Got a TV Licence?

You need one to watch live TV on any channel or device, and BBC programmes on iPlayer. It’s the law.

Find out more
I don’t have a TV Licence.

Habari za moja kwa moja

Na Ambia Hirsi, Abdalla Seif Dzungu na Dinah Gahamanyi

time_stated_uk

  1. Hadi hapa ndio tunafikia mwisho wa matangazo yetu ya moja kwa moja kwa leo, tukutane tena hapo kesho.

  2. Mwanaume ashikiliwa kwa tisho la bomu la Paris katika ubalozi mdogo wa Iran

    f

    Polisi wenye silaha mjini Paris wamemkamata mwanaume mmoja baada ya kuripotiwa kuwa alionekana akiingia kwenye ubalozi mdogo wa Iran karibu na Mnara wa Eiffel huko Paris.

    Vyombo vya habari vya Ufaransa vilisema shahidi alimwona mtu anayeshukiwa akiingia kwenye ubalozi huo, na maafisa wa kikosi cha Ufaransa cha kuingilia kati cha BRI walilizingira jengo hilo.

    Shahidi alimwona mwanamume huyo akiwa amebeba guruneti au fulana ya vilipuzi.

    Ripoti kutoka Ufaransa zinasema mshukiwa hatimaye aliondoka kwenye jengo hilo, na alikamatwa muda mfupi baadaye. Kisha alitafutwa na maafisa wa BRI na kukutwa akiwa hana vilipuzi.

    Wakati huo huo, ubalozi wa Marekani mjini Paris- umeshirikisha tahadhari ya usalama kwenye mtandao wa X , ukisema "Mamlaka ya Paris inawataka watu kukaa mbali na eneo la ubalozi wa Iran mjini Paris kutokana na operesheni ya usalama inayoendelea."

  3. Rekodi zisizosaulika kwenye Dabi ya Simba vs Yanga

    Mwishoni mwa juma hili Simba na Yanga zinakutana katika mchezo wao mzunguko wa pili wa ligi kuu Tanzania, baada ya matokeo ya 5-1 kwenye mchezo wa kwanza yapo mengi yakutazamwa kwenye mchezo huu wenye kuvutia watu wengi zaidi ukanda wa Afrika Mashariki.

    Je unayafahamu baadhi ya matokeo ya kustaajabisha yaliyowahi kutokea tangu zilipokutana mara ya kwanza mwaka 1965?:

    Video content

    Video caption: Tazama: Rekodi zisizosaulika kwenye Dabi ya Simba vs Yanga
  4. Mkuu wa Umoja wa Mataifa ataka kukomesha 'mzunguko hatari wa kulipiza kisasi'

    g

    Antonio Guterres - katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa - anasema ni "wakati mwafaka wa kukomesha mzunguko hatari wa kulipiza kisasi katika Mashariki ya Kati", kulingana na taarifa kutoka kwa msemaji wake.

    Anaongeza kuwa Guterres "analaani kitendo chochote cha kulipiza kisasi na anatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kufanya kazi pamoja ili kuzuia maendeleo yoyote zaidi yanayoweza kusababisha madhara makubwa kwa eneo zima na kwingineko".

  5. Israel na Iran: Blinken asisitiza kwamba Marekani 'haikuhusika' katika mashambulizi ya Iran

    h

    Alipoulizwa na mwandishi wa BBC Jessica Parker kwa nini anakataa kujadili matukio mara moja, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Blinken

    Alisema kwamba atakuwa "mchoshi sana", kama njia ya mwanadiplomasia huyo mkuu wa Marekani ya kukataa kuzungumzia shambulio la wazi la Israel dhidi ya Iran.

    Blinken amesema kwamba Marekani "haikuhusika" katika operesheni yoyote ya kijeshi na inaendelea kufanya juhudi za kwa ajili ya kuhakikisha pande mbili zinapunguza kasi ya mzozo.

    Katika kujibu swali la pili kuhusu jinsi atakavyoonyesha hali ya sasa ya mahusiano ya Marekani na Israel, Blinken amesema "tunazungumza mara kwa mara, kila siku".

    "Tumejitolea kuisaidia Israel kujilinda na kama ni muhimu kushiriki katika utetezi wake, kama ulivyoona siku chache zilizopita."

  6. Francis Ogolla: Kenya inachunguza ajali iliyomuua mkuu wa kijeshi

    d
    Image caption: Jenerali Ogolla alikua mkuu wa majeshi ya Kenya mwezi Aprili mwaka jana

    Serikali ya Kenya imetuma timu kuchunguza ajali ya helikopta iliyoua mkuu wa jeshi Jenerali Francis Ogolla na wengine tisa.

    Haijabainika mara moja kilichosababisha ajali hiyo.

    Jenerali Ogolla alikuwa miongoni mwa watu 12 waliokuwa ndani ya ndege hiyo ya kijeshi iliyoanguka Alhamisi alasiri muda mfupi baada ya kupaa kaskazini-magharibi mwa nchi.

    Miili ya waliofariki ilisafirishwa hadi Nairobi na manusura wawili wamelazwa hospitalini kutibiwa.

    Akitangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa, Rais William Ruto alisema vifo hivyo ni "wakati wa huzuni kubwa" kwa nchi.

    b
    Image caption: Jenerali Ogolla aliteuliwa kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Kenya mwezi Aprili mwaka ja

    Bw Ruto alimtaja mshauri wake mkuu wa kijeshi kuwa afisa shupavu aliyefariki akiwa kazini.

    “Nchi yetu imempoteza mmoja wa majenerali wake shupavu, maafisa shupavu, wanaume na wanawake wa huduma,” Bw Ruto aliambia taifa.

    Jenerali Ogolla alijiunga na Jeshi la Ulinzi la Kenya kwa mara ya kwanza tarehe 24 Aprili 1984, kulingana na tovuti ya wizara ya ulinzi ya Kenya.

    Alitarajiwa kuadhimisha miaka 40 katika jeshi wiki ijayo.

  7. Shambulio la Israel dhidi ya Iran: Maafisa wa Magharibi wanasema Israel 'inatikisa tu kiberiti'

    Raia wa Iran waliamka na kusikia taarifa za shambulio la "ndege ndogo zisizo na rubani" kwenye eneo la kijeshi huko Isfahan, katikati mwa Iran.

    Baadhi ya maafisa wa nchi za magharibi wanaofahamu uwezekano wa Israel kulipiza kisasi dhidi ya mashambulizi ya Iran yasiyo na kifani na makombora dhidi ya Israel wanaamini kuwa hii ni "hatua ya kwanza".

    "Mkakati ni: Mashambulizi madogo ya kuifanya Iran kujibu kwa jibu kubwa kwenye maeneo ya nyuklia", kulingana na mwanadiplomasia wa magharibi huko Lebanon.

    Wakati huo huo, afisa wa kijeshi wa nchi za magharibi anasema kwamba kulingana na ripoti kutoka Syria na Iran - baadhi ya rada muhimu zililengwa na mashambulio ya ndege zisizo na rubani katika nchi zote mbili, "Waisraeli wanaaishutumu Iran na washirika wake kama Hezbollah kwa kujaribu kwanza kuharibu rada, kuunda malengo ya uongo pamoja na kujaribu kuharibu rada ili kuzima mifumo ya kuingilia kati," walisema.

    Bado kuna habari nyingi zinazokinzana zinazotoka Iran kuhusiana na tukio hilo, huku vyombo vya habari vinavyohusishwa na jeshi la Iran-IRGC, Tasnim vikikana "shambulio lolote dhidi ya Iran" vikinukuu "vyanzo vya habari".

    Wakati baadhi ya maafisa wa Irani waliviambia vyombo vya habari kwamba "hakutakuwa na majibu yoyote kutoka kwa Iran kwa tukio hilo".

    Lakini swali ni je, kweli hili lilikuwa kisasi kilichotarajiwa cha Israeli? Maafisa wa Magharibi wanaamini i haikuwa hivyo. Wameiambia BBC kuwa shambulio hilo lililuwa ni "mtego" tu "kutikisa kiberiti."[Ili kuona iwapo Iran itajibu]

  8. Bell UH-1H Huey II: Ifahamu ndege iliohusika katika ajali na kumuua mkuu wa majeshi ya Kenya

    .
    Image caption: Ndege aina ya Bell UH-1H Huey II

    Ajali mbaya ya helikopta iliyoumuua mkuu wa majeshi ya Ulinzi (CDF) Francis Ogolla na maafisa wengine tisa wakuu wa kijeshi eneo la Marakwet Mashariki imeiweka nchi katika kipindi cha maombolezo.

    Ogolla ambaye alikuwa pamoja na maafisa hao alikuwa katika safari ya kuwatembelea wanajeshi waliotumwa Kaskazini mwa eneo la bonde la Ufa chini ya Operesheni Maliza Uhalifu na kukagua kazi zinazoendelea za ukarabati wa shule katika shule tano.

    Lakini ndege iliopata ajali ni ndege ya aina gani?

    • Uchunguzi unapoanza, maelezo muhimu yanajitokeza kuhusu ndege hiyo iliyoharibika, na kutoa maarifa ya kuelewa kilichoharibika.
    • Ndege hiyo ni mojawapo ya helikopta sita za Bell UH-1H Huey II zilizonunuliwa na Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) kutoka Marekani mwaka wa 2016.
    • Imeundwa na kampuni ya anga ya Marekani Bell Helikopta.
    • Ni helikopya ya kwanza ya familia ya Huey, na vile vile ni helikopta ya kwanza yenye nguvu ya turbine katika huduma ya jeshi la Marekani.
    • Maafisa walisema kwamba helikopta hizi zilinuiwa kuimarisha uwezo wa kijeshi wa Kenya.
    • Hii ni katika operesheni za kukabiliana na ugaidi na msaada kwa wanajeshi wanaohudumu katika ujumbe wa Umoja wa Afrika katika eneo hilo.
    • Ndege hiyo ni toleo lililoboreshwa la helikopta ya hali ya juu ya Bell UH-1H, inayojumuisha vifaa kama vile fremu za hewa zisizo na muda zilizorekebishwa na injini zilizoboreshwa.
    • Bell UH-1H ilitumiwa kwa mara ya kwanza na jeshi la Marekani katika operesheni za mapigano wakati wa Vita vya Vietnam mnamo 1962.
    • Ilitumika kwa madhumuni mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kufanya usaidizi wa jumla, mashambulizi ya anga, usafiri wa mizigo, uokoaji, utafutaji, vita vya kielektroniki, na misheni ya mashambulizi ya ardhini.
    • Maboresho haya yanaipa helikopta uwezo ulioboreshwa wa kuelea na mbali na kuifanya kuwa bora zaidi na ya kuaminika.
    • Ina uwezo wa kubeba abiria wakiwemo wahudumu wawili .
    • Ina urefu wa mita 17 na upana wa mita nne.
    • Ndege hii ina uwezo wa kusafiri kwa kasi ya 209km/h
  9. Israel inasubiri kuona iwapo Iran italipiza kisasi

    James Landale

    Mwandishi wa masual ya kidiplomasia

    Uchambuzi

    Shambulio lililoripotiwa la Israel dhidi ya Iran lilikuwa ni zawadi kali ya siku ya kuzaliwa kwa Kiongozi Mkuu wa nchi hiyo, Ayatollah Ali Khamenei, ambaye leo anatimiza umri wa miaka 85.

    Watu wa Israeli walikuwa wakijiandaa kwa ajili ya kuanza kwa likizo ya Pasaka wiki ijayo. Sasa watasubiri kuona ni lini na vipi Iran itaamua kulipiza kisasi.

    Asubuhi hii mitaa ya Jerusalemu ilikuwa na shughuli nyingi lakini tulivu kabla ya kuanza kwa Sabato.

    Ikiwa hili ni shambulizi dogo kwa malengo ya kijeshi yanayohusiana na shambulio la Iran dhidi ya Israeli wikendi iliyopita - kama vile kambi ya anga au kituo cha kuhifadhi makombora - basi hilo linaweza kuonekana kama jibu dogo la Israeli kuliko maafisa wengine wa magharibi walivyohofia.

    Shambulio lolote ambalo lingepiga vifaa vya nyuklia vya Iran, lingesababisha vifo vya raia lineonekana kuwa kubwa zaidi.

    Ingawa Israel haijakubali rasmi shambulio hilo, wachambuzi wanasema ishara ambayo nchi hiyo ilikuwa ikituma ni kwamba inaweza kushambulia ndani kabisa ya ardhi ya Iran.

    Jonathan Conricus, msemaji wa zamani wa jeshi la Israel -IDF, amesema kwenye mtandao wa kijamii: "Iran inataka kurudi kwenye kivuli na inapuuza shambulio la Israeli kwenye mji wa kimkakati wa Isfahan, lakini nadhani wamepata ujumbe: Israeli inaweza kupenya ulinzi wa Iran na kupiga popote inapotaka.”

    Lakini baadhi ndani ya serikali ya Israeli wameonekana kutopendezwa sana. Waziri wa Usalama wa Kitaifa wa mrengo wa kulia kabisa, Itamar Ben Gvir, alichapisha kwenye X (zamani Twitter) neno moja kuhusu shambulio hilo lililotafsiriwa vyema kama: "Dhaifu."

    g
  10. Maisha ya kila siku mjini Tehran yanaonekana kutoathirika baada ya shambulio la Israel

    Vyombo vya habari vya Iran na maafisa wamepuuza ripoti za shambulio kwenye tovuti katikati mwa mji wa Isfahan na mji wa kaskazini-magharibi wa Tabriz.

    Hossein Dalirian, msemaji wa Kituo cha Kitaifa cha Nafasi ya Mtandao na Shirika la Anga la Iran, katika chapisho X alikanusha kuwa kulikuwa na shambulio la kombora la moja kwa mojakutoka nje ya nchi, jambo ambalo linakinzana na maelezo yamaafisa wa Marekani kwamba kombora la Israel limeipiga Iran.

    h
    Image caption: Watu wanatembea katika barabara za mji mkuu wa Iran Tehran asubuhi ya leo
    h
    Image caption: Mwanamume akiwalisha njiwa kwa sanamu mjini Tehran
    g
    Image caption: Wakazi na wasafiri wakitembea mtaani
  11. 'Iran haina mpango wa kulipiza kisasi haraka' - afisa wa Iran

    Afisa mkuu wa Iran ameliambia shirika la habari la Reuters "Iran haina mpango wa kulipiza kisasi mara moja dhidi ya Israel," saa chache baada ya shambulio dhidi ya mji wa Isfahan nchini Iran, ambalo linaripotiwa kufanywa na Israel.

    Maafisa wawili wa Marekani waliambia vyombo vya habari kwamba shambulio hilo lilitoka Israel, lakini Israel haijadai kuhusika hadi sasa.

    "Chanzo cha kigeni cha tukio hilo hakijathibitishwa. Hatujapokea shambulio lolote kutoka nje, na majadiliano yanaegemea zaidi katika kujipenyeza kuliko kushambuliwa," afisa huyo wa Iran alisema kwa sharti la kutotajwa jina.

    Saa moja tu iliyopita, mchambuzi wa Iran aliiambia Televisheni ya serikali ya Iran kwamba "Ndege ndogo zisizo na rubani zilizodunguliwa na walinzi wa anga huko Isfahan zilirushwa na wavamizi kutoka ndani ya Iran", akipuuza ripoti kwamba Israel ilifanya shambulio hilo.

    Oman yalaani shambulizi la Israel

    Wakati huo huo Oman imelaani shambulizi lililoripotiwa na Israel dhidi ya Iran.

    Katika taarifa kutoka kwa wizara ya mambo ya nje, wamelaani "mashambulizi ya mara kwa mara ya jeshi la Israel katika eneo hilo".

    Oman imekuwa ikifanya kazi kama mpatanishi katika Mashariki ya Kati ikijaribu kuondoa hali hiyo.

    Ufaransa pia uhasama upunguzwa katika eneo hilo, huku Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Jean-Noel Barrot akisema "msimamo wa Ufaransa ni kutoa wito kwa wahusika wote kupunguza kasi ya mashambulizi na kujizuia".

  12. Marekani yadhibiti usafiri kwa wafanyakazi wa ubalozi nchini Israel

    Marekani imeweka vikwazo vya kusafiri kwa wafanyakazi wake wa ubalozi nchini Israel na wanafamilia wao "kutokana na tahadhari" kufuatia ripoti za mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Israel dhidi ya Iran.

    Ubalozi huo ulisema wafanyakazi wameambiwa wasisafiri nje ya eneo la Tel Aviv - ikiwa ni pamoja na Herzliya, Netanya, na Even Yehuda - na maeneo ya Jerusalem na Be'er Sheva hadi ilani nyingine itakapotolewa.

    "Mazingira ya usalama yanasalia kuwa magumu na yanaweza kubadilika haraka kulingana na hali ya kisiasa na matukio ya hivi majuzi," ilisema katika taarifa siku ya Ijumaa.

    Huku hayo yakijiri Iran imeondoa marufuku ya usafiri wa anga iliyokuwa imeweka.

    Kulingana na tovuti ya uangalizi ya FlightRadar24 wakati habari zilipoibuka mapema juu ya uwezekano wa shambulio la Israeli dhidi ya Iran shughuli za usafiri wa ndege zilianza kudhibitiwa katika anga ya nchi hiyo.

    Flydubai pia aliambia vyombo kadhaa vya habari kwamba itaahirisha safari zote za ndege kwenda Iran siku ya Ijumaa, na kwamba safari ya ndege kutoka Dubai hadi Tehran imegeuzwa.

    Iran sasa inaashiria kwamba usitishaji huo umekwisha na kwamba biashara zimerejelea hali kawaida katika viwanja vyake vya ndege.

    Shirika la habari la serikali IRNA liliripoti kuwa safari za ndege zimeanza tena katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Imam Khomeini mjini Tehran.

  13. Liverpool yaondolewa mashindano ya Yuropa

    .

    Matumaini ya Liverpool kumaliza ufalme wa Jurgen Klopp kwa kunyakua taji la Uropa yamekamilika baada ya kushindwa kupindua matokeo ya mechi ya mkondo wa kwanza dhidi ya Atalanta.

    The Reds walisafiri hadi Italia baada ya kuchapwa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Anfield Alhamisi iliyopita na, licha ya kudhibiti mchezo huo kwa vipindi virefu, hawakuweza kupata mabao yaliyohitajika na kupoteza kwa jumla ya mabao 3-1.

    Bao la penalti la Mohamed Salah dakika ya saba, baada ya krosi ya Trent Alexander-Arnold, liliwapa matumaini.

    Kipindi cha kwanza kilipokaribia mwisho, mshambuliaji huyo wa Misri alipiga juu alipopigiwa pasi moja safi, lakini kikosi cha Klopp kilijitahidi kutengeneza nafasi zaidi katika kipindi cha pili.

    Hatua hiyo inakamilisha msururu mgumu wa siku 12 kwa The Reds, ambao walitoka sare na Manchester United na kupoteza nyumbani kwa Crystal Palace na kusalimisha uongozi wao kileleni huku wakisalimisha uongozi wao wa ligi ya Premier kwa Mancity.

    Macho yote sasa yanaelekezwa kwenye mbio za ubingwa wa ligi huku Liverpool ikishika nafasi ya tatu nyuma ya Arsenal inayoshika nafasi ya pili na pointi mbili nyuma ya vinara Manchester City.

  14. Raia wa Poland akamatwa kwa kupanga njama ya kumuua rais wa Ukraine

    Wanajeshi wa Marekani walionekana kwenye Uwanja wa Ndege wa Rzeszow-Jasionka mnamo 2022

    Mwanaume mmoja raia wa Poland amekamatwa na kushtakiwa kwa kupanga kushirikiana na idara za ujasusi za Urusi kusaidia uwezekano wa mauaji ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, mamlaka ilisema.

    Waendesha mashtaka wa Poland walisema mwanamume huyo kwa jina la Pawel K, alidaiwa kukusanya taarifa kuhusu uwanja wa ndege nchini Poland unaotumiwa na rais wa Ukraine.

    Kukamatwa kwake kulifanyika kwa msingi wa ujasusi wa Ukraine, waliongeza.

    Mamlaka haikubainisha ikiwa mtu huyo kweli alitoa taarifa yoyote.

    Anaweza kufungwa jela miaka minane ikiwa atapatikana na hatia.

    Mshukiwa yuko chini ya ulinzi na uchunguzi unaendelea.

    Katika taarifa, waendesha mashtaka wa Poland walidai Pawel K alikuwa ametoa huduma zake kwa ujasusi wa kijeshi wa Urusi.

    Aliwasiliana na Warusi "wanaohusika moja kwa moja katika vita vya Ukraine," waliongeza.

    Walisema Pawel K alikuwa amepewa jukumu la kukusanya taarifa kuhusu usalama katika Uwanja wa Ndege wa Rzeszow-Jasionka kusini-mashariki mwa Poland.

  15. Kuvuna maji na uzito wa majengo wazamisha nusu ya miji ya China

    Jengo linapungua na kuanguka katika mkoa wa Guangxi

    Takriban nusu ya miji mikuu ya China inazama kwa sababu ya uvunaji wa maji na uzito unaoongezeka wa upanuzi wake wa haraka, watafiti wanasema.

    Baadhi ya miji inapungua kwa kasi, huku moja kati ya sita ikizidi milimita 10 kwa mwaka.

    Ukuaji wa haraka wa miji wa China katika miongo ya hivi karibuni unamaanisha kwamba maji mengi zaidi sasa yanachotwa ili kukidhi mahitaji ya watu, wanasayansi wanasema

    Katika miji ya pwani, hali hii inatishia mamilioni ya watu na kutokewa mafuriko wakati viwango vya bahari vinaongezeka.

    China ina historia ndefu ya kushughulikia visa vya ardhi kuzama, huku Shanghai na Tianjin zikionyesha ushahidi wa kuzama katika miaka ya 1920.

    Shanghai imezama zaidi ya mita 3 katika karne iliyopita.

    Katika nyakati za hivi karibuni, nchi imeshuhudia kupungua kwa majiji mengi ambayo yamepanuka haraka katika miongo ya hivi karibuni.

    Ili kuelewa ukubwa wa tatizo hilo, timu ya watafiti kutoka vyuo vikuu kadhaa vya China wamechunguza majiji 82, yakiwemo yote yenye wakazi zaidi ya milioni 2

    Wametumia data kutoka kwa setilaiti za Sentinel-1 kupima mienendo ya ardhi wima kote nchini.

    Pia unaweza kusoma:

    Majumba marefu ya New York yanasababisha mji huo kuzama ni nini kifanyike kuukomboa mji huo

    Jakarta, mji unaozama kwa kasi ya juu zaidi duniani

  16. Video: Tazama wakaazi wa mji wa Isfan nchini Iran wakirekodi milipuko

    Video content

    Video caption: Tazama: Wakaazi wa mji wa Isfahan wakirekodi milipuko

    Vyombo vya habari vya serikali ya Iran vinasema kuwa walinzi wa anga wa nchi hiyo walidungua ndege tatu zisizo na rubani juu ya mji wa Ifsahan.

    Wakaazi kutoka jiji hilo wamietuma idhaa ya BBC Persia kanda hii ya milipuko.

  17. Habari za hivi pundeShambulio la Israel nchini Iran: Tunachokijua kufikia sasa

    Ni takriban saa mbili tangu tuliposikia kwa mara ya kwanza ripoti za milipuko nchini Iran. Hivi ndivyo tunavyojua hadi sasa:

    • Maafisa wawili wa Marekani wameithibitishia BBC mshirika wa Marekani CBS News kwamba kombora la Israel limeipiga Iran
    • Mapema Ijumaa asubuhi, milipuko ilisikika karibu na mji wa kati wa Isfahan, vyombo vya habari vya Irani viliripoti, vikisema kuwa ndege tatu zisizo na rubani ziliharibiwa baada ya mifumo ya ulinzi wa anga ya nchi hiyo kuanza kutumika.
    • Isfahan ni nyumbani kwa kambi ya anga ya Iran na mkoa huo una maeneo kadhaa ya kijeshi. Hakuna ripoti hadi sasa kwamba kuna kitu kilichopigwa na vyombo vya habari vya Irani vinasema vifaa vyote vya nyuklia viko salama
    • Wakati huo huo, safari kadhaa za ndege zimeelekezwa kwengine kwenye anga ya Iran, tovuti za kufuatilia zinaonyesha
    • Wanajeshi wa Israel na Pentagon wote wamekataa kutoa maoni yao hadi sasa
  18. Shambulio la Israel nchini Iran: Bei ya mafuta yapanda

    .

    Bei ya mafuta yapanda

    Bei ya mafuta na dhahabu duniani zapanda huku hisa zikishuka baada ya maafisa wa Marekani kusema kuwa kombora la Israel liliipiga Iran.

    Katika biashara ya bara Asia siku ya Ijumaa asubuhi, Mafuta ghafi yameripotiwa kupanda kwa zaidi ya 3% hadi karibu $90 kwa pipa, huku dhahabu ikiuzwa kwa bei ya juu Zaidi ya hadi $2,400 .

    Masoko ya hisa ya Japan, Hong Kong na Korea Kusini pia yalianguka baada ya ripoti hizo.

    Wawekezaji wamekuwa wakifuatilia kwa karibu majibu ya Israel kwa shambulio la ndege zisizo na rubani na kombora la Iran wikendi iliyopita.

    Ving'ora vyasikika kaskazini mwa Israeli - kijeshi

    Shirika la habari la Reuters linaripoti kuwa ving'ora vimelia kaskazini mwa Israel, likinukuu jeshi la Israel.

    Hakuna maelezo zaidi kwa sasa na jeshi la Israel linasema halitoi maoni "kwa wakati huu".

    Mifumo ya ulinzi wa anga ya Iran ipo tayari kukabiliana na mashambulio - vyombo vya habari vya serikali

    Shirika la habari la serikali IRNA linaripoti kuwa mifumo ya ulinzi wa anga ya nchi imewekwa tayari katika majimbo kadhaa.

    IRNA ilisema kuwa nchi hiyo imefungua "betri zake za ulinzi wa anga".

    Waziri wa mambo ya nje wa Iran aonya kuhusu jibu la 'haraka' kwa shambulio lolote la Israel

    Katika masaa yaliyotangulia ripoti za leo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian alionya kwamba jibu la nchi yake kwa kulipiza kisasi kwa Israeli litakuwa "mara moja na kwa kiwango cha juu".

    Alitoa maoni hayo wakati wa mahojiano kwenye CNN siku ya Alhamisi.

    Mapema wiki hii, alisema mashambulizi ya nchi yake dhidi ya Israel siku ya Jumamosi - ambayo yalihusisha zaidi ya ndege zisizo na rubani 300 na makombora - yalifikia "kutumia haki ya ulinzi halali".

    Tehran imeshikilia kuwa hatua iliyochukua ni kulipiza kisasi kwa kile kinachodhaniwa kuwa ni shambulio la anga la Israel kwenye ubalozi wake mdogo nchini Syria tarehe 1 Aprili, ambapo watu 13 waliuawa.

  19. Habari za hivi pundeNdege tatu zisizo na rubani ziliharibiwa juu ya Isfahan - Televisheni ya taifa ya Iran

    Televisheni ya taifa ya Iran imeripoti kuwa ndege tatu zisizo na rubani zilionekana angani mjini Isfahan mwendo wa saa 12:30 GMT na kwamba ziliharibiwa baada ya mfumo wa ulinzi wa anga wa nchi hiyo kuanza kutumika, kulingana na Reuters.

    Hapo awali, shirika la habari la Fars liliripoti kwamba "milipuko" imesikika karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Isfahan.

    Mkoa wa Isfahan ni nyumbani kwa kituo kikubwa cha anga, eneo kubwa la uzalishaji wa makombora na maeneo kadhaa ya nyuklia.

  20. Israel Gaza: Marekani yaonya tena dhidi ya mashambulizi ya Rafah

    Msichana wa Gaza

    Maafisa wa Marekani wameibua tena wasiwasi wao kwa Israel kuhusu mipango ya nchi hiyo kufanya operesheni za kijeshi katika mji wa Rafah kusini mwa Gaza.

    Ikulu ya White House ilisema wawakilishi wa waziri mkuu wa Israel wamekubali "kuzingatia masuala haya".

    Mara kwa mara Marekani imeitaka Israel isifanye mashambulizi makubwa mjini Rafah ili kuepusha majeruhi zaidi ya raia huko Gaza.

    Huku hayo yakijiri, Marekani ilipiga kura ya turufu azimio la Umoja wa Mataifa la kutoa hadhi kamili ya mwanachama kwa taifa la Palestina.

    Katika hatua nyingine, Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin alizungumza na Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant "kujadili vitisho vya kikanda na hatua za Iran za kuvunja amani katika Mashariki ya Kati".