Got a TV Licence?

You need one to watch live TV on any channel or device, and BBC programmes on iPlayer. It’s the law.

Find out more
I don’t have a TV Licence.

Habari za moja kwa moja

Na Asha Juma, Lizzy Masinga na Ambia Hirsi

time_stated_uk

  1. Tunakomea hapo kwa leo. Kwaheri.

  2. Uturuki yapongeza Hamas kwa kukubali pendekezo la kusitisha mapigano

    Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amekaribisha hatua ya kundi la Hamas kukubali pendekezo la kusitisha mapigano na kusema kwamba anatumai Israel atafuata mkondo huo, kulingana na ripoti ya shirika la habari la Reuters.

    Shirika hilo linasema Erdogan pia anatoa wito kwa nchi za Magharibi kuongeza shinikizo lao kwa Israel.

    Wiki iliyopita, Uturuki ilisitisha biashara kati yake na Israel kutokana na mashambulizi yake dhidi ya Gaza, ikitoa mfano wa "janga la kibinadamu linalozidi kuongezeka" katika ukanda huo.

    Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu walikutana Septemba 2023, wiki chache kabla ya Hamas kushambulia Israel.
    Image caption: Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu walikutana Septemba 2023, wiki chache kabla ya Hamas kushambulia Israel.
  3. Kauli ya Hamas yaleta matumaini baada ya mazungumzo magumu

    xx

    Kauli ya Hamas kwamba inakubali pendekezo la kusitisha mapigano inafuatia majuma kadhaa ya mazungumzo ya upatanishi yaliyooneka kukwama.

    Mazungumzo hayo yamekuwa magumu, yakihusisha sio tu Hamas na Israel kwa njia isiyo ya moja kwa moja bali pia Marekani, Qatar na Misri.

    Kufikia sasa, haijulikani haswa Hamas ina maananisha kukubali nini hasa, lakini katika siku za hivi karibuni ripoti ambazo hazijathibitishwa ziliangazia juu ya makubaliano ya hatua kwa hatua ambayo yatachangia mateka kadhaa wa Israeli waachiliwe kama malipo ya idadi kubwa zaidi ya wafungwa wa Kipalestina huko Israeli wakati wa usitishaji mapigano.

    Hamas imekuwa ikishikilia kukomesha kabisa vita hivyo lakini Israel imeweka wazi kuwa hilo ni jambo ambalo haiwezi kulikubali, kwani lingewaruhusu Hamas kuendelea kuishi.

    Kauli ya Hamas imekuja saa chache baada ya Israel, kwa mara ya kwanza, kuwaamuru Wapalestina kuhama kutoka sehemu Rafah kusini mwa mji wa Gaza kwa ajili ya kujiandaa kwa operesheni - hatua ambayo ingeongeza shinikizo kwa Hamas kuepusha hilo.

  4. Hamas yakubali masharti ya makubaliano ya kusitisha mapigano

    Uongozi wa Hamas unasema umekubali masharti ya makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza.

    Kundi hilo linasema limewafahamisha wapatanishi wa Qatar na Misri kuhusu uamuzi huo.

    Katika taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti yake rasmi, Hamas inasema kiongozi wake, Ismail Haniyeh, alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani, na Waziri wa Ujasusi wa Misri, Abbas Kamel, na kuwafahamisha kuhusu uamuzi wa Hamas wa kukubali pendekezo lao kuhusu makubaliano ya kusitisha mapigano.

    Maelezo zaidi kuhusiana na uamuzi huo bado hayajatatolewa, ikiwa ni pamoja na mapigano yatasitishwa kwa muda gani na hatma ya mateka wanaozuiliwa huko Gaza.

    Soma zaidi:

    Vita vya Gaza: 'Wanangu hawaniachilii wakiogopa mbwa wanaovamia makaburi ya Rafah yaliyopo karibu na makazi yetu'

  5. Hofu yatanda kambi ya watu waliokimbia makazi baada ya shambulizi DRC

    Hifadhi ya wakimbizi

    Shambulio la bomu katika kambi ya watu waliokimbia makazi yao huko Mugunga, mashariki mwa DRC wiki iliyopita Ijumaa limewaacha wakazi katika hofu. Fikiri Nvano, mkimbizi katika kambi hiyo, aliiambia BBC kuwa alikuwa akijaribu kukusanya nguvu kuutazama mwili wa mkwe wake aliyeuawa katika shambulio hilo.

    Nvano alisema familia yake ilihuzunika na haijui jinsi ya kuendelea na mipango ya mazishi na kuongeza kuwa mkwe wake aliacha mtoto mchanga.

    "Tunaogopa sana." Placide Hakizimana mkimbizi mwingine katika kambi hiyo alisema.

    ''Tunataka tu serikali kupambana na adui ili tuweze kurejea nyumbani." Aliongeza.

    Takribani watu 15, wengi wao, watoto waliuawa katika shambulizi hilo.

    Picha za kutisha zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilionesha miili ikiwa imelala chini kwenye kambi hiyo.

    Jeshi la Congo na waasi wa M23 walilaumiana kwa shambulio hilo. Taarifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani iliishutumu Rwanda kwa shambulio hilo ikisema kuwa mabomu hayo yalitoka katika maeneo yanayoshikiliwa na Jeshi la Ulinzi la Rwanda na kundi la waasi la M23.

    Rwanda imekuwa ikishutumiwa vikali kwa kuunga mkono kundi la waasi na kuyataja mashtaka hayo ya Marekani kuwa ya "kijinga".

    Barabara kuu za kuelekea Goma zimeshindwa kupitika baada ya miezi kadhaa ya mapigano kati ya waasi na vikosi washirika vya serikali ya DRC.

    Maisha mjini Goma yamekuwa magumu huku bei ya vyakula ikipanda.

    Taarifa ya vikosi vya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) nchini DRC vimesema vitaanzisha operesheni ya kuwaangamiza waasi wa M23.

    Imeongeza kuwa operesheni hiyo italenga kuweka mazingira salama pamoja na kuwalinda raia na mali zao.

  6. Uvamizi wa Rafah: Biden kuzungumza na Netanyahu baadaye leo

    Rais wa Marekani Joe Biden atazungumza na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu baadaye leo, kwa mujibu wa msemaji wa Baraza la Usalama la Taifa.

    Wanasema kuwa White House haiwezi kuzungumza kwa niaba ya jeshi la Israel, lakini "tumeweka wazi msimamo wetu juu ya uvamizi wa Rafah kwa serikali ya Israel, na rais atazungumza na waziri mkuu leo".

    Washington imesema mara kwa mara haiungi mkono uvamizi wa Rafah bila mpango wa kuwasaidia raia wanaohifadhiwa katika mji huo.

    Hapo awali mshauri mkuu wa zamani wa kisiasa wa kundi la Hamas Ismail Haniyeh - ambaye anachukuliwa kuwa kiongozi mkuu wa kundi hilo ameambia BBC kwamba, kundi hilo lililopigwa marufuku nchini Uingereza, Marekani na nchi nyingine za magharibi, liko makini kuhusu usitishaji vita na kuilaumu Israel na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kwa mkwamo uliyokumba mazungumzo ya amani - akisema viongozi wa Hamas wako tayari kufikia "makubaliano mengi mazuri" .

    “Netanyahu ndiye amekuwa kizingiti na anapaswa kulaumiwa kwa yote yaliyotokea. mpaka sasa nadhani Hamas wameambia Misri, Qatar na hata Marekani kwamba wako tayari kuzingatia pendekezo lililowasilishwa na nchi hizo tatu," anasema.

  7. Mwamuzi wa ligi ya Premia kuvaa kamera kwenye mechi

    Ni kwa mara ya kwanza mwamuzi atavaa kamera ya video katika mechi ya Ligi Kuu

    Mwamuzi atavaa kamera ya video kwa mara ya kwanza katika mchezo wa Ligi Kuu ya Uingereza wakati wa mechi ya Jumatatu kati ya Crystal Palace dhidi ya Manchester United.

    Jarred Gillett atatumia kifaa kilichopachikwa kichwa kiitwacho 'RefCam', ingawa picha hazitaonyeshwa moja kwa moja.

    Video hiyo itatumika katika programu inayotoa maarifa kuhusu usimamizi wa Ligi Kuu. Mnamo Februari, mwamuzi wa Bundesliga Daniel Schlager alivaa kamera na kipaza sauti wakati wa sare ya 2-2 kati ya Eintracht Frankfurt na Wolfsburg.

    Video hiyo pia ilitumika kwa programu inayoitwa 'Referees Mic'd up - Bundesliga'.

    Mwaka jana, mwamuzi wa Premier League Rob Jones alivaa kamera kwa ajili ya mechi ya 2023 Summer Series kati ya Chelsea na Brighton mjini Philadelphia.

    Utumiaji wa kamera za mwili pia ulijaribiwa na Chama cha Soka katika soka la watu wazima mwaka jana katika juhudi za kupunguza unyanyasaji wa maafisa wa ngazi hiyo.

  8. 'Lazima tusitishe mapigano sasa' - Waziri Mkuu wa zamani wa Israel

    Ehud Olmert akizungumza mwaka wa 2007
    Image caption: Ehud Olmert akizungumza mwaka wa 2007

    Waziri mkuu wa zamani wa Israel,Ehud Olmert, ametoa onyo dhidi ya mashambulizi huko Rafah akisema "lazima tusitishe mapigano sasa."

    Akiongea na kipindi cha BBC Radio 4 kuhusu uwezekano wa shambulio kama hilo, anasema: "Uwezekano wa ushindi wa ziada wa kijeshi wenye matokeo makubwa ni mdogo sana."

    Olmert amekuwa mkosoaji mkubwa wa Waziri Mkuu wa sasa wa Israel Benjamin Netanyahu na kwa muda wa miezi kadhaa amekuwa akitaka vita vikomeshwe na kuepusha mashambulizi dhidi ya Rafah.

    Anasema hoja kwamba mashambulizi katika mji wa kusini mwa Gaza yanahitajika kuwafuata watu ambao Israel inawajibisha kwa shambulio la Oktoba 7, akiwemo kiongozi wa mrengo wa kisiasa wa Hamas huko Gaza, Yahya Sinwar, inaweza kufanya vita hivyo kuendelea "milele" na kwa "gharama ya kupoteza maisha ya mateka".

    Olmert pia aliongeza kuwa mauaji ya wanajeshi wanne wa Israel ndani ya usiku mmoja yanaonyesha Hamas bado ni hatari huku akionya kwamba kuendelea na mapigano pia kutasababisha maafa.

  9. Kenya yatuma vifaa vya uokoaji na boti katika maeneo yaliyokumbwa na mafuriko

    Helikopta

    Operesheni za anga na majini zinaendelea kuokoa makumi ya familia zilizokwama katika makazi yao katika eneo la Nyando Magharibi mwa Kenya huku kukiwa na mafuriko yanayoendelea kote nchini.

    Siku ya Jumamosi, Mto Nyando ulipasua kingo zake, na kuzamisha vijiji kadhaa na kulemaza usafiri kwenye barabara kuu ya Kisumu-Nairobi.

    Zaidi ya kaya 1,000 zililazimika kukimbia makazi yao, vyombo vya habari vya ndani viliripoti.

    Hakukuwa na ripoti za mara moja za majeruhi lakini polisi wa eneo hilo walisema viwango vya maji bado vinaongezeka.

    Timu ya pamoja ya Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya, Huduma za Walinzi wa Pwani ya Kenya na Huduma ya Wanyamapori ya Kenya (KWS) wanatumia boti na helikopta kufikia vijiji vilivyofunikwa na maji.

    Helkopta ya Shirika la Kenya Wildlife Services (KWS) inawasafirisha kwa ndege waliookolewa, huku kukiwa na hofu kwamba familia nyingi zililala kwenye baridi katika vijiji vilivyoathiriwa.

    Haya yanajiri huku serikali ikiwahamisha watu zaidi kutoka maeneo yanayokumbwa na mafuriko.

    Rais William Ruto Jumatatu alisema serikali itaipa kila familia iliyoathiriwa $70 (£60) ili kuwasaidia kutafuta makazi mbadala kwa miezi mitatu.

    Katika taifa zima, mafuriko hayo yamegharimu maisha ya watu 228 tangu Machi, huku 72 wakiwa bado hawajulikanu walipo, kulingana na takwimu za serikali.

    Kenya na nchi jirani ya Tanzania ziliepuka uharibifu mkubwa wa Kimbunga Hidaya kilichopungua baada ya kupiga Jumamosi.

  10. Uchaguzi Chad: Upinzani wadai kuwepo kwa dosari katika upigaji kura

    Wapiga kura

    Baadhi ya waangalizi wa upinzani wamelaani kile wanachodai kuwa ni dosari katika upigaji kura unaoendelea katika uchaguzi wa rais wa Chad.

    Mwangalizi wa uchaguzi kutoka chama cha upinzani cha Transformers' Party, ambaye alikuwa katika kituo cha kupigia kura mjini N’Djamena, alitilia shaka rekodi za karatasi za kupigia kura na mwenendo wa upigaji kura.

    "Idadi ya wapiga kura waliojiandikisha hapa ni 226... Lakini ANGE (Tume ya Uchaguzi), liliwasilisha karatasi 156 pekee.

    Je, karatasi 70 zilizobaki ziko wapi?", Gauthier Saldnba alisema, akiongeza "kuna tatizo hapa."

    Lakini Kaigo Patcha, afisa wa uchaguzi, alisema ni kweli kuna ukosefu wa karatasi za kupigia kura lakini si mchezo mchafu, akisisitiza "tayari tumewaita wale wanaosimamia, na hivi karibuni wataleta karatasi zilizosalia za kupigia kura".

    Pia kuna ripoti ya baadhi ya maafisa wa uchaguzi kutowaruhusu baadhi ya wapiga kura kupiga kura.

    Watu waliojiandikisha kupiga kura katika mikoa mingine nje ya N'Djamena, hawakuruhusiwa kupiga kura katika vituo vya kupigia kura katika mji mkuu.

    Maafisa wa uchaguzi walitetea hili, wakisema walikuwa wakifuata kanuni za uchaguzi. Matokeo ya muda ya duru ya kwanza yanatarajiwa kufikia tarehe 21 Mei.

  11. Zuma 'atahudhuria' kikao cha nidhamu licha ya ANC kukifuta

    Zuma

    Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma atahudhuria kikao cha kamati ya nidhamu ya chama cha African National Congress (ANC) siku ya Jumanne licha ya chama tawala kusema kimefutwa.

    Alhamisi iliyopita, Bw Zuma aliitwa na Kamati ya Kitaifa ya Nidhamu ya ANC kuhusu uamuzi wake wa kujiunga na chama kipya cha Umkhonto weSizwe (MK) kilichoanzishwa mwezi Desemba mwaka jana, ambacho sasa ndiye kiongozi wake, licha ya kuwa bado ni mwanachama wa ANC.

    Kama tulivyoripoti hapo awali, ANC ilikuwa imetangaza siku ya Jumapili kuwa inaahirisha mkutano huo, uliotarajiwa kufanyika katika makao yake makuu ya Luthuli House mjini Johannesburg.

    Siku ya Jumatatu, msemaji wa ANC alithibitisha hilo kwa BBC, akisema kuwa mkutano huo "haufanyiki". Hata hivyo msemaji wa MK aliiambia BBC, kwamba "ninavyofahamu, Rais (Zuma)atakuwa Luthuli House kesho saa 10 asubuhi",

  12. Mabaharia kadhaa waokolewa Kenya baada ya Kimbunga Hidaya kuikumba Tanzania

    Kimbunga hichokilisababisha mvua kubwa na upepo mkali

    Watu watatu wanafahamika kufariki dunia na wengine zaidi ya 100 wameokolewa, baada ya kimbunga Hidaya kilichopungua nguvu kutua Tanzania mwishoni mwa wiki.

    Ingawa kasi ya kimbunga hicho ilipungua ilipokaribia ufuo wa Tanzania, bado ilisababisha mvua kubwa na upepo mkali katika mikoa ya kusini mwa nchi hadi Jumamosi.

    Zaidi ya mabaharia 20 kutoka Tanzania na Zanzibar walikuwa miongoni mwa waliookolewa, ripoti zinasema, baada ya boti zao kuserereka katika eneo la maji ya Kenya.

    Hata hivyo baharia mmoja anasemekana kupoteza maisha kutokana na machafuko ya baharini. Watu wengine 80 waliookolewa walikuwa katika Kisiwa cha Kilwa nchini Tanzania.

    Hitilafu kubwa ya umeme iliyosababishwa na kimbunga hicho ilikumba sehemu kubwa ya Tanzania siku ya Jumamosi.

    Huduma za feri kati ya kitovu cha kibiashara cha Tanzania, Dar es Salaam, na Zanzibar pia zilisitishwa kwa sababu za kiusalama. Picha zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zilionesha nyumba kadhaa zilizoharibiwa na upepo mkali na miti iliyoanguka katika kisiwa cha Mafia.

    Nchi jirani ya Kenya iko katika hali ya tahadhari kufuatia uharibifu huo.

  13. Netanyahu alisema shambulio la Rafah litatokea bila kujali makubaliano na Hamas

    .

    Kufuatia maoni ya afisi ya waziri wa ulinzi wa Israel, hebu tuangalie nyuma matamshi ya hivi karibuni ya waziri mkuu wa nchi hiyo kuhusu shambulio la Rafah.

    Benjamin Netanyahu alisema wiki iliyopita kwamba Israel itaanzisha uvamizi katika mji wa kusini wa Gaza bila kujali mazungumzo ya kusitisha mapigano na Hamas, akisema kwamba atafanya hivyo "kwa au bila" makubaliano ya kusitisha mapigano.

    "Wazo kwamba tutasitisha vita kabla ya kufikia malengo yake yote sio lakujadiliwa," alisema.

    "Tutaingia Rafah na tutaondoa Hamas huko kwa makubaliano au bila makubaliano, ili kupata ushindi kamili," kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi ya Netanyahu.

    Zaidi ya nusu ya wakazi wa Gaza milioni 2.5 wako Rafah, wakiwa wamekimbilia huko kukwepa mapigano katika maeneo mengine ya eneo hilo. Hali katika jiji lenye msongamano mkubwa wa watu ni mbaya, na watu waliohamishwa huko wamezungumza juu ya ukosefu wa chakula, maji na dawa.

    Marekani, pamoja na Umoja wa Mataifa, wametoa maoni yao kupinga uvamizi wa Rafah.

    Soma zaidi:

    Jeshi la Israel lawataka raia wa Gaza kuondoka sehemu za Rafah

    Familia za mateka Israel 'wanaogopa sana' shambulizi dhidi ya Rafah

  14. Upigaji kura unaendelea Chad huku zoezi likicheleweshwa katika baadhi ya maeneo

    .

    Upigaji kura umeanza katika uchaguzi wa rais wa Chad, hatua kubwa inayopelekea kumalizika kwa kipindi cha mpito cha miaka mitatu nchini humo.

    Upigaji kura huo ulikumbwa na ucheleweshaji, na kufunguliwa saa moja baada ya muda uliopangwa katika baadhi ya maeneo.

    Rais wa mpito Mahamat Déby alianza zoezi hilo kwa kupiga kura yake katika mji mkuu wa N'Djamena.

    Alisema anajivunia kutimiza ahadi yake ya kuheshimu tarehe ya mwisho ya "uchaguzi ambao utaashiria kurejea kwa utaratibu wa kikatiba."

    "Ni juu ya watu wa Chad kupiga kura kwa wingi na kuchagua rais wao," aliongeza.

    "Tutapiga kura, ni jukumu letu… hata kama itachukua muda," alisema mpiga kura ambaye alisimama kwenye foleni ndefu akisubiri zamu yake ya kupiga kura.

    Wapiga kura milioni nane wanamchagua rais kutoka miongoni mwa wagombea 10, akiwemo kiongozi wa kijeshi Déby na waziri mkuu, Succès Masra.

    Matokeo ya awali yanatarajiwa kufikia tarehe 21 Mei, lakini duru ya pili inaweza kufanyika mwezi Juni ikiwa hakutakuwa na mshindi wa moja kwa moja katika duru ya kwanza ya uchaguzi.

    Soma zaidi:

    Uchaguzi wa urais wa Chad kumaliza utawala wa kijeshi

  15. Familia za mateka Israel 'wanaogopa sana' shambulizi dhidi ya Rafah

    .
    Image caption: Picha kutoka maktaba

    Familia za mateka nchini Israel zimekuwa zikielezea hofu yao kuhusu jinsi operesheni ya Rafah inaweza kumaanisha kwa wapendwa wao.

    Shangazi wa Gil Dickman aliuawa wakati wa mashambulizi ya Oktoba 7 na Hamas huku binamu zake wawili wakichukuliwa mateka. Mmoja aliachiliwa na mwingine akasalia Gaza kama mateka.

    "Sasa kwa bahati mbaya tunaogopa sana kama familia za mateka kuhusu kitakachotokea," aliambia kipindi cha Newsday cha BBC.

    "Tunaogopa sana kwamba IDF ikiingia Rafah itahatarisha maisha sio tu ya watu wasio na hatia, sio tu ya wanajeshi lakini pia ya baadhi ya mateka ambao wanaweza kuwa hatarini kwa sababu ya shambulio la Rafah."

    Vita hivyo vilianza baada ya mawimbi ya watu wenye silaha wa Hamas kuvamia mpaka wa Gaza na kuingia Israel tarehe 7 Oktoba, na kuua takriban watu 1,200 na kuchukua zaidi ya mateka 250. Kundi hilo limeelezwa na nchi nyingi za Magharibi kama shirika la kigaidi.

    Wakati wa kampeni za kijeshi za Israel huko Gaza, zaidi ya Wapalestina 34,600 wameuawa na zaidi ya 77,900 wamejeruhiwa, kulingana na takwimu kutoka wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas.

    Soma zaidi:

    Jinsi mzozo wa mateka wa Israeli utakavyoubadili ulimwengu milele" - The Telegraph

  16. Kikao cha kinidhamu cha Zuma chacheleweshwa kwa sababu za usalama

    .
    Image caption: Jacob Zuma alikuwa rais kutoka 2009 hadi 2018

    Chama tawala nchini Afrika Kusini, African National Congress (ANC), kimeahirisha kikao cha kinidhamu dhidi ya rais wa zamani Jacob Zuma kutokana na wasiwasi wa kiusalama.

    ANC ilikuwa imemshtaki rais huyo wa zamani kwa kukiuka katiba ya chama kwa kukumbatia chama kipya cha Umkhonto we Sizwe (MK).

    Chama cha MK, kinachoongozwa na Bw Zuma, kimepewa jina la tawi la zamani la kijeshi la ANC.

    Alikuwa ameratibiwa kufika mbele ya kamati ya nidhamu ya chama siku ya Jumanne lakini hilo litafanyika baadaye baada ya uchaguzi.

    Katibu Mkuu wa ANC, Fikile Mbalula alisema Jumapili kwamba ofisi yake imeshauriwa dhidi ya kufanya vikao vyovyote kwani vinaweza "kuvutia mikusanyiko mikubwa ambayo inaweza kusababisha vurugu au usumbufu... hasa karibu na siku ya uchaguzi".

    Afrika Kusini inatazamiwa kufanya uchaguzi mkuu tarehe 29 Mei.

    Hatua za kinidhamu zilipaswa kufanywa baada ya Bw Zuma kutangaza kuwa angepiga kura dhidi ya ANC katika uchaguzi huo, huku akiwa bado mwanachama.

    Alikuwa ameshtakiwa kwa kukiuka katiba ya chama, na alisimamishwa Januari.

    Hatua za kinidhamu zilipaswa kuchukuliwa baada ya Bw Zuma kutangaza kuwa angepiga kura dhidi ya ANC katika uchaguzi huo, huku akiwa bado mwanachama.

    Alikuwa ameshtakiwa kwa kukiuka katiba ya chama.

    Bw Zuma, ambaye alikuwa rais kutoka 2009 hadi 2018, bado ana nguvu kubwa ya kisiasa nchini Afrika Kusini.

    Soma zaidi:

    Je, chama cha ANC kitaathiriwa na kujiondoa kwa Jacob Zuma?

  17. Jeshi la Israel lawataka raia wa Gaza kuondoka sehemu za Rafah

    .

    Jeshi la Israel limeanza kile inachokiita "uhamisho mdogo na wa muda" wa raia kutoka sehemu za mashariki mwa Rafah kusini mwa Gaza, ambapo zaidi ya watu milioni 1.4 wametafuta hifadhi.

    Takriban watu 100,000 katika eneo la mashariki mwa mji huo, karibu na mpaka wa Israel, wanahimizwa kuhamia maeneo yaliyopanuliwa ya kibinadamu katika maeneo ya Al Mawasi na Khan Younis.

    Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) linasema mahema, chakula, maji na dawa zinapatikana.

    Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesisitiza kuwa operesheni ya kijeshi huko Rafah ni muhimu ili kuwashinda wapiganaji waliosalia wa Hamas, lakini kumekuwa na wasiwasi mkubwa wa kimataifa juu ya hatima ya raia waliotafuta hifadhi huko.

    Haya yanajiri huku mazungumzo yenye lengo la kupata makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza na kuachiliwa kwa mateka yakiwa yamekwama.

    Soma zaidi:

    Vita vya Gaza: 'Wanangu hawaniachilii wakiogopa mbwa wanaovamia makaburi ya Rafah yaliyopo karibu na makazi yetu'

    Wanajeshi watatu wa Israel wauawa katika shambulizi la roketi Gaza

  18. Watalii waliopatikana wamekufa katika kisima cha Mexico walipigwa risasi kichwani

    .

    Miili ya watalii watatu iliyopatikana kwenye kisima kaskazini-magharibi mwa Mexico yote ilikuwa na majeraha ya risasi vichwani, mamlaka zilisema.

    Ndugu wa Australia Jake na Callum Robinson, 30 na 33, na rafiki yao Mmarekani Jack Carter Rhoad, 30, walitoweka tarehe 27 Aprili walipokuwa kwenye safari ya kuteleza kwenye mawimbi huko Ensenada.

    Jamaa wa wanaume hao watatu walitambua miili yao siku ya Jumapili baada ya kusafiri kwenda Mexico kusaidia mamlaka, mwendesha mashtaka wa serikali alisema.

    Maafisa wanaamini kuwa watu hao walishambuliwa walipokuwa wakijaribu kuzuia jaribio la wizi wa gari lao.

    Washambuliaji walitaka gari hilo kwasababu ya matairi yake na kuwapiga risasi watalii hao walipokataa, mwendesha mashtaka wa jimbo la Baja California Maria Andrade alitoa maoni yake.

    Miili yao ilipatikana katika kisima chenye kina cha 4m (15ft) karibu kilomita 6 kutoka eneo la shambulio katika mji wa Santo Tomás siku ya Ijumaa.

    Mahema yaliyotelekezwa, lori jeupe lililoungua na simu iliyohusishwa na watalii waliotoweka zilipatikana karibu na eneo la tukio.

    Mwili wa nne ulipatikana kwenye kisima lakini ulikuwa hapo kwa muda mrefu na haukuunganishwa na kesi hiyo, maafisa walisema.

    Washukiwa watatu wamezuiliwa kwa tuhuma za kuhusika moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika shambulio hilo.

    Hapo awali, FBI ilisema inachunguza kisa hicho na inawasiliana na washirika wa kimataifa.

    Baja California ni mojawapo ya majimbo yenye vurugu zaidi Mexico, huku magenge ya dawa za kulevya nchini humo yakipigana vita.

  19. Uchaguzi wa urais wa Chad kumaliza utawala wa kijeshi

    .

    Chad inatazamiwa kuwa nchi ya kwanza barani Afrika inayoongozwa na jeshi kuhamia utawala wa kidemokrasia kwa kura ya urais siku ya Jumatatu.

    Itamaliza kipindi cha mpito cha miaka mitatu kilichowekwa baada ya kifo cha ghafla cha kiongozi wa muda mrefu Idriss Deby Itno alipokuwa akipambana na waasi.

    Lakini kama mwanawe, na mrithi, Jenerali Mahamat Déby ni mmoja wa watu wanaopendekezwa kushinda, kuna shaka kuhusu kama hii italeta mabadiliko.

    Waziri Mkuu Succès Masra ni miongoni mwa wapinzani wake tisa na anaonekana kuwa mpinzani wake mkubwa.

    Wanasiasa wengine kumi ambao walikuwa na matumaini ya kugombea, wakiwemo watu wawili mashuhuri, Nassour Ibrahim Neguy Koursami na Rakhis Ahmat Saleh, walitengwa na baraza la katiba kwa sababu ya "ukiukaji taratibu". Kwa mfano, Bw Koursami alishtakiwa kwa ulaghai.

    Lakini wengine wamedai kuwa uamuzi wa kuwazuia watu fulani ulichochewa kisiasa.

    Mpinzani mwingine, Yaya Dillo, aliuawa na vikosi vya usalama mwezi Februari wakati akidaiwa kuongoza mashambulizi dhidi ya Shirika la Usalama la Taifa katika mji mkuu, N'Djamena.

    Wanaharakati wametoa wito wa kususia uchaguzi huo ambao waliutaja kuwa njama ya kutoa mwanga wa uhalali wa kidemokrasia kwa nasaba ya Deby.

    Wengi bado wako uhamishoni kwa msako mkali dhidi ya wapinzani kufuatia maandamano ya Oktoba 2022.

  20. Ghost Flights: Qantas yakubali kutoa malipo ya safari za ndege ambazo zilikuwa zimeghairiwa

    th

    Kampuni kubwa ya ndege nchini Australia Qantas imekubali kulipa faini ya A$100m ($66.1m, £52.7m) kutatua kesi ya kisheria inayoituhumu kuuza maelfu ya tikiti za ndege ambayo tayari ilikuwa imeghairi.

    Chini ya makubaliano na Tume ya Ushindani na Watumiaji ya Australia (ACCC), kampuni hiyo pia itazindua mpango wenye thamani ya hadi A$20m ili kuwafidia abiria walioathirika.

    Afisa wa ngazi ya juu waQantas, Vanessa Hudson, alisema uamuzi huounawakilisha hatua muhimu kuelekea "kurejesha imani kwa shirika hilola kitaifa."

    Kile kinachojulikana kama "Ghost flight", ambayoni kesi iliyozinduliwa na ACCC mwezi Agosti, ilidai kuwa katika baadhi ya matukio Qantas iliuza tikiti za ndege ambazo zilikuwa zimekatishwa kwa wiki.

    Mkataba wa adhabu kati ya Qantas na ACCC sasa itabidi uidhinishwe na Mahakama ya Shirikisho ya Australia.

    Chini ya mpango huo, wateja walionunua tikiti za ndege ambazo tayari zilikuwa zimeghairiwa kwa siku mbili au zaidi watastahiki kulipwa fidia.

    Kulingana na shirika hilo la ndege, watapata A$225 kwa safari za ndani na A$450 kwa tikiti za kimataifa.

    Unaweza pia kusoma

    Usafiri wa Anga: 'Ghostflights' ni nini? kwanini ndege hizi huzunguka tupu?