Kwanini raia wa Zimbabwe wanaandamana?

Rais Emmerson Mnangagwa aliingia madarakani mwaka 2017

Chanzo cha picha, Getty Images

Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa ameshutumu vyama vya upinzani, na nchi za kigeni kwa kutekeleza vitendo vya 'uchokozi' dhidi ya nchi yake huku makundi ya watetezi wa haki za binadamu wakisema polisi na wanajeshi wameendelea kuwakatama wakosoaji mbalimbali.

Picha za vikosi vya usalama vikiwapiga raia zimesababisha ghadhabu miongoni mwa raia na wito Afrika Kusini kutaka kufungwa kwa ubalozi wa Zimbabwe nchini humo mpaka pale haki za binadamu zitakapofuatwa.

Mnangagwa ameapa kupambana vikali na wapinzani na wanaharakati wa haki za binadamu baada ya kuongezeka kwa maandamano ya kupinga vitendo vya rushwa na kutoridhishwa na namna hali ya uchumi inavyoshughulikiwa nchini humo.

Uchumi wa Zimbabwe umeporomoka, serikali ikinyooshea kidole vitendo vya unyonyaji wa kiuchumi na vikwazo vilivyowekwa na nchi za magharibi. Hashtag ya Zimbabweanlivesmatter ni kampeni iliyo maarufu duniani kote wakati huu.

Mnangagwa anasema vikwazo dhidi ya Zimbabwe ni moja ya sababu ya kutetereka kwa uchumi wa nchi hiyo

Chanzo cha picha, EPA

Akitoa hotuba kwa njia ya Televisheni siku ya Jumanne, Bwana Mnangagwa alikemea kile alichokiita '' mipango ya uharibifu ya makundi ya kigaidi ya upinzani''.

''Wale wanaochochea chuki na kuvunja umoja hawatashinda. Watu ambao wamejaribu kuwagawa watu wetu na kudhoofisha mifumo yetu watashughulikiwa,'' alisema.

Wapinzani na wanaharakati juma lililopita waliitisha maandamano dhidi ya serikali, lakini taasisi za kiulinzi ziliwataka watu kusalia majumbani mwao.

Wanasheria wa wanaharakati wa haki za binadamu wamesema zaidi ya watu 60 wamekamatwa.

Mnangagwa katika hotuba yake amesema ''vikosi vya usalama vitaendelea kutekeleza majukumu yao''.

Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa ameshutumu vyama vya upinzani, na nchi za kigeni kwa kutekeleza vitendo vya uchokozi dhidi ya nchi yake

Chanzo cha picha, Getty Images

Sera ya mkono wa chuma dhidi ya wanaharakati wa upinzani

Robert Mugabe alipoondolewa madarakani kwa mapinduzi ya mwaka 2017, watu wengi nchini humo walikuwa na matumaini ya kuwa ni mwisho wa 'ukandamizaji na uongozi mbaya' uliokuwepo kwa miaka 37 alipokuwa madarakani.

Mnangagwa aliingia madarakani akiwa ametoa ahadi ya kufanya mabadiliko lakini wakosoaji wake wamekuwa wakimhusisha na matendo yale yale yaliyoeleza sifa ya Mugabe: utawala wa mabavu, matumizi mabaya ya fedha, kutetereka kwa uchumi na hali ya maisha..

Mnangagwa, 77, ambaye alitegemewa kuwa kiongozi ambaye angekuwa wa tofauti na kiongozi aliyemtangulia, wanaharakati wanamuona kuwa ni rais mkali zaidi kuliko hayati Mugabe.

Kwa mujibu wa New York Times, idadi ya wanaharakati wa upinzani walioshtakiwa kwa vitendo vya uhaini wakati wa utawala wa miaka mitatu wa Mnangagwa ni idadi kubwa kuliko ilivyokuwa kipindi cha Mugabe chote cha kuwepo madarakani, kwa mujibu wa utafiti wa muungano wa mashirika 22 ya wanaharakati wa Zimbabwe.

Wanaharakati wapinzani walikuwa na matumaini ya kufanya mkutano Ijumaa juma lililopita, kupinga miongoni mwa mengine wimbi la vitendo vya ukamataji na utekaji nyara mwezi Mei, pale wanaharakati wanawake watatu, akiwemo Mbunge, walitekwa, kupigwa na kudhalilishwa kingono na watu waliodaiwa kuwa mawakala wa serikali, shutuma ambazo serikali ilikana kuhusika nazo na baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini wanawake hao walishtakiwa kwa kutoa shutuma za uongo dhidi ya serikali.

Polisi wamesema watasimamia kwa nguvu masharti ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona

Chanzo cha picha, Getty Images

Zimbabwe na virusi vya corona

Jinsi serikali inavyoshughulikia janga la virusi vya corona pia kumeibua hisia kuhusu hali ya mfumo wa afya nchini humo na kuchochea zaidi shutuma za rushwa, hali iliyosababisha ongezeko la ghadhabu miongoni mwa raia.

Tayari kumekuwa na hali ya siutafahamu hata kabla ya kuingia kwa janga la virusi vya corona nchini, hospitali hazina dawa za kutosha, vifaa vya kujilinda vya wahudumu wa afya na wafanyakazi wengine kwa kuwa madaktari wengi na wauguzi wameelekea nje ya Zimbabwe kwa ajili ya kutafuta mishahara mizuri, au kuingia kwenye mgomo kupinga malipo duni.

Ofisi ya kamishna wa Umoja wa mataifa inayoshughulikia haki za binadamu imesema ''imesikitishwa'' na kwamba ni kama vile Zimbabwe inavyotumia janga la Covid 19 kama kisingizio cha kubana uhuru wa raia.

Mwezi uliopita polisi walimkamta mwandishi wa habari za uchunguzi na kiongozi wa upinzani, wakishutumiwa kuchochea vurugu.