Got a TV Licence?

You need one to watch live TV on any channel or device, and BBC programmes on iPlayer. It’s the law.

Find out more
I don’t have a TV Licence.

Habari za moja kwa moja

Na Ambia Hirsi

time_stated_uk

  1. 'Israel itajifanyia maamuzi yenyewe'- Netanyahu asema baada ya mazungumzo na Cameron

    .

    Benjamin Netanyahu amemwambia Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Cameron kwamba Israel "itafanya maamuzi yake" kuhusu jinsi ya kujibu mashambulizi ya Iran.

    Alisema serikali yake "itafanya kila linalohitajika kujilinda" wakati wa mazungumzo ambayo serikali ya Uingereza ilitarajia itasaidia kuzuia kuongezeka kwa mzozo huo.

    Bw Netanyahu ameapa mara kwa mara kulipiza kisasi shambulio hilo ambalo halijawahi kushuhudiwa kwa makombora na ndege zisizo na rubani mwishoni mwa juma.

    Akizungumza na waandishi wa habari mjini Jerusalem baada ya mkutano na Bw Netanyahu, Bwana Cameron alisema yuko pale "kuonyesha mshikamano wetu" baada ya shambulio "baya" la Iran.

    Aliendelea kusema: "Tunatumai kuwa kila kitu ambacho Israel hufanya kina kikomo na lengo na busara iwezekanavyo.

    "Si kwa manufaa ya mtu yeyote kwamba tunaona ongezeko la hili na hilo ndilo tulilosema waziwazi kwa watu wote ambao nimekuwa nikizungumza nao hapa Israel."

    Baada ya mkutano huo, waziri mkuu wa Israel alisema: "Nataka kuweka wazi - tutafanya maamuzi yetu wenyewe, na Taifa la Israel litafanya kila linalowezekana kujilinda."

    Soma zaidi:

    David Cameron afanya mazungumzo Israel kupinga vita na Iran

  2. Cubana chief priest: Mwanamitandao maarufu Nigeria ashtakiwa kwa kurusha pesa hewani ili watu waokote

    .

    Mwanamitandao maarufu nchini Nigeria na mfanyabiashara Cubana chief priest amekuwa wa hivi punde zaidi kushtakiwa kwa kutumia vibaya pesa za noti.

    Mwanamitandao huyo, ambaye jina lake halisi ni Pascal Okechukwu, alikana mashtaka matatu ya kutumia vibaya noti alipofikishwa mahakamani Jumatano.

    Mamlaka zinasema alirusha pesa hewani katika hafla mbalimbali za kijamii.

    Hili kimsingi ni kosa kwani noti huanguka chini ambapo zinaweza kukanyagwa.

    Kitendo hicho, "maarufu", mara nyingi hufanyika katika harusi na sherehe za Nigeria.

    Pesa hutupwa hewani na kuanguka chini ambapo wageni huanza kuokota.

    Siku ya Jumanne, shirika mashuhuri la kupambana na uhalifu nchini Nigeria, Tume ya Uhalifu wa Kiuchumi na Kifedha (EFCC), ilisema inaongoza harakati dhidi ya "aina zote za matumizi mabaya ya naira [fedha]".

  3. Mvua kubwa yasababisha mafuriko huko Dubai

    Video content

    Video caption: Mvua kubwa yasababisha mafuriko katika jiji la UAE la Dubai

    Mvua kubwa imenyesha katika maeneo ya Ghuba na kusababisha mafuriko ambayo yamesababisha vifo vya watu 20 na kutatiza safari za ndege katika uwanja wa ndege wa pili wenye shughuli nyingi zaidi duniani.

    Uwanja wa ndege wa Dubai ulisema ulikuwa unakabiliwa na "wakati mgumu sana" siku ya Jumatano. Ilishauri abiria wasijitokeze kwani njia za kupaa kwa ndege zilikuwa zimejaa maji.

    Kaskazini zaidi, mwanamume mmoja alifariki baada ya gari lake kukabiliana na mafuriko.

    Huko Oman, waokoaji walipata mwili wa msichana huko Saham, na kufanya idadi ya vifo nchini kufikia 19 tangu Jumapili.

    Mamlaka pia ilionya kuwa mvua nyingi zaidi za radi, mvua kubwa na upepo mkali zilitabiriwa, huku maeneo mengi ya mabondeni yakiwa bado chini ya maji.

    Zaidi ya watu 1,400 wamehamishwa hadi kwenye makazi salama. Shule na ofisi za serikali zimefungwa kama tahadhari.

    UAE inajulikana kwa hali ya hewa ya joto na jua, ingawa mvua kubwa imekuwa ya kawaida katika miaka ya hivi karibuni.

  4. Shambulizi la makombora la Urusi kaskazini mwa Ukraine laua watu 14

    .

    Shambulizi la kombora la Urusi limeua watu 13 katika mji wa Chernihiv kaskazini mwa Ukraine, kulingana na maafisa wa Ukraine.

    Waziri wa mambo ya ndani wa Ukraine amesema kuwa kuna zaidi ya watu 60 waliojeruhiwa katika shambulizi hilo lililokumba jengo la orofa nane katika eneo lenye watu wengi.

    Makombora matatu yalishambulia karibu na katikati mwa jiji, maafisa walisema.

    Shambulio hilo lilitokea saa chache baada ya ripoti za shambulizi la Ukraine kwenye uwanja wa ndege wa jeshi la Urusi huko Crimea inayokaliwa.

    Maelezo bado hayajathibitishwa, ingawa vituo vya mitandao ya kijamii vilishirikisha video ya moto unaoonekana kwenye uwanja wa ndege huko Dzhankoy kaskazini mwa Crimea.

    Huko Chernihiv, kaimu meya Oleksandr Lomako alisema jengo moja lilikumbwa na mlipuko wa moja kwa moja kutoka kwa moja ya makombora ya Urusi na ghorofa kadhaa zimeharibiwa.

    Ofisi ya rais mjini Kyiv ilisema majengo mengine manne ya juu, hospitali, makumi ya magari na taasisi ya elimu ya juu yote yameharibiwa katika shambulio hilo.

    Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ukraine Ihor Klymenko alisema kuwa watoto wawili walikuwa miongoni mwa waliopoteza maisha, na polisi walikuwa wakitafuta vifusi kwa waathiriwa zaidi.

    Pia unaweza kusoma:

    Je, Ukraine ina uwezo wa kuzuia mabomu ya kuongozwa ya Urusi

  5. Muundo wa jengo linalofanana na pedi wazua gumzo mitandao

    .

    Muundo unaopendekezwa wa kituo cha treni katika mji wa Nanjing nchini China umevutia watumiaji wa mtandao wa China - kwa sababu zote zisizo sahihi.

    Mamlaka zinasema muundo wa kituo cha Nanjing Kaskazini ulipata msukumo kutoka kwa maua ya plum, ambayo ni maarufu katika jiji hilo.

    Lakini mtandaoni, wengine wanaashiria kufanana kwake na kitu tofauti – pedi au sodo za wanawake wanazovaa wakiwa kwenye hedhi.

    "Hii ni pedi kubwa. Inatia aibu kusema kuwa inaonekana kama maua ya plum," mmoja alisema kwenye tovuti ya kijamii ya Weibo.

    Mada hiyo imesababisha gumzo kwa mamilioni ya watu katika majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii ya China.

    "Kwa nini sote tunaweza kusema kuwa ni pedi mara moja, lakini wasanifu hawawezi?" mtumiaji mmoja wa Weibo alisema.

    "Nadhani tunapaswa kuchukua nafasi hii kuitaka jamii kuzingatia unyanyasaji dhidi ya hedhi. Ubunifu huu uko mbele ya wakati wake," mtumiaji mwingine alitania.

    Kulingana na gazeti linalomilikiwa na serikali la Nanjing Daily, muundo wa awali uliangaziwa na serikali ya jimbo la Jiangsu na Kampuni ya Reli ya Jimbo la China.

    Ujenzi unatarajiwa kuanza katika nusu ya kwanza ya 2024, kulingana na vyombo vya habari vya ndani.

    Soma zaidi:

    Nyumba 8 zenye muundo wa ajabu zaidi duniani

  6. David Cameron afanya mazungumzo Israel kupinga vita na Iran

    .

    David Cameron ameitaka Israel kufanya "kila iwezekanavyo ili kupunguza" wasiwasi Mashariki ya Kati, kabla ya mazungumzo na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.

    Israel imeapa kulipiza kisasi baada ya shambulio la Iran la kombora na ndege zisizo na rubani mwishoni mwa juma.

    Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza ataishinikiza Israel kudhibiti kiwango cha mwitikio wake kutokana na hofu kwamba inaweza kusababisha vita zaidi.

    Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuwasili Jerusalem siku ya Jumatano, Bwana Cameron alisema alikuwa huko "kuonyesha mshikamano baada ya shambulio hilo baya la Iran".

    Aliendelea: "Ni sawa kuweka maoni yetu wazi juu ya nini kinapaswa kutokea baadaye, lakini ni wazi Waisraeli wanafanya uamuzi wa kuchukua hatua.

    "Tunatumai watafanya hivyo kwa njia ambayo haitazidisha mzozo. Na kwa njia ambayo, kama nilivyosema jana, ni busara na thabiti.

    "Lakini hitaji la kweli ni kuangazia tena Hamas, kurejelea suala la mateka, msaada wa kibinadamu, kurejelea mazungumzo ya kusitishwa kwa mzozo wa Gaza."

    Baadaye, Bwana Cameron atasafiri kwenye mkutano wa mawaziri wa G7 nchini Italia, ambapo atashinikiza kuratibiwa kwa vikwazo dhidi ya Iran.

    Ameishutumu Tehran kwa kuwa "nyuma ya shughuli nyingi mbaya" katika Mashariki ya Kati na kutoa wito kwa nchi nyingine kuchukua hatua zilizopangwa kuzuia ushawishi wa Iran.

    Soma zaidi:

    Marekani na EU kuiwekea vikwazo vipya Iran baada ya shambulio

  7. Video: Tazama dereva 'mzembe' akinusurika kifo Uingereza

    Video content

    Video caption: Maafisa wa polisi wamekuwa wakiwataka madereva kuwatumia video za madereva wanaopeleka magari vibaya barabarani

    Picha ya Dashcam ya gari lililoipita nyingine kwenye barabara ya mashambani ya Yorkshire Mashariki, ikilikosa gari lililokuwa likikaribia, imetolewa na polisi.

    Wakichapisha kwenye mitandao ya kijamii, Polisi wa Humberside walisema "vitendo vya uzembe vya dereva" kwenye Barabara ya Daisy Hill, huko Burton Pidsea, Mei 2023 vilinaswa kwenye kamera na kuwasilishwa kwa Timu ya Operesheni ya Kikosi hicho.

    Kampeni ya usalama barabarani imeshuhudia takriban makosa 2,000 ya magari yakikamatwa tangu tarehe 1 Aprili 2023.

    Polisi wa Humberside walisema: “Operesheni Snap inatusaidia kuwalinda watumiaji wote wa barabara, hasa wale walio katika mazingira magumu kama vile waendesha baiskeli, waendesha farasi na watembea kwa miguu.

    "Iwapo una picha za dashcam za mtu anayeendesha gari kwa njia hatari, tafadhali ripoti kupitia tovuti yetu ya Op Snap ili tuweze kuichunguza na kuchukua hatua zinazofaa."

  8. Bilionea wa Rwanda aliyekimbia nchi Tribert Rujugiro afariki dunia

    Yves Bucyana

    BBC Swahili

    Tribert Rujugiro alikimbia Rwanda mwaka 2010
    Image caption: Tribert Rujugiro alikimbia Rwanda mwaka 2010

    Bilionea wa Rwanda Tribert Rujugiro Ayabatwa, ambaye alikuwa amekimbia Rwanda kwa miaka mingi mingi iliyopita, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 83.

    Katika mahojiano na gazeti la New Vision la nchini Uganda la mwaka 2019, alisema kuwa hajui umri wake kamili kwa sababu wakati alipozaliwa hakukuwa na njia ya serikali kurekodi watoto waliozaliwa, ila kaambiwa kuwa alizaliwa mwanzoni mwa miaka ya 1940.

    Mmoja wa mawakili wake aliambia BBC kuhusu kifo cha Rujugiro, na kuongeza: "Hatuna taarifa zaidi za kutoa kwa sasa."

    Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, alikuwa akiishi Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

    Rujugiro alikuwa mmoja wa wafadhili muhimu wa Rwanda ambaye aliwasaidia kifedha waasi wa RPF-Inkotanyi katika vita walivyopigana na Jeshi la Rwanda (FAR) enzi hizo kuanzia tarehe mosi Oktoba mwaka 1990, hadi RPF ilipochukuwa madaraka Julai mwaka 1994.

    Mnamo mwaka wa 2014, jarida la Forbes lilitangaza kuwa Rujugiro ndiye mfanyabiashara tajiri zaidi wa tumbaku barani Afrika.

    Kabla ya kutofautiana na serikali ya Rwanda na kukimbilia Afrika Kusini mwaka 2010, alikua mshauri wa Rais wa Rwanda Paul Kagame.

    Nchini Rwanda, Rujugiro anajulikana sana kwa jengo lake lililo kati kati ya jiji la Kigali ambalo lilijulikana kama UTC (Union Trade Centre), ambalo ni moja ya majengo ya kwanza kujengwa baada ya mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994.

    Jengo hilo linakadiriwa kuwa na thamani ya takriban dola milioni 20 za kimarekani.

    Lilifungua milango yake mnamo 2006. Serikali ilipiga mnada jengo hilo mwaka 2017 ikidai kuwa Rujugiro, mwenye hisa nyingi, anadaiwa kodi ya zaidi ya dola milioni moja, jambo ambalo ameendelea kukanusha.

    Wakati jengo hilo likipigwa mnada, tayari kulikuwa na kesi kati ya Rujugiro dhidi ya serikali ya Rwanda katika Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) kuhusu uvamizi wa jengo hilo mwaka 2013 na wilaya ya Nyarugenge kwa madai kuwa ‘’mali isiyo na wamiliki’’.

    Mnamo Agosti 2022, mahakama hiyo yenye makao yake makuu mjini Arusha, Tanzania, iliamuru serikali ya Rwanda imlipe Rujugiro fidia ya dola milioni moja kwa sababu ya kudhibiti na kuuza jengo hilo kinyume cha sheria.

    Wakati huo, baada ya uamuzi wa mahakama katika rufaa hiyo, Rujugiro aliiambia BBC kwamba kwake pesa hizo zilitosha, "kwa sababu kilichonipeleka huko [mahakamani] sio wao kunipa fidia kilichonipeleka pale ni kutaka warudishe jengo langu."

    Alipoulizwa iwapo jengo hilo halitarejeshwa kwake ataendelea kushtaki, alijibu: "Hapana, hatutabishana, nitasubiri, kwa sababu wanasema kwamba hakuna mvua inayonyesha daima.

    "Naweza kusubiri serikali hiyo iondoke, na nyingine itanirudishia".

    Rujugiro pia amekuwa maarufu nchini Burundi tangu miaka ya 1970, katika tasnia kilimo cha tumbaku.

    Biashara yake ilivuka Rwanda na Burundi, alikuwa pia na shughuli za biashara katika nchi kama Uganda, Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Angola, Sudan Kusini, Afrika Kusini na Nigeria.

  9. Video: Tazama bata mkali akiwatatiza wapita njia huko Birmingham

    Video content

    Video caption: Bata awatatiza wapita njia Birmingham
  10. Afrika Kusini: Watoto wala sumu ya panya wakifikiri ni pipi

    xx

    Zaidi ya watoto 40 walipelekwa hospitalini nchini Afrika Kusini Jumatatu baada ya kula sumu ya panya kwa bahati mbaya wakifikiri ni pipi.

    "Baada ya uchunguzi wa kimatibabu, 17 walilazwa kwa uangalizi zaidi, huku 24 waliosalia wakiruhusiwa nyumbani wakiwa katika hali nzuri," mamlaka za afya za kikanda za Gauteng zilisema.

    Siku ya Jumatatu pia, kundi la watu 10 wakiwemo watoto wanane walipewa rufaa kwenda katika hospitali tofauti katika mkoa huo huo.

    Mamlaka za afya zinasema kuwa hii yote ni sehemu ya ongezeko "la kutisha" la jumla ya visa vya sumu ya chakula - jumla ya matukio kama hayo 863 yaliripotiwa tangu Oktoba mwaka jana.

    Wanawashauri wazazi na walezi kuchukua tahadhari zaidi ili kuwalinda watoto, na wanasema mtu yeyote aliye na dalili za sumu ya chakula - kama vile kichefuchefu, kuhara, kutapika na kuumwa na tumbo - atembelee kituo cha afya kilicho karibu naye haraka iwezekanavyo.

  11. Adidas yafanikiwa kujiondoa kwenye mkataba na rapa Kanye West

    xx

    Kampuni ya Adidas hatimaye imejinasua kutoka kwa mgogoro mkali wa kisheria na rapa Kanye West na inasema inatarajia kupata faida ya euro milioni 700 mwaka 2024.

    Mwezi Februari kampuni hiyo kubwa ya mavazi ya Ujerumani ilisema inapanga kuuza bidhaa zake za Yeezy zilizosalia kutokana ushirikiano wake na West kwa bei nzuri.

    Tamko la kusisimua lililotolewa Jumanne na Adidas linakuja mwezi mmoja baada ya kampuni kupata hasara kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 30.

    Inatengeneza viatu vya Samba, Gazelle na Campus. Kampuni hiyo ilisema kuwa takwimu zilizorekebishwa zilikuwa euro milioni 200 zaidi ya ilivyotabiriwa hapo awali na kushuka hadi kiwango bora kuliko ilivyotarajiwa robo ya kwanza ya mwaka.

    Kampuni hiyo ilisema faida yake ya robo mwaka ilifikia euro milioni 336, kutoka euro milioni 60 mwaka mmoja kabla ya kukumbwa na mvutano na West.

    Adidas zaidi ilisema kuwa imeuza bidhaa nyingine za Yeezy zenye thamani ya euro milioni 150 katika robo ya mwaka, kwa faida ya karibu euro milioni 50.

  12. Mbappe aisaidia PSG kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa

    Mbappe

    Kylian Mbappe alifunga mara mbili wakati Paris St-Germain ilipoizaba Barcelona na kubadilisha matokeo ya awali na kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa.

    PSG ilikuwa nyuma kwa mabao 3-2 baada ya mechi ya mkondo wa kwanza iliyochezwa Ufaransa lakini ikafika hatua ya nne bora kwa mara ya kwanza tangu 2021 baada ya pambano lisilo la kawaida nchini Uhispania.

    Kikosi cha Luis Enrique kitamenyana na Borussia Dortmund katika nusu fainali baada ya kuifunga Atletico Madrid kwa jumla ya mabao 5-4 katika pambano kali nchini Ujerumani.

    Wageni hao walianza vyema kati ya wawili hao ambao wamekuwa kwenye nyumba ya muda ya mabingwa mara tano wa Barcelona - Estadi Olimpic Lluis Companys.

    Lakini ni timu ya Catalan ndiyo iliyofunga bao la kwanza wakati Lamine Yamal alipoendesha upande wa kulia, akimshinda Nuno Mendes na kumsogelea Raphinha kufunga akiwa karibu na goli.

  13. Rais wa Ukraine ataka anga ya Ukraine kulindwa sawa na ilivyolindwa Israel

    .
    Image caption: Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky

    Rais wa Ukraine Volodymir Zelensky ametoa wito kwa washirika wa Ukraine kuilinda kwa njia sawa na walivyoweza kuilinda Israeli kutokana na shambulio la anga kutoka Iran.

    Katika hotuba yake ya Jumatatu jioni, rais huyo wa Ukraine alisema kwamba baada ya shambulio la Iran, "ulimwengu mzima uliona vitendo vya washirika katika anga ya Israel na nchi jirani jinsi umoja wa kweli unaweza kuwa na ufanisi katika kulinda dhidi ya ugaidi ikiwa nia ya kutosha ya kisiasa ni msingi wa umoja.”

    "Israel si mwanachama wa NATO, na hakukuwa na haja ya kitu chochote kama kuwezesha Ibara ya 5 [ya Mkataba wa NATO juu ya ulinzi wa pamoja wa wanachama wote wa muungano]. Na hakuna mtu aliyeingizwa kwenye vita. Walisaidia tu kulinda maisha, "Zelensky alisema.

    Siku ya Jumapili usiku, Iran ilirusha zaidi ya makombora 300 na ndege zisizo na rubani kuelekea Israel.

    Kulingana na wanajeshi wa Israeli na Magharibi, ulinzi wa anga wa Israeli na washirika wake, wakiungwa mkono na ndege za kijeshi kutoka Marekani, Uingereza na Ufaransa, waliharibu 99% ya makombora haya.

    Maelezo zaidi:

    Je, Ukraine ina uwezo wa kuzuia mabomu ya kuongozwa ya Urusi

    Fahamu Ndege mpya za kivita za Urusi aina ya Su-57 na kwanini zinatumika kwa kificho?

    Je Ukraine kupewa ndege za kivita za F-16 kutaipa ushindi dhidi ya Urusi?

  14. Mwanafunzi afutiwa hotuba ya kuhitimu kufuatia mvutano wa chuki ya Israel-Gaza

    Asna Tabassum

    Chuo Kikuu cha Kusini mwa California (USC) kimefuta hotuba ya kuhitimu ya mwanafunzi kufuatia chuki zilizuibuka dhidi ya shughuli zake katika mitandao ya kijamii kuhusu Israel.

    Asna Tabassum alisema alikuwa mlengwa wa "kampeni ya chuki iliyokusudiwa kunyamazisha sauti yangu".

    USC ilitaja "hatari kubwa" kwa usalama wa chuo katika uamuzi wa kusitisha anwani ya mwanafunzi Muislamu.

    Bi Tabassum ni mwanafunzi wa valedictorian wa 2024, mwanafunzi aliyechaguliwa kwa alama za juu za masomo na kuhusika katika maisha ya chuo kikuu.

    Uamuzi wa kufuta hotuba yake ulifuatia madai kwamba shughuli zake kwenye mitandao ya kijamii hazikuhusu dini.

    Mjadala kuhusu uhuru wa kujieleza kwenye vyuo vya Marekani umeongezeka tangu vita vya Israel na Gaza vilipozuka Oktoba mwaka jana.

    Akaunti ya Instagram ya Bi Tabassum inaunganisha kwenye tovuti ambayo inaikosoa Israel na kutaka "ikomeshwe kabisa", badala yake inabishana kuhusu "suluhisho la serikali moja... ambapo Waarabu na Wayahudi wanaweza kuishi pamoja".

    Tovuti hiyo pia inadai kwamba "Uzayuni ni itikadi ya kibaguzi ya walowezi-wakoloni ambayo inatetea jamii ya Kiiyahudi lililojengwa kwenye ardhi ya Palestina".

    Pia unaweza kusoma:

    Kuna tofauti gani kati ya chuki dhidi ya Wayahudi na chuki ya Uzayuni?

    'Kwa manufaa ya nchi yetu, lazima tubadili uongozi' - Magazeti ya Israel

    Hadithi ya umwagaji damu ya kuzaliwa taifa la Wayahudi la Israel

  15. Salman Khan: Watu wawili wakamatwa kwa kufyatua risasi nyumbani kwa nyota wa Bollywood

    Nyota huyo wa Bollywood ameshiriki katika uigizaji wa zaidi ya filamu 100
    Image caption: Nyota huyo wa Bollywood ameshiriki katika uigizaji wa zaidi ya filamu 100

    Polisi nchini India wamewakamata wanachama wawili wa genge la wahalifu kwa shambulio la bunduki lililolenga nyumba ya mwigizaji wa Bollywood Salman Khan.

    Nyota huyo ambaye ameshiriki katika filamu zaidi ya 100, alikasirisha genge la Bishnoi kwa kuwaua swara wawili zaidi ya miaka 20 iliyopita, polisi wanasema.

    Genge hilo ni la madhehebu ya kidini ambayo humchukulia mnyama huyo kuwa mtakatifu.

    Bw Khan hajadhurika, lakini hili ndilo tukio la hivi punde zaidi katika mfululizo wa vitisho ambavyo mwigizaji huyo amepokea katika miaka ya hivi karibuni.

    Polisi mjini Mumbai walisema watu hao wawili walitumia pikipiki mapema Jumapili asubuhi na kufyatua risasi tano kwenye nyumba ya Khan katika kitongoji cha cha Bandra kabla ya kukimbia.

    Vicky Gupta, 24, na Sagar Kumar Palak, 21, walikamatwa karibu na hekalu katika wilaya ya Kutch huko Gujarat Jumatatu usiku.

    Kulingana na polisi, wawili hao walikiri kuhusika kwao katika tukio la ufyatuaji risasi nje ya Makazi ya Galaxy.

  16. Dhoruba kali yakumba Falme za Kiarabu huku Dubai ikielekeza ndege kwingine

    XX

    Mvua kubwa imenyesha katika baadhi ya mataifa ya Ghuba, na kusababisha mafuriko katika eneo hilo na kuzifanya safari za ndege kuelekea uwanja wa ndege wa kimataifa wenye shughuli nyingi zaidi kuelekezwa kwingine.

    Uwanja wa ndege wa Dubai ulisema shughuli "zilibadilishwa kwa muda" - ingawa zimeanza tena.

    Mamlaka nchini Oman imesema watu 18 wamefariki kutokana na mafuriko.

    Mataifa kadhaa yalipata mvua ya takriban mwaka mmoja kwa siku moja.

    Video ambayo haijathibitishwa kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai ilionekana kuonyesha ndege zikiacha mawimbi wakati zikishuka kwenye njia za ndege zilizofurika.

    Katika taarifa, uwanja wa ndege ulisema safari za ndege za ndani zilizopaswa kuwasili Jumanne jioni zilielekezwa "kutokana na tukio la hali ya hewa linaloendelea kwa sasa katika UAE".

    Safari za kuondoka zitaendelea kama ilivyopangwa, iliongeza. Safari za ndege baadaye zilirejelewa tena baada ya kukatizwa kwa saa mbili.

  17. Marekani na EU kuiwekea vikwazo vipya Iran baada ya shambulio

    Jeshi la Israel linaonyesha kile linachosema ni kombora la balistiki la Iran lililopatikana kutoka Baharini

    Marekani na Umoja wa Ulaya wanasema wanatazamia kuiwekea Iran vikwazo zaidi, baada ya mashambulizi yake dhidi ya Israel mwishoni mwa juma.

    Waziri wa Fedha wa Marekani Janet Yellen alisema anatazamia kuchukua hatua "katika siku zijazo", huku mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell akisema umoja huo unalifanyia kazi.

    Israel imewataka washirika wake kuwekea vikwazo dhidi ya mpango wa makombora wa Tehran.

    Vikwazo vya Umoja wa Mataifa kuhusu mpango huo vilikwisha muda wake Oktoba.

    Vikwazo hivyo vilihusishwa na mapatano mapana zaidi ya kupunguza mpango wa nyuklia wa Iran.

    Hata hivyo nchi kadhaa zikiwemo Marekani, EU na Uingereza zilidumisha vikwazo na kuongeza vingine vipya.

    Mkuu wa majeshi ya Israel, Lt Jenerali Herzi Halevi, alisema siku ya Jumatatu kuwa shambulio la Iran halitapita bila kujibiwa.

    Shambulio la kwanza la moja kwa moja la Iran dhidi ya Israel siku ya Jumamosi lilishuhudia wimbi la zaidi ya makombora 300 na ndege zisizo na rubani kurushwa kutoka Iran, Iraq, Syria na Yemen, huku nyingi zikiangushwa na Israel na washirika wake.

    Tehran ilisema shambulio hilo lilikuwa la kulipiza kisasi shambulizi linalodhaniwa kuwa la anga la Israel dhidi ya ubalozi wake mdogo nchini Syria tarehe 1 Aprili, ambapo watu 13 waliuawa.

    Soma zaidi:

    Iran yaonya kufanya shambulizi baya zaidi ikiwa Israel italipiza kisasi

    Ni silaha gani zilitumika katika mashambulio ya Iran na Israeli ilizuiaje?

    Iron Dome: Fahamu jinsi mfumo wa ulinzi wa anga wa Israel unavyofanya kazi

  18. Natumai hujambo.