, ambalo limekubaliwa," alisema mkuu wa tume ya uchaguzi Mosotho Moepya siku ya Alhamisi.

    “Chama ambacho kimemteua kimefahamishwa,” Bw Moepya aliambia wanahabari.

    Bw Zuma ana hadi tarehe 2 Aprili kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

    Pia unaweza kusoma:

    Uchaguzi Afrika Kusini 2024: Utafanyika lini na je, ANC iko hatarini kupoteza?

  13. Wagonjwa scotland huenda wakapewa msaada wa kukatisha maisha yao

    .

    Scotland inaweza kuwa taifa la kwanza la Uingereza kutoa msaada kwa watu walio wagonjwa mahututi ili kukatisha maisha yao ikiwa mswada ambao umewasilishwa Holyrood utaidhinishwa.

    Wanaopendelea sheria hiyo wanasema itapunguza mateso.

    Wapinzani wana wasiwasi kwamba baadhi ya watu wenye ugonjwa usiotibika wanaweza kuhisi kuwa chini ya shinikizo la kukatatisha maisha yao.

    Assisted Dying for Terminally Ill Adults (Scotland) Bill is drafted by the Lib Dem MSP, Liam McArthur.

    Mswada huo wa Kukatisha Maisha unatarajia kujadiliwa msimu huu wa vuli.

    Mswada huo ulichapishwa Alhamisi na kuna uwezekano wa kupigiwa kura mwaka ujao.

    Serikali ya Scotland inasema mawaziri na wafuasi wa SNP hawataelekezwa jinsi ya kupiga kura, kwa kuwa suala hilo ni suala la dhamira ya mtu binafsi.

    Waziri wa Kwanza Humza Yousaf, ambaye ni Muislamu, amedokeza kuwa kuna uwezekano mkubwa akapiga kura dhidi ya mswada huo, ambao pia unapingwa na Kanisa la Scotland, Kanisa Katoliki la Scotland, na Jumuiya ya Misikiti ya Scotland.

    Chini ya mapendekezo hayo, mgonjwa angeweza tu kuomba usaidizi wa kimatibabu ili kukatisha maisha yake ikiwa alikuwa na ugonjwa mbaya na alikuwa ameamuliwa kuwa sawa kiakili kufanya uamuzi na madaktari wawili.

    Pia unaweza kusoma:

    Waliochoshwa na maisha kusaidiwa kufa Uholanzi

    Mtu mgonjwa kupitia kiasi apoteza kesi ya kutaka kusaidiwa kufa

  14. Basi latumbukia kwenye daraja Afrika Kusini na kuua watu 45

    .

    Watu 45 wamefariki dunia nchini Afrika Kusini baada ya basi walilokuwamo kutumbukia umbali wa mita 50 kutoka kwenye daraja kwenye korongo, mamlaka zilisema.

    Msichana wa miaka minane, ambaye ndiye pekee aliyenusurika, alipelekwa hospitalini akiwa na majeraha mabaya.

    Basi hilo lilianguka kwenye kizuizi na kuwaka moto lilipogonga ardhini katika mkoa wa kaskazini-mashariki mwa Limpopo.

    Abiria hao walikuwa ni mahujaji waliokuwa wakisafiri kutoka mji mkuu wa Botswana Gaborone kuelekea ibada ya Pasaka katika mji wa Moria.

    Gari hilo lilipoteza mwelekeo na likatoka kwenye daraja njia ya mlima ya Mmamatlakala kati ya Mokopane na Marken, karibu kilomita 300 (maili 190) kaskazini mwa Johannesburg, kulingana na shirika la utangazaji la Afrika Kusini SABC.

    Shughuli za uokoaji ziliendelea hadi Alhamisi jioni, huku baadhi ya waliouawa ikiripotiwa kuwa vigumu kuwafikia katikati ya vifusi.

    Waziri wa Uchukuzi Sindisiwe Chikunga, ambaye alienda eneo la tukio, alitoa "rambirambi zake za dhati kwa familia zilizoathiriwa na ajali mbaya ya basi".

    Alisema serikali ya Afrika Kusini itasaidia kurejesha miili hiyo na kufanya uchunguzi kamili kuhusu chanzo cha ajali hiyo.

    Pia unaweza kusoma:

    Tahadhari unazopaswa kuzingatia ili kulinda maisha yako unapoogelea

  15. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 29/03/2024