Got a TV Licence?

You need one to watch live TV on any channel or device, and BBC programmes on iPlayer. It’s the law.

Find out more
I don’t have a TV Licence.

Habari za moja kwa moja

Na Asha Juma na Ambia Hirsi

time_stated_uk

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo haya ya moja kwa moja. Kwaheri.

  2. Kenya yajiandaa kwa mvua zaidi huku idadi ya waliofariki kutokana na mafuriko ikifikia 70

    Vitongoji duni na makazi yasiyo rasmi jijini Nairobi yameathiriwa sana na mafuriko

    Mafuriko makubwa yamesababisha mamia ya maelfu ya watu kuyahama makazi yao kote Afrika Mashariki - na nchini Kenya waokoaji na mamlaka "wanajiandaa kwa uharibifu zaidi.

    "Hali inaendelea kuwa mbaya. Kufikia jana usiku tulikuwa tukiripoti zaidi ya watu 70 walikufa kote nchini," Seneta Edwin Sifuna, Seneta wa Kaunti ya Nairobi iliyoathiriwa zaidi na mafuriko, aliambia BBC.

    Mafuriko hayo yamesababishwa na mvua kubwa inayohusishwa na hali ya hewa ya El Niño

    Bw Sifuna aliongeza kuwa timu za uokoaji zinakadiria kuwa watu 100,000 wamelazimika kuyahama makazi yao.

    Michael Aiyabei, mkuu wa kamati ya kitaifa ya kushughulikia majanga, pia ameelezea wasiwasi. "Tunajiandaa kwa wakati mgumu zaidi," alisema.

    Zaidi ya watu 150 wamefariki kutokana na mafuriko katika nchi jirani ya Tanzania.

    Nchini Burundi, karibu watu 100,000 wamekimbia makazi yao.

  3. Rais Samia: Maamuzi yaibeba miaka 60 ya muungano Tanzania

    .
    Image caption: Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan

    “Tuna kila sababu ya kujivunia muungano wetu, nchi hii Tanzania imetokana na maamuzi yetu wenyewe katika kipindi chote cha miaka 60. Taifa hili likiwa na watu zaidi ya makabila 120 kwa bahati nzuri tunaunganishwa na lugha moja ya kiswahili,” ameeleza

    Rais wa Tanzania Samia Suluhu

    Rais Samia ametoa kauli hiyo katika Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano zilizofanyika jijini Dar es Salaam leo ambapo amewataka watanzania waendelee kuyaenzi maono ya viongozi hao.

    Tanganyika na Zanzibar ziliungana mwaka 1964 na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, muungano uliodumu muda mrefu zaidi Afrika.

    Samia alisema kama taifa kuna mengi ya kujivunia na kwamba amani iliyopo imeongeza nguvu katika muungano uliopo.

    "Kwa niaba yenu Wananchi Watanzania ninawashukuru kwa dhati Waasisi wa Muungano huu Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume pamoja na viongozi waliofuata baada yao kwa kutuleta pamoja na kujenga taifa huru, madhubutu na lenye matumaini,” alisema na kuongeza kuwa zawadi pekee anayoweza kuwapa wananchi ni kuendeleea kudumisha muungano huu na kuyaenzi maono yao.

    Ushirikiano wa kikanda

    Rais Samia amesisitiza kuongezeka kwa ushirikiano wa kikanda bila kujali mipaka

    Alisema, “Rais wa Kenya Ruto alininongoneza hapa anasema wajaluo wa Tanzania na wajaluo wa kwingine wako sawa na hata Rais Hichilema amesema hivyo hivyo, huwezi kutofautisha ukifika pale mpakani mwa Zambia na Tanzania, huwezi kuwatofautisha kwa hivyo tunashukuru waafrika wote ni wa moja.”

    Sherehe hizo zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwe Rais wa Kenya William Ruto, Rais wa DRC Felix Tshisekedi, Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye, Rais wa Umoja wa Comoros Azali Assoumani, Rais wa Jamhuri ya Zambia Hakainde Hichilema, Rais wa Shirikisho la Somalia Hassan Sheikh Mohamud na Rais wa Jamhuri Namibia Nangolo Mbumba.

  4. Vita vya Urusi na Ukraine: Marekani yaonya kuichukulia hatua China

    .
    Image caption: Antony Blinken

    Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken ameonya kuwa Washington itachukua hatua ikiwa China haitaacha kuipatia Urusi vitu vilivyotumika katika kuishambulia Ukraine.

    Akizungumza na BBC mjini Beijing, mwanadiplomasia mkuu wa Marekani alisema amewaeleza wazi wenzake "wanasaidia kusababisha tishio kubwa zaidi" kwa usalama wa Ulaya tangu Vita Baridi.

    Hakusema ni hatua gani Marekani ilikuwa tayari kuchukua.

    Lakini Bw Blinken pia alikuwa na nia ya kusisitiza hatua zimepigwa katika baadhi ya maeneo.

    Aliipongeza Beijing kwa kufanya juhudi katika kusimamisha usambazaji wa dawa ya fentanyl kufika Marekani.

    Uchina inasalia kuwa chanzo kikuu cha dawa ya fentanyl kwa Marekani, ambayo Ikulu ya White imesema inasababisha shida ya afya ya umma kote nchini.

  5. Onyo la kisheria la DR Congo kwa Apple ni 'hatua ya kwanza' - wakili

    The Apple logo

    Hatua ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutoa notisi rasmi kwa kampuni ya Apple ni "ya kwanza" ya nchi hiyo katika harakati za kupinga "unyonyaji" wa madini yake ghafi, wakili anayewakilisha serikali ya DR Congo ameiambia BBC.

    Wakili Mfaransa William Bourdon alizungumza na kipindi cha Newsday baada ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuishutumu Apple kwa kutumia madini "yaliyonyonywa kinyume cha sheria" katika bidhaa zake.

    Alikuwa miongoni mwa timu wanasheria ambao siku ya Alhamisi walituma notisi rasmi kwa kampuni kubwa ya teknolojia kwa niaba ya DR Congo, wakidai kuwa madini yanayotumiwa na Apple yanatoka kwenye migodi ambapo haki za binadamu zinakiukwa na waasi.

    Notisi hiyo ilionya hatua za kisheria iwapo vitendo hivyo vinavyodaiwa vitaendelea.

    Apple hapo awali ilisema hakuna ushahidi wowote wa wasambazaji wake walifadhili au kunufaisha vikundi vyenye silaha nchini DR Congo au nchi yoyote jirani.

    Bw Bourdon alisema: "Hii ni hatua ya kwanza, tutaendelea. Hii ni hatua ya kwanza ya sera mpya ya DRC. Tunataka kuweka maadili kwa jinsi malighafi inavyotumiwa katika nchi hii."

    Mawakili wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanaishutumu kampuni ya Apple kwa kununua madini yaliyotoroshwa kutoka mashariki mwa Kongo hadi nchi jirani ya Rwanda, ambapo yanasafishwa na kuunganishwa katika mnyororo wa kimataifa wa ugavi.

  6. UN yakosoa marufuku ya Burkina Faso dhidi ya BBC

    Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imesema "ina wasiwasi" kuhusu mamlaka nchini Burkina Faso kusitisha matangazo ya BBC na Voice of America(VOA).

    Kama tulivyoripoti hapo awali, mamlaka ya kudibiti vyombo vya habari nchini Burkina Faso imesitisha kwa muda wa wiki mbili matangazo ya vituo hivyo viwili vya habari kwa kuangazi ripoti ya shirika la kutetea binadamu la Human Rights Watch (HRW) ambayo ilishutumu jeshi la Burkina Faso kwa mauaji ya raia.

    Msemaji wa Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa Marta Hurtado alisema katika taarifa yake: "Vikwazo dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari na nafasi ya kiraia lazima vikome mara moja. Uhuru wa kujieleza ikiwa ni pamoja na haki ya kupata habari ni muhimu katika jamii yoyote hasa ikizingatiwa mamlaka iliyo madarakani ni ya mpito nchini Burkina Faso."

  7. Kenya 'inajadiliana' na DR Congo kuhusu kukamatwa kwa wafanyakazi wa KQ

    Hapo awali, tuliripoti kuwa shirika la ndege la Kenya Airways linashutumu kitengo cha kijeshi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa kuwazuilia wafanyikazi wake kwa wiki moja.

    Afisa wa Kenya sasa amezungumza kuhusu suala hilo, akisema ujumbe wa Kenya katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kinshasa, "unashughulikia suala hilo".

    Katibu Mkuu wa Masuala ya Kigeni, Korir Sing'Oei alisema kwenye mtandao wa kijamii wa X: "Kenya imekerwa sana na tukio la kukamatwa na kuwekwa kizuiliwa kwa raia wake wanaofanya shughuli za kibiashara nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo."

    Mamlaka ya DRC bado haijatao tamko lolote kuhusiana na tuhuma hizo.

    Hata hivyo, leo (Ijumaa) mchana shirika la habari la Reuters liliripoti kwamba Patrick Muyaya, msemaji wa serikali ya DR Congo, alisema atatoa jibu "baadaye".

  8. Mtoto aliyeokolewa kutoka tumboni mwa mama aliyeuawa Gaza afariki

    mtoto

    Mtoto aliyeokolewa kutoka tumboni mwa mamake aliyekuwa mahututi baada ya shambulizi la anga la Israel kusini mwa Gaza amefariki, BBC imebaini.

    Mtoto Sabreen al-Sakani alizaliwa kupitia upasuaji katika hospitali ya Rafah muda mfupi baada ya saa sita usiku Jumapili.

    Katikati ya matukio ya machafuko madaktari walimfufua mtoto, kwa kutumia pampu ya mkono kupeleka hewa kwenye mapafu yake.

    Hata hivyo alifariki siku ya Alhamisi na amezikwa karibu na mamake yake.

    Mtoto Sabreen alikuwa miongoni mwa watoto 16 waliouawa katika mashambulizi mawili ya anga huko Rafah wikendi iliyopita.

    Wote waliuawa katika shambulio la bomu lililolenga nyumba walimokuwa wakiishi.

    Video content

    Video caption: Tazama mtoto huyo alivyookolewa.
  9. Gaza: Marekani yaanza kujenga bandari ya kuelea kuwezesha uwasilishaji misaada

    xx

    Jeshi la Marekani limeanza kujenga badari kubwa inaloelea kwenye pwani ya Gaza ili kuwezesha uwasilishaji wa misaada ya kibinadamu, idara ya ulinzi imesema

    Meli zitapeleka misaada kutoka Cyprus hadi kwenye bandari hiyo ambapo itapakiwa kwenye malori na kusafirishwa hadi Gaza. Kambi hiyo itaunganishwa na ufuo kwa kutumia daraja la muda, ambayo itatumiwa lori za kubeba mizigo.

    Maafisa wa Marekani wanasema bandari hiyo itaanza kufanya kazi mapema mwezi Mei lakini wanajeshi wa Marekani hawatakanyaga ardhi ya Gaza.

    Mpango huo ulitangazwa kwa mara ya kwanza na Rais Joe Biden mwezi Machi kama sehemu ya juhudi za kukabiliana na njaa huko Gaza iliyochangiwa na matatizo ya utoaji wa misaada, wakati Israel ikiendelea na operesheni yake ya kijeshi dhidi ya Hamas.

    Umoja wa Mataifa umeonya kuwa njaa katika Ukanda wa Gaza ni "tatizo isiyoepukika" na watoto wanakufa kwa njaa.

    Zaidi ya wanajeshi 1,000 wa Marekani wanatarajiwa kuhusika katika ujenzi wa bandari inayoelea, lakini Pentagon iliweka wazi tangu mwanzo kwamba wafanyikazi wake hawatakanyaga ardhini.

    Njia kuu itaunganishwa baharini, ili kuwezesha vikosi vya Marekani kutokanyaga ardhini.

    Na chombo cha majini cha Uingereza katika eneo la mashariki mwa Mediterania kitakuwa bweni linaloelea kwa wanajeshi na mabaharia wa Marekani.

    Wataishi na kulala ndani ya RFA [Royal Fleet Auxiliary] Cardigan Bay.

    Msemaji wa Pentagon, Meja Jenerali Pat Ryder, aliuambia mkutano wa waandishi wa habari siku ya Alhamisi: "Meli za kijeshi za Marekani... zimeanza kujenga hatua za awali za bandari ya muda na njia kuu baharini." Alisema kuwa barabara hiyo itaunganishwa na bandari ya muda, "ambayo iko nje ya bahari, na njia ambayo hatimaye itaungaishwa na nchi kavu na kutiwa nanga."

    Marekani inasema kwamba mara mfumo huo utakapofanya kazi, hadi lori 150 za msaada zinaweza kuwasilishwa kwa siku na milo milioni mbili, ya kutosha kulisha karibu wakazi wote milioni 2.3 wa eneo hilo.

  10. Marta: Mchezaji wa Brazil kustaafu soka ya kimataifa

    Marta alifunga mabao 17 katika michuano sita ya Kombe la Dunia
    Image caption: Marta alifunga mabao 17 katika michuano sita ya Kombe la Dunia

    Mchezaji wa Brazil Marta anasema atastaafu soka ya kimataifa mwaka huu.

    Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 38 ndiye mfungaji bora Brazil katika soka ya kimataifa.

    Marta anaweza kucheza mechi yake ya sita kwenye Michezo ya Olimpiki ikiwa atachaguliwa kwenye kikosi cha Brazil msimu huu wa joto huko Paris.

    "Iwapo nitateuliwa kushiriki michezo ya Olimpiki, nitafurahia sana, kwa sababu, bila kujali kama nitashiriki kwenye Olimpiki au la, huu ni mwaka wangu wa mwisho kuiwakilisha timu ya taifa," aliiambia kituo cha habari cha CNN huko Brazil.

    "Hakutakuwa na Marta tena kutoka 2025 katika timu ya taifa kama mchezaji."

    Alishinda fedha za Olimpiki huko Athens 2004 na Beijing 2008, na kupoteza kwa Marekani mara zote mbili.

    Marta ndiye mfungaji bora wa mabao katika Kombe la Dunia, wanaume na wanawake, akifunga mara 17 katika mechi 23 katika matoleo sita ya michuano hiyo

    Alikaribia kuchukua ubingwa wa Kombe la Dunia mwaka wa 2007 wakati Brazil ilipomaliza ya pili nyuma ya Ujerumani.

    Baada ya Brazil kushindwa kufika hatua ya mtoano katika Kombe la Dunia la majira ya joto lililopita, alisema "hakuna tena Kombe la Dunia kwa Marta".

    Marta, ambaye amechezea klabu ya Orlando Pride tangu 2017, alisema anafurahi kupokezana kijiti hicho kwa kizazi kijacho cha wanasoka wa Brazil.

    "Tuna timu iliyofuzu haswa na wasichana wenye talanta ambao, kadiri miaka inavyosonga, utaona ninachozungumzia," alisema.

    "Kwa sababu ya hili najisikia raha sana kusema: 'Sikiliza, ninapita kwako, nakupokeza kijiti nawe wewe uendelee kupokezana urithi huu.'

  11. Burkina Faso yasitisha matangazo ya BBC kwa kuripoti madai ya mauaji

    BBC Monitoring

    Mwanajeshi kaskazini mwa Burkina Faso mnamo 2019.

    Mamlaka ya kudhibiti vyombo vya habari nchini Burkina Faso amesimamisha kwa muda wa wiki mbili vipindi vya BBC Afrique na Voice of America (VOA) kwa kuangazia ripoti ya shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch inayoshutumu jeshi la Burkina Fasso kwa kutekeleza dhuluma dhidi ya raia.

    Upatikanaji wa tovuti na majukwaa ya kidijitali ya BBC, VOA, na Human Rights Watch pia umesitishwa ndani ya Burkina Faso.

    "Kwa hivyo, BBC na VOA, kupitia waandishi wao huko Burkina Faso, waliamriwa kwa njia ya simu kuacha mara moja kutangaza tena kipindi hicho kwenye majukwaa yao yote," shirika la habari linalomilikiwa na serikali la Agence d'Information du Burkina (AIB) liliripoti Alhamisi.

    Baraza Kuu la Mawasiliano (CSC) lilionya zaidi vyombo vyote vya habari vya humu nchini dhidi ya kusambaza makala hiyo, likitishia kuwawekea vikwazo wanaokiuka agizo hilo.

    VOA ilisema katika makala iliyochapishwa Ijumaa kwamba "inasimama na kuripoti yake kuhusu Burkina Faso na inakusudia kuendelea kuangazia kikamilifu na kwa haki shughuli nchini humo".

    HRW ilichapisha ripoti hiyo siku ya Alhamisi ikilishutumu jeshi la Burkina Faso kwa kuwaua raia 223 mnamo tarehe 25 Februari kaskazini mwa nchi.

    Mnamo Desemba 2023, taifa hilo la Afrika Magharibi lilifungia gazeti la Ufaransa la Le Monde likiishutumu kwa kuripoti upendeleo.

    Pia ilisimamisha vyombo vingine vitatu vya habari vya kimataifa kwa nyakati tofauti mwaka jana, ikiwa ni pamoja na jarida la lugha ya Kifaransa Jeune Afrique, kituo cha televisheni chaUfaransa La Chaîne Info (LCI) na shirika la habari la Ufaransa la Ufaransa24.

    Soma:

    Burkina Faso: Je, wakosoaji wa serikali huadhibiwa kwa kupelekwa mstari wa mbele wa vita?

  12. Shirika la ndege la Kenya laishtumu DR Congo kwa kuwazuilia wafanyakazi wake

    xx

    Shirika la ndege la Kenya (KQ) limelishutumu jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa kuwashikilia wafanyakazi wake wawili tangu wiki iliyopita, licha ya uamuzi wa mahakama kuwaachilia huru.

    Wawili hao walikamatwa na kitengo cha kijasusi cha kijeshi cha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Ijumaa iliyopita kwa madai ya kutokuwa na nyaraka za forodha kwenye shehena ya "thamani", KQ ilisema katika taarifa.

    Shirika hilo la ndege lilisema halikusafirisha mizigo hadi Kinshasa kutokana na kutokamilika kwa nyaraka.

    "Juhudi zote za kuwaeleza maafisa wa kijeshi kwamba KQ haikukubali shehena hiyo kwa sababu ya kutokamilika kwa nyaraka ziliambulia patupu," iliongeza.

    Maafisa hao wa kijeshi waliwazuilia wafanyikazi hao wawili wa KQ hadi Jumanne, wakati maafisa wa ubalozi wa Kenya na timu ya shirika la ndege waliporuhusiwa kuwatembelea kwa muda mfupi.

    Mnamo Alhamisi, KQ ilisema mahakama ya kijeshi ilikubali ombi lake la kutaka wafanyikazi hao waachiliwe huku uchunguzi ukiendelea.

    "Licha ya maagizo ya mahakama, kitengo cha kijasusi cha kijeshi bado kinawashikilia kwa siri, lakini hawa ni raia wanaozuiliwa katika kituo cha kijasusi cha kijeshi," shirika hilo la ndege liliongeza.

    Simu za wafanyikazi hao zilichukuliwa wakati wa kukamatwa kwao, kulingana na KQ.

    Haijulikani ni shehena gani iliyotajwa na mamlaka nchini DR Congo bado hazijatoa maoni kuhusu suala hilo.

  13. Tazama: Waandamanaji wanaoiunga mkono Palestina wakabiliana na polisi katika chuo kikuu Marekani

    Video content

    Video caption: Waandamanaji wa Gaza wakabiliana na polisi katika Chuo kikuu cha Emory

    Video inaonyesha machafuko yakitokea katika Chuo kikuu cha Emory katika jimbo la Atlanta Greorgia nchini Marekani wakati polisi walipokuwa wakiondoa kambi iliyowekwa na waandamanaji wanaoiunga mkono Palestina.

    Kulingana na Chuo hicho kikuu ‘’watu wasio na uhusiano’’, na shule hiyo wamekamatwa.

    Afisa kutoka jeshi la polisi wa chuo hicho aliwambia waandishi wa habari kwamba wale waliokamatwa watashtakiwa kwa makosa ya uhalifu na kuwashambulia maafisa wa polisi.

  14. China yaionya Marekani dhidi ya "kuvuka mipaka yake"

    .

    Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi amemuonya mwenzake wa Marekani Antony Blinken dhidi ya Marekani "kuvuka mipaka yake", wakati wanadiplomasia wakuu wa nchi hizo mbili walipokutana mjini Beijing siku ya Ijumaa.

    Bw Wang alifungua mkutano huo kwa swali ambalo lilisikika zaidi kama onyo: "Je, China na Marekani zinapaswa kufuata mwelekeo sahihi wa kusonga mbele kwa utulivu au kurudi nyuma tulipokuwa?"

    Uhusiano wa China na Marekani unaanza kuwa imara, lakini bado unajaribiwa na "sababu hasi", aliongeza.

    Nchi zote mbili zinaweza kujihusisha katika ushirikiano au makabiliano, na hata "kuingia kwenye mzozo", Bw Wang alisema.

    Aliweka kile alichokiita mipaka ya China kuhusu mamlaka yake, usalama na maendeleo yake na kuionya Marekani kutoivuka.

    "Mambo hasi katika uhusiano wa [Marekani na China] bado yanaongezeka na uhusiano huo unakabiliwa na kila aina ya usumbufu," Bw Wang alisema.

    "Haki halali za maendeleo ya China zimekandamizwa bila sababu na maslahi yetu ya msingi yanakabiliwa na changamoto," aliongeza.

    Bw Wang hakutaja changamoto hizi, lakini kuna mambo kadhaa nyeti kati ya mataifa hayo mawili yenye nguvu, ikiwa ni pamoja na misimamo yao kuhusu Bahari ya Kusini ya China, uungaji mkono wa Marekani kwa serikali ya Taiwan, na haki za binadamu.

    Bw Blinken, ambaye yuko katika ziara yake ya pili nchini China katika muda wa chini ya mwaka mmoja, alikuwa mwangalifu zaidi katika matamshi yake kwa Bw Wang mbele ya waandishi wa habari.

    China na Marekani zina jukumu la pamoja la kuendeleza uhusiano na "diplomasia hai", alisema.

    Hata hivyo, alisema atakuwa wazi kuhusu tofauti za nchi zao ili kuepuka maneno potofu katika kile alichokiita uhusiano wenye athari kubwa zaidi duniani.

    Kuishi katika maeneo ya uhasama wa kivita kati ya Marekani na China

  15. Mahakama ya Juu Zaidi ya Marekani yagawanyika kuhusu iwapo Trump anaweza kushtakiwa au la

    .

    Kwa takriban saa tatu siku ya Alhamisi, Mahakama ya Juu Zaidi ilijadili iwapo marais wa zamani wana kinga dhidi ya kushtakiwa na nini maana yake hasa ikiwa kinga hiyo ipo.

    Matokeo yake yataamua ikiwa Rais wa zamani Donald Trump anaweza kushtakiwa kwa madai ya kujaribu kuharibu uchaguzi wa 2020.

    Kwa uamuzi wowote, kila haki ilionyesha kwamba ingetengeneza demokrasia ya Marekani kwa miaka ijayo.

    "Tunaandika sheria ya vizazi," Jaji Neil Gorsuch alisema.

    Kesi hiyo, iliyosikilizwa katika kikao maalum yalijikita kwenye madai ya Bw Trump kwamba ana haki ya kutoshtakiwa kwa makosa ya jinai kwa vitendo vinavyofanywa akiwa ofisini.

    Kulingana na Bw Trump, kinga hii inamkinga dhidi ya mashtaka ya uhalifu yaliyoletwa na Wakili Maalum wa Marekani Jack Smith kwamba alidaiwa kujaribu kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa 2020.

    Kesi hiyo itasitishwa hadi mahakama itakapotoa uamuzi wake, unaotarajiwa mwezi Juni.

    Soma zaidi:

    Je, Trump anaweza kufungwa jela na maswali mengine muhimu

  16. Chanjo ya kwanza ya mRNA ya saratani ya ngozi yaanza kufanyiwa majaribio Uingereza

    .

    Jaribio muhimu la chanjo ya kwanza ya mRNA dhidi ya aina hatari zaidi ya saratani ya ngozi - melanoma - sasa inaendelea nchini Uingereza.

    Steve Young, 52, kutoka Stevenage, Herts, ambaye alikuwa na uvimbe kwasababu ya melanoma alikatwa ngozi ya kichwa chake Agosti iliyopita, ni mmoja wa wagonjwa wa kwanza kufanyiwa majaribio ya chanjo hiyo.

    Imeundwa kusaidia mfumo wake wa kinga kutambua na kufuta seli zozote za saratani zilizobaki.

    Na kwa matumaini, hiyo inamaanisha saratani yake haitarudi.

    Chanjo, mRNA-4157 (V940), hutumia teknolojia sawa na chanjo za sasa za Covid na inajaribiwa katika majaribio ya Awamu ya Tatu ya hatua ya mwisho.

  17. Kampuni mama ya China yasema hakuna mpango wa kuuza programu ya TikTok

    .

    Kampuni mama ya TikTok ya China ya ByteDance inasema haina nia ya kuuza programu hiyo maarufu ya video baada ya Marekani kupitisha sheria ya kuilazimisha kuiuza au kupigwa marufuku Marekani.

    "ByteDance haina mpango wowote wa kuuza TikTok," kampuni hiyo ilichapisha kwenye akaunti yake rasmi ya Toutiao, mtandao wa kijamii unaomiliki.

    TikTok haikujibu mara moja ombi la maoni kutoka kwa BBC.

    Mapema wiki hii, TikTok ilisema itapinga mahakamani sheria hiyo iliyo "kinyume cha katiba".

    Kauli hiyo kutoka kwa ByteDance inawadia baada ya ripoti za vyombo vya habari kwamba ilikuwa inachunguza chaguzi za kuuza TikTok bila algorithm inayoiwezesha.

    "Ripoti za vyombo vya habari vya kigeni kuhusu ByteDance kuuza TikTok sio kweli," kampuni hiyo ilisema.

    Hatua ya kuuza au kupiga marufuku ilitiwa saini kuwa sheria na Rais wa Marekani Joe Biden siku ya Jumatano.

    Ilianzishwa kwa sababu ya wasiwasi kwamba TikTok inaweza kushirikisha data ya mtumiaji na serikali ya Uchina - madai ambayo imekuwa ikikana kila wakati.

    Hata hivyo, TikTok haikabiliani na marufuku ya mara moja nchini Marekani.

    Sheria mpya inaipa ByteDance miezi tisa ya kuuza programu hiyo, na muda wa ziada wa miezi mitatu, kabla ya marufuku inayoweza kutekelezwa kutokea.

    Hiyo ina maana kwamba tarehe ya mwisho ya kuuza ina uwezekano mkubwa itakuwa wakati fulani mnamo 2025, baada ya mshindi wa uchaguzi wa urais wa 2024 kuchukua ofisi.

    Maelezo zaidi:

    Ni kwanini Marekani ina wasiwasi kuhusu usalama wa TikTok ?

    Je, Mmiliki wa TikTok yuko tayari kupoteza programu yake maarufu?

    Wakosoaji wa TikTok wanaogopa nini - na tuhuma zao zina uhalali gani?

  18. China inataka kuagiza mamilioni ya lita za maziwa ya ngamia wa Wasomali wa Kenya

    f

    Ngamia sio mifugo! Ni msemo maarufu katika jamii ya wafugaji wa Kisomali, msemo huo ni muhimu zaidi kuliko maneno yake, sababu ni kwamba ngamia ndiye kitu cha thamani zaidi katika maisha yao.

    Ngamia ni mnyama maarufu kutokana na maziwa yake yanayopendwa sana, na kutokana na hilo serikali ya Uchina imewasilisha ombi la maziwa ya ngamia kwa serikali ya Kenya kama ilivyofichuliwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara na Wenye Viwanda nchini Kenya, Dk Erick Rutto, ambaye alisema China inataka kununua lita milioni 9 kwa mwaka.

    b

    Dk Erick Rutto alibainisha kuwa hii ni fursa nzuri kwa wafugaji katika eneo la Kaskazini Mashariki mwa Kenya. Alisema kuwa soko lililo tayari la maziwa ya ngamia litafawafaisi wafugaji wa Kisomali wanaoishi katika eneo la Kaskazini Mashariki mwa Kenya.

    Aliongeza kuwa kiasi hicho ambacho ni sawa na fedha za Kenya shilingi bilioni 5.2, ambazo sawa na takriban dola milioni 40 za Marekani, zinaweza kupatikana kila mwaka kutoka kwa soko hili.

    Soma zaidi:

    Zifahamu faida za maziwa ya ngamia zisizojulikana

  19. Vita vya Ukraine: Ukraine yaondoa mizinga ya Abrams vitani kwa sababu ya ndege zisizo na rubani – AP

    g

    Jeshi la Ukraine limeondoa vifaru vya vyake vya Abrams M1A1 katika vita vyake na Urusi kutokana na upelelezi na ndege zisizo na rubani za Urusi, ambazo sasa zinavamia anga la uwanja wa vita. Mizinga iligeuka kuwa hatari sana kwa droni, liliandika shirika la habari la Associated press (AP)

    Maafisa wawili wa kijeshi wa Marekani waliozungumza na waandishi wa habari kwa sharti la kutotajwa majina yao kuhusu hatua ya Waukraine ya kuiondoa mizinga ya Abrams katika maeneo ya vita, na katika mahojiano na AP Makamu mwenyekiti muungano wa wakuu wa majeshi nchini Marekani alisema kwamba wanamgambo wa Marekani na Ukraine sasa wanafikiria pamoja kuhus jinsi ya kutumia mizinga katika hali mpya ambayo inapojitokeza.

    Marekani ilipeleka a mizinga 31 ya Abrams kwenda Ukraine mnamo Januari 2023. Halafu ilipangwa kwamba mizinga hii na mingine iliyopelekwa huko na washirika ingesaidia jeshi la Ukraine kuvunja mistari ya ulinzi ya Urusi na kuyateka tena maeneo yaliyochukuliwa.

    Lakini tangu wakati huo hali imebadilika sana:anga la juu ya mstari wa mbele wa mapigano limejaa ndege zisizo na rubani. "Hakuna nafasi wazi ambayo unaweza kupenya bila kuogopa kutambuliwa," afisa mmoja wa kijeshi aliwaeleza wanahabari siku ya Alhamisi.

    Kulingana naye, mizinga mitano ya Abrams kati ya 31 tayari imepotea.

    "Kuhusiana na jinsi teknolojia ilivyobadilika, silaha nyingi katika mazingira yaliyojaa ndege zisizo na rubani zinaweza kuwa hatarini," Adm. Christopher Grady, Makamu mwenyekiti muungano wa wakuu wa majeshi nchini Marekani, aliiambia AP.

    "Tutafanya kazi na washirika wetu wa Ukraine na washirika wengine mashinani na kuwasaidia kufikiria jinsi ya kutumia teknolojia hii katika mazingira yaliyobadilika ambapo kila kitu kinaonekana mara moja," Admiral Grady aliahidi.

    Vita vya Ukraine: Mengi zaidi

  20. Vitabu vyenye sumu ya arseniki vyaondolewa katika maktaba ya Ufaransa

    .

    Vitabu vinne vimeondolewa kwenye maktaba ya kitaifa ya Ufaransa kwa wasiwasi kwamba majalada yao yanaweza kuwa yametiwa sumu hatari ya arseniki.

    Vitabu vya karne ya 19, vilivyochapishwa nchini Uingereza, vyote vina majalada ya kijani kibichi.

    Arseniki ilikuwa kawaida kutumika kwa rangi za vitabu wakati huo.

    Vitabu vilivyotolewa kwenye maktaba vilitambuliwa kuwa hatari na watafiti wa Chuo Kikuu cha Delaware.

    Maktaba hiyo ilisema kwamba vitabu hivyo vitasababisha madhara madogo tu kwa wanaovishika au kuvisoma.

    "Tumeweka vitabu hivi katika karantini na maabara ya nje itavichambua ili kutathmini ni kiasi gani cha arseniki kilichopo katika kila jalada," msemaji kutoka Maktaba ya Kitaifa ya Ufaransa alisema.

    Timu imechunguza mamia ya majalada ya vitabu tangu 2019 na kuandaa orodha ya vitabu ambavyo vinaweza kuwa hatari.

    Wachapishaji wa enzi za Victoria walitumia arseniki kupaka rangi kwenye majalada ya vitabu.

    Kundi linalohusika na vitabu aina hiyo wanasema vitabu vilivyowekwa sumu vinapaswa kuhifadhiwa kwa tahadhari na vinaweza kuhatarisha afya kwa wale wanaovitumia.

    Shirika la Afya Ulimwenguni linaonya dhidi ya mfiduo wa muda mrefu wa arseniki kuanzia maji ya kunywa hadi chakula, likisema kwamba dutu hii "ni sumu kali".

    Pia unaweza kusoma:

    Muuza sumu anayehusishwa na vifo vya watu 130 waliojiua Uingereza akabiliwa na BBC