Biden na Netanyahu wajadili mpango wa usitishaji mapigano Gaza

Israel na Hamas wanasadikiwa kupiga hatua katika mazungumzo hayo lakini bado hawajaafikiana kuhusu vipengele muhimu vya makubaliano hayo.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma & Ambia Hirsi

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo haya ya moja kwa moja. Kwaheri.

  2. Fury atangaza tena kustaafu mchezo wa ndondi

    Tyson Fury walipigana mara ya mwisho mwezi Desemba

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Tyson Fury alipigana mara ya mwisho mwezi Desemba

    Bingwa wa zamani wa uzito wa juu duniani Tyson Fury ametangaza kustaafu kucheza ndondi.

    Fury alipigana mara ya mwisho Desemba alipopoteza mechi yake ya marudiano dhidi ya WBA (Super), WBC na bingwa wa WBO Oleksandr Usyk.

    Fury mwenye umri wa miaka 36 hapo awali alitangaza kustaafu baada ya kumpiga Dillian Whyte mnamo Aprili 2022 lakini akarejea miezi sita baadaye.

    Muingereza huyo amefurahia nafasi mbili kama bingwa wa uzani wa juu na ana rekodi ya kushinda mara 34, kushindwa mara mbili na sare moja.

    "Ningependa kutangaza kustaafu kwangu kutoka kwa ndondi, nilifurahia kila dakika na nitamalizia na hili; Dick Turpin alivaa barakoa."

    Muingereza huyo alimshangaza bingwa wa dunia aliyetawala mchezo huo kwa muda mrefu Wladimir Klitschko mwaka wa 2015 na kushinda mataji ya WBA (Super), IBF, WBO, IBO, na The Ring heavyweight.

    Baada ya zaidi ya miaka miwili na nusu nje ya ulingo, ambapo alishughulikia maswala ya afya ya akili, Fury alirejea ulingoni mnamo 2018 na kuwa bingwa mara mbili kwa kumshinda Deontay Wilder na kutwaa mkanda wa WBC mnamo 2020.

  3. Wachimbaji madini saba waokolewa kutoka kwenye mgodi Afrika Kusini

    Wanaume saba wameokolewa kutoka kwenye mgodi nchini Afrika Kusini baada ya kunaswa ndani ya shimoni kwa zaidi ya miezi miwili.

    Hilo ndilo kundi la kwanza kuokolewa kama sehemu ya oparesheni inayoendelea ya kuwaokoa mamia ya wachimbaji madini haramu waliokwama chini ya ardhi.

    Muungano wa wafanyikazi umetoa kanda ya video zinazoonyesha jinsi wachimba haramu hao wamekuwa wakiishi katika hali duni.

    Kanda hiyo iliyotolewa na Muungano wa wafanyakazi wa General Industries nchini Afrika Kusini inaonyesha makumi ya wanaume wakiwa wamekaa kwenye sakafu chafu.

    Baadhi yao hawana shati na wanaonekana wamedhoofika. Nyuso zao zikiwa na vumbi.

    Sauti ya kiume inayosikika kwenye kanda hiyo inasema kuwa wanaume hao wana njaa na wanahitaji usaidizi. Mtu huyo anaongeza kuwa wachimbaji 96 tayari wamekufa na wanaomba chakula na vifaa.

    Video nyingine inaonyesha kile kinachoonekana kuwa maiti ikiwa imefungwa kwa kwenye mifuko ua plastiki kwenye mgodi

    Muungano huo unasema kanda hiyo ilirekodiwa siku ya Jumamosi.

    Vyombo vya habari vya ndani vinaripoti kuwa wachimbaji hao wameomba barakoa ili kuwasaidia kukabiliana na harufu ya matiti iliyoharibika.

    BBC haijafanikiwa kuthibitisha video hizo kwa ukamilifu.

    Ripoti kuhusu idadi kamili ya wachimba midini walionaswa chini ya ardhi zinatofautiana, lakini inaaminika kuwa takriban wanaume 500 wamenaswa kwenye mgodi katika mji wa Stilfontein kaskazini magharibi mwa Afrika Kusini tangu Novemba mwaka jana.

    Ijumaa iliyopita Mahakama Kuu iliamuru serikali kuwatoa watu hao kwenye mgodi huo.

    Shughuli ya uokoaji ilianza leo Jumatatu asubuhi na inaweza kuchukua siku kadhaa kukamilika.

    Polisi walikosolewa mwishoni mwa mwaka jana kwa kuwanyika chakula na maji wakidai wanataka kuwatoa wachimbaji hao haramu ili wakamatwe.

  4. Mke wa mchezaji wa Arsenal, Havertz afichua jumbe za matusi kutoka mtandao wa kijamii

    Hu

    Chanzo cha picha, Mike Marsland/WireImage

    Maelezo ya picha, Mke wa Kai Havertz, Sophia aliweka hadharani ujauzito wake mwezi Novemba

    Mke wa mshambuliaji wa Arsenal Kai Havertz amechapisha jumbe za matusi alizopokea kwenye mitandao ya kijamii wakati wa mechi ya Jumapili ya Kombe la FA dhidi ya Manchester United, ikiwa ni pamoja na vitisho dhidi ya mtoto wake ambaye hajazaliwa.

    Mshambuliaji huyo, 25, alikosa nafasi ya kushinda goli katika mchezo huo katika muda wa kawaida na kisha penalti yake ikaokolewa na kipa wa United, Altay Bayindir kwenye mikwaju ya penalti na United ikishinda 5-3 kwa penalti kufuatia sare ya 1-1.

    Mke wa Mjerumani huyo Sophia alichapisha kwenye akaunti yake ya Instagram jumbe mbili alizopokea moja kwa moja kwenye mtandao huo.

    Arsenal wameripoti matusi hayo kwa polisi na wanafanya kazi kwa kushirikiana na kampuni ya data ili kuwajua watuhumiwa.

    "Mtu kufikiria kuwa ni sawa kuandika kitu kama hiki inanishtua sana. Aibu juu yako," aliandika huku akiambatanisha picha ya ujumbe huo.

    Wawili hao wamekuwa pamoja tangu 2018 na walifunga ndoa mwaka jana na Sophia alitangaza mwezi Novemba kuwa ni mjamzito.

    Pia unawez kusoma:

  5. Biden na Netanyahu wajadili mpango wa usitishaji mapigano Gaza

    xx

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Marekani Joe Biden na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wamezungumza kwa njia ya simu - katika wiki ya mwisho ya Biden ofisini - huku kasi kuelekea usitishaji vita vya Gaza na kuachiwa kwa mateka ikiongezeka.

    Israel na Hamas wanasadikiwa kupiga hatua katika mazungumzo hayo lakini bado hawajaafikiana kuhusu vipengele muhimu vya makubaliano hayo.

    Ikulu ya White House ilisema Biden alijadili "mazingira ya kikanda yaliyobadilika kimsingi" baada ya Israel kusitisha mapigano na Hezbollah nchini Lebanon, kuanguka kwa utawala wa Assad nchini Syria, na kudhoofika kwa nguvu ya Iran katika eneo hilo.

    Ofisi ya Netanyahu ilisema Biden ameangazia juu ya maagizo aliyowapa wakuu wa mazungumzo huko Doha "ili kuendeleza mpango wa kuachiwa kwa mateka".

  6. Chama cha upinzani Chad chapinga matokeo ya awali ya uchaguzi wa ubunge

    Chama cha upinzani cha Chad National Rally of Chadian Democrats (RNDT) kimekosoa Tume ya Uchaguzi cha nchi hiyo, baada ya matokeo ya awali ya uchaguzi wa ubunge kuonyesha kuwa chama tawala cha MPS kilishinda theluthi mbili ya viti.

    Chama cha Patriotic Salvation Movement (MPS) cha kiongozi wa kijeshi Mahamat Deby kilishinda viti 124 kati ya 188 vya Bunge la Kitaifa katika uchaguzi wa tarehe 29 Desemba.

    Matokeo hayo yametafsiriwa kama njia ya kuimarisha nguvu ya Deby katika taifa hilo la Afrika ya Kati.

    Albert Pahimi Padacké, ambaye chama chake cha National Rally of Chad Democrats (RNDT) kilipata viti 12 pekee, alielezea mchakato huo kama "dhihaka'' akihoji uhuru na kutaka tume hiyo kutoegemea upande wowote inapotekeleza wajibu wake.

    "Tulishinda katika uchaguzi wa wabunge, zaidi ya viti 50," alisema bila kutoa uthibitisho wowote.

    Wakati huo huo, maafisa wa chama tawala cha MPS wamekuwa wakisherehekea ushindi wao ambao ulikuwa umetabiriwa kabla ya uchaguzi kufanyika.

    Uchaguzi huo wa Desemba ambao ulikuwa wa kwanza kuandaliwa kwa pamoja tangu 2011, ulijumuisha chaguzi za kikanda na manispaa.

  7. Jeshi la Nigeria lawaua raia 16 'kimakosa' katika shambulio la anga

    xx

    Chanzo cha picha, Nigeria Air Force HQ/Facebook

    Takriban raia 16 wameuawa katika Jimbo la Zamfara kaskazini-magharibi mwa Nigeria wakati wa shambulio la anga la jeshi la nchi hiyo, kwa kudhaniwa kuwa magenge ya wahalifu.

    Wakazi waliambia vyombo vya habari vya ndani kuwa waathiriwa walikuwa wanachama wa makundi ya walinzi wa eneo hilo na raia wanaojilinda dhidi ya magenge yenye silaha yanayowateka watu kwa lengo la kupata kikombozi.

    Mashambulizi hayo yalilenga magenge ya wanamgambo katika maeneo ya Zurmi na Maradun na gavana wa jimbo hilo, Dauda Lawal, alitoa rambirambi zake kwa jamii.

    Jeshi limekiri kufanya mashambulizi ya angani, ambayo ilisema ni "pigo kubwa kwa majambazi wanaovamia vijiji katika eneo hilo".

    Jeshi la Wanahewa la Nigeria (NAF) lilisema linachunguza "ripoti za kuawa kwa wakazi".

    "Ijapokuwa operesheni hiyo ilifanikiwa kuwaondoa majambazi kadhaa na kusaidia kupatikana kwa baadhi ya waathiriwa wa utekaji, NAF inasikitikakuwa raia kadhaa walipoteza maisha wakati wa operesheni," ilisema katika taarifa.

    Shirika la habari la AFP lilimnukuu mmoja wa wakazi akisema kuwa raia hao walikuwa wakirejea vijijini mwao baada ya kuwafukuza majambazi waliposhambuliwa kwa mabomu.

    Wanakijiji "walipata miili 16 kutokana na mashambulizi na kuwapeleka hospitali watu wengine kadhaa waliojeruhiwa vibaya", Sa'idu Ibrahim alinukuliwa akisema.

  8. Jeshi la Sudan laukomboa mji mwingine wa kimkakati katika jimbo la Gezira

    XX

    Chanzo cha picha, AFP

    Jeshi limetangaza kuwa limeudhibiti mji mwingine muhimu wa Gezira, siku moja baada ya kuuteka mji mkuu wa jimbo hilo la kati, Wad Madani, kutoka kwa wanamgambo wa RSF.

    "Vikosi vya jeshi letu kwa ushirikiano na vikosi vinavyounga mkono na upinzani, vimefanikiwa kuchukua udhibiti kamili wa mji wa Tamboul, na kuukomboa kutoka kwa wanamgambo waasi wa Dagalo [RSF].

    Wanamgambo hao walikabiliwa vikali na walipata hasara kubwa," jeshi hilo lili ilichapisha kwenye mtandao wa Facebook.

    Siku ya Jumamosi Januari 11, jeshi na washirika wake waliuteka tena Wad Madani, mji wa pili kwa ukubwa nchini Sudan baada ya Khartoum, kufuatia siku kadhaa za mapigano makali dhidi ya RSF.

    Kundi la wanamgambo lilikuwa limeuteka mji wa Wad Madani mnamo Desemba 2023.

    Kiongozi wa RSF Luteni Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana pia kama Hemedti, alithibitisha kuwa wapiganaji wake walipoteza mji huo, lakini akaapa kuendelea kupigana.

    Kutekwa tena kwa Gezira ni hatua kubwa kwa jeshi la jeshi tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan vilipoanza Aprili 2024, kulingana na baadhi ya wachambuzi.

    Vyombo vya habari vya Kenya vinaripoti kuwa RSF inatazamiwa kufanya mkutano na waandishi wa habari mjini Nairobi, Kenya hii leo ili kushughulikia masuala ya usalama, masuala ya kibinadamu na mazungumzo ya kusitisha mapigano.

    Soma pia:

  9. India: Mwanamke adai kubakwa na wanaume 64 katika kipindi cha miaka mitano

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mwanamke mwenye umri wa miaka 18 wa Dalit kutoka jimbo la Kerala kusini mwa India amewashutumu wanaume 64 kwa kumdhulumu kingono tangu akiwa na umri wa miaka 13.

    Polisi wamewakamata watu 28 kuhusiana na kesi hiyo hadi sasa - wanaume hao wako chini ya ulinzi na hawajatoa taarifa yoyote kwa umma.

    Washtakiwa hao, ambao wana umri wa kati ya miaka 17 na 47, ni pamoja na majirani wa mwanamke huyo, wakufunzi wa michezo na marafiki wa babake, polisi waliambia BBC.

    Mwanamke huyo aliripoti madai ya kudhulumiwa baada ya timu ya washauri wanaofanya kazi chini ya mpango wa serikali kumtembelea nyumbani kwake.

    Dalit wako chini kabisa katika tabaka la Wahindu na wanakabiliwa na ubaguzi mkubwa nchini humo licha ya kuwepo kwa sheria za kuwalinda.

    Kesi zaidi zinatarajiwa kusajiliwa siku zijazo kwani polisi bado wanachunguza kisa hicho. Timu ya watu 25 imeundwa.

    Polisi wanasema kwamba madai ya unyanyasaji yalianza msichana huyo alipokuwa na umri wa miaka 13. Jirani yake anadaiwa kumnyanyasa na kumpiga picha za ngono, tovuti ya News Minute iliripoti.

    Jirani yake anadaiwa kumnyanyasa kingono tena alipokuwa na umri wa miaka 16, alirekodi video za unyanyasaji huo na kuwashirikisha wengine kadhaa ambao waliendelea kumnyanyasa mwanamke huyo kwa miaka mingi.

    Polisi wanasema kuwa mwanamke huyo alidaiwa kubakwa na genge la watu mara tatu katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

    Inasemekana kuwa wanyanyasaji wake walitumia nambari ya simu ya babake kuwasiliana naye na mwanamke huyo akahifadhi mawasiliano yao kwenye simu. Polisi sasa wanatumia simu kuwatafuta watuhumiwa.

    Familia ya mwanamke huyo iliripotiwa kutofahamu madai ya unyanyasaji huo.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Ukraine inasema imezima shambulio la ndege zisizo na rubani la Urusi

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Urusi imefanya shambulizi la ndege zisizo na rubani 110 za aina ya Shahed, Ukraine imesema.

    Jumla ya ndege 78 zilidunguliwa katika mikoa 12, ikiwa ni pamoja na Kyiv, Jeshi la Wanahewa la Ukraine limetoa taarifa.

    "Kuanguka kwa ndege zisizo na rubani za adui katika mikoa ya Sumy, Kyiv, Zhitomir na Zaporizhia, kumesababisha uharibifu wa majengo ya biashara, taasisi za kibinafsi na za serikali, nyumba za kibinafsi na magari (lakini hakukuwa na majeruhi)," ripoti hiyo inasema.

    Katika mkoa wa Kyiv, kama ilivyoripotiwa na utawala wa kijeshi wa kikanda, kutokana na kuanguka kwa vifusi kutoka kwa ndege zisizo na rubani katika moja ya makazi, nyumba nne za kibinafsi, nyumba ya kulala wageni na kituo cha matibabu ziliharibiwa.

    Uharibifu huo ni mdogo, ripoti hiyo inasema.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Mamilioni ya watu waanza kuoga kwenye mito mitakatifu katika tamasha kubwa zaidi la Wahindu

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mamilioni ya watu wanahudhuria tamasha la Kihindu la Kumbh Mela - linalofafanuliwa kama mkusanyiko mkubwa zaidi wa watu - katika jiji la Prayagraj kaskazini mwa India siku ya Jumatatu.

    Tukio hilo - linalofanyika mara moja kila baada ya miaka 12 - linaanza Jumatatu na kuendelea kwa zaidi ya wiki sita zijazo, wacha Mungu wataoga huko Sangam – katika mto mtakatifu zaidi wa Ganges wa India na mto wa Yamuna na Saraswati ya kufikirika.

    Wahindu wanaamini kwamba kuoga katika mto mtakatifu kutawaondolea dhambi, kutakasa roho zao na kuwakomboa kutoka kwa mzunguko wa kuzaliwa na kifo - kwani lengo kuu la Uhindu ni wokovu.

    Takriban mahujaji milioni 400 wanatarajiwa kuhudhuria tamasha hilo la siku 45, ambalo ni kubwa kiasi cha kuweza kuonekana kutoka angani.

    Leo Jumatatu, waumini milioni tano hadi nane wataoga huku siku inayofuata, idadi hiyo ikitarajiwa kuzidi milioni 20.

    Tamasha la Jumanne litakuwa la kipekee kwani litawashuhudia watakatifu wa Kihindu waliopakwa majivu wakiwa na vazi la nywele zilizochanika, wanaojulikana kama Naga sadhus, wakijizamisha ndani ya maji na baadaye kutoka katika jiji la kaskazini mwa India alfajiri.

    Lakini mamlaka hazijitayarisha kikamilifu kuwakaribisha mamilioni ambao wataendelea kumiminika katika tamasha hilo.

    Pia unaweza kutazama:

  12. Idadi ya vifo na majeruhi ya wanajeshi wa Korea Kaskazini nchini Ukraine yazidi 3,000 - Seoul

    .

    Chanzo cha picha, @ZelenskyyUa

    Vifo na majeruhi wa wanajeshi wa Korea Kaskazini nchini Ukraine huenda vimezidi 3,000, vikiwemo vifo 300 na majeruhi 2,700, mbunge wa Korea Kusini aliyearifiwa na shirika la kijasusi la nchi hiyo amesema.

    Mamlaka ya Korea Kaskazini inaonekana kuwa imetoa wito kwa wanajeshi wake kujiua kwa kujilipua ili kukwepa kukamatwa, mbunge huyo alisema akinukuu Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS).

    Wanajeshi wa Korea Kaskazini waliotekwa hajaonyesha nia ya kwenda Korea Kusini, ingawa Korea Kusini itashirikiana na Ukraine iwapo kutakuwa na ombi, shirika la habari la Yonhap pia liliripoti, likinukuu NIS.

    Soma zaidi:

  13. ‘Niko tayari kwa mabadilishano ya wanajeshi wa Korea Kaskazini’ – Zelensky

    ,

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema yuko tayari kuwakabidhi wanajeshi wawili waliokamatwa kutoka Korea Kaskazini kurudi katika nchi yao ili kubadilishana na wafungwa wa kivita wa Ukraine nchini Urusi.

    "Kwa wale wanajeshi wa Korea Kaskazini ambao hawataki kurejea, kunaweza kuwa na machaguo mengine," Zelensky alisema kwenye mtandao wa kijamii, na kuongeza "wale wanaoonyesha nia ya kuleta amani kwa kueneza ukweli juu ya vita hivi nchini Korea, watapewa fursa hiyo".

    Ukraine ilisema Jumamosi kwamba watu hao walikamatwa tarehe 9 Januari.

    Alipoulizwa mwaka jana, Rais Vladmir Putin hakukanusha kuwa Urusi ilikuwa ikitumia wanajeshi wa Korea Kaskazini katika vita vyake dhidi ya Ukraine, akisema huo ni uamuzi wa Urusi.

    Huduma ya Usalama ya Ukraine ilisema wanajeshi hao wawili wako Kyiv na wanapokea matibabu.

    Wanazungumza Kikorea pekee na wanahojiwa kwa usaidizi wa (Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi) nchini Korea Kusini, idara ya ujasusi ilisema.

    Zelensky alichapisha picha kwenye mitandao ya kijamii Jumamosi zikiwaonyesha wanaume hao, ambao wamejeruhiwa.

    Ofisi ya Zelensky ilisema katika taarifa yake Jumamosi kwamba Warusi "wanajaribu kuficha ukweli kuwa hawa ni wanajeshi kutoka Korea Kaskazini kwa kuwapa hati zinazodai wanatoka Tuva au maeneo mengine chini ya udhibiti wa Moscow".

    Habari za BBC na vyombo vingine vya habari vya kimataifa bado havijathibitisha madai ya Ukraine ya wafungwa na kukamatwa kwao.

    Ukraine na Korea Kusini ziliripoti mwishoni mwa mwaka jana kwamba Korea Kaskazini ilituma takriban wanajeshi 10,000 nchini Urusi.

    Ikulu ya White House ilisema kuwa wanajeshi wa Korea Kaskazini ndio wenye kuathirika kwa kupata majeraha makubwa.

    Mnamo mwezi Desemba, shirika la ujasusi la Korea Kusini liliripoti kwamba mwanajeshi wa Korea Kaskazini anayeaminika kuwa wa kwanza kukamatwa akiunga mkono vita vya Urusi nchini Ukraine alikufa baada ya kuchukuliwa akiwa hai na vikosi vya Ukraine.

    Zelensky alisema Jumapili "hapana shaka kwamba jeshi la Urusi linategemea msaada wa kijeshi kutoka Korea Kaskazini".

    Soma zaidi:

  14. LA: Idadi ya waliofariki katika moto wa nyika yaongezeka huku upepo mkali ukitarajiwa

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Watabiri wa hali ya hewa huko California wanaonya upepo mkali ambao ulisababisha moto karibu na Los Angeles unatarajiwa kushika kasi tena wiki hii, huku vikosi vya zima moto wakiendelea kujitahidi kudhibiti mioto mitatu ya nyikani.

    Maafisa walionya kwamba baada ya wikendi ya upepo uliopungua kasi kiasi, upepo uliokauka wa Santa Ana utavuma tena kuanzia Jumapili usiku hadi Jumatano, na kufikia kasi ya hadi 60mph (96km/h).

    Kabla ya kurejea tena kwa upepo huo, kuna hatua ambazo zimefikiwa kuzuia kuenea kwa mioto mikali ya Palisades na Eaton, ambayo inawaka pande tofauti za jiji.

    Wazima moto wa eneo hilo wanasaidiwa na wafanyakazi kutoka majimbo mengine manane, pamoja na Canada na Mexico, ambao wanaendelea kuwasili.

    Mchunguzi wa afya wa Kaunti ya LA alitoa taarifa za idadi ya waliofariki hadi Jumapili kufikia 24.

    Awali, maafisa walisema takriban wengine 16 hawajulikani walipo.

    Kumi na sita kati ya waliofariki walipatikana katika eneo la moto la Eaton, huku wanane wakipatikana katika eneo la Palisades.

    Moto unaendelea kuwaka katika maeneo matatu karibu na Los Angeles.

    Moto mkubwa zaidi ni Palisades, ambao sasa umeteketeza zaidi ya ekari 23,000 na kudhibitiwa kwa 11%.

    Moto wa Eaton ni wa pili kwa ukubwa na umeteketeza zaidi ya ekari 14,000. Umedhibitiwa kwa asilimia 27.

    Moto wa Hurst umeenea hadi ekari 799 na karibu unadhibitiwa wote kabisa.

    Siku ya Jumapili, wazima moto waliweza kuzuia haraka kuenea kwa moto uliokuwa unaanza kuwaka katika Msitu wa Kitaifa wa Angeles, unaozunguka eneo ambalo ni kitovu cha mpango wa anga za juu wa Marekani na una teknolojia ya siri ya juu.

    Soma zaidi:

  15. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya leo ikiwa ni tarehe 13/01/2025