Got a TV Licence?

You need one to watch live TV on any channel or device, and BBC programmes on iPlayer. It’s the law.

Find out more
I don’t have a TV Licence.

Habari za moja kwa moja

Na Ambia Hirsi na Asha Juma

time_stated_uk

  1. Israel yadai Iran iwekewe vikwazo dhidi ya mpango wake wa makombora

    Huku kila mmoja akisubiri kuona jinsi Israel inavyoijibu kijeshi Iran, nayo inachukua hatua kidiplomasia.

    Israel inaonekana kutengwa kidogo kwani angalizo sasa limepungua sana kwa Gaza na watakuwa na matumaini ya kufaidika na hili kuweka shinikizo la kimataifa kwa Iran.

    Waziri wa mambo ya nje wa Israel amesema ameziandikia barua nchi 32 akitaka Iran iwekewe vikwazo zaidi. Hii ni pamoja na, alisema, vikwazo kwa mpango wa makombora wa Iran.

    Msururu wa vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya mpango wa makombora wa Iran uliisha Oktoba mwaka jana kwa sababu vilihusishwa na mapatano mapana zaidi kuhusu Mpango wa Nyuklia wa Iran.

    Nchi zikiwemo Marekani, Uingereza na EU tayari zimedumisha vikwazo na kuongeza vingine vipya.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel pia alitoa wito kwa Jeshi la Ulinzi la Iran Islamic Revolutionary Guard Corps (IRGC) kutangazwa kuwa shirika la kigaidi.

    Marekani tayari imefanya hivyo lakini Uingereza bado.

    Mjadala kuhusu kufuata njia hii umekuwa mgumu na wenye mgawanyiko ndani ya serikali.

    Wengine wanapendelea kupigwa marufuku na wengine wanapinga kwa sababu wanafikiri kuwa IRGC ni sehemu ya serikali badala ya shirika la kigaidi, na marufuku hiyo ingesababisha Iran kufunga njia za mawasiliano kati ya nchi hizo mbili.

    Soma zaidi:

    Israel yazitaka nchi kadhaa kuiwekea Iran vikwazo

  2. Jordan asema Netanyahu anataka 'kuondoa angalizo Gaza'

    .

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan anasema jumuiya ya kimataifa inapaswa kumzuia Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, kuondoa angalizo katika vita vya Gaza kwa kuzidisha makabiliano yake na Iran.

    Ayman Safadi anasema Iran ilikuwa ikijibu mashambulizi dhidi ya ubalozi wake mdogo na ilitangaza kuwa "haitaki mababiliano yaongezeke zaidi".

    "Tunapinga kuzidisha vita. Netanyahu anataka kuondoa angalizo Gaza na kujikita katika makabiliano yake na Iran," Safadi alisema kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Berlin.

    Ofisi ya Netanyahu imesema jumuiya ya kimataifa "lazima iendelee kusimama kidete kupinga uchokozi huu wa Iran, ambao unatishia amani duniani".

    Soma zaidi:

    Jeshi la Israel laendelea na operesheni huko Gaza

    Israel yazitaka nchi kadhaa kuiwekea Iran vikwazo

  3. UN yasema Israel inaweka vikwazo vilivyo 'kinyume cha sheria' kwa misaada kuingia Gaza

    .

    Umoja wa Mataifa unasema Israel bado inaweka "vizuizi visivyo halali" kwa msaada kwa Gaza, licha ya kukabiliwa na shinikizo kubwa la kuruhusu misaada zaidi ya kibinadamu kuingia.

    Ravina Shamdasani, msemaji wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, anasema Israel pia inatekeleza "uharibifu mkubwa wa miundombinu ya raia".

    Shirika la Israel linaloratibu misaada huko Gaza - Cogat - linasema msafara wa chakula uliingia Gaza jana kupitia kivuko kipya cha kaskazini.

    Shirika hilo lilisema kwenye mtandao wa X kwamba "malori 126 ya misaada yanaratibiwa kaskazini mwa Gaza kwa usiku mmoja", akiongeza kuwa viwanda viwili vya kuoka mikate vinafanya kazi kaskazini mwa Gaza "vinasambaza mikate 800,000 kwa wakazi wa eneo hilo".

    Soma zaidi:

    Israel yazitaka nchi kadhaa kuiwekea Iran vikwazo

  4. Jeshi la Israel laendelea na operesheni huko Gaza

    .

    Licha ya mvutano unaoendelea kati ya Iran na Israel, jeshi la Israel linaendelea na operesheni yake dhidi ya Hamas katika Ukanda wa Gaza.

    Vikosi vya Israel vilianza operesheni ya kijeshi katika mji wa Beit Hanoun, kaskazini mashariki mwa Ukanda wa Gaza, alfajiri ya leo, huku makumi ya vifaru na magari ya kivita yakiingia kutoka pande za mashariki na kaskazini na kuzingira shule tatu zinazohifadhi maelfu ya watu waliokimbia makazi yao.

    Uvamizi huo ulianza kwa mashambulizi makali ya anga na mizinga, ikifuatiwa na kuingia kwa vikosi viwili vya magari ya kivita na vifaru.

    Mohamed Muhanna, mwanahabari mwanaharakati wa eneo hilo, anaiambia BBC: "Wanajeshi wa Israel walisonga mbele mjini Beit Hanoun na kuzingira shule kwa kuwasha moto mkubwa, na kufyatua risasi kutoka kwa ndege zisizo na rubani za Quadcopter katika shule hiyo, ambayo huhifadhi mamia ya watu waliokimbia makazi yao."

    Katikati ya Gaza, IDF inasema ndege na wanajeshi wa kutembea kwa miguu wamekuwa katika hatua dhidi ya kile wanachokiita maeneo ya Hamas katika ukanda wa kati wa Gaza.

    Soma zaidi:

    Mkuu wa jeshi la Israel aapa kulipiza kisasi shambulizi la Iran

    Vita vya Israel na Gaza: Kwanini inaonekana kuwa vigumu zaidi kufikia amani kuliko wakati mwingine wowote

  5. Je Iran na Israel zina silaha za nyuklia?

    .

    Israel inadhaniwa kuwa na silaha zake za nyuklia lakini inadumisha sera rasmi ya utata wa makusudi.

    Iran haina silaha za nyuklia na pia inakanusha kuwa inajaribu kutumia mpango wake wa nyuklia wa kiraia kuwa taifa lenye silaha za nyuklia.

    Mwaka jana shirika la uangalizi wa nyuklia duniani lilipata chembechembe za urani zilizorutubishwa hadi asilimia 83.7% - karibu sana na daraja la silaha - katika eneo fulani chini ya ardhi ya Iran. Iran ilisema "mabadiliko yasiyotarajiwa" katika viwango vya urutubishaji yanaweza kutokea.

    Iran imekuwa ikirutubisha madini ya uranium kwa asilimia 60 kwa zaidi ya miaka miwili kwa kukiuka makubaliano ya nyuklia ya 2015 na mataifa yenye nguvu duniani.

    Hata hivyo makubaliano hayo yamekaribia kuporomoka tangu Rais wa Marekani Donald Trump alipojiondoa kwa upande mmoja na kurejesha vikwazo vilivyolemaza Iran mwaka 2018. Israel ilikuwa imepinga makubaliano hayo ya nyuklia hapo awali.

    Soma zaidi:

    Israel yazitaka nchi kadhaa kuiwekea Iran vikwazo

    Tunachokijua kufikia sasa kuhusu mvutano wa Israel na Iran

  6. Israel yazitaka nchi kadhaa kuiwekea Iran vikwazo

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel anasema anaongoza "mashambulizi ya kidiplomasia dhidi ya Iran", huku serikali ikizingatia jibu la kijeshi kwa shambulio la kombora na ndege zisizo na rubani dhidi yake mapema Jumapili.

    Waziri wa mambo ya nje, Israel Katz, ameziandikia makumi ya nchi akitaka vikwazo viwekewe mpango wa makombora wa Iran.

    "Leo asubuhi nilituma barua kwa nchi 32 na kuzungumza na mawaziri kadhaa wa mambo ya nje na watu mashuhuri ulimwenguni kuomba mradi wa makombora wa Iran uwekewe vikwazo," Katz aliandika kwenye X.

    Vile vile ametoa wito kwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) kutangazwa kuwa shirika la kigaidi, "kama njia ya kuzuia na kuidhoofisha Iran". Anaongeza: "Iran lazima idhibitiwe - kabla mambo hayajaenda mrama".

  7. Tunachokijua kufikia sasa kuhusu mvutano wa Israel na Iran

    tgh

    Baraza la mawaziri la vita la Israel limekutana kujadili jinsi itakavyojibu mashambulizi ya Iran ya droni na makombora.

    Kwa upande wa Iran inasema itajibu ikiwa Israel itaishambulia, lakini haina mpango wa kuendeleza mashambulizi ikiwa Israel haitoshambulia.

    Huu hapa ni muhtasari wa mambo yaliyotokea jana kuhusu mvutano wa nchi hizi mbili:

    • Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian alisema shambulio la nchi yake ni sawa na "kutumia haki yake ya kujilinda" na Iran haitasita kulinda maslahi yake katika siku zijazo.
    • Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak alitoa wito kwa pande zote "kujizuia" na viongozi wengine kadhaa wa ulimwengu pia wametaka mvutano usikuzwe.
    • Ikulu ya Marekani na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Cameron wameeleza shambulio la Iran halikufaulu.
    • Ubelgiji, Ufaransa na Ujerumani ni miongoni mwa nchi zilizowaita mabalozi wa Iran na kulaani huku zikiongeza shinikizo la kimataifa dhidi ya Tehran.
    • Msemaji wa masuala ya usalama wa taifa wa Ikulu ya Marekani, John Kirby alidai kiasi cha misaada inayoingia Gaza kimeongezeka katika siku za hivi karibuni.
    • Lakini watu wengi wa Gaza bado wameyahama makazi yao kutokana na mapigano na kushindwa kurejea nyumbani, huku mashirika ya misaada yakionya juu ya baa la njaa.
  8. Msako waanzishwa baada ya washukiwa 'hatari' kutoroka seli Namibia

    z

    Polisi nchini Namibia wameanzisha msako mkali kuwasaka wafungwa 11 waliotoroka kutoka kwa seli ya polisi kaskazini-mashariki mwa mkoa wa Zambezi, vyombo vya habari vya serikali vimeripoti.

    Washukiwa hao waliokuwa wakisubiri kufikishwa mahakamani walikata paa la kituo cha polisi cha Katima Mulilo kabla ya kutoroka Jumatatu, Kisco Sitali, msemaji wa polisi katika eneo hilo, aliambia tovuti ya habari ya NBC.

    Vipande vya chuma na kamba zilizotengenezwa kwa blanketi, vitu vinavyoshukiwa kutumika katika mapumziko ya jela, vilipatikana kwenye seli, polisi walisema.

    Wenyeji wameonywa kuwa waangalifu kwani waliotoroka wanasubiri kufikishwa mahakamani kwa makosa makubwa, huku mmoja wao akiwa mkiukaji sheria wa mara kwa mara.

    "Wao ni hatari sana," Bw Sitali alisema, akiongeza kuwa mmoja wao alikuwa mfungwa wa zamani wa mauaji.

    Polisi walisema watatu kati ya waliotoroka tayari wamekamatwa tena.

    Zaidi ya wafungwa 100 ambao wanasubiri kufikishwa mahakamani waliwekwa katika seli hiyo, ambayo inaweza kuwazuia watu 16 pekee, vyombo vya habari vya serikali vilisema.

    Wakazi wamehimizwa kuripoti shughuli zozote zinazotiliwa shaka au vikundi vya watu kwa polisi.

  9. Radi na mvua yaua makumi ya watu nchini Pakistan

    Huku mvua zaidi ikitarajiwa katika siku zijazo, mamlaka ya Pakistani pia imeonya kuhusu maporomoko ya ardhi na mafuriko makubwa
    Image caption: Huku mvua zaidi ikitarajiwa katika siku zijazo, mamlaka ya Pakistan pia imeonya kuhusu maporomoko ya ardhi na mafuriko makubwa

    Takriban watu 39 wameuawa nchini Pakistan baada mvua kubwa kunyesha kusini magharibi mwa nchi hiyo kwa siku kadhaa.

    Baadhi ya waliouawa walikuwa wakulima waliopigwa na radi wakati wakivuna ngano, mamlaka ilisema.

    Picha mtandaoni zinaonyesha maeneo mengi ya mashamba yaliyosombwa na maji ya mvua.

    Mafuriko makubwa pia yametatiza usambazaji wa umeme na miundombinu ya usafirishaji.

    Pakistan imeshuhudia ongezeko la matukio ya hali ya hewa kali, kwani inakabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

    Mnamo 2022, theluthi moja ya nchi ilisombwa kabisa na mafuriko ambayo hayajawahi kutokea, na kuua zaidi ya watu 1,700 na kujeruhi maelfu ya wengine.

    Mamilioni waliachwa bila makao na kukosa maji safi ya kunywa kwa miezi kadhaa baadaye.

    Baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko ya 2022, ikiwa ni pamoja na Khyber Pakhtunkhwa na Balochistan, yameathiriwa tena na dhoruba za hivi majuzi.

    Huku mvua zaidi ikitarajiwa katika siku zijazo, Mamlaka ya Kitaifa ya Kukabiliana na Majanga ya Pakistan pia imeonya kuhusu maporomoko ya ardhi na mafuriko makubwa.

  10. Mkuu wa jeshi la Israel aapa kulipiza kisasi shambulizi la Iran

    xx

    Viongozi wa Israel wanaonekana kuhitimisha kuwa ili kuidhibiti Iran ipasavyo, ni lazima walipize kisasi shambulio lake kubwa ya makombora.

    Akitembelea kambi ya anga ya Nevatim, ambayo iliharibiwa kidogo na shambulio la Iran, mkuu wa jeshi la Israel, Herzi Halevi, aliwaambia wanajeshi wa jeshi la anga kwamba hatua ya Iran kurusha msururu wa makombora haiwezi kuachwa kupita bila kujibiwa.

    Changamoto kwa baraza la mawaziri la vita ni kutafuta njia ya kutoa ujumbe mkali bila kuchochea mgogoro wa kikanda.

    Iran ilifanya shambulizi lake ambalo halijawahi kushuhudiwa kulipiza kisasi kwa shambulio baya la anga jumba ladhidi ya ubalozi wake mjini Damascus, ambalo linadaiwa kufanywa na Israel, na imeashiria kwamba haina nia ya kuendelea na mashambulizi zaidi.

    Viongozi wa dunia wameelezea hofu kwamba sasa kuna uwezekano wa vita vya wazi zaidi kati ya mahasimu hao wa muda mrefu na ghasia zinazotokana na vita vya Gaza kuenea zaidi.

    Soma zaidi:

    Iran yaonya kufanya shambulizi baya zaidi ikiwa Israel italipiza kisasi

    Ni silaha gani zilitumika katika mashambulio ya Iran na Israeli ilizuiaje?

    Iron Dome: Fahamu jinsi mfumo wa ulinzi wa anga wa Israel unavyofanya kazi

  11. Video: Tazama kiongozi wa upinzani Georgia akimpiga ngumi mbunge wakati wa mjadala bungeni

    Video content

    Video caption: Kiongozi wa upinzani Georgia akimpiga ngumi Mbunge wakati wa mjadala

    Kiongozi wa upinzani Aleko Elisashvili alimpiga ngumi mbunge Mamuka Mdinaradze wakati wa mjadala kuhusu sheria iliyozua utata.

    Wakosoaji wanasema mswada wa "ushawishi wa kigeni" umechochewa na sheria za kimabavu zinazotumiwa na Urusi kukandamiza upinzani.

    Maelfu ya waandamanaji waliandamana katika mji mkuu wa Georgia Tbilisi siku ya Jumatatu wakitaka muswada huo uondolewe.

  12. Ethiopia: Mapigano yazuka katika mpaka wa Tigray na Amhara

    Mapigano ya mara kwa mara huzuka katika maeneo yanayozozaniwa kati ya majimbo ya Amhara na Tigray.
    Image caption: Mapigano ya mara kwa mara huzuka katika maeneo yanayozozaniwa kati ya majimbo ya Amhara na Tigray.

    Mapigano yamepamba moto katika moja ya maeneo yanayozozaniwa kati ya majimbo ya Tigray na Amhara nchini Ethiopia katika kipindi nadra cha vurugu baada ya makubaliano ya amani yaliyotiwa saini mwishoni mwa 2022 kumaliza moja ya vita mbaya zaidi barani Afrika.

    Wilaya ya Raya Alamata- inayozozaniwa na majimbo yote mawili- ilikuwa chini ya Tigray kusini kabla ya vita kuanza lakini tangu wakati huo imekuwa chini ya udhibiti wa vikosi vya Amhara.

    Wakazi waliambia BBC kwamba mapigano yalianza wikendi na kuendelea kwa siku kadhaa.

    Maafisa wa Amhara waliwashutumu wapiganaji wa kundi la Tigray Peoples Liberation Front (TPLF) kwa kuanzisha mashambulizi huku mkuu wa eneo la Kusini mwa Tigray akisema wanamgambo wa Amhara walifyatua risasi.

    Chama cha upinzani cha National Movement of the Amhara (NaMA) katika taarifa kililaumu TPLF ambayo ilisema ilikuwa ikianzisha "uvamizi."

    Akiandika kwenye X, Getachew Reda- mkuu wa utawala wa muda wa Tigray, aliyeanzishwa baada ya makubaliano ya amani- alisema "maendeleo" ya hivi karibuni katika maeneo hayo hayakuhusisha migogoro kati ya vikosi vya Tigray na serikali ya shirikisho au kati ya mikoa jirani ya Tigray na Amhara.

    Alilaumu "maadui" wa mpango wa amani "kutoka karibu au mbali" kwa matukio bila kutaja wao ni nani.

    Haijabainika kama kuna majeruhi wowote lakini vyombo vya habari vinavyounga mkono Amhara viliripoti kwamba vikosi vya Tigray viliingia katika baadhi ya wilaya siku ya Jumatatu.

    Hivi majuzi serikali ya shirikisho imesema jeshi litadhibiti maeneo yenye migogoro hadi suluhu litakapotolewa.

    Kuna wasiwasi kwamba hii inaweza kuzidisha mzozo unaoendelea tangu Agosti mwaka jana katika eneo la Amhara- Ethiopia lenye watu wengi zaidi- kati ya wanamgambo wa ndani na jeshi.

    Soma:

    Kwa nini wanamgambo wa Amhara nchini Ethiopia wanapambana na jeshi?

    Mgogoro wa Tigray Ethiopia: Fahamu uwezo wa jeshi la Tigray

  13. Bei ya mafuta yapanda huku Israel ikitathmini majibu kwa shambulio la Iran

    xx

    Bei ya mafuta ilipanda siku ya Jumanne huku uchumi wa China ukikua kwa kasi zaidi kuliko ilivyotarajiwa.

    Hata vivyo hali ya wasiwasi katika Mashariki ya Kati inaendelea kuweka soko kwenye msukosuko mkali baada ya Israel kusema kuwa itajibu shambulio la wikendi la Iran dhidi yake.

    Hatima ya Brent kwa usambazaji wa Juni ilipanda kwa senti 48, au 0.5%, hadi $90.58 kwa pipa kufikia leo Jumanne.

    Bei ya mafuta ghafi nchini Marekani kwa usambazaji wa Mei ilipanda kwa senti 49, au 0.6%, hadi $85.90 kwa pipa.

    Vigezo vilipanda juu ya ukuaji thabiti wa uchumi nchini China, mwagizaji mkuu wa mafuta duniani. Pato la taifa lilikua 5.3% katika robo ya kwanza, mwaka baada ya mwaka, data ya serikali ilionyesha, na kushinda matarajio ya wachambuzi.

    Iran inazalisha zaidi ya mapipa milioni 3 kwa siku ya mafuta ghafi kama mzalishaji mkuu ndani ya Shirika la Nchi Zinazouza Petroli (OPEC).

    Maelezo zaidi:

    Kwa nini wazalishaji wakuu wa mafuta duniani wanapunguza usambazaji wa bidhaa hiyo?

  14. Video: Tazama shujaa mmoja akimkabili mtu aliyebeba kisu aliyewaua watu sita Australia

    Video content

    Video caption: Video inaonyesha mshukiwa aliyewaua watu sita katika duka moja mjini Sydney Australia

    Mfaransa mmoja ambaye alijaribu kuzuia shambulio la mauaji katika duka moja kubwa mjini Sydney ameahidiwa visa ya Australia.

    Damien Guerot alipewa jina la shujaa baada ya kanda zake akikabiliana na Joel Cauchi aliyebeba kisu wakati wa shambulio la Jumamosi kusambaa mitandaoni.

    Joel Cauchi aliwaua watu sita na kuwajeruhi wengine 12 kabla ya kupigwa risasi na afisa wa polisi.

    Shambulio hilo la eneo la Bondi, ambalo polisi wanasema linaonekana kuwalenga wanawake, limetia hofu taifa zima.

  15. NASA: 'Mpango mpya unahitajika kusafirisha sampuli ya miamba kutoka Mars'

    Kusafirisha hadi duniani sampuli za miamba kutoka sayari ya Mars ni kazi ngumu sana ambayo itachukua miaka kadhaa.
    Image caption: Kusafirisha hadi duniani sampuli za miamba kutoka sayari ya Mars ni kazi ngumu sana ambayo itachukua miaka kadhaa.

    Jitihada za kurejesha sampuli za miamba kutoka sayari ya Mars hadi Duniani ili kuona ikiwa zina alama za maisha ya zamani zitapitia marekebisho makubwa.

    Shirika la anga za juu la Marekani linasema muundo wa sasa wa misheni haukuweza kurejesha vifaa kabla ya 2040 ikizigatiwa gharama ya dola bilioni 11 zitakazohitajika kufanya hivyo mapema si wazo endelevu.

    Nasa itatafuta maoni ya turubai kwa mbadala wa bei nafuu na wa haraka zaidi.

    Inatumai kuwa na suluhu litapatikana baadaye mwakani.

    Kurejesha sampuli za miamba kutoka Mars kunachukuliwa kuwa kipaumbele kimoja muhimu zaidi katika uchunguzi wa sayari, na imekuwa kwa miongo kadhaa.

    Kama vile mawe ya Mwezini yaliyoletwa nyumbani na wanaanga wa Apollo yalivyobadilisha uelewa wetu wa historia ya awali ya Mfumo wa Jua, vivyo hivyo nyenzo kutoka kwenye Sayari Nyekundu zinaweza kuelekeza mawazo yetu upya kuhusu uwezekano wa maisha katika sayari nyingine kado na dunia.

    Lakini Nasa sasa inakubali jinsi hali ilivyo mpango wa kuleta sampuli hizo ardhini hauwezi kufikiwa katika mazingira ya sasa ya kifedha.

    Maelezo zaidi:

    Mambo ya ajabu yaliogunduliwa sayari ya Mars

    Kwa picha: Siku 100 za kwanza za chombo cha Nasa katika sayari ya mars

    Mpango wa Marekani kupeleka watu Mars kufikia 2030

  16. Hofu ya dawa ya kikohozi: Tanzania, Rwanda na Afrika Kusini zaungana na Kenya na Nigeria kusitisha matumizi

    XX

    Mataifa ya Tanzania, Rwanda na Afrika Kusini yamejiunga pamoja na Kenya na Nigeria kusitisha matumizi ya dawa ya kikohozi kwa watoto kwa jina Benylin.

    Hii ni kutokana na wasiwasi kuhusu usalama wake baada ya vipimo vya maabara nchini Nigeria kubaini kuwa dawa hizo za kikohozi za kampuni ya Johnson & Johnson zilikuwa na sumu.

    Dawa hiyo ina kiungo ambacho uchunguzi umebaini kwamba kilisababisha vifo vya watoto nchini Gambia, Uzbekistan na Cameroon tangu mwaka 2022.

    Kemikali ya Diethylene glycol ni sumu kwa binadamu inapotumiwa na inaweza kusababisha figo kushindwa kufanya kazi.

    Dawa ambazo zimepigwa marufuku zilitengenezwa nchini Afrika Kusini mwaka 2021 na zinatarajia kupitisha muda wake wa matumizi mwezi huu wa Aprili mwaka 2024.

    Bodi ya madawa nchini Kenya imesema ya kwamba imeanzisha uchunguzi huku ikiwataka wananchi walionunua dawa hizo kuziregesha mara moja.

    Pia unaweza kusoma:

    Kashfa ya dawa ya kikohozi Gambia: akina mama wadai haki

    Dawa ya sumu za kikohozi ilitumwa vipi nchini Gambia?

  17. Mchezaji wa timu ya Al-Ittihad acharazwa viboko na shabiki Saudia

    Abderrazak Hamdallah alikuwa sehemu ya kikosi cha Morocco kwenye Kombe la Dunia la 2022
    Image caption: Abderrazak Hamdallah alikuwa sehemu ya kikosi cha Morocco kwenye Kombe la Dunia la 2022

    Shirikisho la Soka la Saudi Arabia litakagua upya kanuni za maadili ya mashabiki baada ya shabiki mmoja kuonekana akimchapa viboko mchezaji wa Al-Ittihad.

    Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa mechi baada ya Al-Ittihad kufungwa na Al-Hilal katika michuano ya Saudi Super Cup mjini Abu Dhabi.

    Picha zinaonyesha mshambuliaji wa Al-Ittihad, Abderrazak Hamdallah akimrushia maji shabiki, ambaye kisha anampiga mchezaji huyo mara mbili kwa kile kinachoonekana kama mjeledi.

    SAFF ilisema "imeshtushwa na matukio ya aibu".

    Hamdallah wa Morocco aliifungia timu yake ilipopoteza kwa mabao 4-1.

    "Kandanda nchini Saudi Arabia ni mchezo wa familia na, tunashukuru, machafuko ya mashabiki ni nadra sana," SAFF ilisema.

    "Ndio maana vitendo vya shabiki ''huyu'' vinaenda kinyume na yote ambayo soka la Saudia linawakilisha na tunalaani vikali tukio hilo."Kutakuwa na ukaguzi wa kina wa maadili ya mashabiki. Ukaguzi huo utahakikisha sheria na kanuni zilizoboreshwa zinawekwa ili kutoa adhabu kwa haraka ili kuzuia kurudiwa kwa matukio kama haya."

  18. Baraza la mawaziri la vita Israel lakutana kujadili jibu la shambulio la Iran

    Baraza la mawaziri la vita pia lilikutana Jumapili, kama inavyoonekana katika nakala hii ya serikali ya Israeli
    Image caption: Baraza la mawaziri la vita pia lilikutana Jumapili, kama inavyoonekana katika nakala hii ya serikali ya Israel.

    Baraza la mawaziri la vita la Israel limekutana kujadili jibu lake kwa mashambulizi ya Iran yasiyo na kifani. Israel haikuweka hadharani iwapo uamuzi ulikuwa umefikiwa.

    Washirika wake wamelaani vikali vitendo vya Iran, lakini wameitaka serikali ya Benjamin Netanyahu kujizuia.

    Wakati Iran ikiashiria kwamba inazingatia suala hilo kumalizwa, mkuu wa jeshi la Israel alisema shambulio hilo halitakosa jibu. "Tunatathmini hatua zetu dhidi ya shambulio hili la makombora mengi, makombora ya kusafiri, UAV hadi eneo la taifa la Israeli litajibiwa," Luteni Jenerali Herzi Halevi alisema.

    Hakutaja hatua itakayochukuliwa, au kutoa mpangilio wa nyakati.

    Mkuu wa zamani wa CIA David Petraeus aliambia kipindi cha World Tonight cha BBC Radio 4 kwamba Washington haitaki kuhatarisha ustawi wa uchumi wa dunia kutokana na Israel kulipiza kisasi dhidi ya Iran.

    Jenerali Petraeus, ambaye pia aliviongoza vikosi vya kimataifa vya Iraq na Afghanistan, alisema shambulio la Iran lilikuwa "jambo kubwa sana", na kwamba nchi za Magharibi zilipaswa kuelewa jinsi hii ilikuwa muhimu kwa Israel.

    Maelezo zaidi:

    Iran yaonya kufanya shambulizi baya zaidi ikiwa Israel italipiza kisasi

    Ni silaha gani zilitumika katika mashambulio ya Iran na Israeli ilizuiaje?

    Iron Dome: Fahamu jinsi mfumo wa ulinzi wa anga wa Israel unavyofanya kazi

  19. Hujambo na karibu