Got a TV Licence?

You need one to watch live TV on any channel or device, and BBC programmes on iPlayer. It’s the law.

Find out more
I don’t have a TV Licence.

Habari za moja kwa moja

Na Abdalla Seif Dzungu na Asha Juma

time_stated_uk

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu ya moja kwa moja. Kwaheri

  2. Jinsi mijadala ya maadhimisho inavyokinzana na hali halisi ya waandishi lakini wengi wana matumaini

    Sammy Awami

    BBC News, Dar es Salaam

    Mwaka mpya wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari lakini ahadi za viongozi wa juu kuhusu tasnia ya habari na wanahabari wengine si mpya sana.

    Wakati wa hotuba yake ya kuhitimisha kilele cha maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Habari Duniani, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amedai kwamba serikali ya awamu ya sita imefanya mengi kuunga mkono uhuru na maslahi mapana ya vyombo vya Habari.

    “Serikali imekuwa ikijizatiti na kujitolea kulinda haki za wanahabari pamoja na swala la kuunga mkono uhuru wa wanahabari katika kutekeleza majukumu yenu ya kila siku,” alisema Majaliwa

    Wakati kauli hizi zinapamba sherehe za maadhimisho kama haya, waana habari wengi hawafaidi haki au uhuru unaotajwa na waziri mkuu.

    Kwa mujibu wa takwimu za utafiti uliofanywa na asasi ya kiraia Twaweza Novemba 2023, asilimia 76 walisema hawako huru kufanya habari zinazokosoa kauli na vitendo vya serikali.

    Chama Kikuu cha waandishi wa habari pia kimekuwa kikinakili makumi ya vitendo vya unyanyasaji dhidi ya waandishi wa habari vinavyofanywa na watumishi wa serikali.

    Katika hili, waandishi wa habari waliozungumza katika utafiti wa Twaweza walisema asilimia 56 ya vyanzo vya vitisho katika kazi zao ni maofisa umma katika ngazi ya serikali za mitaa.

    Hata hivyo, wahudhuriaji wa maadhimisho haya wanadai kutiwa moyo na kauli za kuhakikishiwa kutoka kwa waziri mkuu juu ya kuboreshwa kwa mazingira ya uandishi wa habari nchini.

    “Mimi nafurahi kwamba unamsikia waziri mkuu au waziri wa sekta, akijifunga mbele ya hao wanahabari. Ni vizuri tufanye majaribio ya kufanya kazi zetu, na kila tunapopata tukio lolote linaloathiri usalama wetu sisi kama waandishi wa habari tunaseme mara moja” alisema Ernest Sungura, Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania.

    Matumaini ya mwandishi wa The Chanzo Dodoma, Jackline Kuwanda yapo katika dhana ya kukumbushana juu ya nini kinachoweza kufanyika hata kama haamini kuna kitu kikubwa sana kitatokea baada ya maadhimisho haya.

    “Maadhimisho haya yana umuhimu mkubwa kwasababu yanakumbusha kwamba vyombo vya habari vifanye nini,” alisema Kuwanda.

  3. Msemaji wa serikali: Kimbunga Hidaya kinapungua nguvu Tanzania

    Serikali ya Tanzania imethibitisha kuwa kimbunga ‘Hidaya’ kinaendelea kusogea kuelekea pwani ya nchi hiyo.

    Msemaji mkuu wa serikali ya Tanzania, Mobhare Matinyi amesema, hata hivyo amesema kuwa kasi ya kimbunga hicho inapungua.

    “Mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa baharini inaonesha uwezekano wa kasi ya kimbunga hicho kupungua zaidi ndani ya saa 12 zijazo, jambo ambalo ni taarifa njema huku kikiendelea kusogelea pwani ya Tanzania. Kimbunga hiki kinatarajiwa kuendelea kuwepo hadi tarehe 5 Mei na kitaendelea kupungua nguvu kwa mujibu wa vipimo vya wataalamu wetu.” Alifafanua.

    Msemaji huyo mkuu wa serikali ameeleza zaidi kuwa “Uwepo wa kimbunga Hidaya karibu na pwani ya nchi yetu kunatarajiwa kutawala na kuathiri mfumo wa hali ya hewa hapa nchini ikiwa ni pamoja na kusababisha vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani ikiwa na pamoja na kisiwa cha Mafia, Dar es Salaam, pamoja na mikoa ya Tanga, Morogoro na visiwa vya Unguja na Pemba. Tayari vipindi vya mvua na upepo vimeanza katika mikoa ya Pwani na Lindi”.

    Amewataka wakazi wa maeneo yaliyotajwa kuathirika na kimbunga ‘Hidaya’ kuendelea kufuatilia taarifa za mamlaka ya hali ya hewa na maelekezo ya taasisi za serikali na pia kuchukua tahadhari.

    Mara ya mwisho Tanzania Bara kupigwa kimbunga kikali ilikuwa mwaka 1952 wakati huo ikiitwa Tanganyika na kuathiri eneo la mkoa wa Lindi. Kabla ya hapo kimbunga kingine kikali kiliipiga Zanzibar mwaka 1872.

    Katika miaka ya karibuni kulitokea kimbunga Jobo mwaka 2021 ambacho hakikuwa na athari kubwa zaidi ya mvua za wastani na upepo. Hali kama hiyo ilitokea mwaka 2019 wakati wa kimbunga Kenneth huko mkoani Mtwara lakini kilikuwa na madhara makubwa nchini msumbiji na Malawi.

  4. Mafuriko Kenya: Nyumba za mabanda zilizojengwa karibu na mito bomolewa

    Matukio kutoka Mukuru Kwa Reuben yanaonyesha kubomolewa kwa mamia yamakazi yenye nyumba za mabanda katika Kaunti ya Nakuru nchini Kenya. Hatua hii inafuatia agizo la Rais wa Kenya William Ruto.

    Agizo hilo linaamuru kuondolewa kwa majengo yoyote yaliyo ndani ya mita 40 kutoka kwenye mto. Hizi ni baadhi ya picha kutoka eneo la Mukuru Kwa Reuben:

    h
    g
    b
    BBC
  5. Kimbunga Hidaya kimeendelea kuimarika zaidi huku kasi ya upepo ikiongezeka hadi kufikia kilomita 140 kwa saa

    .

    Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kutoa taarifa ya mwenendo wa kimbunga HIDAYA kilichopo katika Bahari ya Hindi mashariki mwa pwani ya nchi yetu.

    ‘’Kimbunga HIDAYA kimeendelea kuimarika na kusogea kuelekea maeneo ya pwani ya nchi yetu ambapo hadi kufika saa tatu asubuhi ya tarehe 03 Mei 2024 kilikuwa umbali wa takriban Kilomita 342 Mashariki mwa pwani ya Mtwara,’’ TMA imesema.

    Katika kipindi hiki kimbunga HIDAYA kimeendelea kuimarika zaidi huku kasi ya upepo ikiongezeka hadi kufikia Kilomita 140 kwa saa.

    Mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa baharini inaonesha uwezekano wa Kimbunga HIDAYA kupungua nguvu kiasi kwa saa 12 zijazo huku kikiendelea kusogea karibu kabisa na pwani ya Tanzania.

    Kimbunga hiki kinatarajiwa kuendelea kuwepo hadi tarehe 05 mwezi Mei 2024 na kupungua nguvu baada ya tarehe 05 Mei 2024.

  6. Rais awaambia Wakenya kujiandaa kukabiliana na kimbunga

    .

    "Huenda Kenya ikakabiliwa na kimbunga cha kwanza kabisa," Rais William Ruto amewaambia raia katika hotuba ya kitaifa, huku nchi ikikabiliwa na mafuriko mabaya na maporomoko ya ardhi ambayo yameathiri mamia kwa maelfu ya watu.

    Maafisa wanakadiria zaidi ya watu 200 wamefariki nchini Kenya tangu mwezi Machi, huku wengine 90 wakitoweka. Watu wengine 155 wamefariki nchini Tanzania, na 29 nchini Burundi.

    Akizungumza siku ya Ijumaa, rais wa Kenya alisema hakuna sehemu yoyote ya nchi ambayo imeepuka "mafuriko" na kuonya kwamba hali inatarajiwa kuwa mbaya zaidi katika siku zijazo na kunatajiwa hali mbaya zaidi ya hewa.

    "Kimbunga hiki, kwa jina Hidaya, kinaweza kupiga wakati wowote na kinatabiriwa kusababisha mvua kubwa, upepo mkali na mawimbi makali na hatari ambayo inaweza kutatiza shughuli za baharini katika Bahari ya Hindi na makazi katika pwani ya Kenya," alisema.

    "Nchi yetu lazima ichukue hatua madhubuti na haraka ili kupunguza athari mbaya za mzozo uliopo na kulinda maisha na mali."

    Rais Ruto pia ameagiza shule zote zifungwe kwa muda usiojulikana kufuatia mvua kubwa inayonyesha.

    Soma zaidi:

    Mafuriko Kenya: Rais William Ruto aahirisha kufunguliwa kwa shule zote kwa muda usiojulikana

  7. Nyoka hawajasombwa na mafuriko - Mamlaka ya makumbusho

    .
    Image caption: Ripoti za mtandaoni zilikuwa zimeeleza kuwa wanyama hao hatari watambaao wakiwemo mamba, walibebwa na mafuriko makubwa yanayoendelea kuharibu sehemu kubwa za nchi.

    Mamlaka ya Kenya imekanusha ripoti kwamba nyoka wenye sumu kali katika jiji kuu la Nairobi, walisombwa na mafuriko kutoka maeneo yao ya hifadhi.

    Ripoti za mtandaoni zilikuwa zimeeleza kuwa wanyama hao hatari watambaao, wakiwemo mamba, walibebwa na mafuriko hayo makubwa yanayoendelea kuharibu sehemu kubwa za nchi.

    Katika taarifa, Makavazi ya Kitaifa ya Kenya yalisema kuwa nyoka wote na maonyesho mengine yalihifadhiwa vyema.

    "Hii ni kufahamisha umma kwamba katika Makavazi ya Kitaifa ya Kenya, usalama wa maonyesho yetu yote ya moja kwa moja ni muhimu," ilisema taarifa ya umma.

    Mbuga ya nyoka katika jumba la makumbusho jijini Nairobi ni kivutio maarufu, huku wageni wakipita kutazama aina mbalimbali za wanyama watambaao.

    Makavazi ya Kitaifa ya Kenya yaliwahakikishia umma kuwa wanyama wote watambaao wamehesabiwa, na hivyo kuwaondoa hofu kwamba wanaweza kuzurura mjini na hatarisha maisha ya wakazi.

    Takriban watu 210 wamekufa kutokana na mafuriko kote nchini.

  8. Kanisa katoliki la Uganda lakabiliwa na uhaba wa divai – vyombo vya habari

    .

    Mvinyo ya madhabahu ni sehemu muhimu ya ibada ya Kikristo ya ushirika mtakatifu.

    Kanisa Katoliki nchini Uganda linakabiliwa na uhaba mkubwa wa divai ya madhabahuni, vyombo vya habari vya nchini vinaripoti.

    Uhaba huo unasemekana kuwepo tangu Februari na unahusishwa na vita huko Gaza, ambayo imechelewesha uagizaji wa bidhaa kutoka nje.

    Vyombo vya habari vya ndani vinaripoti kwamba kampuni sambaza bidhaa hiyo kwa kanisa, JW InterServices, wiki hii ilitahadharisha dayosisi kuhusu suala hilo, na kuwashauri kutumia kwa uangalifu divai iliyosalia.

    Kanisa hupata divai yake kutoka Uhispania na bidhaa hiyo kawaida husafirishwa kupitia Bahari ya Mediterania na Bahari ya Shamu.

    Lakini kwa sababu ya mabadiliko ya njia, shehena ambayo ilipaswa kuwasili mwanzoni mwa Aprili, sasa ilitakiwa kufika mwisho wa mwezi huu.

    "Meli hizo zimeelekezwa kubadilisha njia ndefu na salama kupitia Atlantiki na Bahari ya Hindi jambo ambalo limesababisha mgogoro mkubwa na ucheleweshaji wa kufika bandari ya Mombasa," gazeti la Observer lilimnukuu Mkurugenzi mkuu wa JW InterServices', Papa Asiku Alfred Tulu.

    Mvinyo ya madhabahuni ni sehemu muhimu ya ibada ya Ushirika Mtakatifu - ambayo kwayo Wakristo hukumbuka dhabihu ya kifo cha Yesu.

  9. Wamalawi wakamatwa nchini Israel kwa kuacha kazi ya shambani

    .
    Image caption: Kumekuwa na madai ya utumwa mambo leo katika miaka ya hivi karibuni (picha ya kawaida tu kutoka maktaba)

    Raia kadhaa wa Malawi wametiwa mbaroni nchini Israel kwa kuacha vituo vyao vya kazi vilivyotengwa katika mashamba na kutafuta ajira katika mji mmoja, mamlaka ilisema.

    Walikuwa miongoni mwa wafanyakazi 40 wa kigeni ambao waliacha kazi zao za shambani kusini mwa Israel na kutafuta kazi katika duka la mikate katika jiji la Bnei Brak, mashariki mwa Tel Aviv, Waziri wa Habari wa Malawi Moses Kunkuyu aliviambia vyombo vya habari vya ndani.

    Hakusema kama Malawi inashirikiana na mamlaka za Israel kuhusu suala hilo, lakini aliwataka tu Wamalawi walioko huko kuheshimu masharti ya ajira zao na kuepuka kujihusisha na shughuli haramu.

    Austin Chipeta, kiongozi wa jumuiya ya Malawi nchini Israel, aliiambia tovuti ya habari ya The Nation ya Malawi kwamba kundi hilo, ambalo lilikimbia mashamba ya Arava na Simba, lilizuiliwa katika gereza lenye ulinzi mkali kusini mwa Tel Aviv, karibu na kitongoji cha Shapira, wakisubiri kurejeshwa katika nchi zao.

    Mishahara katika mashamba ni ya chini sana na Wamalawi walikuwa wakitafuta kazi zenye malipo bora katika miji ya karibu, Bw Chipeta alisema.

    Mwaka jana, Wamalawi 221 waliondoka kwenda Israel kufanya kazi kama vibarua mashambani katika mkataba wa mauzo ya kazi uliotiwa saini kati ya nchi hizo mbili mwaka 2022.

    Mpango huo unalenga kuzalisha mapato zaidi ya fedha za kigeni kwa Malawi na kutoa fursa za ajira kwa raia wake.

    Hata hivyo, mpango huo umekabiliwa na ukosoaji na utata, huku baadhi ya wanasiasa wa upinzani na mashirika ya kutetea haki za binadamu yakielezea wasiwasi wao kuhusu usiri unaozingira mpango huo na hatari zinazoweza kutokea kwa usalama wa wafanyakazi.

  10. Kimbunga HIDAYA kimeendelea kuimarika huku kasi ya upepo ikiongezeka hadi kilomita 130 kwa saa

    .

    Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tena taarifa ya mwenendo wa kimbunga “HIDAYA” kilichopo katika Bahari ya Hindi mashariki mwa pwani ya nchi yetu.

    “Kimbunga HIDAYA kimeendelea kuimarika na kusogea kuelekea maeneo ya pwani ya nchi yetu ambapo hadi kufika saa tisa usiku wa tarehe 03 Mei 2024 kilikuwa kimeimarika zaidi na kufikia hadhi ya Kimbunga kamili kikiwa umbali wa takriban Kilomita 401 Mashariki mwa pwani ya Mtwara,” TMA ilisema.

    Mamlaka ya Hali ya Hewa iliongeza, “Katika kipindi hiki kimbunga HIDAYA kimeendelea kuimarika zaidi huku kasi ya upepo ikiongezeka hadi kufikia Kilomita 130 kwa saa”.

    Mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa baharini bado inaonesha uwezekano mkubwa wa Kimbunga HIDAYA kusalia katika hadhi ya Kimbunga kamili kwa saa 12 zijazo huku kikiimarika, na kuendelea kusogea karibu kabisa na pwani ya Tanzania.

    imbunga hiki kinatarajiwa kuendelea kuwepo hadi tarehe 06 mwezi Mei 2024 na kupungua nguvu baada ya hapo.

    Soma zaidi:

    Yote unayotakiwa kuyafahamu kuhusu Kimbunga Hidaya

  11. Ukraine inaweza kutumia silaha za Uingereza ndani ya Urusi - Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza

    .

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Cameron amesema ni juu ya Ukraine kuamua jinsi ya kutumia silaha za Uingereza na kusisitiza kuwa ina haki ya kushambulia maeneo ya ardhi ya Urusi.

    Wakati wa ziara yake Kyiv, alisema Uingereza itatoa £3bn ($3.75bn) kwa mwaka kwa muda ambao itahitajika kufanya hivyo.

    "Kama vile Urusi inavyoshambulia ndani ya Ukraine, unaweza kuelewa kwa nini Ukraine inahisi hitaji la kuhakikisha kuwa inajilinda," Cameron alisema.

    Urusi ilishutumu kile ilichokiita "kauli nyingine hatari sana".

    "Hii ni ongezeko la moja kwa moja la mvutano katika mzozo wa Ukraine, ambao unaweza kuwa tishio kwa usalama wa Ulaya," msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alisema.

    Imeripotiwa kuwa Marekani imeitaka Ukraine kusitisha mashambulizi yake dhidi ya viwanda vya kusafisha mafuta nchini Urusi, ikihofia kwamba huenda ikazidisha mzozo huo.

    Bw Peskov pia alimlenga Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, ambaye alisema wiki hii kwamba nchi za Magharibi "kihalali" zitalazimika kufikiria kutuma wanajeshi wa ardhini nchini Ukraine "ikiwa Warusi watavuka mstari wa mbele, ikiwa kuna ombi la Ukraine."

    Matamshi ya Bw Macron kwa gazeti la The Economist yalikuwa "mwelekeo hatari sana", alisema msemaji wa Kremlin. Hata hivyo, kiongozi huyo wa Ufaransa aliweka wazi katika mahojiano yake kwamba ikiwa Urusi itashinda Ukraine, hakutakuwa na usalama barani Ulaya.

    Vikosi vya Urusi vimeteka vijiji kadhaa mashariki mwa Ukraine hivi karibuni, na kuchukua fursa ya uhaba wa silaha na wafanyikazi upande wa Ukraine.

    Maafisa wa ujasusi wa Ukraine pia wanaamini kuwa Urusi inajiandaa kwa mashambulizi ya majira ya joto katika mikoa ya kaskazini-mashariki ya Kharkiv na Sumy.

    Soma zaidi:

    Vita vya Ukraine: Kwanini Ukraine inaweza kushindwa na Urusi 2024?

  12. Habari za hivi pundeMafuriko Kenya: Rais William Ruto aahirisha kufunguliwa kwa shule zote kwa muda usiojulikana

    ,

    Rais William Ruto ameiagiza Wizara ya Elimu kuahirisha tarehe ya ufunguzi wa shule kufuatia mafuriko uliosababishwa na mvua kubwa inayoendelea kunyesha.

    ''Naagiza shule ambazo zilikuwa zifunguliwe Jumatatu zisifunguliwe mpaka pale serikali itakapotoa muongozo zaidi'' amesema Bw Ruto.

    Agizo hilo jipya limetolewa ikiwa zimesalia siku chache tu kabla ya muda uliokuwa umetangazwa awali wa kufunguliwa kwa shule Mei 6.

    Awali shule hizo zilipangwa kufunguliwa Aprili 29, lakini iliahirishwa na Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu kutokana na mvua kubwa kunyesha.

    Machogu alisema wamepata taarifa kuwa baadhi ya shule zimeathiriwa vibaya na mafuriko yanayoendelea.

    Alisema kuwapeleka wanafunzi na wafanyikazi katika shule zilizoathiriwa kutakuwa kuhatarisha maisha yao.

    Awali, wizara ya elimu ilitoa mwongozo na kusema kuwa wazazi na wasimamizi wa shule ndio watakaowajibika kwa usalama wa wanafunzi shule zitakapofunguliwa.

    Pia iliongeza kuwa familia zilizoathiriwa na mafuriko ambazo kwa sasa zinaishi katika taasisi za shule pia zitahamishwa katika maeneo mengine.

    Katika hotuba yake, Rais William Ruto amesema huenda Kenya ikakabiliwa na kimbunga chake cha kwanza kabisa na Kimbunga Hidaya kinaweza kupiga wakati wowote na kuongeza kwamba Idara ya Hali ya Hewa ya Kenya na Kituo cha Utabiri wa Hali ya Hewa cha IGAD, wametoa onyo kali.

    "Taarifa za hali ya hewa zinatoa taswira ya kutisha. Mvua zitaendelea kunyesha kwa muda na kasi kwa kipindi kizima cha mwezi huu na pengine baada ya hapo," alisema.

    "Kimbunga hicho kinatabiriwa kusababisha mvua kubwa, upepo mkali na mawimbi yenye nguvu na hatari, ambayo yanaweza kutatiza shughuli za baharini katika Bahari ya Hindi na makazi kwenye pwani ya Kenya."

    Pia unaweza kusoma:

    Kenya yapiga marufuku shughuli za baharini Lamu kufuatia tahadhari ya Kimbunga Hidaya

  13. Kenya yapiga marufuku shughuli za baharini Lamu kufuatia tahadhari ya Kimbunga Hidaya

    .

    Wakaazi wa kaunti ya Lamu hawataruhusiwa kusafiri baharini kuanzia leo jioni hadi siku ya Jumanne kufuatia tahadhari ya Kimbinga Hidaya.

    Wavuvi na abiria wameshauriwa kukatiza safari zao.

    Viongozi wa Lamu walikutana kujadili namna ya kuepuka maafa wakati Kimbunga Hidaya kikitarajiwa.

    William Samoe, Kamanda wa Polisi eneo la Lamu ametoa wito kwa wakaazi kutii maagizo wanayopewa na kwamba suala hili litachukuliwa kwa uzito mkubwa.

    Abiria kwa sasa wametakiwa kuvaa majaketi ya kuokoa maisha na pia kutopakia abiria wengi kupita kiasi kwasababu kwasasa bahari itakuwa inashuhudia mawimbi makali na mvua.

    Soma zaidi:

    Mafuriko Kenya: Serikali yaamuru kuhamishwa kwa watu huku ikionya kuwa mabwawa yanaweza kufurika

  14. Roketi ya China yaanza safari kuelekea upande wa mbali wa Mwezi

    .

    China imezindua uchunguzi wa kukusanya sampuli kutoka sehemu ya mbali wa Mwezi, katika kile kinachodaiwa kuwa wa kwanza ulimwengu.

    Roketi inayojiendesha yenyewe iliyokuwa imebeba chombo Chang'e-6 imerushwa kutoka Kituo cha Uzinduzi cha Anga cha Wenchang saa 17:27 saa za eneo hilo.

    Misheni hiyo ya siku 53 inalenga kuleta karibu kilo mbili za sampuli kutoka kwenye mwezi duniani kwa utafiti.

    Itajaribu kuzindua upya kutoka upande wa mwezi unaotazama mbali na Dunia.

    Huu unafafanuliwa kuwa upande wa giza wa Mwezi kwa sababu hauonekani kutoka Duniani, sio kwa sababu haupati miale ya jua.

    Ina ganda zito la zamani na kreta nyingi, ambazo zimefunikwa kidogo na mtiririko wa lava ya zamani kuliko upande wa karibu.

    Hii inaweza kufanya iwezekane zaidi kukusanya sampuli ambazo husaidia kutoa mwanga juu ya jinsi Mwezi ulivyoundwa, wanasayansi wanatumai.

    Soma zaidi:

    Nini kinachofanya wakati kwenda kwa kasi mwezini ikilinganishwa na duniani?

  15. Ruto kuhutubia Wakenya huku kukiwa na shinikizo kutokana na mafuriko makubwa

    .

    Rais wa Kenya William Ruto anatarajiwa kuhutubia taifa huku kukiwa na shinikizo kubwa la kutangaza mafuriko makubwa yanayoendelea kuwa janga la kitaifa.

    Msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed, ambaye alitoa tangazo hilo, hakutoa maelezo kuhusu hotuba hiyo leo Ijumaa.

    Lakini Rais Ruto anatarajiwa kuzungumzia mvua kubwa inayoendelea kunyesha ambayo imeua takriban watu 188 tangu Machi na kusababisha mamia kwa maelfu kuyahama makazi yao.

    Hotuba hiyo inajiri siku moja baada ya baraza la mawaziri kuonya kuwa eneo la pwani huenda likakumbwa na kimbunga, kikiambatana na mvua kubwa, mawimbi makubwa na upepo mkali unaoweza kuathiri shughuli katika Bahari ya Hindi.

    Baraza la Mawaziri, ambalo lilikutana kwa mara ya pili wiki hii, pia lilisema kuwa mvua za wastani hadi juu ya wastani zitaendelea kunyesha kote nchini.

    Serikali imeamuru watu wanaoishi karibu na mabwawa kuhama mara moja au kulazimishwa kuhamia maeneo salama.

    Kiongozi wa upinzani Raila Odinga ametoa wito kwa rais kutangaza mafuriko hayo kuwa janga la kitaifa ili kuandaa njia ya kuungwa mkono na kimataifa.

    Nchi jirani ya Tanzania, ambako takriban watu 155 wameuawa katika mafuriko na maporomoko ya ardhi, pia inatarajiwa kuhisi nguvu ya Kimbunga Hidaya.

  16. Habari za hivi pundeVikosi vya Urusi vyaingia kwenye kambi ya Niger inayohifadhi wanajeshi wa Marekani - Austin

    .
    Image caption: Hivi karibuni viongozi wa jeshi la Niger waliwaamuru wanajeshi wa Marekani kuondoka nchini humo

    Vikosi vya Urusi vimeingia katika kambi ya anga nchini Niger ambapo wanajeshi wa Marekani bado wamesalia kufuatia uamuzi wa jeshi la Niger kuwatimua nchini humo.

    Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin alithibitisha kuwa wanajeshi wa Urusi wameingia katika kambi ya wanahewa lakini walikuwa katika kambi tofauti.

    Aliuambia mkutano wa waandishi wa habari nchini Marekani kwamba haikuwa suala muhimu kwa kuwa hawakuwa na uwezo wa kufikia wanajeshi wa Marekani au vifaa.

    Kambi ya "Airbase 101 ambapo majeshi yetu [yalipo], ni kambi ya jeshi la anga ya Niger ambayo iko pamoja na uwanja wa ndege wa kimataifa katika mji mkuu.

    Warusi wako katika eneo tofauti na hawana ufikiaji wa vikosi vya Marekani au ufikiaji wa vifaa vyetu, "alisema.Afisa mkuu wa ulinzi wa Marekani hapo awali aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba hali si nzuri lakini inaweza kudhibitiwa kwa muda mfupi.

    Uhusiano wa kijeshi na kidiplomasia kati ya Marekani na Urusi umekuwa wa baridi tangu Urusi ilipovamia Ukraine.

    Kabla ya mapinduzi ya Niger mwaka jana, Marekani ilikuwa mshirika mkuu wa nchi hiyo pamoja na washirika wengine katika mapambano dhidi ya waasi wa Kiislamu katika eneo hilo.

    Niger iko katika eneo la Sahel barani Afrika, ambalo linachukuliwa kuwa kitovu kipya cha kimataifa cha kundi la Islamic State.

    Baada ya mapinduzi hayo, viongozi wa kijeshi wa Niger wametafuta uhusiano wa karibu na Urusi, baada ya kuzorota kwa uhusiano na nchi za Magharibi, pamoja na Ufaransa.

  17. Mauzo ya Apple iPhone yaanguka katika karibu masoko yote

    .
    Image caption: Simu aina ya iphone

    Mauzo ya simu aina ya iPhones yameshuka katika karibia masoko yote ulimwenguni, kulingana na matokeo ya hivi punde kutoka Apple.

    Kampuni hiyo kubwa ya teknolojia ilisema mahitaji ya jumla ya simu zake mahiri yamepungua kwa zaidi ya 10% katika miezi mitatu ya kwanza ya mwaka huu, huku mauzo yakishuka katika kila eneo la kijiografia isipokuwa Ulaya.

    Apple ilisema kuwa kwa ujumla, mapato katika kampuni yote yalipungua kwa 4% hadi $90.8bn (£72.5bn), ambayo ilikuwa kushuka kukubwa zaidi kwa zaidi ya mwaka mmoja.

    Hatahivyo, matokeo hayakuwa mabaya kama ilivyotarajiwa na bei ya hisa ya Apple ilipanda katika biashara ya saa baada ya saa huko New York.

    Kampuni hiyo ilisema takwimu hizo zilipotoshwa na usumbufu wa usambazaji unaohusiana na Covid, ambao ulisababisha mauzo yenye nguvu isiyo ya kawaida katika kipindi kama hicho mwaka jana.

    Iliahidi kwamba mauzo yangerejea katika ukuaji katika miezi ijayo, ikibainisha uzinduzi ujao wa bidhaa na uwekezaji katika akili mnemba (AI).

    Kwa iPhone, mauzo katika soko kuu la China yalipungua kwa 8%. Bw Cook alijaribu kuwahakikishia wawekezaji kuhusu hali ya biashara katika uchumi wa pili kwa ukubwa duniani, akibainisha kuwa mauzo ya iPhone yalikuwa yameongezeka nchini China.

  18. Nyani aliyejeruhiwa aonekana akitumia mmea kujitibu jeraha

    Nyani mwenye jeraha

    Nyani aina ya Orangutan wa Sumatran nchini Indonesia amejitibu kwa kutumia kibandiko kilichotengenezwa kwa mimea ili kuponya jeraha kubwa kwenye shavu lake, wanasema wanasayansi.

    Ni mara ya kwanza kwa kiumbe porini kurekodiwa akitibu jeraha kwa mmea wa dawa. Baada ya watafiti kumuona Rakus akipaka dawa hiyo usoni mwake, jeraha hilo lilifungwa na kupona baada ya mwezi mmoja.

    Wanasayansi wanasema tabia hiyo inaweza kutoka kwa babu mmoja aliyeshirikiwa na wanadamu na nyani wakubwa.

    Timu ya watafiti katika Mbuga ya Kitaifa ya Gunung Leuser, Indonesia ilimwona Rakus akiwa na jeraha kubwa shavuni mnamo Juni 2022.

    Wanaamini kwamba alijeruhiwa akipigana na orangutan wa kiume hasimu kwa sababu alilia kwa sauti kubwa, siku chache kabla ya kuona jeraha.

    Timu hiyo kisha ikamwona Rakus akitafuna shina na majani ya mmea unaoitwa Akar Kuning, mmea wa kuzuia bakteria ambao pia hutumiwa ndani kutibu malaria na kisukari.

    Mara kwa mara alitumia kioevu hicho kwenye shavu lake kwa dakika saba.

    Rakus kisha alipaka majani yaliyotafunwa kwenye jeraha lake hadi likafunikwa kabisa.

    Watafiti hawakuona dalili ya kuambukizwa na jeraha lilifunga ndani ya siku tano. Baada ya mwezi mmoja, Rakus alikuwa mzima kabisa.

    Wanasayansi walihitimisha kwamba Rakus alijua alikuwa akitumia dawa kwa sababu orangutan mara chache sana hula mmea huo na kwa sababu ya urefu wa matibabu.

  19. Kasi ya Kimbunga Hidaya yaimarika hadi kilomita 110 kwa saa

    Abdalla Dzungu

    BBC Swahili, Nairobi

    .
    Image caption: Kimbunga

    Mienendo ya mifumo ya hali ya hewa baharini bado inaonyesha uwezekano mkubwa wa Kimbunga Hidaya kuendelea kusogea karibu na pwani ya Tanzania na kuendelea kuwepo hadi tarehe sita mwezi Mei 2024, kwa mujibu wa Mamlaka ya hali ya Hewa Tanzania TMA.

    Kulingana na mamlaka hiyo, kimbunga hicho kinaendelea kuimarika na kwamba hadi kufikia usiku wa kuamkia leo kasi yake ilikuwa imeimarika na kufikia kilomita 110 kwa saa.

    Taarifa hiyo inasema kwamba kimbunga hicho kitaendelea kuimarika na kuwa kikubwa zaidi katika saa 24 zijazo.

    Imesema kwamba uwepo wa kimbunga hicho katika pwani ya Tanzania utavuruga mifumo ya ali ya hewa nchini na kusababisha mvua kubwa na upepo mkali.

    Baadhi ya maeneo yatakayoathirika sana ni Mikoa ya Mtwara, Dar es Salaam, Lindi, maeneo ya Tanga, Morogoro , visiwa vya pemba na Unguja pamoja na maeneo Jirani.

    Taarifa hiyo imeongezea kwamba tayari vipindi vya mvua nyepesi na upepo wa wastani vimeanza kujitokeza katika maeneo ya Mtwara.

    TMA imesema kwamba ongezeko la mvua na upepo mkali utakaoambatana na mawimbi makubwa baharini vinatarajiwa kusambaa katika maeneo mengi ya ukanda wa pwani kuelekea tarehe 4 hadi 6 mwezi Mei 2024.

    Kutokana na hilo, TMA imetoa tahadhari kwa wananchi katika maeneo husika na wote wanaojihusisha na shuguli mbalimbali baharini .

    VIlevile Mamlaka hiyo imewataka Watanzania kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiriwa hali ya Hewa.

    Freddy: Kimbunga kilichodumu zaidi ya mwezi mmoja

    Kimbunga Jobo chatoweka baada ya kuwasili pwani ya Tanzania

    Kimbunga Jobo: Mamlaka ya hali ya hewa yatoa tahadhari ya kimbunga kikali Pwani ya Tanzani

  20. Bado tunashirikiana na Junta - Marekani

    .
    Image caption: Wanajeshi wa Marekani wamekuwa wakisaidia mataifa ya Afrika Magharibi kupambana na waasi wa Kiislamu

    Marekani bado inashirikiana na Niger na Chad, licha ya kuwaondoa wanajeshi wake katika nchi hizo, afisa mkuu wa jesi la Marekani barani Afrika ameiambia BBC.

    Siku ya Jumatano, makumi ya wanajeshi wa Marekani waliondoka Chad baada ya viongozi wa kijeshi wa nchi hiyo kueleza wasiwasi wao kuhusu kuwepo kwao kabla ya uchaguzi wa tarehe 6 Mei.

    Jenerali Michael Langley aliambia BBC kuwa ni "mabadiliko ya muda ya kijeshi’ .

    Mwezi uliopita, wanajeshi wa Marekani waliondoka nchi jirani ya Niger baada ya kuagizwa na jeshi la nchi hiyo.Wakufunzi wa kijeshi wa Urusi wamewasili Niger kama sehemu ya makubaliano mapya na viongozi wa kijeshi.

    Nchi nyingine kadhaa zinazoongozwa kijeshi katika eneo la Sahel pia hivi karibuni zimeimarisha uhusiano na Urusi na kukata uhusiano na Ufaransa, aliyekuwa mkoloni wake, huku zikijaribu kupambana na waasi wa Kiislamu katika eneo hilo.

    Eneo la Sahel linachukuliwa kuwa kitovu kipya cha kimataifa cha kundi la Islamic State.

    Jenerali Langley alisema kuwa mashirika yenye itikadi kali ndio tishio kubwa kwa uthabiti wa Afrika.