Got a TV Licence?

You need one to watch live TV on any channel or device, and BBC programmes on iPlayer. It’s the law.

Find out more
I don’t have a TV Licence.

Habari za moja kwa moja

Na Asha Juma, Lizzy Masinga na Ambia Hirsi

time_stated_uk

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo ya moja kwa moja. Kwaheri.

  2. Mazungumzo ya mapatano ni 'nafasi ya mwisho' ya kuwaachia mateka wa Israel - Hamas

    Afisa mkuu wa Hamas anasema ujumbe wake, ambao unaondoka kuelekea Cairo kujadili mazungumzo ya mapatano, yatakuwa "nafasi ya mwisho" ya kuwaachiwa kwa mateka wa Israel.

    Akizungumza na shirika la habari la AFP bila kutaja jina, afisa huyo anasema wapatanishi wa Hamas mapema leo waliahirisha mipango ya kusafiri kutoka Qatar hadi mji mkuu wa Misri.

    Afisa huyo anasema "uamuzi wa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuivamia Rafah" umeonyesha kuwa yeye na jeshi la Israel "walifanya uamuzi wa kuwaacha wafungwa (mateka) wafe".

    "Hii itakuwa nafasi ya mwisho kwa Netanyahu na familia za wafungwa wa Kizayuni kuwarejesha watoto wao," afisa huyo anasema.

    Hamas iliwateka nyara watu 252 wakati wa mashambulizi dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba, 128 bado hawajulikani waliko.

    Israel inasema inafanya "mashambulizi maalum" dhidi ya Hamas huko Rafah kwa lengo la kutafuta kile wanachokiita "miundombinu ya kigaidi".

  3. Guterres aitaka Israel kufungua tena vivuko vya Gaza

    xx

    Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anasema makubaliano kati ya Israel na Hamas ni muhimu kuelekea kukomesha "mateso ya Wapalestina na mateka wa Israel huko Gaza".

    Anasema huu ni "wakati muhimu" utakaoamua "hatma ya eneo zima".

    Quote Message: Narudia ombi langu la dhati kwa pande zote mbili kuonyesha ujasiri wa kisiasa na kujitahidi kufikia makubaliano ya kukomesha umwagaji damu, kuwakomboa mateka.

    "Nimefadhaishwa na shughuli mpya ya kijeshi inayofanywa na Vikosi vya Ulinzi vya Israeli huko Rafah."

    Anaongeza kuwa kufungwa kwa vivuko vya Rafah na Kerem Shalom kunazorotesha hali mbaya ya kibinadamu, na anatoa wito kwa vivuko hivyo kufunguliwa mara moja.

    "Kwa mfano, tunakabiliwa na tishio la kukosa mafuta jioni hii," anasema.

    Kivuko cha Rafah kilitumiwa kusafirisha silaha kwa Hamas -Israel

    Huku hayo yakijiri, Msemaji wa serikali ya Israel, David Mencer, anasema kuwa mahandaki ya chini ya mpaka wa Rafah yalikuwa yakitumiwa na Hamas kuingiza silaha Gaza.

    Anasema taarifa za kijasusi zinaonyesha kivuko cha Rafah kimetumika kwa "malengo ya kigaidi".

    "Chini ya miundombinu hiyo mikubwa ya mpakani kuna vichuguu vya kuvuka mpaka chini ya ardhi, vinavyoendeleza na kutoa njia ya kuokoa maisha kwa Hamas," Mencer anasema.

    Mapema asubuhi ya leo, Israel ilitangaza kuwa imewaua wapiganaji 20 wa Hamas, na kupata mashimo matatu ya handaki katika eneo karibu na kivuko hicho.

  4. Afrika Kusini: Waokoaji wawasiliana na manusura 11 walionasa katika jengo lililoporomoka

    Jengo lililoporomoka

    Waokoaji nchini Afrika Kusini wanasema wamewasiliana na manusura wengine 11 katika magofu ya jengo la ghorofa lililoporomoka katika mji wa pwani wa George siku ya Jumatatu.

    Takribani watu watano wamethibitishwa kufariki na zaidi ya 50 hawajulikani walipo baada ya jengo lililokuwa kwenye ujenzi wa ghorofa tano kuporomoka kwa sababu ambazo bado hazijajulikana.

    "Tunawasiliana na watu 11, wanne kati yao wamenaswa katika chumba cha chini ya ardhi," Colin Deiner, mkurugenzi mkuu wa udhibiti wa majanga, alisema.

    Picha za video zilizochukuliwa karibu zilionesha wingu kubwa la vumbi huku jengo likianguka. Katika eneo la tukio Jumanne asubuhi, wafanyakazi wa dharura walikuwa wapeana zamu kufanya kazi kwenye eneo dogo, wakiondoa matofali ya zege na uchafu kwa mikono.

    Kila mara kiongozi wa timu aliinua mkono wake, akiashiria kuwa kimya. Kila mtu alisimama na kutazama kwa matumaini kwamba mtu atakuwa amepatikana.

    Wafanyakazi wengi waliokuwa kwenye eneo la ujenzi bado hawajulikani walipo na imekuwa ni mchakato mrefu na wa polepole kuwatoa manusura.

  5. Njama ya Urusi ya kumuua Zelensky ilitibuliwa, Kyiv yasema

    Rais Volodymyr Zelensky
    Image caption: Rais Volodymyr Zelensky

    Idara ya usalama ya Ukraine (SBU) inasema kuwa imetibua njama ya Urusi ya kutaka kumuua Rais Volodymyr Zelensky na maafisa wengine wa ngazi za juu wa Ukraine.

    Kanali wawili wa kitengo cha ulinzi wa serikali ya Ukraine wamekamatwa.

    SBU ilisema ilikuwa sehemu ya mtandao wa mawakala wa huduma ya usalama wa serikali ya Urusi (FSB).

    Inasemekana walikuwa wakitafuta "watekelezaji" miongoni mwa walinzi wa Bw Zelensky ili kumteka nyara na kumuua.

    Walengwa wengine ni pamoja na mkuu wa ujasusi wa kijeshi Kyrylo Budanov na mkuu wa SBU Vasyl Malyuk, shirika hilo liliongeza.

    Kundi hilo liliripotiwa kupanga kumuua mkuu wa ujasusi wa kijeshi wa Ukraine Bw Budanov kabla ya Pasaka ya Orthodox, ambayo mwaka huu iliangukia tarehe 5 Mei.

    Kulingana na SBU, kundi hilo lilikuwa linapanga kutumia fuko kupata habari kuhusu eneo lake, ambalo wangeshambulia kwa roketi na ndege zisizo na rubani.

    Mmoja wa maafisa ambaye alikamatwa baadaye alikuwa tayari amenunua ndege zisizo na rubani na migodi ya kuzuia wafanyikazi, SBU ilisema

    Mkuu wa SBU Vasyl Malyuk alisema shambulio hilo lilipaswa kuwa "zawadi kwa Putin kabla ya kuapishwa" - Vladimir Putin aliapishwa kama rais wa Urusi leo Jumanne.

    Operesheni hiyo iligiuka na kuchangia kushindwa kwa huduma maalum za Urusi, Bw Malyuk alisema.

    "Lakini hatupaswi kusahau - adui ana nguvu na uzoefu, hawezi kudharauliwa," aliongeza.

    Maafisa hao wawili wa Ukraine wanazuiliwa kwa tuhuma za uhaini na kuandaa kitendo cha kigaidi.

  6. 'Ikiwa Hamas wameamua kwa dhati, kutakuwa na makubaliano' - Afisa wa Israel

    Habari kwamba Hamas imekubali kusimamisha mapigano ziliibua maandamano kuwataka viongozi wa Israel kufanya vivyo pia

    Mbunge wa zamani wa Israel wa chama cha Benjamin Netanyahu cha Likud anasema anaamini kama Hamas wana nia ya dhati ya kukubali makubaliano ambayo yatawafanya mateka wote kurejeshwa Israel, basi Israel itatia saini mkataba huo pia.

    Michael Kleiner, ambaye sasa ni rais wa mahakama ya ndani ya chama cha Likud, akiambia kipindi cha Leo cha BBC Radio 4 kwamba Israel haiwezi kutangaza ushindi katika hatua yake ya kijeshi dhidi ya Hamas hadi mateka wote wawe nyumbani.

    Lakini kwa sasa, maafisa wa Israel watakuwa wakichunguza jinsi Hamas ilivyo "na nia" katika kukubali pendekezo la mpango mpya wa kusitisha mapigano Gaza na kuwaachilia mateka na Israel, anasema.

    Wakati huo huo huko Rafah, Kleiner anaongeza, "utekelezaji.. hautaharakishwa, ni hatua ya maandalizi tu, sio vita kamili". "Ikiwa (kiongozi wa Hamas) Sinwar yuko makini, kutakuwa na mpango," anasema.

  7. Wajumbe wa Israel waelekea Cairo kwa mazungumzo zaidi - ripoti

    Hamas na Israel zimekuwa chini ya shinikizo kukubali makubaliano mapya ya kusitisha mapigano na utekaji nyara

    Kundi la wajumbe wa Israel watakwenda Cairo katika saa chache zijazo ili kuona kama Hamas wanaweza kushawishiwa kubadilisha pendekezo la hivi karibuni la kusitisha mapigano, afisa mkuu wa Israel ameliambia shirika la habari la Reuters.

    Afisa huyo anakariri kwamba pendekezo la sasa halikubaliki, akiongeza: "Ujumbe huu unaundwa na wajumbe wa ngazi ya kati.

    Kama kungekuwa na makubaliano ya kuaminika katika hatua hiyo, wakuu wangekuwa wakiongoza ujumbe." Hamas ilisema jana kwamba itakubali mpango ulioandaliwa na wapatanishi wa Misri, lakini haijabainika ni nini hasa katika mapatano ambayo Hamas imekubali na Israel ilikataa pendekezo hilo, ikisema "hayakidhi" matakwa yake ya msingi.

  8. Mashtaka ya ufisadi dhidi ya makamu wa rais wa Malawi yatupiliwa mbali

    Saulos Chilima anakanusha tuhuma za ufisadi dhidi yake

    Mahakama ya Malawi imefuta mashtaka ya rushwa dhidi ya Makamu wa Rais Saulos Chilima baada ya mwendesha mashtaka wa serikali kuwasilisha notisi ya kusitisha kesi hiyo. Hakuna sababu zilizotolewa za uamuzi huo.

    Dk Chilima alikamatwa Novemba 2022 kwa madai kwamba alikubali pesa ili kutoa kandarasi za serikali. Alikanusha mashtaka.

    Hatua ya hivi karibuni imezua maswali kuhusu jinsi serikali inavyoshughulikia mashtaka kuhusu madai ya ufisadi.

    Kukamatwa kwa makamu huyo wa rais kulifuatia shutuma alizopokea ili kushawishi utoaji wa kandarasi kwa Xaviar Ltd na Malachitte FZE, kampuni mbili zinazohusishwa na mfanyabiashara wa Uingereza Zuneth Sattar.

    Bw.Sattar pia alikanusha mashtaka dhidi yake.

    Makamu wa rais amefika mara kadhaa mahakamani tangu kukamatwa kwake, ingawa kesi ya msingi haikuanza.

    Siku ya Jumatatu, hakimu mfawidhi Redson Kapindu aliamuru kuachiliwa kwake mara moja akitaja jalada kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) alilolitoa Ijumaa iliyopita la "kusitishwa kwa mashtaka dhidi ya mshtakiwa kuhusiana na makosa matatu ya rushwa".

    DPP sasa ana siku 10 kulieleza rasmi bunge sababu za uamuzi wa kufuta mashitaka dhidi ya makamu wa rais kama inavyotakiwa na katiba, Jaji huyo alisema.

    Wakili wa Dk Chilima, Khumbo Soko, alieleza kufarijika kwa uamuzi wa kuwafutia mashtaka. "Kufikia sasa, hatujui sababu za kusitishwa, inatosha kusema ni bunge pekee ndilo lenye mamlaka ya kujua," shirika la habari la Reuters lilimnukuu akisema. Wakosoaji wa Rais wa Malawi Lazarus Chakwera wanasema hatua hiyo ni dalili zaidi ya ugumu kwake katika kupambana na madai ya ufisadi.

  9. China yashukiwa kudukua taarifa za mishahara ya wanajeshi wa Uingereza

    Mwanajeshi

    Serikali ya Uingereza inashuku China ilihusika na udukuzi wa mfumo wa malipo wa vikosi vya jeshi, BBC imefahamu.

    Waziri wa Ulinzi Grant Shapps hatataja waliotekeleza uhalifu huo atakapowahutubia wabunge leo, lakini anatarajiwa kuonya juu ya hatari inayoletwa na ujasusi wa mtandao kutoka kwa mataifa hasimu.

    Mfumo unaotumiwa na Wizara ya Ulinzi (MoD) unajumuisha majina na maelezo ya benki ya wafanyakazi wa jeshi. China ilisema "inapinga aina zote za mashambulizi ya mtandao".

    Katika idadi ndogo sana ya matukio, data inaweza kujumuisha anuani za binafsi.

    Mfumo huo, ulio na "taarifa za binafsi za mamlaka ya kodi, HMRC" kwa wanachama wa sasa na wa zamani wa Jeshi la Wanamaji la Kifalme, Jeshi la anga kipindi cha miaka kadhaa, ulisimamiwa na mkandarasi wa nje.

    Serikali ilifahamu kuhusu udukuaji wa data katika siku za hivi karibuni, na haijapata ushahidi wa wadukuzi walioondoa data kwenye mfumo.

    Waziri wa Baraza la Mawaziri Mel Stride aliiambia Sky News serikali inachukulia usalama wa mtandao "kwa uzito mkubwa" na kuchukua hatua "haraka sana".

    Vyanzo vya habari vimeiambia BBC kwamba uchunguzi wa ni nani alihusika na tukio hilo, ambao utaonekana kuwa wa aibu kwa MoD, uko katika hatua ya awali.

    Inaweza kuchukua miezi, wakati mwingine miaka, kukusanya ushahidi wa kutosha.

  10. Mwanajeshi wa Marekani akamatwa nchini Urusi akituhumiwa kwa wizi

    Mwanajeshi wa Marekani akamatwa nchini Urusi akituhumiwa kwa wizi

    Mwanajeshi wa Jeshi la Marekani aliyekuwa kikazi Korea Kusini amezuiliwa nchini Urusi, jeshi la Marekani limesema.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi ilisema mashtaka hayo hayahusiani na "siasa au ujasusi" bali "uhalifu wa nyumbani".

    Sgt Gordon Black anashutumiwa kwa kumuibia mwanamke, inaripoti mshirika wa BBC wa Marekani CBS.

    Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Urusi, Sgt Black alikuwa akimtembelea mwanamke ambaye alikuwa na uhusiano naye wa kimapenzi.

    Msemaji wa Baraza la Usalama la Kitaifa John Kirby aliwaambia waandishi wa habari kuwa Marekani "inafahamu kisa hiki na masuala mengine yanayohusiana na Urusi".

    Katika kikao cha White House mnamo Jumatatu, Bw Kirby alisema hawezi kutoa maelezo zaidi.

    Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Marekani, askari huyo anakabiliwa na mashtaka ya utovu wa nidhamu.

    "Jeshi liliifahamisha familia yake na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani inatoa usaidizi ufaao wa kibalozi kwa Askari huyo nchini Urusi," alisema msemaji wa Cynthia Smith.

    Mwanajeshi huyo alikuwa katika harakati za kubadilisha vituo vya kazi kutoka Korea Kusini kurudi Fort Cavazos katika jimbo la Texas Marekani, kulingana na CBS.

  11. Hali huko Rafah inatia wasiwasi sana - shirika la Umoja wa Mataifa

    Huku Israel ikidai udhibiti wa kivuko cha Rafah huko Gaza, shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, limeonya juu ya athari za kupungua kwa misaada itakayokuwa nazo kwa raia.

    "Tatizo kubwa tulilonalo katika saa 24 hadi 48 zilizopita ni kuvuka mpaka na kutokuwa na vifaa vya kutosha vya msaada," Louise Waterridge, msemaji wa shirika hilo, aliambia kipindi cha BBC Radio 4.

    Hali "inatia wasiwasi sana", anasema.

    Akiangalia mbele, ameonya juu ya hatari kwa afya za raia wa Gaza, akisema hali ya usafi inazidi kuwa mbaya na joto la juu sana linatarajiwa katika majira ya joto na watu wengi kwa sasa wamejificha kwenye mahema ya plastiki.

    Waterridge, ambaye yuko Rafah, anasema angahewa imepungua. Wengi wanasubiri kuona kitakachofuata, huku wengine wakiondoka jijini, anasema.

    Soma zaidi:

  12. Wapalestina watazama uharibifu uliofanyika baada ya Israel kushambulia Rafah

    Israel ilifanya mashambulizi katika mji wa kusini mwa Gaza wa Rafah usiku kucha, baada ya kuwaonya Wapalestina kuhama maeneo ya mashariki mwa mji huo.

    Wakazi wamekuwa wakikagua uharibifu uliosababishwa na mashambulizi ya leo asubuhi katika jiji hilo, ambapo watu milioni 1.4 wametafuta hifadhi:

    .
    ,
    ,
  13. Habari za hivi pundeJeshi la Israel linasema limechukua udhibiti wa upande wa Gaza wa kivuko cha Rafah

    Jeshi la Israel linasema wana "udhibiti wa uendeshaji wa upande wa Gaza wa kivuko cha Rafah", kulingana na afisa wa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF).

    Hapo awali vifaru vya Israel viliingia kwenye eneo hilo, ambalo ni kituo cha kusini kabisa cha kutoka Gaza na mpakani mwa Misri.

    "IDF ilianza operesheni sahihi ya kukabiliana na ugaidi katika eneo la mashariki la Rafah. Kufuatia taarifa za kijasusi zilizoashiria kuwa kivuko cha Rafah mashariki mwa Rafah kilikuwa kikitumika kwa madhumuni ya kigaidi, wanajeshi wa IDF walipata udhibiti wa operesheni upande wa Gazan wa kivuko hicho usiku kucha (Jumatatu)," taarifa inasema.

    Wanajeshi wanaendelea kusema kuwa kama sehemu ya operesheni yao, "walishambulia na kumaliza malengo ya ugaidi ya Hamas katika eneo la Rafah," na "takriban magaidi 20 wameangamizwa na mahandaki matatu yamepatikana".

    BBC haijathibitisha habari hii.

    Inaongeza kuwa IDF itaendelea kufanya operesheni dhidi ya Hamas mashariki mwa Rafah na katika eneo la kivuko cha Rafah.

  14. Boeing yakabiliwa na uchunguzi mpya juu ya mashaka ya ukaguzi wa ndege zake

    .

    Marekani imeanzisha uchunguzi mpya kuhusu kampuni ya ndege ya Boeing iliyokumbwa na matatizo, baada ya kampuni hiyo kuwaambia wadhibiti wa usalama wa anga kuwa huenda haikukagua ipasavyo ndege zake 787 Dreamliner.

    Shirika la Usimamizi wa Safari za Ndege (FAA) lilisema litaangalia ikiwa wafanyikazi walikuwa wameweka rekodi za uwongo.

    Lilisema Boeing ilikuwa ikikagua tena ndege zote 787 ambazo bado ziko kwenye laini ya utengenezaji.

    Boeing italazimika kuunda "mpango wa utekelezaji" ili kushughulikia wasiwasi kuhusu ndege ambazo tayari zinahudumu, iliongeza.

    Hata hivyo, Boeing haikutoa maoni.

    Taarifa ya ndani ya shirika kwa wafanyakazi wiki iliyopita iliyoonekana na BBC News ilisema,"Tulipitia suala hilo haraka na kugundua kuwa watu kadhaa wamekuwa wakikiuka sera za kampuni kwa kutofanya majaribio yanayohitajika, lakini wanaweka rekodi kuonyesha kuwa kazi imekamilika," Scott Stocker, mkuu wa mpango wa Boeing 787, alisema katika barua pepe kwa wafanyikazi.

    FAA ilisema kwamba Boeing ilijitokeza "kwa hiari" mwezi uliopita kuonya kwamba "huenda haikukamilisha" ukaguzi unaohitajika ili kuthibitisha ulinzi wa kutosha wa umeme eneo ambapo mbawa hizo hujiunga na bodi kuu ya 787 Dreamliner, ndege kubwa ambayo mara nyingi hutumika kwa safari za kimataifa.

    "FAA inachunguza ikiwa Boeing ilikamilisha ukaguzi na ikiwa wafanyikazi wa kampuni wanaweza kuwa waliweka rekodi za uwongo za ndege," ilisema.

    "Wakati uchunguzi ukiendelea, FAA itachukua hatua zozote zinazohitajika - kama kawaida - kuhakikisha usalama wa watu wanaosafiri kwa ndege."

    Hili ndilo tatizo la hivi punde kuzuka katika Boeing tangu Januari, wakati mlango wa kutokea wa dharura ulipofunguka ghafla wa ndege mpya ya 737 Max 9 muda mfupi baada ya kupaa, na hivyo kuelekeza angalizo katika mchakato wake wa utengenezaji na usalama.

    Soma zaidi:

    Boeing 737 Max 9: Safari za ndege zasitishwa baada ya hitilafu kutokea

  15. Mwanamke anayedaiwa kuwaua watu watatu kwa kuwalisha uyoga wa sumu akanusha shitaka la mauaji

    .

    Mwanamke wa Australia aliyedaiwa kuwaua watu watatu kwa kuwalisha uyoga wenye sumu kwenye chakula cha mchana amekanusha shitaka la mauaji.

    Erin Patterson, 49, anakabiliwa na mashtaka matatu ya mauaji na makosa mawili ya kujaribu kuua mnamo Julai mwaka jana.

    Polisi pia wanadai kuwa alijaribu kumuua mumewe aliyeachana naye katika matukio mengine matatu.

    Bi Patterson daima amedumisha kutokuwa na hatia.

    Amekuwa akisema mara kwa mara hakuwatilia sumu wageni wake kwa makusudi, na Jumanne katika Mahakama ya Latrobe Valley aliombwa kujibu rasmi mashtaka dhidi yake.

    "Sina hatia mheshimiwa," alisema, akionekana kupitia video.

    Kesi hiyo imekuwa ikifuatiliwa katika maeneo mengi ulimwenguni.

    Bi Patterson aliandaa chakula cha mchana nyumbani kwake huko Leongatha - kusini-mashariki mwa Melbourne - tarehe 29 Julai.

    Waliohudhuria walikuwa wakwe zake wa zamani Gail na Don Patterson, pamoja na dada ya Gail Heather Wilkinson na mume wa Heather Ian.

    Polisi wamesema mume wa Bi Patterson aliyeachana naye Simon Patterson pia alialikwa lakini hakuweza kufika dakika za mwisho.

    Saa kadhaa baada ya kula chakula hicho, wageni wote wanne waliugua kwa kile walichofikiri ni sumu kali ya chakula.

    Baada ya siku chache, wanandoa wa Patterson, wote 70, na Bi Wilkinson, 66, walifariki dunia. Bw Wilkinson, 68, alinusurika, baada ya kukaa karibu miezi mitatu hospitalini.

    Polisi wanasema wanaamini kuwa wanne hao walikula aina ya uyoga - ambao ni hatari sana unapomezwa.

    Bi Patterson alitajwa na polisi kuwa mshukiwa kwa kuonekana kuwa yeye hakudhurika popote baada ya chakula hicho cha mchana.

    Baada ya uchunguzi wa miezi kadhaa, wapelelezi walidaiwa kufichua majaribio mengine matatu ya mauaji ambayo Bi Patterson aliyafanya dhidi ya mumewe waliyeachana kati ya 2021 na 2022, na mnamo Novemba alikamatwa na kushtakiwa rasmi kwa makosa manane kwa jumla.

    Kesi yake sasa itafuatiliwa kwa haraka katika Mahakama ya Juu Zaidi ya Victoria huko Melbourne huku kusikilizwa kwake kwa mara ya kwanza kukipangwa kuwa tarehe 23 Mei.

  16. Wafanyikazi wa shirika la ndege la Kenya Airways waliozuiliwa na Congo waachiliwa huru

    ,

    Wafanyakazi wa Shirika la ndege la Kenya Airways waliokuwa wamekamatwa katika nchi ya Kidemokrasia ya Congo wameachiliwa huru, afisa mwandamizi kutoka wizara ya mambo ya nje nchini Kenya amesema.

    Kenya Airways itarejelea safari zake za kuelekea Kinshasa, afisa mkuu mtendaji wa Shirika hilo Allan Kilavuka, amesema alipozungumza na BBC Newsday.

    Kitengo cha ujasusi wa kijeshi cha Congo kiliwazuilia wafanyakazi wawili wa shirika hilo la ndege mnamo Aprili 19, kwa madai ya kukosa nyaraka za forodha kwenye baadhi ya mizigo ya thamani.

    Kampuni hiyo ilisema haikumiliki shehena hiyo kwa sababu karatasi za msafirishaji hazikuwa zimekamilika na kuelezea kukamatwa kwao kama "kinyume cha sheria" na kusimamisha safari za ndege kuelekea mji mkuu wa DRC siku iliyofuata.

    Wawili hao walizuiliwa licha ya agizo la mahakama kutaka waachiliwe.

    Mmoja wa wafanyikazi alikuwa Mkenya, mwingine raia wa Congo.

  17. Israel yakosoa masharti ya kusitisha mapigano Gaza na Hamas lakini mazungumzo yanaendelea

    th

    Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema pendekezo jipya la usitishaji vita hukoGaza "liko mbali na mahitaji ya kimsingi ya Israel" lakini mazungumzo yataendelea.

    Maoni yake yalikuja baada ya Hamas kusema kuwa imekubali masharti ya mapatano yaliyotolewa na wapatanishi wa Qatar na Misri.

    "Mpira sasa uko upande wa Israel," afisa katika kundi hilo la Wapalestina alisema.

    Usiku kucha, vikosi vya Israel na vifaru vilionekana karibu na kivuko cha mpaka cha Rafah kusini mwa Gaza, ripoti katika vyombo vya habari vya Israel zilisema.

    Hapo awali, jeshi la Israel lilifanya mashambulizi ya anga katika mji wa Rafah, mpakani na Misri, baada ya kuwaonya Wapalestina kuhama maeneo ya mashariki mwa mji huo.

    Makumi ya maelfu ya wakaazi wanaaminika kuathiriwa na operesheni hiyo na wengi walionekana wakining’iniakwenye magari au kwenye mikokoteni ya punda siku ya Jumatatu.

    Israel imetishia kwa muda mrefu mashambulizi dhidi ya Hamas katika mjihuo wa watu milioni 1.4, ambao wengi wao wametafuta hifadhi huko kutokana na mashambulizi ya Israel katika maeneo mengine ya Gaza.

  18. Urusi kufanya mazoezi ya nyuklia kufuatia 'vitisho' vya nchi za Magharibi

    .

    Urusi imeanza maandalizi ya mazoezi ya makombora karibu na Ukraine yakiiga matumizi ya silaha za kimkakati za nyuklia ili kukabiliana na "vitisho" vya maafisa wa nchi za Magharibi.

    Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alisema kauli za hivi majuzi za Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Cameron ni "duru mpya kabisa ya kuongezeka kwa mvutano".

    Wiki iliyopita, Bw Macron alikataa kuondoa uwezekano wa kupeleka wanajeshi wa Ufaransa, iwapo Ukraine itawaomba kufanya hivyo, huku David Cameron akisema kuwa Ukraine ina haki ya kutumia silaha za Uingereza kwa mashambulizi ndani ya Urusi.

    Siku ya Jumatatu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi ilisema kwamba "hisia kali yenye chuki" ya David Cameron inapingana na hakikisho la hapo awali la Uingereza kwamba makombora ya masafa marefu yaliyotumwa Ukraine hayatatumika katika ardhi ya Urusi na kumaanisha kwamba Uingereza ilikuwa "mshirika wa mzozo" huo.

    Wizara hiyo iliongeza kuwa majibu ya mashambulizi ya Ukraine kwa kutumia silaha za Uingereza dhidi ya Urusi yanaweza kuhusisha kulenga vituo na vifaa vyovyote vya kijeshi vya Uingereza katika eneo la Ukraine na kwingineko.

    Pia ilisema kwamba kauli ya Bw Macron kuhusu uwezekano wa kutumwa kwa wanajeshi wa Ufaransa nchini Ukraine inaweza kuchukuliwa kuwa "tayari kwa makabiliano ya moja kwa moja na Urusi".

    Mabalozi wa Uingereza na Ufaransa walioko Moscow waliitwa Jumatatu.

  19. Watu watano wafariki dunia huku zaidi ya 50 wakinaswa chini ya vifusi baada ya jengo kuporomoka Afrika Kusini

    .

    Watu watano sasa wamethibitishwa kufariki na zaidi ya 20 wanapokea matibabu katika hospitali za karibu, huku kumi wakiwa katika hali mbaya.

    Chanzo cha habari kinasema waokoaji wamewasiliana na baadhi waliofukiwa chini ya vifusi.

    Awali, watu 24 waliondolewa kutoka kwenye vifusi na wengine kulazwa hospitalini kufuatia kuporomoka kwa jengo katika mji wa George nchini Afrika Kusini siku ya Jumatatu.

    Wengine zaidi ya 50 bado wamenaswa chini ya vifusi vya eneo la ujenzi.

    Vikundi vya utafutaji na uokoaji vilifanya kazi usiku kucha ili kuwatafuta wafanyakazi kadhaa wa ujenzi waliokuwa wamekwama kwenye jengo hilo.

    Zaidi ya wafanyakazi 100 wa dharura na mbwa wa kunusa kwa sasa wako katika eneo la tukio wakitafuta manusura chini ya vifusi na kwenye matofali ya zege na kiunzi kilichochongwa.

    Wanafamilia walipiga kambi katika jengo la manispaa iliyo karibu ili kusubiri habari za jamaa zao.

    Mamlaka ya eneo hilo ilisema wafanyikazi 75 wa ujenzi walikuwa kwenye eneo la tukio wakati jengo la ghorofa tano lilipoporomoka.

    Sababu ya kuanguka kwa jengo hilo bado haijajulikana.

  20. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 07/05/2024