Got a TV Licence?

You need one to watch live TV on any channel or device, and BBC programmes on iPlayer. It’s the law.

Find out more
I don’t have a TV Licence.

Habari za moja kwa moja

time_stated_uk

  1. Tunakomea hapo kwa leo. Kwaheri.

  2. Watu 12 wakamatwa kwa kula hadharani wakati wa mfungo Zanzibar

    Vitafunwa

    Maafisa wa polisi katika kisiwa cha Unguja kisiwani Zanzibar wamewakamata watu 12 kwa tuhuma za kula mchana hadharani wakati huu wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

    Kwa mujibu wa kaimu kamanda wa polisi Mkoa wa Magharibi Abubakar Ally, hatua hiyo inajiri baada video iliosambaa ikiwaonesha baadhi ya watu wakila hadharani wakat wa mchana.

    Kamanda huyo amesema kwamba baada ya msako walifanikiwa kuwakamata watu hao waliokula hadharani kutoka maeneo tofauti ya mjini.

    Afisa huyo ameongezea kwamba polisi inaendelea kukamilisha upelelezi ili washukiwa waweze kuwasilishwa mahakamani.

    Kwa sasa watu hao wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Madema.

    Maelezo zaidi:

    Kwanini ni 'marufuku' kula mchana wa mwezi wa Ramadhan visiwani Zanzibar

  3. Rwanda yapokea kundi la pili la watu wanaotafuta hifadhi ndani ya wiki moja

    .
    Image caption: Zaidi ya wakimbizi 2,200 na wanaotafuta hifadhi wamewasili Rwanda kutoka Libya tangu 2019.

    Rwanda imepokea wakimbizi 57 wa Eritrea na 35 wa Sudan wanaotafuta hifadhi, siku chache baada ya wakimbizi wengine 91 na waomba hifadhi kuwasili nchini kutoka Libya.

    Wakimbizi 183 wanaotafuta hifadhi watasalia Rwanda wakisubiri kushughulikiwa kwa maombi yao ya makazi mapya, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi lilisema Jumatano.

    Waliowasili ni sehemu ya mpango unaoungwa mkono na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya.

    Tangu 2019, mpango huo umetuma zaidi ya wakimbizi 2,200 na waomba hifadhi kutoka mataifa mbalimbali kutoka Libya hadi Rwanda.

    Zaidi ya 1,600 kati yao wamepewa makazi mapya Marekani na kote Ulaya.

    Kuwasili kwa hivi punde zaidi kwa wakimbizi na wanaotafuta hifadhi nchini Rwanda kunakuja wakati Uingereza ikijaribu kupitisha sheria mpya ambayo itairuhusu kutuma baadhi ya waomba hifadhi nchini Rwanda.

    Mahakama ya Juu ya Uingereza hapo awali ilibatilisha mpango huo, na kuutaja kuwa ni kinyume cha sheria.

  4. Meli ya kivita ya Urusi yawasili katika bandari ya Eritrea

    .

    Katika ziara isiyo ya kawaida meli ya kivita ya jeshi la wanamaji la Urusi imewasili katika bandari kuu ya Bahari Ya Shamu ya Massawa nchini Eritrea, huku kukiwa na hali ya wasiwasi katika eneo hilo iliyosababishwa na wanamgambo wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran.

    Shaposhinkov ilipowasili Alhamisi huko Massawa, wakuu wa jeshi la Eritrea na maafisa waliipokea. Balozi wa Urusi nchini Eritrea pia alikuwepo.

    Kulingana na Waziri wa Habari wa Eritrea, meli hiyo ni mongoni mwa meli za Urusi zilizopo katika bahari ya pasific

    "Itakuwa katika bandari hiyo kwa siku tano kuadhimisha Miaka 30 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Urusi na Eritrea" Waziri Yemane Gebremeskel aliandika kwenye X.

    Kikosi kazi cha wanamaji cha Marekani kimetumwa katika Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden ili kulinda meli za kibiashara na za kijeshi zinazopanda na kushuka kwenye njia muhimu ya kibiashara kutokana na mashambulizi ya Houthi.

    Eritrea imekuwa ikishuhudia uwepo wa wanajeshi wa Magharibi katika eneo hilo kwa shauku. Taifa hilo la Pembe ya Afrika hivi karibuni limeanzisha uhusiano wa karibu na Moscow.

    Wahouthi wanaodhibiti eneo la kaskazini mwa Yemen wamekuwa wakishambulia meli zinazopita katika Bahari ya shamu kujibu vita huko Gaza. Wanamgambo hao ni sehemu ya ‘mhimili wa upinzani’ dhidi ya Israeli.

    Licha ya madai ya Houthi kwamba wanalenga meli zilizohusishwa na Israel pekee, wamekuwa wakishambulia meli nyingi zisizo na uhusiano na Israel.

    Mnamo Januari, meli za kivita za Marekani na Uingereza, kama sehemu ya "Mlinzi wa Ufanisi" zilianza kulenga shabaha za Houthi kulipiza kisasi mashambulizi ya makombora na droni yanayotekelezwa na wanamgambo.

  5. Burkina Faso yaongeza muda wa hatua za dharura dhidi ya wanajihadi

    xx

    Watawala wa kijeshi nchini Burkina Faso wameamua kuongeza kwa mwaka hatua za dharura zinazolenga kupambana na ghasia za wanamgambo wa kijihadi.

    Amri ya awali ilisema kwamba kila mtu aliye na umri wa zaidi ya miaka 18 ambaye alikuwa sawa kimwili angeweza kuitwa jeshini.

    Pia ilisema haki na uhuru wa watu vinaweza kupunguzwa na ilihalalisha uanzishwaji wa vikundi vya ulinzi vya ndani.

    Waandishi wa habari wanasema kumekuwa na visa ambapo wakosoaji wa watawala wa kijeshi wa Burkina Faso wametekwa nyara na kuandikishwa kwa nguvu jeshini ili kusaidia katika vita dhidi ya wanamgambo hao wa kijihadi.

    Tangu mwaka 2015 zaidi ya watu milioni mbili wamekimbia makazi yao kutokana na ghasia za wanajihadi.

  6. Kimbunga hatari chakumba kaskazini mwa Madagacar

    picha

    Kimbunga kilichopiga kaskazini mwa Madagascar siku ya Jumatano kimesababisha vifo vya watu sita na kuwalazimu wengine 2,000 kuhama makwao.

    Habari za eneo hilo zinasema kwamba “mafuriko yalisababisha uharibifu mkubwa” huku barabara na madaraja yakiharibiwa.

    Shirika la habari la AFP, likinukuu mamlaka ya kudhibiti majanga (BNGRC), linakadiria idadi ya waliofariki kutokana na kimbunga Gamane kuwa 11.

    Inaripoti kuwa sita kati ya waathiriwa walikufa maji, huku wengine wakifa baada ya kuagongwa na miti iliyoanguka au kuporomoka kwa nyumba.

    "Ni nadra kuwa na kimbunga kama hiki. Mwendo wake unakaribia kusimama," Jenerali Elack Andriakaja, mkurugenzi mkuu wa BNGRC alinukuliwa na AFP akisema.

    "Mfumo unaposimama katika sehemu moja, unaharibu miundombinu yote. Na hiyo ina madhara makubwa kwa wakazi. Na mafuriko makubwa."

  7. Wabunge wa Ufaransa walaani mauaji ya 1961 ya Waalgeria mjini Paris

    XX

    Bunge la Ufaransa limeidhinisha kwa kauli moja azimio la kulaani mauaji ya 1961 ya Waalgeria mjini Paris.

    Baadhi ya wanahistoria wanasema hadi waandamanaji 300 waliuawa wakati polisi walipovunja maandamano ya kuunga mkono uhuru wa Algeria.

    Wengine walipigwa hadi kufa, wengine walizama kwenye Mto Seine.

    Azimio hilo pia linataka kuwe na siku rasmi ya ukumbusho.

    Mauaji hayo yalitokea katika muktadha wa vita vya uhuru wa Algeria.

    Mkuu wa polisi anayesimamia, Maurice Papon, baadaye alipatikana na hatia ya uhalifu dhidi ya ubinadamu kwa kushirikiana na Wanazi.

  8. Raia wa Uganda wahimizwa kutoa majibu ya ukweli wakati wa sensa

    Rais wa Uganda Yoweri Museveni amewataka raia kushiriki kikamilifu katika sensa ya nchi hiyo mwezi Mei na kuwa wakweli wanapoulizwa maswali ya sensa.

    "Wakusanyaji data wanapokuja nyumbani kwenu wakati wa sensa, tafadhali...wapeni majibu ya ukweli kwa maswali yao," Rais Museveni alichapisha kwenye X.

    "Hii ni kwa ajili ya kuwawezesha [kushughulikia] taarifa sahihi zaidi kukuhusu wewe binafsi, nyumba yako, taasisi na jamii," Bw Museveni alisema, akiongeza kuwa majibu sahihi yatawezesha serikali kupanga kwa usahihi utoaji wa huduma za umma.

    Uganda inatazamiwa kufanya sensa hiyo kati ya tarehe 10 na 19 Mei.

    Ni sensa ya sita katika historia ya nchi na ya kwanza kufanyika kidijitali.

    Zoezi hilo liliahirishwa kutoka tarehe iliyopangwa awali mwezi Agosti mwaka jana kutokana na changamoto za kifedha, huku kukiwa na kupunguzwa kwa ufadhili wa kimataifa kuhusishwa na sheria tata ya Uganda dhidi ya wapenzi wa jinsia moja.

    Imepangiwa kugharimu shilingi bilioni 134 za Uganda sawa na ($34m; £27m).

    Sensa ya mwisho ya Uganda mwaka 2014 ilionyesha idadi ya watu kuwa milioni 36.

    Shirika la takwimu la serikali linakadiria kuwa idadi ya watu imeongezeka kwa zaidi ya 30% tangu wakati huo, na sasa inapita milioni 45.

  9. Tabia ya wanafunzi 'inazidi kuwa mbaya' katika shule za Uingereza - walimu

    .

    Takriban mwalimu mmoja kati ya watano nchini Uingereza amepigwa na mwanafunzi mwaka huu, uchunguzi ulioidhinishwa na BBC unasema.

    Mwalimu mmoja aliiambia BBC kuwa tabia hiyo ilikuwa "vita isiyoisha". Mwingine alisema kutema mate, kutukana na kurusha viti ni miongoni mwa mambo yanayotokea mara kwa mara.

    Muungano unasema wanachama wake wanaripoti ghasia na unyanyasaji unaozidi kuongezeka kutoka kwa wanafunzi tangu janga la Covid.

    Idara ya Elimu (DfE) inasema imewekeza £10m katika vituo vya tabia kusaidia shule.

    Kwa kutumia zana ya uchunguzi ya Teacher Tapp, BBC News iliuliza hadi walimu 9,000 nchini Uingereza mnamo Februari na Machi mfululizo wa maswali kuhusu uzoefu wao na tabia darasani.

    Idadi kubwa ya walimu wa shule za msingi na sekondari waliripoti wanafunzi kupigana na kusukumana ikilinganishwa na miaka miwili iliyopita.

    Lorraine Meah amekuwa mwalimu wa shule ya msingi kwa miaka 35, amesema tabia ya wanafunzi imekuwa mbaya zaidi.

  10. Wanne wauawa katika uvamizi wa visu Marekani

    .

    Watu wanne wameuawa na takriban watano kujeruhiwa baada ya mtu mmoja aliyekuwa na kisu kufanya uvamizi katika jimbo la Illinois nchini Marekani.

    Polisi huko Rockford wanasema mashambulizi hayo yalitokea kufuatia uvamizi wa nyumbani siku ya Jumatano mchana. Mmoja wa waliojeruhiwa yuko katika hali mahututi.

    Waliouawa ni msichana wa miaka 15, mwanamke mwenye umri wa miaka 63, mwanamume mwenye umri wa miaka 49 na mwanamume wa miaka 22.

    Mwanamume, 22, amekamatwa na anahojiwa na polisi.

    Polisi walisema chanzo cha mashambulizi hayo bado hakijafahamika.

    Uvamizi huo wa nyumbani ulitokea katika Mtaa wa Florence lakini mashambulizi hayo yalitokea katika maeneo mengi, polisi wanasema.

    Inasemekana mwanamke kijana alikuwa na majeraha ya kisu mikononi na usoni baada ya kuonekana akimkimbia mshukiwa.

  11. Museveni azindua benki ya kwanza kabisa ya Kiislamu nchini Uganda

    .

    Benki ya Salaam Limited itakuwa taasisi ya kwanza kutoa ufadhili wa Kiislamu nchini Uganda

    Rais wa Uganda Yoweri Museveni amezindua rasmi benki ya kwanza kabisa ya kibiashara ya Kiislamu nchini humo isiyo na riba.

    Salaam Bank Limited, kampuni tanzu ya benki ya Djibouti, ni taasisi ya kwanza kutoa ufadhili wa Kiislamu nchini humo.

    Bw Museveni alisema taasisi hiyo ina uwezo wa kuchangia pakubwa katika maendeleo ya sekta ya fedha Uganda na kuvutia wawekezaji zaidi Waislamu.

    "Ninawahimiza kupigana na umaskini na kuunda utajiri," rais alisema muda mfupi baada ya kuzindua benki hiyo Jumatano katika mji mkuu, Kampala.

    Mnamo Septemba mwaka jana, benki ya Salaam ilipewa leseni yake ya kwanza ya benki ya Kiislamu baada ya bunge la Uganda kupitisha sheria inayoidhinisha benki za Kiislamu, ambazo Bw Museveni alitia saini kuwa sheria.

    Hairuhusiwi kulipa na kupokea riba katika benki ya Kiislamu, bali inategemea kugawana faida.

  12. Polisi wamhusisha mfanyabiashara maarufu wa Afrika Kusini na mauaji ya rapa

    .

    Mfanyabiashara ambaye ni mmoja wa familia yenye nguvu nchini Afrika Kusini amehusishwa na mauaji ya rapa maarufu AKA.

    AKA, jina halisi la Kiernan Forbes, na rafiki yake wa karibu, Tibz Motsoane, waliuawa kwa kupigwa risasi nje ya mkahawa mmoja huko Durban tarehe 10 Februari mwaka jana.

    Taarifa iliyowasilishwa mahakamani na afisa wa uchunguzi ilisema kwamba kampuni inayomilikiwa na mfanyabiashara Sydney Mfundo Gcaba inadaiwa kutuma zaidi ya rand 800,000 ($42,000; £33,000) kwenye akaunti ya benki ya mmoja wa washukiwa wanaoshtakiwa kwa mauaji ya rapper huyo.

    Malipo hayo yanadaiwa kufanywa siku moja baada ya mauaji ya AKA.

    Mwendesha mashtaka, akinukuu rekodi za simu, pia alisema kuwa mshukiwa aliyepokea pesa hizo, Mziwethemba Harvey Gwabeni, alidaiwa kupiga simu kwa Bw Gcaba kabla ya shughuli hiyo kukamilika.

    Bw Gcaba bado hajatoa maoni yake kuhusu kauli ya mwendesha mashtaka.

    Mwendesha mashtaka anadai kuwa pesa hizo ziligawanywa kwa usawa kati ya washukiwa saba.

    Bw Gwabeni alisema katika hati ya kiapo kwamba alipokea fedha hizo kama malipo ya huduma za mashauriano alizotoa kwa kampuni hiyo.

    Lakini mwendesha mashtaka alidai kuwa hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa Bw Gwabeni alitoa huduma yoyote kwa kampuni hiyo ili kuidhinisha malipo hayo.

    Bw Gcaba ni mwanachama wa familia yenye nguvu ya Gcaba, ambayo inamiliki himaya ya teksi na biashara nyingine kadhaa katika jimbo la pwani la KwaZulu-Natal na kote Afrika Kusini.

    Sababu ya madai yake ya kuhusika katika mauaji ya AKA bado haijajulikana.

  13. Uhispania: Waendesha mashtaka wataka aliyekuwa mkuu wa shirikisho la soka afungwe jela baada ya kumbusu mwanasoka wa kike

    .

    Waendesha mashtaka wa Uhispania wanataka aliyekuwa mkuu wa shirikisho la soka nchini humo afungwe jela miaka miwili na nusu, baada ya kumbusu mwanasoka wa kike dhidi ya hiari yake katika ushindi wa Kombe la Dunia wa Uhispania.

    Luis Rubiales anakabiliwa na mashtaka ya unyanyasaji wa kijinsia na kutumia nguvu baada ya kumshika Jenni Hermoso na kumbusu mdomoni Agosti mwaka jana.

    Bi Hermoso na wachezaji wenzake walisema busu hilo halikutakikana na lilidhalilisha.

    Bw Rubiales alilazimika kujiuzulu, lakini amekanusha makosa yoyote.

    Kulingana na hati ya mahakama iliyoonekana na Reuters, mwendesha mashtaka Marta Durantez alimshtaki Bw Rubiales kwa shtaka moja la unyanyasaji wa kijinsia na moja la kulazimishwa kwa madai yake ya vitendo baada ya busu. Mashtaka hayo yana vifungo vya mwaka mmoja na miezi 18 mtawalia.

    Bi Durantez pia alimshutumu kocha wa zamani wa timu ya taifa ya wanawake, Jorge Vilda, mkurugenzi wa sasa wa michezo wa timu hiyo, Albert Luque, na mkuu wa soko wa shirikisho hilo, Ruben Rivera, kwa kumlazimisha Bi Hermoso kusema busu hilo lilikuwa la maelewano.

    Shtaka lilisema walimnyanyasa kupitia "vitendo vya mara kwa mara vya kumpa shinikizo", ikiwa ni pamoja na kupitia marafiki na familia yake.

    Wote watatu walikanusha kutanda makosa hayo walipofika mbele ya mahakama. Kila mmoja anaweza kufungwa jela miezi 18 iwapo atapatikana na hatia.

    Bi Durantez pia anataka wanaume hao wanne walipe fidia ya jumla ya €100,000 (£85,677; $108,000) kwa Bi Hermoso, na Bw Rubiales alipe angalau nusu ya kiasi hicho.

    Pia aliomba amri ya kuzuiwa kwa Bw Rubiales, ikimzuia kufika umbali wa mita 200 (futi 656) kutoka kwa Bi Hermoso na kuwasiliana naye kwa miaka saba na nusu ijayo.

    Kashfa hiyo ilikuwa gumzo wakati wa kihistoria kwa timu ya wanawake ya Uhispania, ambayo wakati huo ilikuwa ikisherehekea ushindi wake wa kwanza wa Kombe la Dunia.

    Wakati wa hafla ya kukabidhi kombe, Bw Rubiales alikishika kichwa cha Bi Hermoso katikati ya mikono yake na kumpiga busu kwenye midomo yake.

    Pia unaweza kusoma:

    Luis Rubiales: Mamake Rais wa FA wa Uhispania asusia kula kwa sababu ya mzozo ‘kupigana busu’

  14. Mgombea wa upinzani Diomaye Faye ndiye rais mteule wa Senegal

    .

    Mgombea wa upinzani Bassirou Diomaye Faye aliibuka mshindi wa uchaguzi wa Jumapili kwa 54.28% ya kura zote, huku mpinzani wake mkuu, Waziri Mkuu wa zamani Amadou Ba wa muungano tawala, akipata 35.79% ya kura zote.

    Idadi ya wapiga waliojitokeza kwa kura hiyo ilikuwa asilimia 61.

    Rais Macky Sall alikuwa amejaribu kuchelewesha upigaji kura uliokuwa umepangwa kufanyika hapo awali Februari, jambo ambalo lilizua maandamano ya ghasia na kusababisha vifo vya watu watatu.

    Baraza la uchaguzi nchini Senegal limemthibitisha mgombea wa upinzani Bassirou Diomaye Faye kuwa mshindi wa uchaguzi wa Jumapili.

    Wapinzani wake wa kisiasa walikuwa wameanza kukubali kushindwa ndani ya saa chache baada ya zoezi la upigaji kura kufungwa.

    Bw Faye aliibuka kutoka kwa mgombeaji maarufu wa upinzani Ousmane Sonko, ambaye aliondolewa kwa sababu ya hatia kumharibia mtu jina iliyositishwa.

    Rais mteule alifungwa kwa takriban mwaka mmoja na kuachiliwa kufuatia msamaha wa rais.

    Alikuwa na siku tisa tu za kufanya kampeni na sasa ni Rais mteule wa Senegal na ndiye mwenye umri mdogo zaidi kuchaguliwa kidemokrasia barani Afrika.

    Ameahidi kupambana na ufisadi na kukabiliana na ukosefu wa ajira, pamoja na gharama kubwa ya maisha.

    .

    Soma zaidi:

    Kutoka jela hadi kuwa rais mwenye umri mdogo kuchaguliwa Afrika

  15. Ufaransa kumshtaki mwanafunzi kwa kuvaa hijab shuleni

    .

    Waziri Mkuu wa Ufaransa anasema msichana mdogo atashtakiwa na serikali kwa kumtuhumu kwa uwongo mwalimu mkuu kwa kumpiga katika majibizano makali kuhusu kuvaa vazi la Kiislamu kichwani.

    Mwalimu mkuu alisisitiza kwamba mwanafunzi avue hijab yake kichwani akiwa shuleni, kwa mujibu wa sheria za Ufaransa.

    Alijiuzulu baada ya vitisho vya kifo kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

    Tishio la Kiislamu kwa shule za Ufaransa limechukuliwa kwa uzito mkubwa tangu mauaji ya walimu wawili.

    Samuel Paty alikatwa kichwa barabarani katika kitongoji cha Paris mnamo 2020 na Dominique Bernard aliuawa katika shule yake huko Arras miezi mitano iliyopita.

    Mwalimu mkuu wa shule ya Paris, ambaye jina lake halijawekwa wazi, alitangaza uamuzi wake katika barua pepe iliyotumwa Ijumaa kwa wenzake huko Maurice Ravel Lycée katika wilaya ya 20 ya Paris.

    "Hatimaye nimechukua uamuzi wa kuacha kazi zangu," alielezea, "kwa kujali usalama wangu na ule wa taasisi."

    "Ninaondoka baada ya miaka saba, tajiri na yenye changamoto, niliyokaa pamoja nawe, na baada ya miaka 45 katika elimu ya umma," aliandika, akiwashukuru wenzake kwa msaada waliomuonyesha katika wiki tatu zilizopita.

    Katika kisa hicho, kilichotokea tarehe 28 Februari, mkuu huyo aliwaambia wanafunzi watatu wa kike kwamba wanapaswa kutii sheria kwa kuvua hijab zao.

    Wawili walitii, lakini wa tatu hakufanya hivyo na kukawa na ugomvi.

    Niqab ni haramu nchini Ufaransa

  16. Wapiga mbizi wapata miili ya waathirika wa daraja lililoporomoka Marekani

    .

    Miili ya watu wawili imeopolewa kutoka kwenye lori nyekundu, iliyokuwa imezama chini ya maji ambapo daraja la Baltimore liliporomoka.

    Wafanyakazi wanane wa ujenzi walikuwa kwenye daraja hilo wakati meli ilipoigonga, na kuwatumbukiza kwenye majini.

    Wawili kati ya wafanyikazi waliokolewa siku hiyo, lakini shughuli ya utafutaji inaendelea kwa wengine wanne - wote wakidhaniwa wamefariki.

    Wafanyakazi wa uokoaji wanafanya kazi kushughulikia nyenzo hatari na wachunguzi wa ajali wako kwenye eneo la tukio.

    Wanne kati ya waathirika sita wa kuporomoka kwa daraja hilo wametambulika kufikia sasa.

    Katika mkutano na waandishi wa habari Jumatano, Polisi wa Jimbo la Maryland walimtambua Alejandro Hernandez Fuentes, 35, na Dorlian Ronial Castillo Cabrera, 26, kama wafanyikazi hao wawili waliopatikana na wapiga mbizi kutoka ndani ya lori. Bw Fuentes anatoka Mexico na Bw Cabrera anatoka Guatemala.

    Lakini wapiga mbizi hawawezi tena kuabiri maji kwa usalama kwa sababu ya saruji na uchafu uliopatikana mtoni, polisi walisema. Sasa wanatumia skana za sonar na wanaamini kuwa magari ambayo yanaweza kuwa na miili mingine "yamefunikwa kwa muundo wa juu na simiti" ambayo ilishuka kutoka kwenye daraja, afisa mmoja alisema.

    Waathirika wengine wawili waliotoweka, ambao wanadhaniwa kufariki, pia wametajwa: Miguel Luna, mwenye asili ya El Salvador, na Maynor Suazo Sandoval, raia wa Honduras.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Mexico ilisema awali kwamba raia wake wawili walidhaniwa kuwa wamefariki - mmoja wao ambaye sasa anajulikana kama Bw Fuentes - huku mwingine akiokolewa kutoka kwa maji.

    Mtu mmoja ambaye alikuwa hospitalini baada ya kuopolewa ndani ya maji aliruhusiwa Kwenda nyumbani, maafisa walisema Jumatano jioni.

    Soma zaidi:

    Watu sita wadhaniwa kufariki baada ya meli kugonga daraja Marekani

    Marekani: Daraja muhimu laporomoka mtoni baada ya kugongwa na meli ya mizigo

  17. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 28/03/2024